Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Abdi Banda anachonga barabara ya kuvuka boda kupitia Dodoma

BANDA Pict


SOKA la Tanzania limewahi kutoa nyota wengi waliobeba heshima ya taifa ndani na nje ya uwanja, Miongoni mwao yupo Abdi Banda, beki wa kati mwenye historia ya kipekee, aliyeanzia soka lake mkoa Tanga hadi Afrika Kusini.


Kiwango alichokionyesha msimu wa 2013/14 akiwa na Coastal Union ya Tanga, kiliwavutia viongozi wa Simba kuhitaji huduma yake ikamsajili akatumika kuanzia 2014 hadi 2017, kisha akatimkia nje na msimu wa 2017-2019 akajiunga na Baroka ya Ligi Kuu Afrika Kusini, ambako nyota yake ikazidi kung’ara.


Katika mahojiano yake na Mwanaspoti, kwa sasa akiichezea Dodoma Jiji aliyojiunga nayo msimu uliyopita dirisha dogo la usajili, anasema kurejea nyumbani na kujipanga upya siyo kitu cha kushangaza, kikubwa anajua kipi akifanye katika kazi yake.

“Ni mara ya pili kurejea kujipanga upya nikitokea nje, msimu wa 2021/22 nilijiunga na Mtibwa Sugar nikitokea TS Galaxy, baada ya kufanya vizuri nikapata ofa ya kujiunga na Chippa United, kisha na Richards Bay zote za Afrika Kusini na sasa nipo ligi ya nyumbani,” anasema Banda.


MAISHA YA DODOMA

Banda anasema hajaona utofauti mkubwa maisha ya Dodoma na Afrika Kusini alikocheza soka la kulipwa, anafafanua timu hiyo haikai kambini wanakutana wakiwa na majukumu ya mechi.

“Afrika Kusini kila mchezaji alikuwa anatokea kwake tunakutana mazoezini ama siku moja kabla ya mechi, katika hilo sijaona utofauti wake, hilo linamsaidia mchezaji kujitambua bila kusimamiwa,” anasema Banda na kuongeza;

“Ingawa tofauti ni aina ya maisha ya Tanzania na Afrika Kusini, kule kila mtu anajali maisha yake hakuna umoja kama tulionao hapa, vyakula na tamaduni zao ni tofauti kabisa.”

Baada ya kipindi kigumu anasema aliamua kurejea nyumbani na kusaini mkataba na Dodoma Jiji FC, klabu yenye malengo mapya na dira pana.

“Maisha ya Dodoma yako vizuri sana, Nimependa mipango ya mwalimu mpya na mipango ya uongozi, Ndio maana nikaamua kuongeza mkataba mwingine wa mwaka.

“Nafurahia kuwa Dodoma kwa sababu ni klabu yenye mazingira mazuri, inayoendeshwa kitaalamu na inanipa uhuru kama mchezaji kuishi maisha ya kawaida bila shinikizo kubwa la kambini.”

BAND 09
BAND 09

DILI LA UARABUNI

Banda anasema mipango yake ilikuwa aende kucheza nje msimu huu, lakini haikuwezekana ndio maana alisajiliwa Dodoma Jiji dakika za jioni mkataba wa mwaka mmoja.

“Nilipataga ajali nilivyomaliza ligi, lakini sikuumia. Nilipoteza vitu muhimu, ikiwemo simu, usajili wa nje ulifungwa, nikaona bora nibaki nyumbani.

“Ingawa sikupata madhara makubwa kiafya, lakini nilipoteza baadhi ya vitu muhimu ikiwemo simu yangu iliyokuwa na mawasiliano ya kimichezo, Hali hii imenirudisha nyuma na kusababisha nikose nafasi ya usajili wa nje kwa wakati.

“Sijavunja moyo, niliona umuhimu wa afya na kuamua kuendelea kujiimarisha huku nikijiweka tayari kwa fursa nyingine mpya msimu ujao baada kutumikia mkataba wangu.”


UTOFAUTI WA BONGO, NJE

Kuhusu tofauti ya maisha ya soka la nje na Tanzania, Banda anasema hakuna utofauti mkubwa zaidi ya mazingira tu na ushindani ambao upo hapa.

“Hakuna tofauti kubwa sana hasa kwa Dodoma, ila nje kuna mazingira mengine ya kipekee. Hapa ushindani ni mkubwa na ligi yetu pia imeimarika sana.”

