Prime
Azam FC ilivyozipiku Simba, Real Valladolid kwa Lameck Lawi
NAHODHA wa timu ya Taifa chini ya miaka 20, Lameck Lawi amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Azam FC akitokea Coastal Union. Hata hivyo, uhamisho wake haukuwa tambarare hata kidogo....ilikuwa vita kubwa kati ya Azam FC na timu mbili kubwa; Simba ya Tanzania na Real Valladolid ya Hispania.
Simba SC
Itakumbukwa msimu uliopita wakati kama huu Lawi alikuwa katikati ya mgogoro mkubwa uliowahusisha Simba na Coastal Union.
Timu hizo mbili kongwe zilishakubaliana kufanya biashara ya mchezaji huyo na Simba tayari ilishaweka pesa kwenye akaunti husika; ya Coastal Union na ya mchezaji mwenyewe.
Hata hivyo, baadaye Coastal Union ikaingia tamaa, ilikuja dili kutoka Ulaya ambalo lilitoa harufu ya pesa nyingi zaidi na Lawi alitakiwa kufanya majaribio na kama angefaulu basi angeuzwa kwa pesa nyingi sana.
Coastal Union ikabadilika, ikairudishia Simba pesa zake na kumpeleka Lawi Ulaya na Wekundu wa Msimbazi ikacharuka na kuamua kumtangaza mchezaji bila hata picha yake.
Kesi ikafika hadi kwenye mamlaka za soka, lakini hakuna kilochobadilka...Simba ikamkosa Lawi na yeye huko Ulaya hakufaulu majaribio, akarudi klabuni kwake kuendelea na majukumu ya kawaida.
Msimu ukaisha na Simba ikarudi tena kwa Coastal Union kutaka kuanzia pale ilipoishia msimu uliopita.
Real Valladolid
Ni timu iliyoshuka daraja msimu uliopita kutoka Ligi Kuu ya Hispania La Liga.
Ilimtaka Lawi kwa muda mrefu na mazungumzo yao na Coastal Union yalienda sawa. Hata hivyo, tatizo ni wakati huo timu hiyo ilikuwa kwenye mchakato wa kubadilisha umiliki.
Itakumbukwa timu hii ilikuwa inamilikiwa na Ronaldo de Lima, nyota wa zamani wa Brazil na klabu kadhaa kubwa Ulaya.
Lakini baada ya kushuka daraja, Ronaldo akaiuza kwa wamiliki wapya. Ni mchakato huu wa mauziano ndiyo uliochelewesha dili la Lawi.
Azam FC
Wakati Simba inaendelea kufanya mazungumzo na Coastal Union na Real Valladolid ikibadilishana hati za mauziano ya klabu, Azam FC ikapiga hodi barabara ya 11 jijini Tanga kuhitaji huduma ya Lawi.
Coastal Union haikuficha kitu, ikaweka wazi ofa ilizonazo mkononi kutoka kwa Simba na Real Valladolid, lakini Azam FC ikafika mara mbili ya ofa hizo na kuondoka na Lawi.
Biashara ilikamilika kabla ya kuisha kwa ligi na Azam FC ikawa inasubiri msimu uishe ili imtangaze, huku Simba ikiendelea kuisumbua Coastal Union bila kujua tayari biashara imeshafanyika.
Kazi ikawa kwa Coastal Union kuitaka Azam FC itangaze ili Simba itulie...na Azam FC haikutaka kutangaza hadi msimu umalizike.
Kule Hispania nako mchakato wa kuuzwa Real Valladolid ukakamilika, ikarudi kwa Lawi, hata hivyo, ikapata taarifa tayari ameshauzwa kwa Azam FC. Hii ikawaumiza sana kwa sababu tayari ilishamuweka kwenye mipango yao. Ikajaribu kuwasiliana na Azam FC, lakini dau ililotajiwa likaikimbiza.
Msimu ulipoisha Azam FC ikamtangaza Lawi, tena kwa kuweka picha yake halisi na taarifa zikawafikia Simba na kukubali yaishe na pamoja na Real Valladolid zikawa zimezidiwa ujanja na Azam FC na sasa Lawi katua Chamazi na anasubiri msimu kuanza.