Bao la Sadio Mane laiingiza Senegal fainali Afcon 2025
Muktasari:
- Mane alifunga bao hilo katika mchezo huo wa nusu fainali uliokuwa wa tahadhari kubwa dakika 12 kabla ya filimbi ya mwisho ya muda wa kawaida, akipiga shuti la mguu wa kulia lililotinga nyavuni upande wa kushoto baada ya mpira kumfikia nje kidogo ya eneo la hatari.
TANGIER, MOROCCO: STAA, Sadio Mane amefunga bao pekee wakati Senegal walipoichapa Misri na kutinga fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2025 (AFCON) na hivyo kumaliza ndoto ya Mohamed Salah ya kushinda taji lake la kwanza la barani Afrika nchini Morocco.
Mane alifunga bao hilo katika mchezo huo wa nusu fainali uliokuwa wa tahadhari kubwa dakika 12 kabla ya filimbi ya mwisho ya muda wa kawaida, akipiga shuti la mguu wa kulia lililotinga nyavuni upande wa kushoto baada ya mpira kumfikia nje kidogo ya eneo la hatari.
Hii ni mara ya tatu kwa mshambuliaji huyo wa Senegal kumzidi ujanja aliyekuwa mchezaji mwenzake wa zamani Liverpool, katika mechi kubwa za kimataifa zenye presha kubwa. Ushindi huo wa awali ulitokea miaka minne iliyopita, ambapo Senegal waliwafunga Mafarao kwa mikwaju ya penalti katika fainali ya AFCON 2021 na pia kwenye mechi ya mchujo ya kufuzu Kombe la Dunia la FIFA 2022.
Salah alikuwa amefunga mabao manne katika safari ya Misri hadi hatua ya nusu fainali, lakini katika mchezo huu alikuwa amepoa kwa kiasi kikubwa, huku Wamisri wakishindwa kumpa majaribu makubwa golikipa wa Senegal, Edouard Mendy, hadi Omar Marmoush alipopiga shuti la mbali lililookolewa katika dakika ya nne ya muda wa majeruhi.
Kikosi cha Pape Thiaw kitakutana na Nigeria au Morocco katika fainali itakayochezwa Jumapili.