“Ligi ya Tanzania kwa sasa inatangazwa vizuri, inawapa wachezaji fursa ya kutambulika kimataifa na kuongeza thamani yao kisoka, pia soko linazidi kuongezeka.


JEZI YA STARS

Banda anasema Kilele cha furaha yake ni kuvaa jezi ya Taifa Stars.

“Mechi kubwa kwangu ni pale ninapovaa jezi ya timu ya taifa na hasa wakati wa kuimba wimbo wa taifa, hapo najiona nimebeba heshima ya Watanzania wote.”

“Hii ni heshima ambayo naitazama kama mafanikio makubwa kuliko fedha, kwani naamini nafasi ya kuwakilisha taifa ni zawadi ya kipekee.”


BAND 01

MSIBA MZITO

Katika safari yake, Banda anasema tukio baya zaidi ni kifo cha Abdul Ahmed Bosnia, aliyekuwa meneja wake na kiongozi wa African Sports.

“Yeye ndiye alinifanya nikae hapa nilipo, Baada ya kufariki dunia, mambo mengi hayakwenda sawa katika maisha yangu ya soka, licha ya kupoteza mtu muhimu, niliamua kujiendeleza kwa nguvu zangu, nikiamini kila mchezaji lazima ajibebe mwenyewe.”


SIMBA DAMU

Banda hajawahi kuficha mapenzi yake kwa Simba, anasema bado yeye ni shabiki wa muda wote kwani hata baba yake aliwahi kuichezea hivyo familia yao yote ni mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi.

“Bado mimi ni shabiki wa Simba kwa sababu baba yangu alichezea Simba na nyumbani kwetu wote ni Simba, ila nikiwa kwenye majukumu yangu kama mchezaji ushabiki nauweka kando.”


BAND 02

IKIJA FRESHI

Banda anasema endapo klabu hiyo itamhitaji, yuko tayari kurejea, lakini si kwa sharti la kukaa benchi, bali pale ambapo atakuwa sehemu ya mipango ya timu.

“Licha ya mapenzi yangu Simba, lakini wakinihitaji sitakataa bali nitataka kupata uhakika wa namba, sitaki kwenda kupoteza muda kukaa benchi tu kwa sababu ya kutaka kuchezea timu kubwa.”


USHINDANI BALAA

Kwa sasa Dodoma Jiji ina ushindani mkubwa wa nafasi, jambo ambalo Banda analiona kwa upande chanya kwa maendeleo ya wachezaji binafsi kwani unaongeza juhudi binafsi.

“Ili timu iwe na matokeo mazuri lazima kuwe na ushindani, hilo haliniogopeshi, bali linanipa nguvu ya kupambana, kila siku jambo ambalo linaongeza kiwango changu.”


BAND 03

SAMATTA, ULIMWENGU AWAPA SALUTI

Banda anasema anamkubali sana Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu, kama wachezaji anaowaona wa mfano katika soka la Tanzania.

“Samatta na Ulimwengu kwangu si wachezaji wa kawaida ni watu wanaonifundisha mambo mengi hasa katika safari ya soka, pia nidhamu zao zilivyoweka rekodi nzuri.

“Hata wazazi wanatamani watoto wao wanaopenda soka wawe kama wao, kwa sababu ya kile ambacho wamekionyesha na mafanikio waliyonayo kutokana na soka.”


HAMZA NI SWALA LA MUDA

Anamtaja mchezaji ambaye anamwona kama mrithi wake Simba kwa sasa licha ya kwamba anakwamishwa na majeraha ya mara kwa mara.

“Hamza ni bora sana japo majeraha yanataka kupunguza kasi yake lakini naimani atarudi vizuri, pia namwona kama mrithi wangu wa nafasi ya ulinzi, ingawa nasikitishwa na majeraha yanayomkabili hasa kwenye mechi muhimu.”


BAND 04

HAIKUWA RAHISI KUONDOKA SIMBA

Wakati wa mashindano ya  COSAFA, 2017  Afrika Kusini ndiyo kipindi Banda alifanya maamuzi ya kujiunga na Baroka FC, ilikuwaje?

Banda anasema iliwezekana kukamilika kwa uhamisho wake huo kutokana na malengo aliyojiwekea.

“Nakumbuka Mo alitaka niongeze mkataba lakini ilibidi nimzungushe kwa sababu nilikuwa na mipango yangu mingine, msimu huo ulikuwa mzuri kwangu licha ya kwanza maisha yangu ndani ya Simba mwanzoni yalikuwa na changamoto nyingi.”

