CUNHA; Nyota wa Brazil anayejenga utajiri England
Muktasari:
- Cunha alifunga bao la ushindi katika mechi dhidi ya Arsenal na kuzidi kujizolea sifa kwa mashabiki wa Man United ambao wamekuwa wakitasabasamu tangu Michael Carrick achukuwe mikoba ya kuwa kocha wa mpito baada ya kufukuzwa kwa Ruben Amorim.
MANCHESTER,ENGLAND: KWA wiki kadhaa jina la Matheus Cunha limekuwa likitajwa sana na mashabiki wa soka hususani wa timu yake Manchester United kutokana na kiwango bora alichoonyesha tangu kuanza kwa msimu huu.
Cunha alifunga bao la ushindi katika mechi dhidi ya Arsenal na kuzidi kujizolea sifa kwa mashabiki wa Man United ambao wamekuwa wakitasabasamu tangu Michael Carrick achukuwe mikoba ya kuwa kocha wa mpito baada ya kufukuzwa kwa Ruben Amorim.
Hata hivyo, mbali ya kuanza kujenga ufalme wake taratibu katika kikosi cha Man United, Cunha pia anazidi kuwa tajiri siku hadi siku kutokana na kiasi cha pesa anachoingiza kama mshahara pamoja na madili mengine nje ya uwanja. Leo tumekusogezea mali anazomiliki na namna anavyopiga pesa.
ANAPIGAJE PESA
Utajiri wa Cunha unakadiriwa kufikia Dola 15 milioni, mshahara wake kwa wiki ni Pauni 200,000 lakini pia hupokea na bonasi zinazotokana na kufunga mabao pamoja na kuasisti.
Staa huyu pia ana ubalozi wa kampuni mbalimbal ikiwamo Nike na EA Sports ambapo kiujumla anakunja takribani Dola 3 milioni kwa mwaka kutokana na madili hayo.
Kwa sasa pia ameanzisha biashara ya kujenga nyumba na kuzipangisha huko Brazil ambayo kwa mujibu wa watu wake wa karibu, amewekeza sana nguvu katika miradi hiyo.
MIJENGO
Mara tu baada ya kutua Man United Juni mwaka jana, ripoti zinaeleza alitoa Pauni 5 milioni kwa ajili ya kununua moja ya mjengo wa kifahari maeneo ya Hale, Greater Manchester.
Nyumba hiyo awali ilikuwa inamilikiwa na mchezaji mwingine wa zamani wa Man United, Zlatan Ibrahimovic.
Kiujumla ina vyumba sita vya kulala na vyoo sita pia. Ina Gym, ukumbi wa kutazama sinema, baa, bwawa la kuogelea na bustani ya kisasa.
Pia kama ilivyoelezwa hapo juu, jamaa anamiliki nyumba kadhaa huko Brazil kwa ajili ya kupangisha.
NDINGA ZAKE
Mercedes-Benz AMG G63 – Dola 200,000
Audi RS7 – Dola 120,000
BMW i8 – Dola 150,000
Porsche 911 Turbo – Dola 180,000
Range Rover Vogue – Dola 90,000
MSAADA KWA JAMII
Kwa asilimia nyingi, Cunha hutoa misaada zaidi nchini Brazil na sio England. Hata hivyo, amekuwa akifanya hivyo kimya kimya bila ya uwepo wa kamera au macho ya watu.
Katika zoezi la kutoa misaada pekee kwa mwaka hutoa takribani Pauni 100,000.
FAMILIA NA MAISHA BINAFSI
Cunha yupo kwenye ndoa na mrembo Gabriela Nogueira ambaye kabla ya kumuoa tayari alishazaa naye mtoto mmoja wa kiume. Ndoa yao ilifanyika mwaka 2024 katika majira ya kiangazi.
Katika siku ya harusi Cunha alisema ndoto yake kubwa ilikuwa ni kumuoa Nogueira kwa sababu ni mwanamke aliyekuwa naye tangu akiwa hana kitu hadi kufikia alipofikia.