Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CAF yazipa mchongo mpya Simba, Yanga, Azam na Singida

WAWAKILISHI Pict


DIRISHA dogo la usajili la msimu wa 2025-2026 kwa Tanzania litafunguliwa Januari Mosi mwakani na timu zitapata nafasi ya kuboresha vikosi vyao.


Dirisha hili ni kwa timu zote, lakini ni muhimu zaidi kwa timu zinazoshiriki michuano ya CAF, yaani Yanga, Simba, Azam FC na Singida Black Stars.


Hii ni kwa sababu kuna unafuu mkubwa wa sheria za usajili za CAF utokanao na mabadiliko ya sheria yaliyofanywa na Kamati ya Utendaji ya CAF, Januari 31, 2025.

Kwa mujibu wa mabadiliko hayo, mchezaji anaruhusiwa kuchezea timu mbili tofauti katika msimu mmoja wa michuano ya CAF katika hatua zote.

Zamani, mchezaji hakuruhusiwa kuchezea timu zaidi ya moja katika michuano hiyo. Akishachezea timu moja halafu akahamia timu nyingine kupitia dirisha dogo, basi haruhusiwi kuichezea timu mpya.

Lakini sasa inawezekana, klabu zinaruhusiwa kusajili wachezaji ambao tayari wameshachezea kwingine katika hatua zilizopita za michuano hiyo ya Afrika ndani ya msimu huo huo.

Kwa mujibu wa Ibara ya 7 ya Sura ya 4 ya sheria ya usajili ya mashindano ya CAF, kila klabu inaruhusiwa kuongeza wachezaji wapya saba katika orodha ya wachezaji iliyonao, ili mradi tu jumla ya wachezaji isizidi 40.

Hii ni kwa sababu CAF iliongeza idadi ya wachezaji kwa klabu moja kutoka 30 hadi 40 tangu mwaka 2020, dirisha dogo la 2020/21 kukabiliana na changamoto ya UVIKO 19.

Idadi hiyo haijapungua hadi sasa, hivyo kama timu ilikuwa haijafikisha wachezaji 40, inaruhusiwa kuongeza wachezaji wapya wasiozidi saba.

Zaidi ya hapo, kila klabu inaweza kusajili wachezaji wengine wapya wanne kwa kuwaondoa wengine wanne waliokuwepo, ili mradi tu hao wanne wanaoondolewa wawe hawakuwahi kucheza mechi yoyote hapo kabla.

Ila hawa wanne wapya wanapaswa kuwemo kwenye orodha ya wale saba.


NEEMA KWA TIMU ZETU

Kwa sasa Ligi Kuu Bara imesimama kupisha AFCON 2025 inayoendelea huko Morocco, Kombe la Mapinduzi 2026 litakaloanza wikiendi hii na baadaye mechi za hatua ya makundi ya CAF...zinatarajiwa kurudi mwishoni wa Januari na Februari na kumalizika Mei!

Timu za Tanzania zinazoshiriki mashindano ya CAF zimecheza mechi chache sana za ligi hadi sasa. Wakati vinara JKT Tanzania wakiwa na mechi 10, Azam, Simba na Singida zina mechi tano huku Yanga ikicheza sita hadi sasa.

Kutoka mwishoni mwa Januari na Februari hadi Mei ni miezi minne...ndani ya muda huo kuna mechi 25 za ligi, mechi za CAF na Kombe la Shirikisho la CRDB.

Hii ina maana timu hizi zitakuwa na ratiba iliyobana sana kuanzia Februari hadi Mei...na wachezaji watakuwa na muda mfupi sana wa kupumzika ili kurejesha miili katika hali ya kawaida.

Hapa bado kuna majeraha na adhabu...wakati mgumu mno!

Kitu pekee timu hizi zinaweza kufanya ni kuongeza ukubwa wa vikosi na hapo ndipo kwenye lengo la andiko hili.

Ijumaa iliyopita, Mwenyekiti wa Bodi ya Simba, Crescentius Magori alisema moja ya sababu za timu yake kufungwa mechi kadhaa za msimu huu ni majeraha ya wachezaji wao muhimu, beki Abdulrazack Mohamed Hamza na kipa Moussa Camara.

Sasa wakati wa kuziba haya mapengo ni huu. Timu hizi zinatakiwa zilitumie vizuri dirisha hili kwa kuongeza wachezaji wengi na wenye uwezo.

