Anko Lao na majibu konki
1. ANKO Lao, binti miaka 19 nina mchumba ana miaka 21 anasoma chuo, ila kwa sasa kabadilika sana na upendo umeisha. Nifanyeje ili malavidavi yarudi kama zamani?
Aisha Fadhil, Chalinze
Jibu: Kama kusoma hujui, basi hata picha kuielewa ni shida? Huyo chalii wako kuna mawili, pengine masomo yanampelekesha au keshapata king’asti kipya huko chuoni. Hivyo kaa kwa akili, ukiona vipi jiongeze tu, kwani hujaolewa hivyo hubanwi bibie!
2. ANKO Lao, kijana miaka 23 nina mke nampenda sana, ila mwenangu anachepuka na kidume kingine. Nifanyeje kwani nateseka kuona nasalitiwa?
James Mshana, Mwanga
Jibu: Wewe unajua mke au unamsikia tu? Huyo ni mkeo kweli au deiwaka unayeishia naye, maana sidhani kama ni mke anaweza kutoka nje ya ndoa nawe ukajua na mkaendelea kuishi. Ila nini? Sioni sababu ya kujitesa, tafuta chaka jipya ule raha, maisha yenyewe mafupi haya tabu ya nini buana!
3. ANKO Lao, nilikuwa na mke niliyezaa naye watoto wawili, lakini alitorokea kwao, nikimfuata arudi hataki. Nifanyeje?
Mwasimba Junior
Jibu: Mke hawezi kutoroka burebure, bila ya shaka we ni pasua kichwa na ameona ni vyema atimkie kwao awe salama. Kama ya lawama, ebu jitathmini kwanza uone unakwamia wapi...pie ujue siku zote ndoa si lelemama, kama haujajipanga mtaishia kukimbiana tu. Ni hivyo tu!
4. ANKO Lao, nina mpenzi lakini ni msumbufu hatari kiasi ananinyima raha, nifanyeje ili aache kunisumbua?
Jenifer, Kyela
Jibu: Sijaelewa anakusumbua vipi? Kama ni ishu ya kupiga shoo...maji ukiyavulia nguo huna budi kuyaoga, ila kama ni mzinguaji tu, kaa naye chini mzungumze, mkiona vipi kila mtu ale kona yake, maisha ni kutafuta na sio kutafutana wee vipi buana?!
5. ANKO Lao, ninaye mume nampenda sana, ila anachoniudhi kila simu ikipigwa kwake anaenda kupokelea nje. Maana yake nini na nifanyeje?
Sukaina, Chunya
Jibu: Huyu jamaa yako anaonekana ni kicheche ndo maana hana jeuri ya kupokea simu mbele yako au huwa ana dili asizopenda we uzijue, ila nini ujue mapema ukimchunguza sana kuku huwezi kumla na kama unakereka jaribu kukaa naye mzungumze ajirekebishe, ukiona vipi akili kichwani mwako!
6. ANKO Lao, nina tatizo ambalo sijui mwisho wake, kwani kila mwanamke ninayekuwa na uhusiano naye, nikishapiga shoo natokea kumchukia na kusaka mwingine. Nifanyeje nami nataka kuwa na familia?
Rashid, Bagamoyo
Jibu: We huna lolote unasumbuliwa na tamaa tu, yaani ni wale vidume visivyopitwa na sketi. Ebu jaribu kubadilika na ujue mapema ukiendelea kujiendekeza utayavagaa, dunia imejaa vijidudu kila kona shauri yako. Tuliza akili chagua pisi kali ufunge ndoa!
7. ANKO Lao, kuna kijana mmoja amenitokea na kusema ananipenda, lakini nimemchunguza na kubaini hajatulia, kwani ana wanawake wengine, japo nikimuuliza anasema walikuwa zilipendwa. Nifanyeje?
