AJE ASIJE! Uchambuzi wa kocha mmoja mmoja wanaosakwa Man United
Muktasari:
- Man United hawakuwa na mpango madhubuti endapo Ruben Amorim angefutwa kazi. Kwa haraka, waliamua kumteua mchezaji wa zamani kama kocha wa muda, Michael Carrick na kushinda kile kilichokuwa kama kinyang’anyiro cha watu wawili dhidi ya Ole Gunnar Solskjaer baada ya wiki moja ya mazungumzo.
MANCHESTER, ENGLAND: SAFARI ya Thomas Tuchel kwenda Manchester United sasa imefikia mwisho.
Mkataba mpya wa Tuchel na timu ya taifa ya England unamweka nje ya mbio za kuinoa Man United majira yajayo ya kiangazi.
Hata hivyo, uwezekano huo haukuwa mkubwa tangu mwanzo. Tuchel hakufurahishwa na mchakato huo na wakati Man United walipomkaribia tena mapema Oktoba 2024, England waliwahi kuwazidi kete na Tuchel hakusita kukubali ofa ya FA.
Man United hawakuwa na mpango madhubuti endapo Ruben Amorim angefutwa kazi. Kwa haraka, waliamua kumteua mchezaji wa zamani kama kocha wa muda, Michael Carrick na kushinda kile kilichokuwa kama kinyang’anyiro cha watu wawili dhidi ya Ole Gunnar Solskjaer baada ya wiki moja ya mazungumzo.
Kama ilivyokuwa miaka minne iliyopita, Man United ina muda wa kutosha kuchagua kocha wao wa kudumu ajaye.
Uteuzi wa Erik ten Hag ulithibitishwa Aprili 2022, huku michezo mitano ikiwa imesalia msimu huo.
Man United pia ilikuwa tayari imekubaliana na Louis van Gaal kabla ya kumfuta kazi David Moyes, Jumatatu ya Pasaka mwaka 2014.
Jose Mourinho alikuwa kwenye mazungumzo na Man United kwa miezi kadhaa kabla Van Gaal hajaondolewa siku mbili baada ya kushinda taji la Kombe la FA mwaka 2016.
Kulikuwa hata na mpango wa kufutwa kazi katikati ya msimu. Man United ilikuwa na maku baliano ya awali na Amorim siku hiyohiyo Ten Hag alipoondolewa.
Michael Carrick alisima mia moja ya viwango bora vya Man United tangu fainali ya FA Cup 2024 katika mechi yake ya kwanza, na timu bado haijapoteza chini yake kama kocha wa muda. Carrick hawezi kupuuzwa, ingawa mfano wa Solskjaer unatoa tahadhari.
Hawa hapa ni baadhi ya machaguo ya makocha ambao Man United inaweza kufanya uamuzi wa kuwapa kazi mwisho wa msimu kwa ajili ya mikikimikiki ya msimu ujao …
Carlo Ancelotti
Ancelotti ana mkataba na Brazil unaoisha baada ya Kombe la Dunia 2026. Angevutia mashabiki kwa mafanikio yake ya kushinda mataji matano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na AC Milan na Real Madrid.
Hata hivyo, mara nyingi huvuna alichopanda mwingine. Vyumba vya kubadilishia nguo vya Milan na Madrid vilikuwa vimejaa wachezaji wa kiwango cha juu waliokuwa tayari kushinda au walishashinda. Ndiyo maana Zinedine Zidane, aliyerithi Madrid msimu uliofuata baada ya Ancelotti kuondolewa, hajapata kazi nyingine licha ya kushinda Ligi ya Mabingwa mara tatu mfululizo kati ya 2016-18.
Man United kwa sasa ina mchezaji mmoja tu wa kiwango cha dunia asiye na shaka, Bruno Fernandes, ambaye huenda akaondoka majira ya kiangazi. Wanahitaji kocha anayeweza kujenga na kuimarisha kikosi haraka. Ancelotti si mtu huyo, na akiwa na miaka 66, huenda umri wake pia ni kikwazo. Kazi yake ya mwisho katika Ligi Kuu England ilikuwa miezi 18 isiyo ya kukumbukwa akiwa Everton.
Mauricio Pochettino
Huyu ndiye mtu ambaye Man United ilipaswa kumwajiri badala ya Solskjaer au angalau kumchukua wakati Solskjaer alipokuwa kwenye presha mara kadhaa.
Thamani ya Pochettino imepungua polepole tangu timu yake ya Tottenham ilipopoteza dhidi ya Solskjaer, Januari 2019 wakati Solskjaer akiwa kocha wa muda Man United.
