DAH! Morrison ana majanga huyo

DAH! Morrison ana majanga huyo

Muktasari:

  • MSHAMBULIAJI Bernard Morrison amekutana na adhabu ya kufungiwa kuzikosa mechi tatu na kulimwa faini ya Sh1 milioni kutokana na kosa la kumkanyaga makusudi beki wa Azam FC, Lusajo Mwaikenda katika mchezo ulioikutanisha timu hiyo na Yanga kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Septemba 6, mwaka huu uliomalizika kwa sare ya kufungana mabao 2-2.

MSHAMBULIAJI Bernard Morrison amekutana na adhabu ya kufungiwa kuzikosa mechi tatu na kulimwa faini ya Sh1 milioni kutokana na kosa la kumkanyaga makusudi beki wa Azam FC, Lusajo Mwaikenda katika mchezo ulioikutanisha timu hiyo na Yanga kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Septemba 6, mwaka huu uliomalizika kwa sare ya kufungana mabao 2-2.

Adhabu hiyo iliyotolewa na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) ilitangazwa Alhamisi na kutokana na hilo, mechi tatu ambazo mshambuliaji huyo raia wa Ghana atakosa ni dhidi ya timu za Ruvu Shooting, Namungo na Simba.

Hapana shaka kumkosa Morrison katika mchezo dhidi ya Simba ni pigo kubwa kwa Yanga kutokana na uhodari wa mshambuliaji huyo raia wa Ghana pindi awapo uwanjani katika kutengeneza nafasi na kufunga mabao.

Morrison kuikosa mechi dhidi ya Simba ni mwendelezo wa nyota huyo kukaa nje katika baadhi ya mechi kubwa hasa za Simba na Yanga pamoja na zile za kimataifa kutokana na kutumikia adhabu zisababishwazo na matukio ya utovu wa nidhamu au yale ya nje ya uwanja, jambo ambalo limekuwa likizigharimu timu zake kwa namna moja au nyingine katika michezo hiyo tangu atue nchini 2020.

Tangu Morrison alipotua nchini 2020 alipojiunga na Yanga kisha akaenda Simba na baadaye akarudi Jangwani, timu hizo mbili kubwa na kongwe nchini zimekutana mara 10 ambapo mshambuliaji huyo amecheza michezo saba huku akikosa mitatu ambayo yote ilitokana na changamoto za utovu wa nidhamu ama matukio ya nje ya uwanja. Makala hii inakuletea orodha ya michezo mikubwa ambayo Morrison alikosa kutokana na changamoto zake.


Yanga 1-1 Simba (Novemba 7, 2020)

Ulikuwa ni mchezo wa kwanza kwa Morrison kuukosa akiwa anaitumikia Simba, alishindwa kucheza kutokana na uwepo wa mgogoro wa kiusajili na Yanga ambayo aliachana nayo, na klabu hiyo kuamua kufungua shauri kuwa nyota huyo alijiunga na timu nyingine huku akiwa na mkataba nao.

Hata hivyo baadaye mshambuliaji huyo alishinda kesi hiyo na kuruhusiwa kuitumikia Simba.


FC Platinum 1-0 Simba ( 23/12/2020)

Mshambuliaji huyo wa Ghana alijikuta akiachwa na Simba katika msafara wa timu hiyo ulioenda Zimbabwe kuumana na FC Platinum katika mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambao Simba ilipoteza kwa bao 1-0.

Inadaiwa kuachwa kwa nyota huyo kulitokana na pendekezo la kocha Sven Vandenbroeck kwa kile kilichodaiwa kuwa ni sababu za kinidhamu.


Simba 4-0 FC Platinum (06/01/2021)

Vandebroeck baada ya kutosafiri na Morrison kwenda naye Zimbabwe katika mchezo wa kwanza dhidi ya Platinum, kocha huyo aliendelea kumfungia vioo katika mechi ya marudiano iliyochezwa Januari 6, 2021 ambayo Simba ilishinda mabao 4-0.


Kaizer Chiefs 4-0 Simba (15/05/21)

Bernard Morrison alikosa mchezo huo wa kwanza wa ugenini wa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2020/2021 kutokana na zuio alilowekewa na mamlaka za uhamiaji za Afrika Kusini kwa kosa alilowahi kulifanya nchini humo miaka ya nyuma kabla la kujiongezea siku za kuishi baada ya ule aliopewa awali kumalizika.


Simba 0-1 Yanga (Septemba, 2021)

Bao pekee la Fiston Mayele lilitosha kuifanya Yanga kuizamisha Simba katika mchezo huo wa Ngao ya Jamii ambao Morrison alishindwa kuichezea Simba kutokana na kutumikia adhabu aliyopewa kwa kosa la kuvua nguo kwenye mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam miezi miwili nyuma ambayo Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0.


Orlando Pirates 1-0 Simba ( 24/04/22)

Sababu ileile iliyomfanya Morrison asiende Afrika Kusini kuichezea Simba dhidi ya Kaizer Chiefs mwaka mmoja uliopita, ilimponza tena wakati timu hiyo ilipokabiliana na Orlando Pirates, Aprili 24 mwaka huu katika mechi ya marudiano ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Katika mchezo huo Simba walipoteza kwa bao 1-0 na ikalazimika mshindi wa kutinga nusu fainali apatikane kwa mikwaju ya penalti ambapo Pirates walishinda kwa penalti 4-3.


Yanga 1-0 Simba (28/05 /2022)

Mchezo huu wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam, Simba walipoteza kwa bao 1-0 lililofungwa na Feisal Salum katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Morrison ambaye alikuwa bado hajajiunga na Yanga, hakuitumikia Simba katika mchezo huo kutokana na likizo aliyopewa na uongozi wa Simba ambao unadaiwa haukufurahishwa na mwenendo wake wa nje ya uwanja.