Tecla Andrew, Arusha
Jibu: Kama umebaini ni kicheche sasa we unachokitafuta kwake ni nini? Kinga ni bora kuliko tiba, unaweza kujibebisha kwake ukaja kujuta. Tafuta chaka jingine la kistaarabu ule malavidavi kwa raha zako bila presha!
8. ANKO Lao, mi ni mfanyabiashara ndogondogo na kuna mteja wangu mmoja amekuwa akinisumbua akidai eti ananizimia na anatamani nimuoe. Unanishauri vipi?
Samson Killer
Jibu: Kama analipa na unadhani atakufaa kwa maisha ya kufa na kuzika, usijikabe sana, lakini kama hasomeki, tuliza ubongo...hapa mjini kuna majambazi wa aina nyingi, shauri yako usije tu ukafilisika!
9. ANKO Lao, binti miaka 20 nimepewa ujauzito na mume wa mtu nilipomjulisha kaniambia nitoe kwa vile hawezi kubeba jukumu sehemu mbili. Nifanyeje nami sitaki kuitoa?
Zamaradi, Mwanza
Jibu: Mwana kulitafuta mwana kulipata, kama ulijua ni mume wa mtu kiherehere gani kilikutuma ukajiachia kizembe? Ishu ya kuflashi mzigo usikubaliane nayo, kwani ni dhambi na kosa kisheria, ila mbane jama’ako hadi kieleweke, kwa vile huo ni msalaba wenu hakuna namna mradi raha mlikula wote kiroho safi!
10. ANKO Lao, kijana miaka 32, najishughulisha na ufundi magari (makenika), ila sioni faida kwani napata fedha ya kula tu. Nifanyeje?
John Kimweri, Kimara Korogwe
Jibu: Inategemea ofisi ipo maeneo gani na kile unachokipata unakitumiaje, kama unadhani umakenika haulipi, jiongeze...kazi zipo kibao muhimu tu kuvaa ujasiri wa kukomaa nazo...kama mambo hayaendi nenda wewe...naamini ukifanyia kazi ushauri huu, utatoboa kwa vile hakuna lisilowezekana.
11. ANKO Lao, ninaishi na mwanamme tunayependana sana, ikiwa ni kama mwezi sasa, lakini ameambiwa anitimue, huku baba’ake mdogo ananiimbisha. Nifanyeje?
Stella, Songwe Mbeya
Jibu: Sijajua huyu mtu wako aliambiwa na nani akutimue? Ila mwembe wenye matunda ndio upopolewao mawe. Kaa chini na wenzako ujue msimamo wake kwako, ukiona hasomeki jiongeze tu, hakuna namna, kwani kisicho riziki hakiliki.
12. ANKO Lao, nina miaka 27 ila nimekuwa na bahati mbaya ya kupendwa na malofa tena wenye wivu hadi wanakera, ila nikipata mwenye nazo anakuwa bahili kinoma. Nifanyeje?
Esther Mtui, Tanga
Jibu: Kinachokusumbua wewe ni tamaa tu, usipoangalia ujue utachakazwa sana. Ila kama vipi saka zako ule laifu usitegemee mifuko ya watu, utadhalilika wakati mwanamke kujiheshimu na kujiamini!
13. ANKO Lao, nina demu beki tatu, ila amekuwa mgumu kutoa mzigo kwani kila nikimpanga anadai yupo bize. Nifanyeje?
Issa Sekatawa, Tanga
Jibu: Bora hata anavyokupanga, kwani unaonekana una fyucha naye zaidi ya kumchezea kwa sababu huwezi kumuita mpenzio beki tatu? Halafu kama kweli unampenda kwanini usifuate taratibu na kumbeba jumla ujilie kwa raha zako badala ya kuvizia kihuni!
14. ANKO Lao, binti miaka 18, nina mpenzi nampenda, ila tatizo lake anapenda sana kupiga shoo hadi anaudhi, japo ananipenda pia. Nifanyeje ili nisiachane naye?