“Kipindi ambacho Mo Dewji alitaka niongeze mkataba ilikuwa kabla ya COSAFA, nilikuwa nikimkwepa kwa kumwambia ajenti wangu hayupo hivyo nisingeweza kuongeza mkataba mwenyewe, ni kweli hakuwepo lakini tulikuwa na makubaliano ya kwamba nisiongeze mkataba kwa sababu kulikuwa na dili nyingine kubwa sana Afrika Kusini,”

“Sikuondoka kwa ubaya nadhani viongozi wanatambua maisha ya mpira yalivyo nikiwa Afrika Kusini kwenye mashindano ya COSAFA, nilionana na ajenti wangu tukiwa hotelini sehemu ambayo alinielekeza na nikasaini mkataba wangu wa kwanza wa kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, ilikuwa ni furaha kubwa sana kwangu,” anasema.


BAND 05

SIMBA YA SASA

Banda anasema utofauti wa Simba ya sasa na wakati aliokuwa anauchezea upo kwenye mkwanja, wakati huo walicheza kwa mapenzi ila sasa ni masilahi zaidi.

“Tofauti ni pesa tu, sasa hivi uwekezaji ni mkubwa sana, malengo yao pia ni makubwa, sisi tulicheza kwa mapenzi ya timu kwanza, mambo mengine yakafuata.”


MAISHA YAKE SAUZI

Mwaka wa kwanza (2017) aliyojiunga na Baroka FC haukuwa mrahisi kwake, anaeleza aliutumia kuyazoea mazingira kama hali ya hewa ya baridi kali, vyakula na  staili yao ya maisha ya  kutokusaidiana tofauti  na Tanzania watu wanavyoishi kijamaa.

“Afrika Kusini hawana kusaidiana, kila mtu na maisha yake iwe unaumwa unatakiwa kwenda mwenyewe hospital bila kutegemea kuna mtu atakuja kukuona kama tulivyozoea hapa kwetu, hivyo mwaka wa kwanza ulikuwa mgumu ila sikukata tamaa;

Anaongeza; “Kwa kuwa nilikuwa na malengo yangu na nilijua kitu kilichonipeleka Afrika Kusini nilikubaliana na mazingira halisi ya nchi ile, kisha nikaendelea na majukumu yangu ya kufanya kazi,” anasema.


BAND 06

WASTAAFU WAMPA FUNDISHO

Banda anasema maisha ya wachezaji wa zamani yaliomwaacha bila msaada yanampa fundisho kubwa, kwani wengi wanaishia kuishi maisha magumu.

“Ni muhimu kutumia muda wako vizuri ukiwa mchezaji, siyo kila aliyepitia maisha magumu baada ya mpira alitaka iwe hivyo, kikubwa ni kumwomba Mungu atupatie mwisho mzuri na kuwashika mkono waliotangulia.”


BAND 07

MAFANIKIO MAKUBWA

Banda anasema mafanikio makubwa si mali, bali heshima na upendo anaoupata kwa mashabiki na watu wengi wa nje, kutokana na kile ambacho amekifanya.

“Kwa kweli kila kitu kwenye maisha yangu ni mpira, kikubwa ni upendo wa watu, heshima na kuthaminiwa kila sehemu ni mafanikio makubwa kuliko pesa.”


MALENGO

Anasema hajakata tamaa ya kurejea soka la nje kwani anajiona kabisa bado hajamaliza safari yake ya kucheza mpira wa kulipwa nje ya Tanzania.

“Bado nina ndoto ya kurudi nje. Wengi husema wachezaji wanakwama, lakini naamini kila mtu ana malengo yake. Mimi bado nina ndoto hiyo na naamini ipo siku itatimia.”


BAND 08

REKODI

Banda ameichezea Simba SC na kupata nafasi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
 

Aliwahi kuwa sehemu ya kikosi cha Taifa Stars kilichopambana kwenye michuano ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).


Alisajiliwa na Baroka FC ya Afrika Kusini, ambako aliimarisha jina lake na kujenga uzoefu mkubwa wa soka la kulipwa.


Rekodi nyingine ni kufunga mabao machache muhimu kama beki, jambo linalomfanya kukumbukwa si kwa ulinzi pekee bali pia kwa mchango wa mabao.