Afrika katika mtego wa fainali Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Kuongezeka kwa idadi ya washiriki kutoka timu 32 hadi 48 kumeipa Afrika nafasi nne zaidi za ushiriki na kufanya bara hilo kuwa na uwakilishi mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika fainali hizo.
MEXICO CITY, MEXICO: PAZIA la Kombe la Dunia 2026 limefunguliwa jana, Alhamisi katika nchi ya Mexico huku Bara la Afrika likiwa katika mtego wa kihistoria wa mashindano hayo, ikiwa na wawakilishi 10 kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa fainali hizo miaka 96 iliyopita.
Kuongezeka kwa idadi ya washiriki kutoka timu 32 hadi 48 kumeipa Afrika nafasi nne zaidi za ushiriki na kufanya bara hilo kuwa na uwakilishi mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika fainali hizo.
Algeria, Cape Verde, Ivory Coast, DR Congo, Misri, Ghana, Morocco, Senegal, Tunisia na Afrika Kusini ambayo ilicheza jana mchezo wa ufunguzi dhidi ya Mexico ndizo zitakazobeba matumaini ya Waafrika zaidi ya 1.4 bilioni katika mbio za kutafuta taji la dunia.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kombe la Dunia, Afrika imefikisha wawakilishi 10, hatua inayotafsiriwa na wadau wengi wa soka kama ushahidi wa ukuaji wa kiwango na ushindani wa soka la bara hilo katika miaka ya karibuni.
Rekodi hiyo imekuja miaka minne baada ya Morocco kuandika historia kwa kuwa timu ya kwanza kutoka Afrika kufika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia nchini Qatar mwaka 2022, mafanikio yaliyobadili mtazamo wa dunia kuhusu uwezo wa timu za Afrika kwenye mashindano makubwa.
Safari ya Morocco iliwafanya wengi kuamini bara hilo lina uwezo wa kwenda mbali zaidi ya robo fainali ambayo kwa miaka mingi ilikuwa kama ukomo wa mafanikio ya timu za Afrika katika Kombe la Dunia.
Sasa, ikiwa na timu 10 kwenye mashindano hayo, Afrika ina nafasi kubwa zaidi ya kuandika historia nyingine na hata kufikiria uwezekano wa kuwa na mwakilishi wake katika fainali kwa mara ya kwanza.
SAFARI NDEFU YA AFRIKA
Historia ya Afrika katika Kombe la Dunia ilianza mwaka 1934 wakati Misri ilipokuwa taifa la kwanza kutoka bara hilo kushiriki fainali za mashindano hayo.
Baada ya hapo, bara hilo lilisubiri kwa muda mrefu kabla ya Morocco kuwa timu ya pili kushiriki mwaka 1970. Miaka minne baadaye, DR Congo, iliyokuwa ikijulikana kama Zaire, nayo ilifika katika fainali hizo.
Tunisia ilifuata mwaka 1978 kabla ya Algeria na Cameroon kuwakilisha Afrika mwaka 1982. Katika miaka hiyo, nafasi za Afrika zilikuwa chache na mara nyingi timu zake zililazimika kupambana vyakutosha ili kupata tiketi za kushiriki mashindano hayo.
Mwaka 1986, Algeria na Morocco ndizo zilizobeba matumaini ya bara hilo huku mwaka 1990 Cameroon na Misri zikiiwakilisha Afrika.
Cameroon iliandika historia mwaka huo kwa kufika robo fainali na kuwa timu ya kwanza kutoka Afrika kufikia hatua hiyo, jambo lililoonyesha kuwa bara hilo linaweza kushindana na mataifa makubwa ya soka duniani.
Mwaka 1994, Cameroon, Morocco na Nigeria zilifuzu, huku mwaka 1998 ukiwa wa kwanza kwa Afrika kuwa na timu tano katika Kombe la Dunia. Timu hizo zilikuwa Cameroon, Morocco, Nigeria, Afrika Kusini na Tunisia. Kuanzia hapo, idadi ya timu tano ikawa kawaida kwa Afrika katika matoleo kadhaa ya mashindano hayo.
Mwaka 2002, Cameroon, Nigeria, Senegal, Afrika Kusini na Tunisia ziliwakilisha bara hilo, huku Senegal ikifanya maajabu kwa kufika robo fainali katika ushiriki wake wa kwanza.
Mwaka 2006, Angola, Ivory Coast, Ghana, Togo na Tunisia zilifuzu huku Ghana ikivutia macho kwa kutinga hatua ya 16 bora.
Afrika iliweka rekodi mpya mwaka 2010 ilipopewa timu sita kutokana na Afrika Kusini kuwa mwenyeji wa mashindano hayo.
Algeria, Cameroon, Ivory Coast, Ghana, Nigeria na Afrika Kusini zilishiriki huku Ghana ikibaki kuwa timu iliyofika mbali zaidi baada ya kutinga robo fainali na kukosa nafasi ya nusu fainali kwa maumivu makubwa dhidi ya Uruguay kupitia mikwaju ya penalti.
