Derby hii kaziipo
MASHABIKI wa Simba na Yanga tayari viroho vimeanza kuwadunda wakati wakiendelea kuhesabu siku kabla ya timu zao kushuka kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam keshokutwa Jumamosi katika pambano lao la mkondo wa pili wa Ligi Kuu ya Bara.
Hilo litakuwa pambano la 108 kwa timu hizo kukutana katika ligi ya Bara tangu mwaka 1965, lakini pia ni la 12 kwao kukutana ndani ya Aprili.
Ndio, tangu mwaka 1965 Simba na Yanga zimeshakutana mara 11 ndani ya mwezi huo na hakuna aliyeibuka mbabe, licha ya Yanga kuongoza msimamo kwa tofauti na bao moja la kufunga dhidi ya watani wao.
Rekodi zinaonyesha katika mechi hizo, Yanga imeshinda michezo mitatu sawa na ilivyo kwa Simba, huku mechi tano zikiisha kwa sare za aina tofauti, Simba ikifunga mabao 13 na Yanga imetupia kambani mabao 14, yaliyowabeba kwenye msimamo wa baina yao.
Hapa chini ni mechi hizo 11 zilizopigwa ndani ya Aprili na kuonyesha namna gani pambano la Aprili 30 linavyoweza kuwa gumu kwa timu zote, kila mmoja ikitaka kutoboa ili kuweka mambo yao sawa.
Yanga inafukuzia ubingwa baada ya kuusotea kwa misimu minne bila mafanikio, ilhali watani wao wakitaka kutetea taji lao ili kurejea ilichowahi kukifanya miaka zaidi ya 40 iliyopita ilipotetea ubingwa wa Bara kwa mara tano mfululizo. Endelea..!
APRILI 29, 1982
Ilikuwa ni Alhamisi moja saafi, Simba na Yanga zilikutana kwa mara ya kwanza katika pambano la Kariakoo Derby.
Ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 katika mechi yao ya mwisho iliyopigwa Septemba 5, 1981 kwa bao la Juma Mkambi ‘Jenerali’, Yanga ilishuka uwanjani kwenye mchezo huo ikiwa na mzuka mwingi.
Kujiamini kwao kuliwabeba, kwani waliendeleza ubabe kwa watani wao kwa kuwanyoosha kwa bao 1-0, lililowekwa kimiani na Rashid Hanzuruni dakika ya pili tu tangu pambano hilo kuanza na bao hilo lilidumu hadi mwisho wa mchezo.
APRILI 16, 1983
Hili ndilo pambano la pili kwa watani wa jadi kukutana ndani ya Aprili na turufu ilikuwa bado ipo kwa vijana wa Jangwani, kwani katika mchezo huo uliopigwa Jumamosi, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-1.
Hiyo ilikuwa ni kati ya mechi 12 za watani ambazo Simba haikuonja ushindi mbele ya watani wao.
Kama hujui Simba ilisubiri miaka sita kufuta uteja kwa Yanga kwani ilishinda mara ya mwisho 1980 na kuchezea vichapo au kuambulia sare mbele ya watani wao hadi mwaka 1986 walipozinduka.
Katika mechi hiyo ya pili ndani ya Aprili, Simba ilikuwa ya kwanza kufunga bao katika dakika ya 14 tu kupitia Kihwelu Mussa kabla ya Yanga kucharuka na kusawazisha katika dakika ya 21 kupitia kwa Charles Boniface Mkwasa kisha Makumbi Juma ‘Homa ya Jiji’ na Omar Hussein ‘Keegan’ kuongeza mengine dakika ya 33 na 84 na kuizamisha Simba.
APRILI 30, 1988
Tarehe kama ya mechi ya msimu huu, lakini iliyopigwa Jumapili watani wa jadi hao walikutana katika mchezo wao wa tatu ambao uliisha bila kutoa mbabe.
