Dodoma jiji kuvunja mwiko 2025/26
Muktasari:
- Dodoma Jiji iliyopanda Ligi Kuu Bara na kushiriki kwa mara ya kwanza msimu wa 2020-2021 baada ya kuwa vinara wa Kundi A katika Ligi Daraja la Kwanza (sasa Championship) 2019-2020, haijawahi kumaliza ligi nafasi tano za juu, lakini uongozi umesema sasa, lazima uvunje huo mwiko.
KILICHOTOKEA katika misimu mitano ya Dodoma Jiji kushiriki Ligi Kuu Bara, uongozi wa klabu hiyo umekaa chini na kupiga hesabu kisha kuna na neno moja. "Msimu huu hatutaki mazoea, tunafanya kweli."
Dodoma Jiji iliyopanda Ligi Kuu Bara na kushiriki kwa mara ya kwanza msimu wa 2020-2021 baada ya kuwa vinara wa Kundi A katika Ligi Daraja la Kwanza (sasa Championship) 2019-2020, haijawahi kumaliza ligi nafasi tano za juu, lakini uongozi umesema sasa, lazima uvunje huo mwiko.
Takwimu zinaonyesha msimu wa 2020-2021, Dodoma Jiji ilimaliza ligi nafasi ya nane, kisha 2021-2022 (11), 2022-2023 (9), 2023-2024 ilishika nafasi ya 12 ambayo imeirudia tena msimu uliopita 2024-2025.
Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na Katibu Mkuu wa Dodoma Jiji, Fortunatus Johnson anayeweka wazi maboresho yaliyofanyika ndani ya timu hiyo ili kufikia malengo waliyojiwekea baada ya kushindwa kuyatimiza misimu miwili mfululizo.
Katika maboresho hayo, Dodoma Jiji imeanza na benchi la ufundi, ikimleta Mrundi, Vincent Mashami ambaye atasaidiana na Guy Bakila na Mbwana Hamis. Hamza Abdallah (Kocha wa Makipa), Yusuph Ndikumana (Kocha wa Utimamu). Wengine wanaounda benchi hilo la ufundi ni Jabir Masoud (Mchua Misuli), Baraka Edwin (Daktari), Samwel John (Mtunza Vifaa) na Charles Komba (Meneja wa Timu).
Mbali na maboresho ya benchi la ufundi ambapo msimu uliopita lilikuwa chini ya Kocha Mkuu, Mecky Maxime, Dodoma Jiji imepandisha wachezaji watatu kutoka timu ya vijana chini ya miaka 20 ambao ni Geoffrey Kasanga, Omary Shaban na Layson Mwakyembe.
"Wachezaji ambao hatutakuwa nao ni Allain Ngeleka, Fadhil Masoud, Paul Obata, Junior Osaghae, Reliants Lusajo, Ibrahim Ajibu, Paul Peter, Hassan Mwaterema na Apollo Otieno," anasema Johson na kuongeza:
"Lakini tulikuwa na wachezaji wawili ambao walikuwa hapa kwa mkopo, Joash Onyango mkopo wake umeisha sawa na Mukrim Issa. Katika wachezaji waliokuwepo msimu uliopita ambao wengine tumewaongeza mikataba na wapo ambao bado walikuwa na mikataba tutaendelea kuwa nao.
"Daniel Mgore, Mohamed Hussein, Dickson Muhilu, Anderson Solomon, Augustino Nsata, Disan Galiwango, Salmin Hoza, Yassin Mgaza, Cletus Emotan, Daudi Milandu, Iddi Kipagwile, Mwana Kibuta, Abdi Banda na Waziri Junior.
Lakini tunayo maingizo mapya. Miraji Abdallah Zambo tumemsajili kutoka Coastal. Tunaye Castor Mhagama golikipa kutoka KenGold. Tunaye Nelson Munganga kiungo kutoka Tabora United. Beno Ngasa ni winga kutoka Tanzania Prisons. Tumemsajili Andy Bikoko ni beki kutoka Tabora.
"Tumemsajili William Edger ni winga kutoka Fountain Gate. Tumemchukua Faraji Kayanda ni mshambuliaji kutoka kutoka KenGold. Lakini Anwar Jabir tumemrudisha kutoka Mtibwa Sugar alikuwa akicheza kwa mkopo.