Mwaka 2014 Afrika iliwakilishwa na Algeria, Cameroon, Ivory Coast, Ghana na Nigeria. Mwaka 2018, Misri, Morocco, Nigeria, Senegal na Tunisia zilifuzu, kabla ya Cameroon, Ghana, Morocco, Senegal na Tunisia kupeperusha bendera ya bara hilo nchini Qatar mwaka 2022.
MOROCCO ILIBADILI HISTORIA
Kombe la Dunia la Qatar mwaka 2022 lilibadilisha kabisa taswira ya Afrika kwenye soka la dunia.
Morocco ilifanya kile ambacho hakuna timu nyingine ya Afrika iliyowahi kufanya kwa kufika hatua ya nusu fainali.
Njiani kuelekea hatua hiyo, iliifunga Ubelgiji katika hatua ya makundi kabla ya kuwaondoa Hispania na Ureno katika hatua za mtoano.
Mafanikio hayo yaliifanya Morocco kuwa timu ya kwanza kutoka Afrika na pia kutoka kwa mataifa ya Kiarabu kufika hatua ya nne bora ya Kombe la Dunia. Safari hiyo ilionyesha kuwa tofauti kati ya Afrika na mataifa makubwa ya soka duniani imeendelea kupungua.
CAPE VERDE NA DR CONGO
Miongoni mwa hadithi kubwa za Kombe la Dunia 2026 ni uwepo wa Cape Verde katika mashindano hayo makubwa zaidi duniani kwa mara ya kwanza katika historia yake.
Taifa hilo la visiwa linalokadiriwa kuwa na watu 529,600 limeingia kwenye ramani ya soka la dunia baada ya miaka mingi ya kujenga timu yenye ushindani. DR Congo nayo imerejea kwenye Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1974 iliposhiriki kama Zaire.
Kurejea kwao kunatoa simulizi nyingine ya kusisimua kwa Afrika katika mashindano haya. Afrika Kusini nayo imerudi tena baada ya kutoshiriki tangu ilipoandaa mashindano hayo mwaka 2010.
Kwa upande mwingine, Algeria, Misri, Ghana, Ivory Coast, Morocco, Senegal na Tunisia zinaingia zikiwa na uzoefu mkubwa wa mashindano hayo na matarajio makubwa ya kufanya vizuri.
ZAIDI YA NAMBA
Kwa Afrika, Kombe la Dunia 2026 si suala la kuongeza idadi ya washiriki pekee. Changamoto kubwa ni kuona kama timu hizo 10 zitaweza kubadilisha rekodi ya uwakilishi kuwa rekodi ya mafanikio uwanjani.
Mashindano yaliyopanuliwa yameongeza nafasi za kushiriki lakini pia yameongeza matarajio kutoka kwa mashabiki wa soka duniani.
Baada ya miaka mingi ya kuonyesha vipaji vikubwa, kuzalisha nyota wanaocheza katika ligi bora duniani na kusogea karibu na mafanikio makubwa, Afrika sasa ina nafasi kubwa zaidi kuliko wakati mwingine wowote wa kuonyesha kuwa inaweza kushindana kwa usawa na vigogo wa soka la dunia.
Kutoka kwa Misri mwaka 1934 hadi timu 10 mwaka 2026, safari ya Afrika imekuwa ndefu, yenye changamoto na mafanikio mengi ya kihistoria.
Sasa macho yote yanaelekezwa kwa Algeria, Cape Verde, Ivory Coast, DR Congo, Misri, Ghana, Morocco, Senegal, Afrika Kusini na Tunisia kuona kama wataigeuza rekodi ya ushiriki kuwa rekodi ya mafanikio ndani ya viwanja vya Marekani, Mexico na Canada.
USHIRIKI WA AFRIKA KATIKA KOMBE LA DUNIA
1934: Misri
1970: Morocco
1974: DR Congo
1978: Tunisia
1982: Algeria, Cameroon
1986: Algeria, Morocco
1990: Cameroon, Misri
1994: Cameroon, Morocco, Nigeria
1998: Cameroon, Morocco, Nigeria, Afrika Kusini, Tunisia
2002: Cameroon, Nigeria, Senegal, Afrika Kusini, Tunisia
2006: Angola, Ivory Coast, Ghana, Togo, Tunisia
2010: Algeria, Cameroon,Ivory Coast, Ghana, Nigeria,Afrika Kusini
2014: Algeria, Cameroon, Ivory Coast, Ghana, Nigeria
2018: Misri, Morocco, Nigeria, Senegal, Tunisia
2022: Cameroon, Ghana, Morocco, Senegal, Tunisia
2026: Algeria, Cape Verde, Ivory Coast, DR Congo, Misri, Ghana, Morocco, Senegal, Afrika Kusini, Tunisia