Kusaini wachezaji kwenye dirisha dogo ni muhimu sana kwa sababu kunavipa vilabu fursa ndogo lakini muhimu katika kuainisha upungufu uliojitokeza ndani ya msimu husika ili kuimarisha timu kwa sehemu ya msimu iliyobaki.


Sababu za msingi za usajili dirisha dogo

Kuainisha mahitaji ya haraka: Dirisha dogo la Januari, kwa ujumla wake, hutoa fursa adhimu kwa vilabu vinavyokabiliana na majeraha ambayo hayakutarajiwa na ya muda mrefu, kushuka ghafla kwa viwango vya wachezaji muhimu au kuongeza kipaji kikubwa kinachoweza kubadilisha kabisa msimu wa klabu husika.

Faida ya kiushindani: Usajili wa mapema na wa kimkakati unaweza kwa namna moja ama nyingine kuinua kiwango cha timu na hatimaye kuongeza ushindani kwenye ligi hata kuchangamsha mbio za ubingwa, kuwania kufuzu kimataifa au kukwepa kushuka daraja. Kupata wachezaji sahihi kwa wakati sahihi kunaweza kubadilisha kabisa kiwango cha timu.

Mwishowe, mkakati madhubuti wa usajili dirisha dogo hupunguza usajili wa kukurupuka. Pia huipa timu uhakika wa kutumia vizuri raslimali zake kufikia malengo bila kuharibikiwa wakati msimu ukiendelea.


NYOTA BORA WALIOWAHI KUSAJILIWA DIRISHA DOGO

WAWA 04
WAWA 04

1. AZAM FC

i. Yeison Fuentes Mendoza 

Raia huyu wa Colombia alijiunga na Azam FC dirisha dogo la 2023/24 na moja kwa moja akaingia kikosi cha kwanza kuchukua nafasi ya nahodha Daniel Amoah.

Mechi ya kwanza ilikuwa dhidi ya Simba iliyofanyika Mwanza na kumalizika kwa sare ya 1-1. Baada ya hapo amekuwa mhimili wa Azam hadi sasa.


KWA NINI NI USAJILI BORA

Mchango wa moja kwa moja: Licha ya kuingia dirisha dogo, Fuentes aliingia kwenye kikosi cha moja kwa moja kuwa tegemeo.

Mhimili katika ulinzi: Anasifiwa kwa matumizi ya akili, nidhamu ya mchezo, uimara kwenye kukaba na ubora katika mipira ya juu. Anajidhirisha yeye ni mlinzi wa daraja la juu.

Uongozi: Japo ni mkimya, Fuentes anajua kujipanga vizuri na kuwaongoza wenzake katika safu ya ulinzi.

Ubora wa kiufundi: Anacheza kwa utulivu mkubwa hata akiwa kwenye presha, ni mlinzi anayeleta utofauti mkubwa na muhimu kwenye ligi.

Thamani ya pesa: Kiwango chake kinazidi kwa mbali matarajio kwa usajili wa dirisha dogo, akiwapa Azam uimara na utulivu katika ulinzi.


Mchango wake kwa Azam:

Ni mchezaji muhimu kwa Azam katika harakati zao za kupambana na magwiji Yanga na Simba.

Ujio wake ulisaidia kuimarisha safu ya ulinzi ya Azam FC na kuisadia klabu hiyo kumaliza ligi kwenye nafasi ya pili na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB msimu wa 2023/24.


ii. Mohmed Mustafa

Usajili wa mkopo kutoka El Merreikh ya Sudan. Alisajiliwa dirisha dogo la 2023/24 baada ya Azam FC kuchoshwa na makosa ya mara kwa mara ya kipa wao namba moja, Abdulahi Idrissou kutoka Ghana.

Alikuja na uzoefu wa kutosha akiwa namba moja wa taifa lake la Sudan, Mustafa alileta utulivu golini kwa Azam FC na kutoa mchango mkubwa.


KWA NINI ULIKUWA USAJILI BORA:

Ubora: Alikuwa anaheshimika sana Sudan na akaenda kuheshimika sana Azam na Tanzania kwa jumla.

Kimkakati: Usajili wake wa mkopo uliogeuka wa kudumu mwisho wa msimu ulifanywa kwa umakini mkubwa, ingizo la muda mfupi kutatua tatizo muhimu kwenye timu.


iii. Adolf Mutasingwa

Anachukuliwa kama mmoja wa viungo bora sana wa kitanzania wanaocheza kwenye ligi ya Tanzania.

