Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dira ya taifa 2050 itakavyoimarisha miundombinu ya michezo

DIRA Pict

Muktasari:

  • Miongoni mwa mambo yaliyopewa kipaumbele Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ni kuimarisha miundombinu ya michezo kutokana na umuhimu wake wa kujenga kizazi bora cha wanamichezo kitakacholeta matokeo chanya ya kuitangaza nchi zaidi kimataifa.

KATIKA Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 (DIRA 2050), michezo imepewa nafasi kubwa zaidi kutokana na kuzalisha wanamichezo wenye uwezo wa kushindana kimataifa, kuimarisha uzalendo, mshikamano mkubwa wa kitaifa na kuchangia ukuaji wa uchumi.

Miongoni mwa mambo yaliyopewa kipaumbele Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ni kuimarisha miundombinu ya michezo kutokana na umuhimu wake wa kujenga kizazi bora cha wanamichezo kitakacholeta matokeo chanya ya kuitangaza nchi zaidi kimataifa.

Kuimarisha miundombinu hasa kwa nchi ya Tanzania, kunahusisha ujenzi na ukarabati wa viwanja, kumbi na vifaa vya kisasa vya michezo, ambavyo vitakuwa ni vichocheo vya maendeleo ya vipaji vingi vya wanamichezo na kuongeza ushiriki wa vijana.

Licha ya jitihada kubwa za na Serikali na kuonyesha mwanga kwa kizazi kijacho, ila kuna mbinu za kuimarisha miundombinu ya michezo na  endapo zitazingatiwa tutakuwa na wanamichezo bora wataoitangaza Tanzania kuanzia ndani na kimataifa.

DIRA 05

UKARABATI WA MIUNDOMBINU

Serikali inapaswa kuongeza uwekezaji katika ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya michezo kwa kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya kujenga viwanja vya kisasa, vituo vya mazoezi kwa ngazi ya halmashauri, wilaya, mikoa na hadi ya kitaifa.

Mbali na kujenga miundombinu mipya, ni muhimu pia kukarabati viwanja vilivyopo ili viendelee kukidhi viwango vya kitaifa na kimataifa na uwekezaji huo mkubwa wa Serikali utasaidia kuongeza nafasi za mazoezi kwenye mashindano mbalimbali.

Licha ya ukarabati wa miundombinu, ila wananchi wanapaswa kuhamasishwa kutunza viwanja vya michezo na kushiriki katika shughuli mbalimbali, huku Serikali za mitaa zikiunda kamati ambayo itasimamia ili kupunguza vitendo vyote vya uharibifu.


USHIRIKIANO WA SERIKALI

Ili Serikali itimize malengo yake ya kupata wanamichezo bora watakaotangaza Tanzania kuanzia ndani hadi nje ya nchi, ni muhimu kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi zitakazoweza kujenga, kuendesha na kufadhili viwanja na vituo ya michezo.

Serikali inaweza kutoa motisha kama vile punguzo la kodi, urahisi wa upatikanaji wa ardhi, au mikataba ya muda mrefu ili kuwavutia pia wawekezaji, jambo litakaloongeza ushirikiano na kupunguza mzigo wa kifedha na kuongeza kasi ya maendeleo.


MICHEZO SHULENI, VYUONI

Ni muhimu kwa Serikali kutambua wazi ili kufikia malengo hayo ni lazima kuendeleza miundombinu ya michezo katika shule na vyuo, jambo litakalosaidia kwa kiasi kikubwa kuona ongezeko la wanafunzi wakishiriki kikamilifu kwenye shughuli hizo.

Serikali kwa kushirikiana na wadau wa elimu inapaswa kuhakikisha kila shule ina viwanja vya msingi na vifaa vya michezo vinavyohitajika, hatua itakayosaidia kuibua vipaji mapema na kuwajengea wanafunzi utamaduni wa kushiriki tangu wadogo.

DIRA 04

VITUO MAALUMU

Licha ya mikakati bora ya Serikali, ila inapaswa kujenga vituo maalumu vya maendeleo ya vipaji katika kila mkoa, vikiwa na vifaa vya kisasa, makocha wenye sifa stahiki, wataalamu wa tiba ya michezo na huduma bora za lishe kwa wanamichezo.

