Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dira ya taifa 2050 itakavyokuza vipaji vya wanamichezo tangu utotoni

DIRA Pict

Muktasari:

  • Lengo kubwa hasa la Serikali kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni kuzalisha wanamichezo wenye uwezo wa kushindana kimataifa, kuimarisha uzalendo, mshikamano wa kitaifa na kuchangia ukuaji wa uchumi kwenye sekta ya michezo na burudani.

DIRA ya Taifa ya Maendeleo 2050 inasisitiza umuhimu wa kutambua, kuendeleza na kuwekeza katika vipaji vya michezo tangu utotoni, ikiwa na lengo la kuwajengea watoto mazingira mazuri ya kushiriki kuanzia shuleni, jamii na vituo vya mafunzo.

Lengo kubwa hasa la Serikali kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni kuzalisha wanamichezo wenye uwezo wa kushindana kimataifa, kuimarisha uzalendo, mshikamano wa kitaifa na kuchangia ukuaji wa uchumi kwenye sekta ya michezo na burudani.

Dira inaeleza kuwekeza katika michezo na shughuli za kiutamaduni kuanzia umri mdogo kunawapa watoto na vijana nafasi ya kutambua na kukuza vipaji vyao, huku pia wakijenga utambulisho wa taifa na mshikamano mkubwa wa kijamii inayowazunguka.

Katika kuhakikisha Serikali inafikia lengo na kuwaona vijana wengi wakinufaika na michezo kwa kukuza vipaji vyao na kutanganza zaidi nchi kimataifa kupitia mashindano mbalimbali, zipo mbinu ambazo zitasaidia kufanikisha jambo hilo.

DIR 06

AKADEMI ZA MICHEZO

Ili kufanikiwa katika suala hili, watoto wanapaswa kupewa nafasi ya kushiriki michezo mbalimbali tangu wakiwa wadogo, kwa maana shule ziwe na vipindi vitakavyofanyika mara kwa mara ili kuwasaidia kugundua vipaji vyao haraka na mapema.

Mfano ni mchezaji mpya wa Yanga, Juma Issa Abushiri 'Messi wa Chuga' aliyeanzia mafunzo ya soka katika Kituo cha Future Stars Academy ya jijini Arusha akiwa na miaka sita, kisha uongozi wa Shule za Fountain Gate ukampa ufadhili wa kimasomo.

Baada ya miaka mitano, alipandishwa kikosi cha wakubwa cha Fountain Gate na kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi wa Ligi Kuu Bara (Oktoba 2025) na kuzivutia klabu nyingi za ndani na nje ya Tanzania ikiwemo pia K.A.A. Gent ya Ubelgiji.

Nyingine ni SK Slavia Prague ya Jamhuri ya Czech, Malmo FF ya Sweden na Como 1907 ya Italia zilizovutiwa na kipaji chake japo, Yanga ilimsajili kwa ajili ya msimu wa 2026-2027, ikionyesha uwekezaji unalipa ikiwa tutawekeza kwa vijana wadogo.

Shule za msingi na sekondari zinapaswa ziwe msingi wa ukuzaji wa vipaji, huku vipindi vya michezo visitazamwe kama muda wa kupumzika pekee, bali viwe ni sehemu ya kujenga taaluma za baadaye kwa lengo la kukuza kizazi bora na cha ushindani.

Mashindano ya shule yakiwemo ya Umitashumta na Umisseta yanawapa watoto nafasi ya kuonyesha uwezo wao mbele ya makocha na wadau wakubwa wa michezo, ikiwa ni njia muhimu ya kugundua vipaji vyao kuanzia wakiwa mashuleni hadi ngazi ya taifa.

Kupitia mashindano ya shule, wilaya, mikoa na taifa hutoa fursa ya kuwatambua wachezaji wenye vipaji vitakavyochagizwa na makocha na wadau wa michezo kuona uwezo wa watoto hao na kuwachagua kwa ajili ya mafunzo ya kiwango cha juu zaidi.

DIR 01

MIUNDOMBINU

Uwekezaji katika miundombinu ya michezo ni muhimu sana, kwa sababu viwanja bora, vifaa vya kisasa na salama vya mazoezi huwapa watoto mazingira mazuri ya kukuza vipaji, jambo ambalo ni muhimu kuzingatiwa ili kupata kizazi chenye ushindani.

Katika maeneo mengi ya Tanzania, watoto hulazimika kufanya mazoezi kwenye viwanja visivyo na ubora au bila ya vifaa vya kutosha, ingawa kuongeza uwekezaji wa viwanja vya shule, vituo vya michezo na akademi kutasaidia kukuza vipaji vyao.

