Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Depu ataweza kweli!


HUKO mtaani na hata katika mitandao ya kijamii mashabiki na wapenzi wa Yanga wanawatambia wenzao wa Simba baada ya mabosi wa klabu hiyo kushusha mashine za maana katika dirisha dogo.


Achana na Mohammed Damaro au Emmanuel Mwanengo, Yanga imemshusha winga kutoka Uganda, Allan Okello ambaye anatajwa kuanza kufuatiliwa na Simba kabla ya mabosi wa Jangwani kusepa naye.

Juzi kati imemtambulisha straika aliyekuwa akicheza barani Ulaya, Laurindo Dilson Maria ‘Depu’, raia wa Angola mwenye mwili jumba na mwewnye rekodi tamu za kucheza na nyavu.

Tayari mashabiki na wapenzi hao wameanza kuwatisha watani wao wa Simba na timu nyingine pinzani kwamba waandae mabeki la sivyo kitawalamba.

Depu mwenye rekodi nzuri za kufunga mabao akiwa na timu ya taifa ya Angola amesajiliwa kutoka klabu ya Radomiak Radom ya Poland ili kuungana na washambuliaji wengine wa timu hiyo akiwamo Prince Dube, Clement Mzize, Offen Chikola na Mwanengo aliyetua kutoka TRA United.

Mshambuliaji huyo ametua Yanga baada ya mabosi wa klabu hiyo kuendelea na msako wa kuziba pengo lililoachwa na Fiston Mayele aliyepo Pyramids ya Misri.

Ndio, kwani tangu straika huyo Mkongomani na Mfungaji Bora wa Afrika na Mchezaji Bora wa Afrika kwa wanaocheza Ligi za Ndani, Yanga imekuwa ikileta na kuondoa washambuliaji mbalimbali bila nafsi zao kutulia.

Fupa hilo gumu liliwashinda kina Kennedy Musonda, Hafiz Konkon, Joseph Guede, Jean Baleke, Andy Boyeli aliyesajiliwa mwanzoni mwa msimui huu kwa mkopo kutoka Sekhukhune United ya Afrika Kusini kabla ya kuachwa katika dirisha hili mbali na Prince Dube anayejikongoja.

Usajili wa Depu umepokelewa kwa shangwe na mashabiki wa Yanga ambao wanatarajia atoe nguvu mpya ndani ya safu ya ushambuliaji ambayo sasa inaongozwa na Prince Dube.

Hata hivyo, swali kuu linabaki...Je Depu atamudu jinamizi la Mayele ambalo limekuwa likiwateza washambuliaji waliotarajiwa makubwa Yanga au atachemsha mapema kama wenzake?


DEPU NI NANI?

Depu mwenye umri wa miaka 26, akiwa amezaliwa Januari 8, 2000) anacheza nafasi ya mshambuliaji wa kati na kabla ya kujiunga na Yanga, amewahi kutumikia klabu mbalimbali Ulaya na Afrika, ikiwa ni pamoja na Gil Vicente ya Ureno na Vojvodina ya Serbia, kabla ya kwenda kuchukua nafasi Radomiak Radom.

Mshambuliaji huyo ana rekodi kali na timu yake ya taifa ya Angola ambapo katika mechi 18 za kimataifa, akiwahi kuwa mchezaji bora wa michuano ya COSAFA na kuchangia kwa kiwango kikubwa.

Katika ligi za Ulaya msimu uliopita (na Radomiak Radom) alicheza michezo kadhaa na kufunga bao 1 huku akitoa asisti 1, licha ya kucheza dakika chache kutokana na ushindani ndani ya kikosi.

Kwa msimu wa 2025/26 mpaka sasa (kabla ya kuanza kucheza rasmi na Yanga), takwimu zinaonyesha Depu ameshiriki michezo 12 na kufunga mabao 3, ikiwemo mashindano ya kimataifa na ligi mbalimbali.

Kabla ya Yanga kumbeba Depu aliwahi kutakiwa na klabu za Al Ahly ya Misri, Orlando Pirates na Kaizer Chiefs za Afrika Kusini, kuonyesha kuwa ni mchezaji aliye lulu na Yanga kumnasa imechangiwa zaidi na uwepo wa Kocha Pedro Goncalves aliyefanya naye timu ya taifa ya Angola.

Depu anatajwa kuwa na sifa nzuri kama kasi, nguvu ya mwili na uwezo wa kumalizia nafasi ndani ya boksi sifa ambazo benchi la ufundi la Yanga limekuwa likizitafuta kwa muda mrefu.


KAZI IPO HAPA

Fiston Mayele aliondoka Yanga akiwa na rekodi ya mabao 33 katika Ligi Kuu Bara pekee ndani ya misimu miwili na alitimka akiwa mfungaji bora wa ligi msimu wa 2022/23.

Pia alisaidia Yanga kushinda mataji ya Ligi na Kombe la Shirikisho (FA) na kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikilikosa taji kwa kanuni ya bao la ugenini kwani matokeo ya jumla yalikuwa mabao 2-2, Yanga ikilala nyumbani 2-1 na kushinda ugenini 1-0 dhidi ya USM Alger ya Algeria, huku yeye akiibuka Mfungaji Bora wa michuano hiyo 2022-2023.

