Ahamada yeye ni Aziz KI, Fei Toto na Foba

Muktasari:
- Katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Ahamada mwenye miaka 33 ambaye kwa sasa yupo kwa mkopo KMC, anaeleza hilo pamoja na mambo mengine kibao kuhusu maisha ya kishua ambayo anaishi nchini pamoja na familia yake licha ya kutoonekana mara kwa mara akitumika katika michezo ya Ligi Kuu Bara.
KAMA ulikuwa unafikiri Azam FC walimsajili Ali Ahamada miaka mitatu iliyopita kwa sababu ya mkwanja mrefu ambao waliuweka mezani, basi ulijidanganya. Mcomoro huyo amezungumza nini kilimfanya akubali kujiunga na timu hiyo licha ya kuwa na ofa ya kuendelea kukipiga Ufaransa.
Katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Ahamada mwenye miaka 33 ambaye kwa sasa yupo kwa mkopo KMC, anaeleza hilo pamoja na mambo mengine kibao kuhusu maisha ya kishua ambayo anaishi nchini pamoja na familia yake licha ya kutoonekana mara kwa mara akitumika katika michezo ya Ligi Kuu Bara.
"Bonjour" ilikuwa salamu kwa Ahamada ambaye aliyekuwa anachezea simu baada ya kumalizika kwa ratiba ya mazoezi kwenye Uwanja wa KMC, akainua macho na kumtambua aliyemsalia kisha akatabasamu na kujibu kwa Kiswahili "poa", ambapo hata hivyo alibaini ni uchokozi wa mwandishi ili kumsogeza karibu kwa ajili ya mazungumzo.

Baada ya hapo, aliulizwa kuwa anaweza kufanya mahojiano kwa Kiswahili? Akasema: "Hapana, naweza kusikia tu na kuzungumza baadhi ya maneno. Naongea Kiingereza, Kifaransa kwa sababu ndizo lugha ambazo nimekuwa nikizitumia mara nyingi katika mawasiliano yangu."
Stori zinaendelea za hapa na pale kabla ya kueleza dili lake lilivyokuwa hadi akaamua kujiunga na Azam FC.
"Sisemi kwa kujivunia, hapana. Lakini nimeucheza mpira kwenye kiwango kikubwa. Nina uzoefu wa kutosha ambao kwa sasa nautumia kusaidia vijana. Nakumbuka wakati ambao nimepata fursa ya kuja kucheza Azam nilikuwa mchezaji wa Santa Coloma ya Andorra," anasema na kuendelea:
"Mbali na kwamba nilikuwa mchezaji wa Santa Coloma pia nilikuwa na ofa ya kurudi Ufaransa ambako nimecheza mpira kwa miaka mingi. Kuna timu ya daraja la pili ambayo ilikuwa ikinihitaji unadhani Azam ingemudu kuning'oa Ulaya na kunifanya niachane na ofa zote ambazo nilikuwa nazo? Hapana ingekuwa ngumu."
Anaongeza kuwa, "nilikaa chini na familia yangu tayari nilikuwa na karibu kila kitu ambacho nilihitaji, hivyo niliamua kuja Afrika kwa ajili ya maisha mpya. Nilihitaji changamoto nyingine tofauti kabisa, hivyo nilikataa nafasi ya kurudi Ufaransa na kuamua kuja Tanzania."
Nani alikuwa nyuma ya usajili wake, ni mtoto wa nne wa bilionea mzawa Said Salim Bakhresa, Yusuf ambaye alihakikisha kipa huyo hatui kinyonge nchini kwa kumpa kila kitu muhimu ambacho mchezaji wa daraja lake anatakiwa kuwa nacho, ikiwemo usafiri wa maana na nyumba ya kishua.

