Prime
Tulijiwekea malengo madogo AFCON 2025
KUNA mtu aliniuliza swali kwamba hivi ni kwa nini tunasherehekea na kufurahia timu yetu ya taifa kuondolewa na Morocco katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika. Nikamshangaa kwamba anadhani tunajivunia kuondolewa na Morocco kwa kuwa ilifika nusu fainali ya Kombe la Dunia nchini Qatar 2022.
Nikamjibu kwamba furaha yetu siyo kuondolewa na Morocco, bali kufanikiwa kufika hatua ya 16 bora baada ya kushindwa kuvuka mara zote tatu za mwanzo tulizofuzu kucheza fainali hizo kubwa barani Afrika.
Kwa hiyo furaha ya Watanzania wengi siyo kuondolewa na Morocco, bali kuvuka hatua ya makundi kwa mara ya kwanza na kuandika historia.
Ni kweli, 1980 timu iliyofuzu kucheza fainali hizo haikuweza hata kuokota pointi moja baada ya kupoteza mechi zote tatu. Hata timu iliyofuzu 2019 haikupata mafanikio hayo, ila iliyofuzu 2022 iliweza kuambulia pointi moja.
Ya mwaka huu iliendeleza rekodi yake ya kutoshinda, lakini ikapata sare mbili zilizoiwezesha kufika hatua ya 16 bora kama mshindi wa tatu bora katika makundi, hali inayoonyesha kuwa fainali za mwaka huu Morocco zina ushindani mkubwa, huku Nigeria pekee ndiyo ikifanikiwa kukusanya pointi zote tisa katika mechi za makundi.
Kumbe jamaa alikuwa anajua yote hayo na akarudi na swali jingine. “Hivi tunapeleka timu fainali za AFCON kwa ajili ya kurekodi takwimu au kwa ajili gani?”€Nikamjibu kuwa tunakwenda kushindana.
“Kumbe uko sahihi. Kila timu inayofuzu kucheza fainali inakuwa na nafasi sawa ya kutwaa ubingwa, ila vitabuni ndio kuna ubashiri mwingi,” akasema.
“Hayo mambo ya kuandika historia ni ya viongozi na si nchi. Kila timu inayokwenda fainali za AFCON au Kombe la Dunia inatakiwa iwe na nia ya kutwaa ubingwa. Kusherehekea mafanikio madogo ni suala la ajabu kwa kudhani mafanikio ni kupata ushindi wa mechi moja au kuvuka hatua ya makundi.”
Jamaa alinifikirisha sana. Ukiweka malengo ya kuvuka hatua ya makundi, unamwekea kiongozi kipimo cha mafanikio kulinganisha na waliomtangulia. Chochote kidogo kitakachotokea ndiyo inakuwa silaha yake kubwa kwamba wenzake hawakuweza kufikia huko. Atasahau misingi waliyomjengea wenzake na kusherehekea kile kidogo kilichopatikana, hata kama hajui kimepatikanaje au alifanya nini kukipata.
Ni sahihi kwa kiongozi wa nchi kupongeza hata mafanikio madogo kwa kuwa si mshiriki wa moja kwa moja wa shughuli za mchezo fulani au taasisi fulani. Kwake kupongeza ni kutia moyo wahusika kuwa wafanye jitihada zaidi kwa kuwa serikali inawaangalia na inawajali.
Lakini kwa kiongozi wa mchezo husika anatakiwa ahakikishe anatafuta mafanikio ambayo viongozi wengine wa soka wa nchi zote wanayatafuta, yaani kutwaa ubingwa na si kujilinganisha na waliopita.
Nchi kama Madagascar ilifanikiwa kufika robo fainali za AFCON iliposhiriki kwa mara ya kwanza ikipata ushindi dhidi ya timu vigogo kama Nigeria 2019, wakati Comoro ilifika hatua ya makundi ilipofuzu kwa mara ya kwanza 2021. Hao washerehekee vipi mafanikio katika ushiriki wao wa kwanza?
Kufurahia huko mafanikio madogo ndiko kunakosababisha tugeuzie kibao waamuzi kwamba ndio waliotukwamisha tusivuke kwenda robo fainali badala ya kuangalia uwezo halisi wa timu kulinganisha na hao waliofika nusu fainali kwa sasa.
Ukweli ni kwamba siku tulipocheza na Morocco tulikuwa tunashangilia jinsi tunavyowadhibiti wasipate bao na si jinsi tunavyowashambulia hadi wanajihami golini kwao. Nafasi tulizopata ndizo hizo tulipoteza wakati wao walitengeneza nafasi tatu wakatumia moja.
Lawama dhidi ya waamuzi zinatokana na tukio lililotokea muda wa majeruhi wakati Iddi Nado alipoonekana amesukumwa ndani ya eneo la penalti, lakini tafsiri ya refa ikawa ni ‘msukumo mwepesi’ ambao hauwezi kuadhibiwa kwa penalti wala filimbi yoyote.
Jamaa akaniuliza, “hivi tungepata ile penalti, tungefanya nini? Timu ingeweza kustahimili mashambulizi ya Morocco katika muda wa nyongeza?”
Nikamjibu kwamba kwa jinsi tulivyostahimili mashambulizi yao kwa muda mwingi, ingekuwa rahisi kumalizia hizo dakika 30 za nyongeza.
Akasema hizo ni hesabu tu na si hali halisi kwa kuwa Wamorocco waliuchukua mchezo kwa muda mwingi na wangeweza hata kufunga mabao mawili zaidi katika muda wa nyongeza.
Ukiangalia unaweza kukubaliana naye kwa kuwa siku ya mechi dhidi ya Nigeria, baada ya Tanzania kusawazisha tu ilikuwa kama Nigeria walistahili kuongoza kwa kuwa walipouweka mpira kati walirudi golini kwetu kushambulia hadi walipopata bao la kuongoza na mambo yakaishia hapo.
Kwa hiyo, kuna haja sana ya kuangalia au kujitathmini uwezo wetu kabla ya kusherehekea au kulaumu waamuzi. Magugu hujitofautisha na mpunga wakati wa mavuno. Hakuna magugu yanayozaa mpunga kwa hiyo ni rahisi kuvuna mpunga kwa kuangalia mazao yake.
Kwa kuangalia timu zilizofika nusu fainali unaona kabisa jinsi mpunga ulivyojitofautisha na magugu. Nigeria, ambayo safari hii inaonekana kurudisha makali yake, Misri, Morocco na Senegal ndizo timu zilizofika nusu fainali.
Misri na Morocco zimewekeza sana katika soka la vijana huku shirikisho la soka la nchi hizo na serikali zikihakikisha miundombinu ya mpira wa miguu inajengwa kila kona, wakati Nigeria na Senegal zinategemea sana mazao ya shule za soka ambazo huuza wachezaji wengi barani Ulaya na hivyo kuwa na vikosi imara vya taifa.
Hakuna kubahatisha wala kufurukuta ili kupata mafanikio, bali ni kuwa na mkakati wa dhati wa kuendeleza michezo ndio tutafikia kiwango cha kulaumu waamuzi. Kwa kuwa tunajiwekea malengo madogo katika fainali hizo, hatuwezi kuepuka kujikita katika kukosoa mambo madogomadogo kama ya uamuzi.
Tungekuwa na malengo makubwa tungejadili zaidi sababu za timu kuzidiwa muda wote katika mechi ya hatua za mtoano wakati tulishajua tangu mwaka jana kuwa Desemba tutashiriki fainali za AFCON nchini Morocco.