Kwa kulinganisha, Depu bado hana rekodi kubwa ya mabao katika ligi za Ulaya kama ilivyokuwa Mayele ndani ya Ligi Kuu Bara, lakini ana uzoefu wa kimataifa pamoja na uwezo wa kufunga kwa timu ya taifa na kushinda tuzo za mfungaji bora katika mashindano ya COSAFA.

Hii ina maana kwamba Depu anaweza kuchukua jukumu kubwa ndani ya Yanga, akionyesha sifa za kuleta tishio langoni, lakini bado ana kibarua kikubwa kuvunja rekodi za Mayele ambazo zimeshindwa na washambuliaji wengi.

kazi kuu kwake kufikia au kuzidi kiwango cha mabao na mafanikio alivyokuwa Mayele aliipata hapa nchini.

Mayele ambaye kwa sasa anakipiga PyMsimu wake wa kwanza ndani ya ligi (2021/22) alifunga mabao 16 akiwa nyuma kwa bao moja dhidi ya aliyekuwa kinara, George Mpole ambaye alifunga mabao 17 akiitumikia Geita Gold.

2022/23 ndio ulikuwa msimu wake wa pili na wa mwisho ndani ya kikosi cha Yanga kabla kutimkia Pyramids FC, aliondoka akiwa ametupia mabao 17 akifungana na aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Simba, Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ wakiibuka wafungaji bora.

Baada ya kuacha rekodi hiyo, Mayele alitimka nchini akiwa ametwaa mataji mawili ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA) sambamba na kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika 2022-2023, kisha akaiacha Yanga ikisafa kusaka mbadala sahihi wa kuziba nafasi yake.

Mayele ndani ya kikosi cha Yanga alicheza kwa kiwango cha juu katika misimu miwili akifunga mabao 33 kwenye Ligi Kuu Bara pekee, nje na michuano mingine ikiwemo ile ya kimataifa ambapo msimu wa 2022-2023 walipocheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, alimaliza na mabao saba akiwa kinara.


WALIMRITHI YANGA

Hapa chini ni orodha ya washambuliaji waliosajiliwa Yanga na kubebeshwa tumaini kubwa la kufukia shimo lililoachwa na pengo la Mayele, lakini mambo hayakuwaendea sawa na kama ujio wa Depu utakuwa ni tiba ya tatizo hilo Jangwani.


PRINCE DUBE

Ndiye mshambuliaji ambaye anatazamwa zaidi kwa sasa kutokana na uzoefu alionao kwenye Ligi ya Bara akihudumu kwa misimu minne ndani ya kikosi cha Azam FC na baadae kutua Yanga ambayo sasa anaitumikia kwa msimu wa pili.

Msimu wa kwanza ilikuwa ni 2020/21 akifunga mabao 14, msimu uliofuata hakuwa bora kwani alikaa sana nje ya uwanja kutokana na kupata jeraha la goti, alitupia bao moja tu.

2022/23 Dube akiwa na Azam FC alifunga mabao 12 na msimu wake wa nne na wa mwisho akicheza nusu msimu alitupia mabao saba kabla ya kuondoka kikosini na kuvunja mkataba na timu hiyo.

Akiwa ndani ya kikosi cha Yanga na anatajwa kuwa anaweza kuwa mshambuliaji tishio ndani ya kikosi hicho kutokana na uzoefu alionao ikiwa ni pamoja na kucheza sambamba na viungo wenye uwezo mkubwa.

Dube alikuwa katikati ya Clatous Chama, Pacome Zouzoua na Stephane Aziz Ki ambaye ndiye alikuwa kinara wa upachikaji mabao Ligi Kuu Bara msimu uliopita kabla hajatimka Yanga kwenda Wydad AC ya Morocco akifunga mabao 21 na kumuacha mzawa Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyefunga mabao 19.

Katikati ya viungo hao bora Dube aliifungia Yanga mabao 13 na asisti nane huku msimu huu akiwa bado hajaonyesha makali akiwa mchezaji wa kikosi cha kwanza amefunga mabao mawili pekee na ameongezawa nguvu.

Msimu ambao Dube ulikuwa bora zaidi kwake alifunga mabao 14, ulikuwa ule wa kwanza 2020-2021, baada ya hapo grafu yake ikawa inapanda na kushuka hadi anaondoka kikosini hapo.


KENNEDY MUSONDA

Wakati Yanga inamsajili straika huyu kipindi cha dirisha dogo msimu wa 2022-2023 kutoka Power Dynamos ya Zambia, alikuwa kinara wa mabao 11 katika Ligi Kuu ya nchi hiyo, hivyo CV yake ilitarajiwa kumuongezea nguvu Mayele ambaye alikuwa kwenye kiwango kikubwa.