Eunice, Ilala
Jibu: We mwana una kiranga, mara hii umeshaanza kuneng’eneka katika umri huo...usipokuwa makini utachezewa uchakae mapema bila hata ndoa...mayanki wa sasa wanapenda kitonga hasa wakipata mteremko...jishikilie...shauri yako!
15. ANKO Lao, kijana miaka 26, nimejenga nyumba na kumiliki usafiri wangu wa bodaboda, tatizo bado sijapata mwenza wa kuishi naye. Nifanyeje?
James, Tunduma
Jibu: Jitathmini kwanza, kwanini pisi kali zinakukwepaje wakati upo freshi kama sio wamekushtukia? Ebu jipime, huenda hujatulia au una mkono wa birika, kitu ambacho pisi kali nyingi hawamaindi...ebu lainisha mambo uone, kwani si unajua hakuna mkate mgumu mbele ya chai.
16. ANKO Lao, Mambo. Mie ni miaka wa miaka 19 na nina wanaume wawili wanaonipenda na kunijali na wote wanataka kunioa. Nifanyeje?
Lily, Boko
Jibu: Unachokitafuta utakipata...yaani miaka 19 una vidume wawili, unadhani sifa? Ebu tuliza akili halafu chagua mmoja unayeamini atakufaa kwa ndoa, akuchumbie na kukuoa, hayo mengine unajidhalilisha tu, wakati umri ulionao ni wa kuipambania kwanza kesho yako kabla ya malavidavi!
17. ANKO Lao, kijana miaka 25 kuna mwanamke nimetokea kumpenda, ila kila nikimuimbisha anaishia kuniambia yeye bado, nashindwa kumuelewa bado kitu gani, nifanyeje?
Jonijo, Fuoni Zanzibar
Jibu: Huna haja ya kupagawa, we kaa naye uzungumze naye ujue anachokimaanisha na kama kweli una mipango naye, si ufanye taratibu za kumbeba jumla buana, kwanini ujipe presha na kujikaba wakati umri unakuruhusu buana!
18. ANKO Lao, msichana miaka 20, nina mchumba anasema anataka kunioa, ila hajatulia kwani kutwa anagandana na wasichana na nikimkataza, anasema nisimfuatilie maisha yake. Nifanyeje?
Edna Justine, Mwanza
Jibu: Kama uchumba tu mnaanza kupigana biti mjue hamwezi kufika salama, ila nawe ujue kuchumbiwa sio kuwa mke buana...huenda jamaa anajibu ovyo kwa vile unakaba sana! Mpe uhuru mwenzio, kwani mapenzi sio kuchunguzana bali ni kuaminiana!
19. ANKO Lao, kijana dereva wa daladala, kuna jirani yangu mmoja amekuwa akinisumbua na kusema ananipenda, lakini simuamini kwani nilishawahi kutendwa. Nifanyeje?
Paul Suka Chile, Kinondoni
Jibu: Unalipiga teke fuko la pesa ujue, kama bibie ni pisi kali na anakuzimia, kwanini umtese?! Fanya uchunguzi umjue vyema na kama jimbo lipo wazi, jiachie mwanawane! Hadi ameamua kujibebisha kwako ujue amekuamini na kutamani uishi naye...usimkatili buana!
20. ANKO Lao, kijana miaka 20 nasoma Chuo cha Uhasibu tatizo langu kila nikimtokea demu nachomolewa mbavuni. Naomba ushauri nifanyeje
Ally Salim, Dar
Jibu: Inategemea na swaga unazowaingia nazo, mademu wengine hawapendi mashauzi au ulokole mwingi. Tumia maujanja yako ya chuo kuwasomesha kwa akili, huku ukilainisha mambo na umatemate sio unawapiga saundi tu. Hapa mjini si unajua hapendwi mtu, linapendwa pochi? We vipi?
Nawe una jambo linakutatiza kwenye malavidavu au maisha ya kawaida: Usisite uliza kupitia namba 0658 - 376417 na Anko Lao atakujibu fresh tu