Alisajiliwa dirisha dogo la 2023/24 akitokea Iceland ambako alicheza kwa muda mrefu. Mutasingwa ni zao la akademi ya Azam FC mwaka mmoja na Yahya Zayid, lakini hakuwahi kuchezea timu kubwa ya Azam.

Kiungo nyota: Alikuja kuwa mchezaji muhimu katika kiungo cha Azam FC kilichokuwa na utajiri kama wa Yahya Zayid, James Akaminko na Sospeter Bajana.

Kuitwa Timu ya taifa: Kiwango chake kikampa utambuzi kwenye timu ya taifa na kuitwa na kocha Hemed Morocco.


WAWA 01

2. SIMBA

i. Elie Mpanzu

Anaitwa Ellie Mpanzu Kibisawala. Wakati akiwa AS Vita ya Kinshasa DRC alikuwa anaitwa Volcano. Alijiunga Simba dirisha dogo la 2024/25 na moja kwa moja akawa msaada mkubwa kwenye timu.


Taarifa muhimu za usajili wake:

Klabu: Simba

Mchezaji: Elie Mpanzu (DR Congo)

Muda wa usajili: Alisainiwa mnamo Septemba au Oktoba 2024 lakini usajili ukafanyika Januari dirisha dogo.

Mkataba: Miaka mitatu.

Umuhimu: Anachukuliwa kama mmoja wa wachezaji wa daraja la juu kwenye ligi ya Tanzania.


KWA NINI NI USAJILI BORA:

Mchango wa haraka: Simba ilihitaji winga mwenye uwezo kama wa Mpanzu kuwapa ushindani waliokuwepo...na akafanya hivyo moja kwa moja alipoanza kuitumikia klabu hiyo na kuisaidia kufika fainali ya Kombe la Shirikisho la Afrika.

Ubora juu ya idadi: Mkakati wa Simba ulilenga kupata wachezaji wa ubora wa juu na Mpanzu akatosha moja kwa moja.

Malengo ya muda mrefu: Simba walimhitaji tangu 2022 na walipompata wakampa mkataba wa miaka mitatu ili kujipa utulivu wao wenyewe na mchezaji pia.


ii. Jean Baleke

Zao la Akademi ya TP Mazembe na mfungaji bora wa DRC msimu wa 2020/21 mbele ya Fiston Mayele aliyekuwa AS Vita.

Alisajiliwa dirisha dogo ya 2022/23 akitokea TP Mazembe na moja kwa moja akawa mchezaji muhimu kikosini akifunga mabao nane.


Taarifa muhimu za usajili wake:

Mchango wa haraka: Alifunga katika mchezo wake wa kwanza na moja kwa moja akajipambanua kama mtu hatari sana mbele ya goli.

Mfungaji wakati akiondoka: Hata akiondoka Simba, alibaki kuwa mfungaji wao bora kwa mabao yake manane katika mechi 19 akidhihirisha ubora wake.

Mafanikio ya muda mfupi: Mkopo wake uliipa Simba ubora na machaguo ya kutosha hivyo kumpunguzia kocha presha.

iii. Luis Miquissone

Alipokuja tanzania akabatizwa jina la Konde Boy, Luis Miquissone ni mmoja wa wachezaji hatari sana kuwahi kucheza Tanzania.

Alisajiliwa dirisha dogo la 2019/20 akitokea U D Songo ya Msumbiji, alikokuwa kwa mkopo kutokea Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.


KWA NINI NI USAJILI BORA:

Mchango wa moja kwa moja: Miquissone aling'ara moja kwa moja, akiisaidia Simba kushinda mataji mawili ya ndani, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Azam Sports, 2020.

Kiwango cha juu: Alionyesha kiwango bora sana, akishinda tuzo ya mchezaji bora wa wiki wa CAF akifunga bao bora na muhimu dhidi ya miamba wa Afrika, Al Ahly, mwaka 2021.

Kipenzi cha mashabiki: Haraka haraka akaja kuwa kipenzi cha mashabiki wa Simba kwa uwezo wake na mchango kwa timu yao.

Akauzwa kwa timu kubwa, kwa bei kubwa: Mafanikio yake na Simba yakawavutia Al Ahly kumnunua kwa bei mbaya, Agosti 2021.


