Mwamba Jet LI unajua maisha yake kwa sasa?
Muktasari:
- Ripoti zinaeleza wazalishaji hao wako tayari kumwaga pesa ndefu kuhakikisha gwiji huyo wa sanaa ya mapigano anakubali kuigiza tena.
BEIJING, CHINA: WIKI iliyopita, staa wa filamu za mapigano duniani, Jet Li, alitajwa sana kwenye vyombo vya habari amepewa ofa nono na baadhi ya kampuni kwa ajili ya kuigiza tena, baada ya kusimama kwa muda mrefu.
Ripoti zinaeleza wazalishaji hao wako tayari kumwaga pesa ndefu kuhakikisha gwiji huyo wa sanaa ya mapigano anakubali kuigiza tena.
Ikiwa dili hilo litafanikiwa, Jet Li ambaye mwaka 2008 alikataa takribani Dola 27 milioni kutoka kwa moja ya kampuni ya Marekani kwa sababu alihitji zaidi kuangalia afya yake, atakuwa ni miongoni mwa wasanii wakongwe walioingiza pesa nyingi kwa mwaka huu.
Lakini ishara zinaonyesha asilimia 90, huenda Jet Li asiikubali ofa hiyo kama alivyowahi kufanya hapo awali, lakini je? jeuri hii ya kukataa pesa nyingi inatoka wapi? Hapa tumekuletea undani wa utajiri alionao.
ANAPIGAJE PESA
Kwa kipindi ambacho alikuwa kileleni, Jet Li alikuwa akilipwa kati ya Dola 15 hadi 20 milioni kwa filamu moja, hasa katika filamu kubwa alizofanya Hollywood kama The Expendables, Romeo Must Die na The Mummy: Tomb of the Dragon Emperor na nyingine nyingi.
Mbali na uigizaji, Jet Li anapata mapato kutokana na mikataba ya matangazo na udhamini wa kampuni mbalimbali za Asia zinazojihusisha na teknolojia na afya.
Inakadiriwa kwa mwaka, mapato yake kutokana na vyanzo vyake binafsi na filamu humwingizia zaidi ya Dola 10 milioni na hapo ni ikiwa hajacheza muvi yoyote.
Kwa nyakati tofauti amewahi kuwa balozi wa kampuni kubwa kama Adidas, Hublot, AUX Group na San Miguel.
Vilevile ana shule yake ya kufundisha Tai Chi ambayo amefungua kwa kushirikiana na Jack Ma ambaye ni bosi na mmiliki wa kampuni ya Alibaba.
Mwaka 2015, Jet Li pamoja na mkewe Nina Li, walitoa takribani Dola 148 milioni kwa ajili ya kununua hisa za kampuni ya Far East Holding International.
MIJENGO
Jet Li anamiliki jumba la kifahari jijini Beijing lenye thamani ya takriban Dola 10 milion na ndani yake lina Gym binafsi ya mazoezi ya mapigano, Bwawa kubwa la kuogelea na Chumba maalum cha tiba na mazoezi ya afya.
Vilevile anamiliki nyumba nyingine Singapore, inayotumika zaidi kwa mapumziko ya familia wenye thamani ya Dola 8 milioni.
NDINGA
Mercedes-Benz S-Class – Dola 120,000
BMW 7 Series – Dola 110,000
Lexus LX – Dola 130,000
Tesla Model X – Dola 100,000
MSAADA KWA JAMII
Jet Li ni mmoja wa mastaa wanaoheshimika zaidi kutokana na msaada anaotoa kwa jamii. Kutokana na taasisi yake ya The One Foundation, amekuwa mstari wa mbele kwa waathirika wa majanga ya asili, elimu kwa watoto wasio na uwezo na huduma za afya kwa watu wasiojiweza.
Inaelezwa kwa mwaka taasisi hiyo hutumia zaidi ya Dola 5 milioni kama sehemu za misaada.
FAMILIA NA MAISHA BINAFSI
Jet Li yupo kwenye ndoa na mrembo Nina Li Chi, ambaye pia alikuwa mwigizaji maarufu wa filamu za Kichina.
Wana watoto wawili wa kike na familia yao imekuwa ikiishi maisha ya utulivu licha ya umaarufu alionao.
Kwa muda mrefu, Jet Li amekuwa akipambana na changamoto za afya, hali iliyomfanya kupunguza sana uigizaji na kujikita zaidi kwenye mambo ya familia yake na kusaidia jamii.