Kiwango kibovu cha Spurs kwenye ligi msimu huo (ushindi mara tatu tu katika mechi 12 za mwisho) kilifunikwa na safari ya bahati hadi fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mjini Madrid, ambako hawakuonyesha kiwango dhidi ya Liverpool.
Pochettino hakumaliza mwaka huo kazini na kutokana na kukata tamaa kwa Man United, alikimbilia Paris Saint-Germain, ambako hata hakushinda ubingwa wa ligi wakati wa utawala wake.
Baada ya PSG kumfuta kazi mwaka 2022, alichukua kazi Chelsea, ambako hakulingana na mazingira na alidumu msimu mmoja tu. Mwaka 2024 alikubali kwa haraka kazi ya kuinoa Marekani, na mara nyingi ameonekana kama anajutia uamuzi huo.
Ikiwa Pochettino atawahi kukaa kwenye benchi la nyumbani Old Trafford, basi itakuwa baada ya muda mrefu. Sir Alex Ferguson ndiye aliyemtaka kuchukua nafasi ya Van Gaal mwaka 2016.
Oliver Glasner
Glasner amekuwa akijitafutia matatizo akiwa Crystal Palace na huenda akajiondoa mwenyewe kwenye nafasi ya kuinoa Manchester United.
Amorim alipata malipo yake ya kuachishwa kazi baada ya kumkosoa hadharani mkurugenzi wa soka Jason Wilcox. Naye Glasner alimkosoa mara kwa mara mwenyekiti wa Palace, Steve Parish, kabla haijathibitishwa kuwa ataondoka mwishoni mwa msimu. Kocha huyo raia wa Austria kwa sasa hayuko katika nafasi imara. Palace wamewapoteza wachezaji wao wawili bora msimu huu, Eberechi Eze na Marc Guehi, huku kiwango chao cha ligi kikishuka vibaya na kupoteza nyumbani dhidi ya Burnley Jumatano usiku.
Chini ya saa 12 baada ya Palace kutolewa kwenye Kombe la FA na Macclesfield ya National League North, Glasner alionekana akicheza muziki wa Taylor Swift katika klabu ya kifahari ya Soho. Inaonekana tayari anaondoka Selhurst Park, lakini safari moja nzuri ya Kombe la FA haitoshi kumpa tiketi ya kuinoa Man United.
Andoni Iraola
Iraola anastahili kazi katika moja ya klabu za Big Six kwenye Ligi Kuu England, hasa Tottenham Hotspur.
Mhispaniola huyo anaonekana kufaa zaidi Spurs, ambao wanahitaji kocha mwenye mtazamo wa kushambulia baada ya Thomas Frank kuondolewa kwenye kibarua hicho.
Iraola amefanya kazi nzuri sana Bournemouth na kumaliza katika nafasi kumi bora itakuwa mafanikio makubwa baada ya kuuzwa kwa Dean Huijsen, Milos Kerkez na Illia Zabarnyi majira ya kiangazi. Antoine Semenyo pia aliuzwa hivi karibuni kwenda kujiunga na Manchester City.
Uzoefu wa Ligi Kuu pia unathaminiwa na viongozi wa Man United, ndiyo maana walikuwa wakimvutiwa Fabian Hurzeler wa Brighton. Bournemouth hivi karibuni ilimaliza mfululizo wa mechi 11 bila ushindi dhidi ya Spurs na kiwango chao kimeimarika mwaka huu wa kalenda. Hata hivyo, Man United inalenga kutwaa ubingwa ifikapo 2028. Kwa kuzingatia lengo hilo, Iraola haonekani kuwa chaguo sahihi.
Xabi Alonso
Kwa nini Man United wasimpigie simu kocha aliyemaliza utawala wa miaka 11 wa Bayern Munich kama mabingwa wa Ujerumani na ambaye pia amewahi kuinoa Real Madrid?
Alonso aliibua taharuki katika chumba cha kubadilishia nguo cha Madrid baada ya Ancelotti kuwa mpole kwa wachezaji. Lakini, kufutwa kazi kwake Madrid, Januari hakupaswi kumtoa kwenye orodha ya chaguo bora miongoni mwa makocha.
Ubingwa wa Bundesliga wa Bayer Leverkusen mwaka 2024 ni miongoni mwa mafanikio makubwa zaidi katika ligi tano bora Ulaya katika muongo huu, aliposhinda bila kupoteza mechi.
Alonso alicheza chini ya makocha mbalimbali wenye mitazamo tofauti kama Ancelotti, Mourinho, Rafael Benitez na Pep Guardiola na England inaonekana kuwa hatua inayofuata kimantiki kwa kocha huyo kutoka Hispania.