LIGI KUU BARA
Ahamada anavutiwa na kiwango cha soka kilichopo Tanzania akisema: "Ni ligi nzuri sana. Tangu nilipofika hapa kila wakati nasema tuna timu nzuri na wachezaji bora. Kwa kweli niliguswa sana nilipofika na kukutana na kiwango hiki cha ushindani."
Anaongeza kuwa licha ya kuwa Ligi Kuu Bara inakutana na changamoto nyingi, anajivunia kuona kiwango cha soka kinavyokua na kwamba, wachezaji wanajitahidi kupambana.
Anaeleza kuwa wengi wa wachezaji wa Tanzania wanajitahidi kufikia malengo na ndoto za soka, na hiyo ni moja ya sababu iliyomfanya kujiunga na Azam. "Licha ya changamoto zilizopo, Tanzania ina ligi nzuri. Wachezaji wanajitahidi sana. Na kama wataendelea kufanya kazi kwa bidii nadhani ndani ya miaka michache ijayo Tanzania inaweza kuwa moja ya ligi bora zaidi Afrika."

CHANGAMOTO KWAKE
Kipa huyo anaelezea baadhi ya changamoto alizokutana nazo tangu alipotua nchini.
"Moja ya changamoto kubwa ni viwanja vya mazoezi, kwani vingi ni vya mchanganyiko (artificial turf). Hii inakuwa vigumu kwa misuli na viungo hasa wakati wa mazoezi na michezo mingi. Lakini hata hivyo, nimemudu hali hiyo. Kama vile unavyojua ni sehemu ya mchakato wa kukubali mazingira," anasema.
Hata hivyo anaeleza kuwa licha ya changamoto hizo, hali ya soka Tanzania inazidi kuwa bora na anafurahi kuwa sehemu ya mfumo wa Ligi Kuu Bara.
WACHEZAJI WENZAKE
Ahamada anazungumzia jinsi anavyoshirikiana na wachezaji wenzake akisema kuwa ni mchezaji mwenye uzoefu mkubwa na ni mchezaji ambaye anajitahidi kuwasaidia wachezaji wenzake, hasa wachezaji wachanga.
Anaeleza, "mimi ni kaka mkubwa kwa wachezaji wenzangu kwa sababu ni mchezaji mwenye uzoefu mkubwa. Napenda kuwasaidia wachezaji wenzangu kwa kuwapa ushauri na kuwaruhusu wafikie malengo."
Kipa huyo anajivunia kuwa sehemu ya wachezaji ambao wanawapa motisha na msaada wachezaji wachanga tangu akiwa Azam.
WACHEZAJI WA KIGENI
Mchezaji huyo anaeleza kuhusu mchango wa wachezaji wa kigeni kwenye ligi ya Tanzania akisema,"wachezaji wa kigeni wanachangia kuboresha kiwango cha ligi yetu. Tuna ligi nzuri na ngumu na kwa wachezaji wa kigeni. Ni fursa nzuri kuja hapa kwa sababu ligi ni ya ushindani. Wachezaji wengi wanapokuja hapa wanakuwa na hamu ya kufanya vizuri na kuchangia kuiboresha.
NI FEI NA AZIZ KI
Akizungumzia wachezaji anaowakubali Bara, mchezaji huyo anasema: "Tangu niwe hapa naweza kuwataja wachezaji wawili bora ambao nimewashuhudia ubora wao ni mkubwa sana. Nina furaha kwa sababu mmoja nimecheza naye, naamini hawa ndio wachezaji bora zaidi kwa sasa Tanzania - ni Feisal na Aziz KI. Wana vipaji vikubwa vya kucheza soka Ulaya."
AZAM NA CHANGAMOTO
Kipa huyo anazungumza changamoto zinazokutana nazo klabu kubwa kama Azam FC akidai ingawa ina kila kitu kinachohitajika, lakini kujenga klabu imara yenye mafanikio ni mchakato wa muda mrefu.
Anasema: "Kama unavyojua kujenga klabu sio jambo la haraka. Hata timu kubwa kama Manchester City au Paris Saint-Germain walichukua muda kufikia mafanikio. Azam FC inahitaji muda na nadhani miaka michache ijayo itakuwa na ushindani mkubwa."
Anaongeza kuwa, Azam FC ni klabu changa na inahitaji muda ili iweze kuwa na mafanikio kama klabu za Simba na Yanga, akiwahakikishia mashabiki wa Azam kwamba itakuwa na mafanikio makubwa ndani ya miaka michache.
FOBA NI TUNU
Pamoja na uwepo wa Moussa Camara na Djigui Diarra kama makipa bora kwa sasa Ligi Kuu Bara huku kila mmoja akiwazungumzia, Ahamada anamtabiria makubwa Zuberi Foba kwamba ana kila kitu ambacho kinaweza kumfanya afike mbali.
"Nimepata nafasi ya kufanya naye kazi. Namjua kwamba ana kitu kikubwa. Anatakiwa kuendelea kujifunza, ana nafasi ya kukua na kuwa bora zaidi. Namuona kama kipa namba moja wa Tanzania miaka ijayo," anasema.