Tanzania inahitaji kuongeza uwekezaji katika viwanja vya michezo, vifaa vya mazoezi na programu za ufadhili kwa ajili ya wanamichezo chipukizi, ambao itawapa watoto mazingira bora na mwishoni kufikia ushindani wa kitaifa na kimataifa.

Serikali imeendelea kutangaza mipango ya kujenga shule za michezo na kuboresha miundombinu kwa lengo la kuibua vipaji nchini, jambo ambalo litasaidia kuona sekta hiyo ikizidi kupiga hatua na kuwaona vijana wengi wakipata fursa mbalimbali.

DIR 05

TEKNOLOJIA

Miongoni mwa sehemu inayoweza kutumika kuendeleza vipaji vya michezo ni kupitia teknolojia na video za mazoezi, uchambuzi wa mechi na matumizi ya mifumo ya kisasa ya kufuatilia maendeleo ya wanamichezo yanaweza kuwasaidia vijana.

Kupitia mitandao ya kijamii, wanamichezo wadogo wanaweza kuonyesha vipaji vyao na kuvutia akademi au klabu za ndani na nje ya nchi kutokana na viwango vyao watakavyokuwa wanavionyesha, jambo litakalowasaidia kuwaona wakipiga hatua zaidi.

DIR 02

LISHE BORA

Huenda ikawa ni eneo lisilopewa kipaumbele zaidi ila lishe bora na huduma za afya ni sehemu muhimu zaidi kwa maendeleo ya wanamichezo, kwani mtoto anayefanya mazoezi makali anahitaji chakula chenye virutubisho vya kutosha ili mwili ukue.

Mchezaji yeyote kijana mwenye ndoto za kufika mbali ni lazima azingatie chakula chenye virutubisho vya kutosha ili mwili wake ukue vizuri, huku uchunguzi wa afya na matibabu unapaswa kupatikana kwa urahisi ili kuzuia majeraha ya muda mrefu.

DIR 04

NIDHAMU, ELIMU

Kipaji pekee kwa mchezaji hakitoshi ikiwa hatokuwa na nidhamu, kwa sababu watoto wadogo wanapaswa kufundishwa mafanikio yoyote yanahitajika kujituma, kuheshimu sheria na maadili mema, jambo litakalorahisisha kutimiza malengo waliyojiwekea.

Elimu huwasaidia wanamichezo maisha mazuri hata baada ya kumaliza kucheza hivyo, shule na akademi zinapaswa kuwahimiza uwiano kati ya masomo na michezo ili kuwasaidia vijana kujiandaa watakapostaafu ili kujitengenezea pia mazingira mazuri.

DIR 03

USHIRIKI WA WAZAZI

Kushirikisha wazazi na jamii katika malezi ya vipaji ni sehemu muhimu ya maendeleo ya watoto kukua na kupiga hatua zaidi katika kuendeleza na kuimarisha sekta ya michezo nchini, jambo litakalosaidia kupata wachezaji bora kwa kizazi kijacho.

Kuendeleza vipaji tangu utotoni ni uwekezaji wenye manufaa makubwa kwa Tanzania, kwa sababu itasaidia kupitia utambuzi wa mapema, kuimarisha michezo shuleni, kuongeza idadi ya makocha wakubwa na wenye ujuzi na kuboresha pia miundombinu.


KAULI ZA WADAU

Kocha wa timu za taifa za Tanzania chini ya miaka 10 na 17, Adam Mbwana Mubesh anasema ni jambo nzuri kuona serikali ikiweka malengo makubwa ya kuhakikisha vijana wengi wanapata fursa ya kuonekana, ili kutimiza pia ndoto walizojiwekea.

"Huu ni muda wa serikali kutanua wigo wa kuhakikisha tunapata vituo vingi zaidi ya watoto, kwa macho yetu tu ya kawaida tutaona tuna vingi, ila kiuhalisia bado ni vichache sana kwa sababu ya mahitaji ya vijana wetu waliopo," anasema Mubesh.

Mshambuliaji wa zamani wa Simba na timu ya Taifa Stars, Emmanuel Gabriel 'Batgoal' anayemiliki kituo cha vijana wadogo kilichopo Kawe jijini Dar es Salaam, anasema licha ya juhudi za serikali ila ni muhimu kuangalia masoko ya wachezaji.

"Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia rais wake, Wallace Karia limekuwa mstari wa mbele kuwafuatilia sana vijana wadogo wenye vipaji, sasa isiwe wao peke yao, bali waongezewe nguvu ili tuone maendeleo nchini," anasema Gabriel.

Aidha, Gabriel anasema ili taifa lifanikiwe kuzalisha vijana wengi na wenye vipaji watakaosaidia mbeleni ni lazima pia serikali iangalie namna bora ya kuwaandaa makocha kuanzia ngazi ya shule za msingi na sekondari ili kuwakuza kitaaluma.