Msimu wake wa pili ambao ndio ulikuwa wa mwisho kwake ndani ya Yanga, Musonda alifunga mabao manne dhidi ya JKT Tanzania, Simba na Mtibwa Sugar alipoifunga mara mbili. Hivyo jumla amefunga mabao sita katika ligi.

Dakika alizocheza na timu alizopambana nazo ni KMC (64), JKT Tanzania (78), Namungo (90), Geita Gold (17), Singida Fountain Gate (18), Simba (72), Coastal Union (59), Mtibwa Sugar (30), Tabora United (64), Kagera Sugar (34), Dodoma Jiji (61), Mashujaa (22), KMC (30), JKT Tanzania (80), Ihefu (60), Geita Gold (90), Simba (18), Coastal (90) na Mtibwa Sugar (90).

Mara Mayele alipouzwa Misri, mashabiki na hata uongozi wa Yanga uliamini Musonda atakuwa mkombozi kwa kuhisi labda nyota yake ilififishwa na uwepo wa Mkongomani huyo, lakini mambyo yalikuwa sivyo na kuamua kumtema dirisha lililopita alipotimkia Israel.


HAFIZ KONKONI

Straika huyu alisajiliwa mwanzoni mwa msimu wa 2023-2024 akitokea Bechem United ya kwao Ghana ikiaminika anakuja kuziba pengo la Mayele ambaye ndiye alikuwa ameondoka kipindi hicho akiacha rekodi kabambe za mabao.

Konkoni ikaonekana amepewa mlima mrefu wa kuupanda akashindwa kuendana na kasi inayotakiwa akajikuta kipindi cha dirisha dogo akitolewa kikosini akiwa amefanikiwa kufunga bao moja katika Ligi Kuu na kukimbilia Cyprus.


JOSEPH GUEDE

Baada ya kasi ya Konkoni kushindwa kuendana na Yanga, uongozi wa timu hiyo ulifanya uamuzi wa kuongeza nguvu dirisha dogo la msimu uliopita kwa kumsajili Guede ambaye ameitumikia timu hiyo kwa miezi sita tu na kutupia mabao sita kwenye ligi.

Guede alianza kwa kusuasua kutokana na kushindwa kuzoea ligi lakini alionyesha uhai dhidi ya Musonda kwa kumzidi mabao mawili, yeye akitupia kambani sita huku Musonda akifunga manne.

Mshambuliaji huyo licha ya kuanza kuzoea ligi uongozi uliamua kuachana naye na kufanya maboresho kwa kumsajili Prince Dube na Jean Baleke, akiwa ameacha kumbukumbu ya kufunga bao tamu la pili lililoizamisha Simba katika mechi ya Kariakoo Derby, zaidi ya hapo hakuwa na maajabu mengi.

Baadae aliibukia Singida BS aliyoitumikia kwa muda mfupi kisha kuondoka kabla ya dirfisha hili kurejeshwa tena na kuanza kuitumikia katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 timu hiyo ikiishia nusu fainali.


JEAN BALEK

Baleke aliichezea Simba  msimu wa 2023/24 na kutoka akiwa na takwimu nzuri ya mabao na mechi kabla ya kuondoka.

Katika mechi 19 za Ligi Kuu Bara, Baleke aliweza kufunga mabao manane na asisti moja, akionyesha uwezo mzuri wa kupachika mabao kabla ya safari yake kuelekea Jangwani.

Usajili wa Baleke kwenda Yanga ulifanyika msimu wa 2024, wakati timu hiyo ilipokuwa ikitafuta kuongeza nguvu safu ya ushambuliaji ikiwa pamoja na usajili wa Prince Dube.

Baleke aliingia katika orodha ya wachezaji waliokuwa Yanga wakiwa tayari kukamilisha usajili wa msimu wa 2024/25 kama sehemu ya mikakati ya kuboresha safu ya ushambuliaji ya Mabingwa wa Ligi Kuu Bara.

Hata hivyo, licha ya kujiunga na Yanga mshambuliaji huyo alijikuta akiingia kwenye vita ya namba na  wachezaji wengine kama Dube na Clement Mzize na kujikuta akifunga bao moja pekee akiwa na timu hiyo kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union. Kisha akatemwa bila kutimiza ile ndoto walizokuwa nazo mashabiki wa Yanga juu yake na kile alichokifanya Msimbazi.


ANDY BOYELI

Huyu alisajiliwa katika dirisha kubwa la msimu huu kutokea Sekhukhune United ya Afrika Kusini na kutarajiwa kuwa ‘Mayele’ mpya Jangwani kwa sifa alizokuwa nazo hasa alipokuwa akicheza Zambia.

Hata hivyo, akiitumikia Yanga kwa muda wa miezi sita tu kati ya mkataba wa mwaka mmoja wa mkopo na kutemwa dirisha hilo dogo litakalofungwa Januari 30 akiwa amefunga mabao mawili tu kupitia mechi ya Ligi Kuu dhidi ya vibonde, KMC iliyocharazwa mabao 4-1.

Ndipo, kuondoka kwake kukafungua milango la Depu kutua Jangwani na nini kitafanywa na straika huyo mpya kutoka Angola? Ngoja tuone!