KUHUSU FAMILIA
Kipa huyo anaeleza kwamba tangu siku ya kwanza alipotua Tanzania alikuja na familia na kwa pamoja wanajivunia kuwa hapa.
"Ndio, familia yangu ilifuatana nami hapa Tanzania. Tangu nilipoanza kazi na tunaendelea vizuri."
Anaongeza kuwa familia inaishi vizuri na wanajivunia maisha katika Jiji la Dar es Salaam akidai kuwa ni mahali pazuri kuishi na mazingira bora kwa watu wanaowapenda wageni.

MTU WA AINA GANI
Ukimuuliza kuwa ni mtu wa aina gani, Ahamada anajibu ni wa kawaida anayependa kuvinjari na kupumzika. Anasema: "Napenda kuzungumza na watu, ni mtu mwenye mtazamo chanya na sipendi makuu. Napenda kuwa na furaha na kama naweza kumsaidia mtu yeyote ni furaha yangu."
Kati ya vitu ambavyo anavifurahia Tanzania ni kula kuku akisema: "Kuku wa Tanzania ni wazuri sana. Nimekuwa nikila na kuwafurahia hakuna kitu ambacho nakimisi cha nyumbani Comoro na hata Ufaransa ambako nimekaa kwa miaka mingi. Chakula ni kizuri sana, nakula pilau, kacholi, chapati na vinginevyo."
UNAMJUA AHMADA?
Mchezaji huyo alizaliwa Martigues, Ufaransa na alianza safari ya soka katika Klabu ya Martigues ambako alidumu kwa miaka tisa kabla ya kuhamia Toulouse 2009.
Kipa huyo alihitaji muda mfupi kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha Toulouse baada ya kuumia kwa kipa wa wakati huo, Olivier Blondel na alijumuishwa kama mbadala mchezo dhidi ya Sochaux Desemba 10, 2009.
Katika msimu wa 2010–11, Ahamada alishiriki kwenye michezo ya maandalizi ya msimu mpya na alionyesha uwezo mkubwa licha ya kuwa hakupata nafasi mara nyingi katika kikosi cha kwanza hadi Novemba. Hatimaye alicheza mchezo wa kwanza Februari 20, 2011 kama mbadala dhidi ya Rennes na alisaini mkataba wa kwanza wa kulipwa na Toulouse miezi minne baadaye.
UMAARUFU WAKE LIGUE 1
Katika msimu wa 2011–12, Ahamada alionyesha kuwa mchezaji muhimu Toulouse huku akiweka rekodi kibao kama kipa chaguo la kwanza.
Alianza msimu vizuri kwa kutoruhusu mabao katika michezo minne mfululizo na aliweka historia katika msimu wa 2012–13 kwa kuwa kipa wa kwanza kufunga bao katika Ligi Kuu Ufaransa likiwa ni la kusawazisha dhidi ya Rennes.
Ingawa alikumbana na changamoto kwa kufanya makosa yaliyomuondoa kwenye kikosi cha kwanza kabla ya wiki chache baadaye kurejea ndani ya msimu huo aliotumika katika michezo 37 ya mashindano yote.

WAPI KWINGINE?
Baada ya kuondoka Toulouse 2015, Ahamada alijiunga na Kayserispor ya Uturuki na katika msimu wa kwanza alikosa michezo kadhaa kwa sababu ya jeraha la mkono.
Hata hivyo alirudi kwa nguvu na baada ya kuondoka Kayserispor 2018 alijiunga na Kongsvinger kisha Brann (zote za Norway) na hatimaye kusaini mkataba katika timu ya Azam FC 2022.