AFCON 2025: Ni fainali ya fahari wawili
Muktasari:
- Wenyeji Morocco itakutana na Senegal katika mechi hiyo ya fainali ya 35 tangu michuano hiyo ilipoasisi mwaka 1957 baada ya mechi mbili za nusu fainali zilizojaa msisimko, presha na njia tofauti za kufuzu kupigwa juzi usiku.
RABAT, MOROCCO: MICHUANO ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 imefikia patamu na Jumapili mashabiki wanatarajia kushuhudia fainali ya aina yake baina ya wenyeji Morocco dhidi na mabingwa wa 2021, Senegal zilizopenya hatua hiyo kwa kushinda mechi zao za nusu fainali juzi usiku.
Wenyeji Morocco itakutana na Senegal katika mechi hiyo ya fainali ya 35 tangu michuano hiyo ilipoasisi mwaka 1957 baada ya mechi mbili za nusu fainali zilizojaa msisimko, presha na njia tofauti za kufuzu kupigwa juzi usiku.
Morocco ilihakikisha nafasi ya fainali ya Jumapili itakayochezwa Rabat baada ya kuifunga Nigeria kwa mikwaju ya penalti 4–2 kufuatia suluhu katika mechi iliyopigwa kwa dakika 120, huku wenyeji ikitegemea tena utulivu na uimara wa safu ya ulinzi katika mechi ya presha kubwa ya mtoano.
Mapema juzi Jumatano huko Tangier, Senegal ilirejea fainali ya AFCON baada ya ushindi mwembamba wa 1–0 dhidi ya Misri, hivyo kuzima ndoto za Mafarao kutwaa taji lao la nane barani Afrika, huku Simba wa Teranga wakionyesha kuendelea kukua katika soka la kiwango cha juu barani Afrika.
Ikiwa na sapoti kubwa ya mashabiki wao kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdellah, Morocco walihimili mashambulizi ya Nigeria kwa dakika 120 katika mechi iliyotawaliwa zaidi na nidhamu kuliko uchezaji wa kuvutia.
Hakuna timu iliyopata bao katika muda wa kawaida wala muda wa nyongeza, huku nafasi za wazi zikiwa chache na safu za ulinzi za pande zote zikisimama imara kadri presha ilivyoongezeka.
Hatimaye, nusu fainali hiyo iliamuliwa kwa mikwaju ya penalti na Morocco ilifunga penalti nne kati ya tano, huku Nigeria wakifunga mbili tu.
Ushindi huo ulizua shangwe kubwa uwanjani huku Simba wa Atlas wakifika fainali yao ya kwanza ya AFCON tangu walipotwaa taji hilo nyumbani mwaka 1976.
Kwa upande wa mechi ya mapema, njia ya Senegal kuelekea fainali ilikuwa ya moja kwa moja zaidi lakini haikukosa ushindani, ilipoifunga Misri 1–0 katika mechi kali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Stade de Tangier.
Mabingwa hao wa mwaka 2021 walionyesha subira na umakini dhidi ya timu yenye uzoefu ya Misri, huku bao la Sadio Mané likiwa tofauti katika mechi ambayo kwa mara nyingine tena, tofauti ndogo ndogo zilitenganisha ushindi na maumivu ya kushindwa.
Kwa Misri, kipigo hicho kilimaliza safari yao ya kutafuta taji jingine la bara, huku ushindi wa Senegal ukithibitisha nafasi yao kama moja ya timu thabiti zaidi kwenye mashindano ya Afrika katika miaka ya karibuni.
KAZI IPO WIKIENDI
Fainali ya Jumapili itakuwa ni hitimisho la michuano hiyo ya 35 iliyoanza Desemba 21 mwaka jana ikishirikisha jumla ya timu za nchi 24 ikiwamo Tanzania iliyotolewa hatiua ya 16 Bora na wenyeji Morocco katika mechi iliyojaa maamuzi yenye utata ya mwamuzi Bpoubou Traore kutoka Mali ambaye hata hivyo amejikuta akiondolewa michuanoni kwa ubabaifu wa mechi hiyo.
Refa huyo aliinyima Tanzania penalti ya wazi dakika za lala salama wakati wenyeji wakiongoza kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na kinara wa mabao wa michuano hiyo hadi sasa, Brahimi Diaz baada ya Idd Seleman 'Nado' kuangushwa langoni mwa Morocco na hakutaka hata kuangali V.A.R.
Mechi hiyo ya fainali ya Jumapili, itakuwa ni kibarua kwa wenyeji Morocco wanaojaribu kukamilisha kampeni ya kihistoria wakiwa nyumbani dhidi ya Senegal wanaolenga kurejesha taji walilotwaa mwaka 2021.
Fainali ya AFCON 2025 itachezwa kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdellah, Rabat, ikiwa imetanguiliwa na pambano la kusaka mshindi wa tatu kati ya Misri na Nigeria zitakazocheza kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Mohammed V, jijini Casablanca.
Kwa uwanja uliojaa mashabiki, taifa mwenyeji linaloota kuandika historia na timu yenye nguvu inayotafuta kuthibitisha ubora wake, mazingira yamewekwa kwa fainali inayotarajiwa kufunga kwa kishindo Kombe la Mataifa ya Afrika lililojaa ushindani nchini Morocco.
MKWANJA WA MAANA
Michuano ya mwaka huu mbali na bingwa kubeba kombe la Afrika pamoja na medali za dhahabu, pia kuna zawadi za fedha za maana kutokana na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuboresha kutokana na wadhamini.
Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa mapema na CAF klupitia Rais Dk Patrice Motsepe ni kwamba bingwa wa michuano hiyo ya AFCON 2025 atazoa kiasi cha Dola 7 milioni (zaidi ya Sh17.3 bilioni) ikiwa ni ongezeko la zaidi ya Dola 3 milioni kulinganisha na ile ya mshindi wa mwaka 2021 aliyezoa Dola 4 milioni.
Mshindi wa pili wa michuano hiyo atakoma kiwango alichopewa bingwa wa mwaka 2021 yaani Dola 4 milioni (karibu Sh10 bilioni), huku timu zilizotinga nusu fainali kila moja itakomba Dola 2.5 milioni (zaidi ya Sh6.1 bilioni), huku zilizotoka Robo fainali zitavuna Dola 1.3 milioni (zaidi ya Sh3.2 bilioni).
Tanzania na timu nyingine zilizong'olewa hatua ya 16 Bora zenyewe zitaambulia kifuta machozi cha Dola 800,000 (karibu Sh2 bilioni) na zile zilizoishia nafasi ya tatu makundi zitapewa 700,000 (zaidi ya Sh1.7 bilioni) na ile iliyoburuza mkia makundi itaambulia Dola 500,000 (zaidi ya Sh1.2 bilioni).
Inakadiriwa fedha zote za zawadi katika michuano hii ya 35 ya Morocco ni Dola 32 milioni (zaidi ya Sh79.2 bilioni) kuonyesha ukubwa wa michuano hiyo ya AFCON 2025. Ngoja tuone ni wenyeji Morocco ya kina Achraf Hakimi na Diaz au Sadio Mane watakaobeba taji? Tusubiri.