Fountain Gate yatumia silaha ya vijana
Muktasari:
- Klabu hiyo, imelazimika kutegemea zaidi wachezaji waliokuwepo msimu uliopita pamoja na vijana wawili waliopandishwa kutoka timu ya Under 20, huku benchi la ufundi likifanya maandalizi ya kutosha kupitia kambi za Morogoro na Arusha.
FOUNTAIN GATE imeingia katika msimu mpya ikiwa na changamoto ya kutokuwa na uwezo wa kusajili wachezaji wapya katika dirisha kubwa la usajili, lakini pamoja na hali hiyo uongozi wa klabu hiyo umeweka wazi kuwa haujaingiwa na hofu, ukisisitiza kuwa kikosi kilichopo kinaweza kupambana na ushindani wa Ligi Kuu Bara.
Klabu hiyo, imelazimika kutegemea zaidi wachezaji waliokuwepo msimu uliopita pamoja na vijana wawili waliopandishwa kutoka timu ya Under 20, huku benchi la ufundi likifanya maandalizi ya kutosha kupitia kambi za Morogoro na Arusha.
MAANDALIZI YA MOROGORO YAWAPA NGUVU
Ofisa habari wa Fountain Gate Issa Mbuzi anasema timu ilianza maandalizi ya msimu mpya kwa kuweka kambi Morogoro kwa muda wa wiki mbili, ikiwa na lengo la kuwapa wachezaji programu kamili ya maandalizi kabla ya kuingia kwenye mashindano rasmi.
“Tuweka kambi Morogoro kwa wiki mbili. walipata muda wa kufanya program zote kwa maana zile za uwanjani, gym, na nje ya uwanja. Hiyo wanaita outside beach, kwa maana inaweza ikawa ni mchangani ama kutafuta sehemu ya kupima kidogo kwa ajili ya wachezaji kupumua na kutafuta nguvu na ule utimamu ambao ulikosekana ama ulipungua kwenye haya mapumziko,” anasema.
"Mbali na mazoezi, Fountain Gate ilipata nafasi ya kupima uwezo wa kikosi kupitia mechi mbili za kirafiki. Kwenye mechi za kirafiki tuliifunga Geita kwa mabao 2-1 kabla ya kupata ushindi mwingine wa mabao 2-0.
"Baada ya kukamilisha wiki mbili za maandalizi Morogoro, timu ilisafiri kuelekea Babati kwa ajili ya kushiriki mashindano ya Tanzanite International Season ambayo yaliahirishwa."
ADHABU YAFUNGA USAJILI
Katika eneo ambalo Fountain Gate imekumbana na changamoto kubwa ni usajili, baada ya klabu hiyo kutumikia adhabu ya kufungiwa madirisha mawili ya usajili.
Hali hiyo imeifanya timu kutoweza kuongeza mchezaji mpya katika dirisha kubwa la msimu huu wa 2026/27.
“Kuhusu maeneo yaliyoongezewa nguvu kwenye usajili, sisi hatujaingiza mchezaji mpya kwenye dirisha kubwa mpaka sasa. Changamoto ilikuwa ni adhabu tunatumikia baada ya kufungiwa madirisha mawili,” anasema.
"Kwa mujibu wa uongozi, adhabu hiyo ilianza kutekelezwa katika dirisha dogo la msimu wa 2025/26 na dirisha kubwa la msimu wa 2026/27 limekuwa la pili. Hivyo, matumaini ya klabu hiyo ni kutumia dirisha dogo la Januari kuongeza damu mpya katika kikosi chake."
JANUARI YATAJWA
Licha ya kutosajili wachezaji wapya kwa sasa, Fountain Gate haijakaa kimya, badala yake imeamua kutumia vijana kutoka kwenye mfumo wake wa malezi.
Klabu hiyo imewapandisha vijana wawili kutoka timu ya Under 20 ambao wataungana na wenzao waliopandishwa tangu msimu uliopita.
“Tumeongezwa vijana wawili kutoka timu ya vijana ambao watakwenda kuungana na wachezaji wengine wa U20 waliopanda tangu msimu uliopita. Timu iko vyema kwa sababu maeneo yote yana wachezaji zaidi ya mmoja,” anasema.
WANNE WANG'OKA
Fountain Gate imepoteza wachezaji kadhaa waliokuwa sehemu ya kikosi cha msimu uliopita, akiwamo Ismail Kada, Timison Mwanuke, David Messi na Juma Issa Bushiri.
Issa Mbuzi anasema, pamoja na kuondokewa na wachezaji hao, uongozi unaamini sehemu kubwa ya kikosi imebaki, hivyo timu bado ina msingi wa kuanzia.
“Ukiachana na hao niliowataaja wengine wote wamebaki, kwa hiyo tunaamini waliobaki wataisaidia timu ingawa tumeumia lakini sio sana na tunaweza kuendana na kasi ya ligi,” anasema.
VIJANA WAPEWA KAZI
Wakati baadhi ya klabu zikiingia kwenye msimu mpya zikiwa na usajili mkubwa, Fountain Gate imeamua kuweka imani zaidi kwa vijana.
Issa Mbuzi anasema uongozi unaamini wachezaji hao wanaweza kutumia nafasi waliyopewa kuonyesha uwezo wao na kuleta ushindani ndani ya kikosi.
“Ukiamini vijana wanakulipa, na hawa tuliowaongeza ni vijana hodari ambao ninafikiri watapenda kuleta surprise,” anasema.
MACHO KWA SINGIDA
Mchezo dhidi ya Singida Black Stars unatajwa kuwa mtihani muhimu kwa Fountain Gate katika kuanza safari yake ya msimu mpya.
“Tunajua haijawahi kuwa rahisi kucheza na Singida. Mechi zote tulizocheza nao ni ngumu kupata matokeo mazuri na huwa na ushindani mkubwa kutokana na mahusiano yaliyopo,” anasema Issa Mbuzi Ofisa habari wa FountainGate.
“Tunatamani kuanza na msingi mzuri kwenye mwanzo huu wa ligi tunataka kutumia mchezo huo kama sehemu ya kujipima na kuanza safari ya ligi kwa msingi mzuri."
MALENGO YA MSIMU UJAO
Ofisa habari huyo anasema kuwa, uongozi wa kikosi hicho unaamini bado inawezekana kufanya vizuri licha ya adhabu ya usajili, huku Januari ikibaki kuwa dirisha muhimu kwa klabu hiyo kuongeza nguvu.
“Mashabiki watarajie kuwaona hao kama Mungu akiwajalia afya na moyo wa kupambana, basi tutatengeneza msingi wa msingi, hata hao watakaokuja wataongeza tu nguvu."
REKODI ZA MSIMU ULIOPITA
Msimu uliopita wa 2025/2026, Fountain Gate FC ilimaliza Ligi Kuu ikiwa katika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi.
Timu hii inayotumia Uwanja wa Tanzanite Kwaraa mkoani Manyara kama uwanja wao wa nyumbani, ilipambana vikali kujihakikishia nafasi ya kusalia ligi kuu kwa msimu unaofuata, ikimaliza nafasi ya 12.