Uhusiano wake wa miaka mitano na Liverpool haupaswi kuwa kikwazo kikubwa. Alonso alizaliwa Tolosa, si Toxteh, Benitez alijaribu kumbadilisha na Gareth Barry mwaka 2008 na Alonso aliondoka Merseyside akiwa na umri wa miaka 27.
Xavi
Kiungo wa zamani wa Hispania amekuwa hana kazi tangu alipoondoka Barcelona mwaka jana, lakini bado anatajwa sana na wabashiri kuwa miongoni mwa wanaoweza kuwa kocha ajaye wa Manchester United.
Xavi aliisifu sana Man United kabla ya michezo miwili ya kusisimua ya hatua ya mtoano ya Europa League kati ya Barcelona na klabu hiyo mwezi Februari 2023.
Hata hivyo, Xavi aliwaambia kwa mzaha marafiki zake wa karibu kuwa hali ya hewa ya mvua nyingi jijini Manchester inaweza kuwa kikwazo endapo Man United wangemfuata.
Mshindi huyo wa Kombe la Dunia alicheza mechi yake ya kwanza Ulaya akiwa na Barcelona katika sare ya kusisimua ya 3-3 dhidi ya Man United kwenye Ligi ya Mabingwa katika Uwanja wa Old Trafford, Septemba 1998.
Xavi, 46, aliiongoza Barcelona kutwaa ubingwa wa La Liga msimu wa 2022-23, lakini uzoefu wake mwingine pekee wa ukocha ulikuwa na klabu ya Al Sadd nchini Qatar.
Akiwa nje ya ukocha kwa sasa, Xavi anajiweka bize kwa kuwekeza katika kampuni ya teknolojia ya akili bandia (AI) iitwayo Kognia, inayotumiwa na klabu kadhaa za soka kwa uchambuzi wa takwimu. Gwiji huyo wa Barcelona angeleta mvuto mkubwa wa jina, lakini huenda si uhakika wa mafanikio ya uwanjani.
Julian Nagelsmann
Kocha wa zamani wa RB Leipzig na Bayern Munich kwa sasa ana mkataba na timu ya taifa ya Ujerumani hadi mwaka 2028, lakini kurejea kwake katika soka la klabu kunaonekana kuwa suala la muda tu kwa kocha huyo mwenye miaka 38.
Nag elsmann ana uzoefu wa kuinoa klabu kubwa kama Bayern na aliwahi kufanya kazi chini ya mfumo wa mkurugenzi wa michezo akiwa Leipzig, ambako alikuwa mwenzake na mkurugenzi wa usajili wa Man United, Christopher Vivell.
Ingawa kuanguka kwa Amorim kulimuweka katika mvutano na Wilcox, kauli yake ya hasira huko Elland Road mwezi uliopita ilionyesha pia huenda kulikuwa na mvutano na Vivell. Man United imempa Vivell mamlaka makubwa kufanya maboresho katika mtandao wa skauti. Kufikia majira ya kiangazi, miamba hiyo ya Old Trafford ilikuwa na skauti kumi tu wa muda wote kwa kikosi cha kwanza.
Hatimaye, wanaofanya maamuzi makuu Man United watakuwa Wilcox na afisa mkuu mtendaji Omar Berrada (ambaye aliongoza harakati za kumleta Amorim), lakini jukumu la Vivell kama mkurugenzi wa usajili linapaswa pia kuhusisha uteuzi wa kocha ajaye.
Luis Enrique
Iwapo mashabiki wa Man United wang eweza kuchagua kocha ajaye, basi huenda wangemchagua Mhispaniola Luis Enrique. Kocha huyo wa zamani wa Hispania aliyefanya kazi katika nchi mbalimbali ni mshindi mara mbili wa Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Barcelona na Paris Saint-Germain.
Anapendelea mtindo wa soka unaovutia, anazungumza Kiingereza kwa ufasaha, anaweza kumfariji mchezaji, lakini pia kuwa mkali inapobidi.
Enrique ameifanya PSG, inayofadhiliwa na utajiri wa Qatar kupendwa zaidi. Wachezaji wenye majivuno wameondoka na nafasi zao kuchukuliwa na wachapa kazi na ushindi wao wa 5-0 dhidi ya Inter Milan katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya uliweka rekodi katika historia ya Kombe la Ulaya.
Kumnyakua Enrique kutoka PSG inayomilikiwa na Qatar kunaonekana kuwa ndoto, hasa wakati bado ana mkataba na mabingwa hao wa Ulaya hadi mwaka ujao.Akiwa na miaka 55, muda unaanza kuyoyoma kwa Enrique ikiwa kweli anataka kutimiza ndoto yake ya kufundisha nchini England, jambo ambalo amewahi kulitamka hapo awali.