Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kilichoiangusha Tanzania Kombe la Dunia Futsal

FUTSAL Pict

Muktasari:

  • Tanzania ambayo ilikuwa kundi C pamoja na Ureno, Japan na New Zeland ilikuwa inashiriki mashindano hayo ya FIFA Women’s Futsal kwa mara ya kwanza na ilifungwa jumla ya mabao 21 huku yenyewe ikifunga manne na kumaliza nafasi ya tatu.

BAADA ya vipigo viwili vizito, timu ya Taifa ya Wanawake ya soka la sakafuni kwenye viwanja vya ndani (Futsal), imeondolewa kwenye mashindano ya Kombe la Dunia yanayofanyika Ufilipino, baada ya kufungwa mabao 9-0 na Japan.

Tanzania ambayo ilikuwa kundi C pamoja na Ureno, Japan na New Zeland ilikuwa inashiriki mashindano hayo ya FIFA Women’s Futsal kwa mara ya kwanza na ilifungwa jumla ya mabao 21 huku yenyewe ikifunga manne na kumaliza nafasi ya tatu.

Mabao manne iliyoyapata, iliifunga New Zeland iliyomaliza mkiani katika ushindi wa mabao 4-2 huku ikishuhudiwa nyota wake Mary Siyame aliyefunga hat-trick akichaguliwa mchezaji bora wa mechi.

Hii ni mara ya kwanza kwa mashindano hayo makubwa ya mchezo huo kufanyika kwa mataifa wanachama wa Fifa yakishirikisha jumla ya nchi 16.

Hapa Mwanaspoti limnakuchambulia Tanzania ilivyofuzu na kutolewa katika mashindano hayo hatua hiyo ya makundi, huku timu za Argentina, Colombia, Ureno, Italia, Hispania, Morocco, Brazil na Japan zikifuzu robo fainali.

FUT 04

ILIVYOFIKA KOMBE LA DUNIA?

Yakiwa ndiyo yameanzishwa mwaka huu 2025, Afrika iliwakilishwa na mataifa mawili ya Tanzania na Morocco iliyotwaa ubingwa wa Afrika.

Kwa Afrika yanajulikana kama Kombe la Mataifa ya Afrika ya Wanawake ya soka la sakafuni (Women’s Futsal Africa Cup of Nations) na yalishirikisha jumla ya timu tisa kati ya mataifa 52 wanachama wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuanzia Aprili 22-30 mwaka 2025, Rabat Morocco na fainali zilicheza Tanzania na Morocco.

Katika mechi hiyo ya fainali Morocco ilishinda mabao 4-3 na hivyo, bingwa na mshindi wa pili kufuzu Kombe la Dunia, Tanzania ikiweka rekodi ya kushiriki kwa mara ya kwanza ikiwa ni mara ya kwanza mashindano hayo kufanyika.

Tanzania ilipangwa kundi C na Madagascar, Senegal huku kundi B likiwa na Angola, Misri na Guinea ilhali Kundi A likiwa na  Morocco, Cameroon na Namibia.


NINI KILICHOIANGUSHA

-UZOEFU

Futsal yanazidi kupiga hatua na mataifa mengi yanaendesha mashindano ya ndani na kuvutia wachezaji wengi wa kike kushiriki.

Hii imechangia kwa kiasi kikubwa mataifa hayo kuwa na uzoefu kwani yamekuwa yakijiandaa vizuri kwa kuwepo na mechi nyingi za kimashindano na za kirafiki, tofauti na Tanzania ambayo ilikosa nguvu ya kupambana na kuishia makundi.

Pia kukosekana kwa miundombinu ya mchezo huo (uwanja maalumu wa sakafu) umechangia kukosa uzoefu na Tanzania ilikuwa ikipoteza mipira mara kwa mara na kushindwa kufanya maamuzi ya haraka wanapokuwa na mpira na kushindwa kuhimili kasi ya mchezo.

Timu pia ilionekana kuingika katika mashindano bila ya kuhofia wapinzani na kujikuta ikishindwa kuhimili kasi yao na kukosa nguvu na utulivu.

Presha ya uwanja na mashabiki waliojaa na kukosa umakini wa kukabiliana hasa dhidi ya Ureno na Japan na walishindwa kuusoma mchezo na kufanya maamuzi kwa haraka.

Hata benchi la ufundi pia lilihitaji uzoefu katika kuwasoma wapinzani na kubadili mifumo ya uchezaji kwa wakati na kufanya mabadiliko ya wachezaji.

Mfano Fatuma Issa akitoka hakuna mbadala wake eneo la ulinzi na timu ilionekana kushambuliwa zaidi. Ikumbukwe katika futsal, sekunde chache zinaweza kuamua mchezo na hivyo inahitajika maamuzi ya haraka.

Pia kutokana na kukosekana kwa miundombinu ya viwanja, nyota wengi wanapatiikana kutoka katika timu za soka la kawaida na hivyo kushindwa kuhimili mashindano ya soka la sakafuni, tofauti na mataifa mengine ambayo yamewekeza vizuri kwenye viwanja.

FUT 05

-UBORA WA KIKOSI

Hii ni sababu nyingine ya kutolewa kwenye mashindano hayo na licha ya baadhi ya wachezaji kuonyesha kiwango na juhudi, kuna ambao walionekana dhaifu.