WAWA 02

3. YANGA

i. Kennedy Musonda

Wakiwa kwenye kipindi kigumu cha kumpoteza Feisal Salum, Yanga ilikimbilia Zambia kumnasa kinara wa mabao wa ligi yao, Kennedy Musonda kutoka Power Dinamos ya Kitwe wakati wa dirisha dogo la 2022/23.


Mchango na mafanikio

Ujio wake uliongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji iliyomtegemea Mayele kwa kiasi kikubwa.

Magoli muhimu: Alifunga mabao muhimu, ikiwemo nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Afrika dhidi ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini na fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports dhidi ya Azam FC.

Mafanikio ya ndani: Wakati akiwa Yanga (hadi katikati ya-2025), Musinda alikuwa mchezaji muhimu katika kipindi ambacho yanga walitawala soka la Tanzania, akichangia ubingwa wa mataji matatu ya Ligi Kuu, mataji matatu ya Kombe la Shirikisho na Ngao ya Jamii mara mbili.

Mchango wake kwa jumla: Katika muda wake wote akiwa Yanga, alifunga mabao 34 na kutoa pasi 13 za mabao kwenye mashindano yote, akiondoka kwa heshima mbele ya mashabiki wa Yanga. 


ii. Israel Patrick Mwenda

Ingizo la dirisha dogo la 2024/25 kwa kopo kutokea Singida Black Stars, kijana huyu zzao la Alliance Akademy ya Mwanza, ni moja ya sajili bora za dirisha dogo.

Aliingia kwa mkopo wa miezi sita na baadaye akasaini mktaba wa kudumu wa miaka mitatu.


Alama ya usajili wa dirisha dogo

Kuimarisha ulinzi: Mwenda alisajiliwa maalumu kutatua changamoto ya ulinzi upande wa kulia baada ya kuumia kwa 'Jeshi' Yao Kouassi.

Kiwango cha haraka: Moja kwa moja akiweka alama kikosini, huku mashabiki wa watangazaji wa mpira wakimsifia kwa ubora wake katika mechi muhimu, ikiwemo dhidi ya timu yake ya zamani, Simba katika mechi ya watani wa jadi.

Mchango kitakwimu: Kiwango chake katika msimu wa 2024/25, ambao alifunga mabao 3 na kutoa pasi mbili za mabao kwenye mechi 17, ilionesha ubora wale katikaupande wa pili wa uwanja...yaani kwenye ushambuliaji.

Kutoka mkopo hadi mkataba wa kudumu: Mafanikio yake katika miezi sita ya mkopo yakaishawishi yanga kumnunua moja kwa moja.


WAWA 03

4. SINGIDA BLACK STARS

i. Jonathan Sowah

Kama kuna usajili ulishtua wengi basi ni wa mshambuliaji raia wa Ghana, Jonathan Sowah, kujiunga na Singida Black Stars.


Taarifa muhimu za usajili:

Klabu: Singida Black Stars

Kutoka: Mchezaji huru

Mchango: Mabao 13 katika mechi 11.

Mkataba: Alisaini miaka miwili, lakini baadaye akatolewa bure kwenda Simba.

Kwanini ni mchezaji muhimu:

Mchango wa haraka: Moja kwa moja akaenda kuwa mfungaji bora wa Singida Black Stars licha ya kuingia dirisha dogo.

Ubora uliodhihirika: Alikuwa nyota wa Medeama SC ya Ghana na akaendelea kuwa muhimu kwa Singida Black Stars.


ii. Amas Obasogie

Kipa raia wa Nigeria  aliyenaswa na Singida Black Stars kutoka Fasil Kenema ya Ethiopia. Aliongeza kitu kikubwa sana kwenye milingoti miwili ya lango la Singida Black Stars na kuwasaidia kufuzu kushiriki mashindano ya kimataifa...na sasa hatua ya makundi.


Taarifa muhimu za usajili:

Jina: Amas Obasogie (raia wa Nigeria, kipa wa timu ya taifa - Super Eagles).

Alikotoka: Fasil Kenema (Ethiopia).

Klabu: Singida Black Stars (Tanzania).

Alijiunga ligi: Januari 2025.

Kwanini ni usajili bora: Aliitwa timu ya taifa ya Nigeria.

Kama timu hizi ziliweza kusajili wachezaji bora kama hawa wakati ule, basi zinaweza tena kusajili wengine.

Cha msingi walitumie tu vizuri hili dirisha dogo!