Kupitia vituo hivyo, vijana wenye vipaji wataweza kupata mafunzo ya kitaalamu na kuandaliwa kwa mashindano ya kitaifa na kimataifa, vikiwa ni sehemu ya kufanya tafiti kuhusu maendeleo ya michezo na mbinu za kuboresha utendaji wa wanamichezo.


TEKNOLOJIA

Teknolojia ni nyenzo muhimu katika kuimarisha miundombinu ya michezo na kwa nchi kama Tanzania inayoendelea kupiga hatua siku baada ya siku, inapaswa kuitumia pia katika ujenzi na usimamizi wa viwanja vinavyoendelea kujengwa kwa wingi.

Matumizi ya teknolojia huongeza ubora wa huduma, hupunguza gharama za uendeshaji kwa muda mrefu na kuboresha uzoefu wa wanamichezo na watazamaji, jambo ambalo Serikali inapaswa kuwekeza nguvu ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kisasa.


UPATIKANAJI WA MAENEO

Katika ukuaji wa miji na makazi mapya, upatikanaji wa maeneo kwa wanamichezo ni jambo lingine linalopaswa kupewa zaidi kipaumbele, ili kutoa fursa ya kutengwa viwanja vya ujenzi na kumbi za michezo zitazobeba dhamira ya Dira ifikapo 2050.

Hatua hii itazuia kwa kiasi kikubwa upungufu wa maeneo ya michezo unaoweza kujitokeza kutokana na ongezeko la ujenzi wa makazi na biashara, jambo litakalosaidia wananchi wote kujitokeza na kuongeza ushiriki wa watoto, vijana na watu wazima.

DIRA 01

RASILIMALI WATU

Mbinu nyingine muhimu ni kuendeleza rasilimali watu katika sekta ya michezo, kwani uwepo wa viwanja vya kisasa pekee hakutoshi ikiwa hakuna wataalamu wa kuvisimamia, jambo ambalo Serikali inapaswa kuwekeza katika mafunzo ya wahandisi.

Tanzania inapaswa kuwekeza katika mafunzo ya wahandisi wa miundombinu ya michezo, wasimamizi wa viwanja, makocha bora, waamuzi, wataalamu wa tiba na mafundi wa matengenezo, ili kuhakikisha miundombinu yote inakidhi vigezo vinavyohitajika.


UFADHILI WA MIUNDOMBINU

Ni muhimu kuanzisha mifumo endelevu ya ufadhili wa miundombinu ya michezo kwani fedha za Serikali na mapato yanaweza kupatikana kupitia wadhamini, mauzo ya tiketi, matangazo na upangishaji wa viwanja kutokana matukio mbalimbali nchini.

Mfumo huu utasaidia kuhakikisha fedha za matengenezo na maendeleo ya miundombinu zinapatikana kwa wakati bila kutegemea chanzo kimoja, jambo litakaloirahisishia Serikali katika kutekeleza miradi yake muhimu kwa manufaa ya wananchi wote.

DIRA 02

UENYEJI WA MASHINDANO

Kuomba uenyeji wa mashindano mbalimbali huchochea uwekezaji katika ujenzi na ukarabati wa viwanja, kuboresha miundombinu ya usafiri na kuongeza ubora wa huduma zinazohusiana na michezo, huongeza utalii na mapato ya nchi kupitia kwa wageni.

Kitendo cha Tanzania, Kenya na Uganda kuandaa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), ni wazi ni njia muhimu ya kuchochea kujengwa viwanja mbalimbali kwa ajili ya mashindano hayo na kuongeza utalii kutokana na wageni watakaokuja.

Uwanja wa Samia Suluhu Hassan unaojengwa jijini Arusha kwa ajili ya mashindano hayo makubwa yatakayoanza rasmi kuanzia Juni 19 hadi Julai 17, 2027, ni ishara ya uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na Serikali ya Tanzania kukuza michezo.

Hatua ya Serikali kujenga viwanja mbalimbali kuanzia Tanzania Bara hadi visiwani Zanzibar ambavyo vitatumika kwa ajili ya mashindano hayo, ni moja ya kuchochea na kutangaza utalii wetu, kutokana na wingi wa wageni wataoanza kuingia nchini.

Kuimarisha miundombinu ya michezo kwa nchi hasa Tanzania, kunahitaji mipango madhubuti, uwekezaji wa kutosha, usimamizi bora na ushirikiano wa wadau wote, huku Serikali ikishirikiana na sekta binafsi, taasisi za elimu na jamii kwa jumla.