Mechi hiyo iliisha kwa sare ya 1-1, Simba ikitangulia kupata bao dkika ya 25 kupitia Edward Chumila na dakika tatu tu, Justin Mtekere aliisawazishia na kuifanya Simba itoke ana alama moja na kupumua baada ya kuchezea vichapo mara mbili.
APRILI 12, 1992
Simba na Yanga zikakutana tena katika mechi nyingine ya Aprili, ikipigwa Jumapili, ikiwa ni baada ya miaka minne kupita bila timu hizo kukutana katika mwezi huo.
Katika pambano hilo tamu na la kusisimua, Yanga iliendeleza ubabe kwa watani wao kwa kuitungua Simba bao 1-0, lililowekwa kambani kwa shuti kali la mbali na beki wa kushoto wa vijana wa Jangwani, Kenneth Mkapa dakika ya 10 ya mchezo huo.
Bao hilo la Mkapa lilikuja ikiwa ni siku chache tangu alifunge pia dhidi ya Ismailia ya Misri katika mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika Yanga ikiwa ugenini.
APRILI 26, 1997
Miaka mitano baadaye watani waka kutana tena Aprili katika mechi iliyoshindwa kutoa mshindi, licha ya Abdallah Msamba ambaye kwa sasa ni marehemu kuandika rekodi ambayo haijawahi kufikiwa tena katika Kariakoo Derby.
Msamba aliyewahi kukipiga Sigara, alifunga bao la mapema zaidi katika derby kwa kutupia sekunde 56 kuifungia Simba bao katika pambano hilo lililopigwa Jumamosi, kabla ya Yanga kuchomoa katika dakika 15 baadaye kupitia Idelfonce Amlima ‘Chinga Two’. Amlima alifunga bao hilo katika dakika ya 16 na kuifanya mechi kuisha kwa sare ya 1-1 ikiwa ni mechi ya pili kumalizika bila kutoa mshindi.
APRILI 17, 2005
Baada ya kuwa mnyonge ndani ya Aprili, Simba ilisahihisha makosa kwenye mchezo huo uliokuwa wa sita kwao kukutana ndani ya mwezi huo.
Tofauti na mechi tano za nyuma, safari hii katika mechi hiyo iliyopigwa Jumapili, Simba ilipindua meza na kuinyoosha Yanga kwa mabao 2-1, licha ya Yanga kutangulia kupata bao kupitia Aaron Nyanda aliyefunga katika dakika ya 39.
Yanga ilishangilia bao hilo kwa muda wa dakika tano tu, kwani Simba ilichomoa kwa bao tamu la Ally Msigwa na kufanya hadi mapumziko matokeo kuwa 1-1 na dakika ya 64 Athuman Machuppa alifunga bao la ushindi na kuizamisha Yanga kwa mara ya kwanza ndani ya Aprili, mechi hiyo ikipigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro.
APRILI 27, 2008:
Simba na Yanga zikakutana tena ndani ya Aprili katika mechi ngumu iliyopigwa Jumapili na kwa mara ya kwanza pambano liliisha bila kufungwa bao lolote, kwani wanaume hao waliishia kutoka suluhu.
Hiyo ilikuwa mechi ya saba kwa timu hizo kukutana Aprili na ilipigwa baada ya kupita miaka mitatu tangu mara ya mwisho kucheza katika mwezi huo wa nne.
APRILI 19, 2009
Mwaka mmoja tena, Simba na Yanga zikakutana ndani ya Aprili ikiwa ni muda mfupi zaidi kwa timu hizo kukutana ndani ya mwezi huo na mechi ilipigwa Jumapili na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Simba ndio iliyokuwa ya kwanza kufunga bao kupitia Ramadhani Chombo ‘Redondo’ anayekipiga kwa sasa Biashara United katika dakika ya 23 tu ya mchezo huo mkali, bao lililodumu hadi mapumziko.
Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kusawazisha bao kupitia Mkenya Ben Mwalala dakika ya 48 na Simba kuongeza bao la pili kupitia Haruna Moshi ‘Boban’ dakika ya 62 na wakati mashabiki wakiamini mechi imeisha kwa Simba kuibuka na ushindi, Yanga ilichomoa bao jioni. Bao hilo lilifungwa na Jerry Tegete dakika ya 90 katika pambano lililochezwa pia Jumapili kwenye Uwanja mpya wa Taifa, sasa Kwa Mkapa.
APRILI 18, 2010
Simba na Yanga zilikutana tena baada ya mwaka mmoja kupita katika ngoma iliyopigwa Jumamosi na Simba kutoka na ushindi mtamu katika pambano hilo la funga nikifunge.
Wekundu wa Msimbazi walipata ushindi wao wa pili dhidi ya Yanga ndani ya Aprili kwa kuifumua mabao 4-3, bao la ushindi likiwekwa kimiani katika dakika za majeruhi na Mkenya, Hillary Echesa.
Simba ilionyesha dhamira ya kutoka na ushindi tangu mapema kwa kupata bao la kuongoza kupitia Uhuru Seleman dakika ya tatu tu ya pambano, kabla ya Yanga kuchomoa katika dakika ya 30 kupitia Athuman Idd ‘Chuji’ na timu kwenda mapumziko zikiwa nguvu sawa.
Kipindi cha pili kilikuwa na balaa kwani Mussa Hassan Mgosi alifunga bao la pili katika dakika ya 53, lililosawazishwa na Jerry Tegete katika dakika ya 69 kabla ya Mgosi kuongeza jingine dakika ya 74 ambalo lilisawazishwa pia na Tegete dakika ya 89.
Mechi ikaongezwa dakika tano na ndani ya muda huo, Echesa akaifungia Simba bao la ushindi lililowanyong’onyeza mashabiki wa Yanga waliokuwa wakiamini ngoma imeisha kwa sare ya mabao 3-3.
APRILI 19, 2014
Ilipita miaka minne kabla ya watani wa jadi kukutana tena ndani ya Aprili, mechi ikipigwa Jumamosi na timu hizo kushindwa kutambiana.
Katika pambano hilo la 10 kwa timu hizo ndani ya Aprili, hadi mapumziko hakuna timu iliyokuwa imeliona lango la mwenzake na kipindi cha pili dakika ya 75 Haruna Chanongo aliitanguliza Simba kwa bao tamu, kabla ya Simon Msuva kuichomolea Yanga dakika 11 baadaye kwa kufunga bao la kusawazisha dakika ya 86.
Mechi ikaisha kwa timu hizo kugawana pointi, huku washambuliaji wa timu hizo wakipoteza nafasi nyingi za wazi kwa kukosa umakini.
APRILI 29, 2018
Katika mechi ya 100 kwa watani wa jadi katika Ligi ya Bara tangu 1965, Simba na Yanga zilikutana tena ndani ya Aprili baada ya kupitia miaka minne.
Mechi hiyo iliyokuwa ya 11 na ya mwisho kwa timu hizo kukutana Aprili ilipigwa Jumapili na Simba iliandika ushindi wake wa tatu katika mwezi huo.
Bao lililoipa jeuri Simba liliwekwa kimiani kwa kichwa na Erasto Nyoni katika dakika ya 37 akimalizia frii-kiki iliyopigwa na Shiza Kichuya na kumpasia kiungo Rafael Daud na mfungaji huyo kuusukumia nyavuni akimtungua kipa Youthe Rostand.
APRILI 30, 2022
Miaka minne tangu Simba na Yanga kukutana ndani ya Aprili, zitakutana tena katika mechi ya kibabe itakayopigwa keshokutwa Jumamosi.
Mechi hii inazikutanisha timu hizo huku zikiwa kwenye mbio za ubingwa, Yanga ikiwa kileleni mwa msimamo huku watani wao ambao ni watetezi wakiwafukuzia nyuma yao. Je, nani atakayeibuka na ushindi? Tusubiri tuone.
Maoni tuandikie: 0693 493 493