Kikosi kiliingia na wachezaji wenye uwezo lakini wasio na uzoefu na mashindano ya kimataifa na hata majina yaliyotajwa ya nyota wenye ubora, hayakufua dafu Ufilipino kwa kushindwa kuonyesha ubora ule ule waliouonyesha kwenye mashindano mbalimbali ya Afrika.

Pia hakukua na kikosi kipana tofauti na mataifa mengine zilibadilisha wachezaji na kucheza kwa ubora. Tanzania ilipofanya mabadiliko bado hali ilikuwa ile ile na kuzidi kuwapa wapinzani nguvu ya kutawala mchezo.

Damu changa pia ilichangia kutolewa na baadhi ya nyota walioifikisha fainali za Afrika, hawakuitwa isipokuwa wawili, Fatuma Issa na Zawadi Hamis na hivyo wengi kukosa uzoefu.

Aisha Mnunka (Simba Queens), Stumai Abdallah (JKT Queens), Anastazia Katunzi (JKT Queens), Naijath Abbas (JKT Queens) waliokuwa na mchango mkubwa na kuivusha Tanzania hawakuwepo kabisa.

FUT 01

-UBORA WA WAPINZANI

Hii inachangiwa kwa kiasi kikubwa na uwekezaji uliofanywa na nchi hizo katika mchezo huu kama ilivyo kwa Japan na Ureno zilizokuwa kundi moja na Tanzania.

Ureno inayoshika nafasi ya tatu kwenye viwango vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Futsal kwao ni kama mchezo wa soka na washindi hao wa pili wa Uefa European Championship mara mbili (2019, 2022), wana mfumo wa mafunzo ya wachezaji tangu ngazi za vijana, wakitumia teknolojia, mbinu za kisasa na ligi yenye ushindani mkubwa.

Hii imesaidia wachezaji kuwa na kasi, pasi za haraka na kuzuia kirahisi wapinzani huku wakicheza kwa nidhamu ya hali ya juu na ili kuwakabili, ni lazima uwe na kikosi imara.

Kwa kiwango cha Tanzania, ushiriki wao kwa mara ya kwanza na kukosa uzoefu, ilikuwa lazima ikumbane na kichapo kizito kutoka kwa Ureno iliyokomaa kimchezo.

Kwa upande mwingine, Japan nao wamewekeza katika Futsal kwa karibu miongo miwili, wakijenga ligi kubwa, miundombinu ya kisasa na mbinu za mafunzo zinazotumia wataalamu kutoka Ulaya na Amerika ya Kusini tofauti na Tanzania ambayo imekuwa ikitumia wachezaji hao hao wanaocheza soka.

Hata Japan pia ina wachezaji wanaocheza nje ya nchi, jambo linaloongeza ukomavu na uzoefu wa kimataifa. Sifa kubwa ya timu ya Japan ni kasi, mazoezi ya kiufundi, umiliki wa mpira na matumizi sahihi ya nafasi ndogo. Hii ilifanya Tanzania kukutana na timu iliyo bora kimbinu, kimfumo na kimwili, jambo lililoonyesha utofauti mkubwa.

Kwa jumla, ubora na uzoefu wa wapinzani hao wakubwa uliifanya Tanzania kuonekana kama timu inayojifunza na kukua wakati timu hizo zikiwa tayari kwa mapambano.

Ni kweli Tanzania iliingia kwa kujifunza kutokana na ugeni wa mchezo huo, hakukuwa na programu maalulu ya kutafuta vipaji, hakuna ligi wala miundombinu ya kusaidia mchezo huo.

FUT 02

MSIKIE KOCHA

Kocha mkuu wa Tanzania, Curtis Reid alisema kukosa uzoefu mkubwa kwenye michuano hiyo kulisababisha wafanye makosa mengi na kuondolewa kwenye michuano hiyo.

“Wachezaji walijituma, walipambana na Tanzania tuna vipaji vingi lakini uzoefu ulitutoa mchezoni, wenzetu tayari walikuwa vizuri na nawapongeza wachezaji kwa kiwango walichoonyesha.”

FUT 03

WADAU WANASEMAJE

Kocha wa Alliance Girls, Sultan Juma alisema, “Ureno wana wachezaji wanaocheza Futsal pekee kwa miaka 10–15. Wachezaji wetu wengi wanatoka soka la kawaida na kuingia Futsal dakika za mwisho. Hii inafanya tucheze bila ya kuwa na utaalamu na uelewa zaidi wa mchezo huo lakini tulijitahidi sana.”

Kocha wa Ceasiaa Queens, Ezekiel Chobanka alisema licha ya Tanzania kuondoshwa kwenye mashindano hayo lakini walioonyesha uwezo wao lakini walikutana na wapinzani wagumu.

“Ureno, Japan ni timu nyingine wenzetu wameshavuka, wamewekeza zaidi kwenye mchezo huo na hata ukiangalia ‘line-up’ ya timu wachezaji wengi wadogo, kwa hiyo wana programu nzuri ya kutafuta wachezaji maalumu kwa mchezo huo sio kama tulivyofanya sisi.”

Mchambuzi wa soka la wanawake, Damas Ndelema alisema “Dada zetu wengi walioenda ni wenye umri mdogo na hawana uzoefu sana, hivyo hii ilikuwa kama platform kwao tofauti na wale walioenda kwenye Futsal ya Afcon wengi walikuwa wazoefu na mashinadano ya kimataifa kuanzia ngazi ya klabu (Simba Queens na JKT).”