"Mkopo wake umeisha kule na tumeona maendeleo yake ni mazuri anaweza kuja kusaidia. Amecheza Championship amehusika na magoli nane hali iliyotupa sura kuona kwamba anaweza kuongeza kitu. Pia Dickson Ambundo na Ally Salim.
MALENGO NAFASI TANO ZA JUU
Akizungumzia nafasi katika msimamo, anasema: "Malengo yetu tumemueleza mwalimu mapema tu kwamba tunataka nafasi tano za juu, tunaangalia hapo zaidi na si vinginevyo. Kwa namna ambavyo kikosi tumekiboresha, tunaamini tutayafikia malengo hayo."
SABABU ZA KUMLETA KOCHA WA KIGENI
Na katika suala la kuwa na kocha wa kigeni, kiongozi huyo anasema, "viko vitu vingi. Ligi yetu ina changamoto ikiwemo mazingira. Kimsingi sio tu kuangalia kocha kutoka nje, huwa tunangalia wasifu wa mwalimu husika awe nje au ndani lakini mwenye uwezo mkubwa.
"Wakati tunasaka kocha, tuliangalia ndani na nje, tukapata makocha karibu watano, wawili ndani kwa maana wazawa na watatu kutoka nje. Tukapitia vizuri wasifu wa kila mwalimu. Tumeridhika na Mashami Vincent. Wasifu wake ni mzuri. Amekaa timu ya taifa akiwa kocha mkuu wa Rwanda kwa miaka tatu.
"Nyie wote ni mashahidi, timu ya Rwanda ilikuwa na kiwango kizuri lakini msimu uliopita alirudishwa kuitumikia Polisi Rwanda. Tumemuona ni mwalimu mzuri na mpya Tanzania. Ligi ni ngeni, hivyo tumpe nafasi na sisi kama uongozi tutampa ushirikiano ili afikie kile ambacho tunatarajia.
"Tuna imani ataifikisha timu katika malengo yetu ambayo tumeyaweka ya kumaliza nafasi tano za juu. Ni mwalimu mzuri sana, lakini kubwa zaidi katika mchezo wa mpira wa miguu pia uhusiano ni kitu cha mwisho kati ya mwalimu na wachezaji, katika hilo yupo vizuri.
"Unajua mchezo wa mpira wa miguu unachezwa sana kichwani, hivyo tuna imani atatuvusha kulingana na vitu ambavyo tumeviona kutoka kwake."
BAJETI SH2.6 BILILIONI
Kuhusu bajeti ya msimu ujao, Fortunatus anasema: "Unajua bajeti katika kuiweka vizuri, inabidi tuseme makadirio kwani inakuwa ni mapato na matumizi ambayo tunayakadiria. Mapato unaweza usiyapate lakini pia mnaweza kuyapata na msiyatumie.
"Hivyo kwa msimu wa 2025-2026 tumekadiria kiasi cha shilingi bilioni mbili na milioni mia sita ambayo itakwenda kufanya shughuli zote za uendeshaji wa timu."
SABABU YA KUTOFANYA TAMASHA
Baadhi ya timu zimefanya matamasha kabla ya ligi kuanza, lakini kwa Dodoma Jiji hilo halikufanyika.
"Mwaka huu tumeshindwa kufanya tamasha kwa sababu ligi imechelewa kumalizika na ratiba nyingine zikiingiliana ikiwemo michuano ya CHAN. Tamasha linataka muda mrefu wa maandalizi sambamba na bajeti, kitendo cha kuongeza siku 30 za uendeshaji wa timu maana yake mnavuruga bajeti yenu," anasema.
"Sisi bajeti yetu ya msimu uliopita ilikuwa inaisha Mei 30, 2025, lakini mechi yetu ya mwisho ya ligi tumecheza Juni 22, 2025, kwa hiyo kuna ongezeko la takribani mwezi mmoja, maana yake inatuongezea bajeti ya kuendesha timu na kutuharibia bajeti ya kuandaa tamasha la msimu huu."
CHANGAMOTO UWANJA WA JAMHURI
"Tunajitahidi sana, uwanja unaendelea vizuri. Ukiangalia changamoto kubwa iliyopo kwenye uwanja ni ya kitaifa kutokana na mazingira yaliyopo mkoa mzima wa Dodoma.
"Uwanja umekuwa ukitumika kwa matumizi mengi ambayo siyo sahihi tofauti na mchezo wa mpira wa miguu na matumizi hayo yanagusa sehemu ya kuchezea. Lakini tunaendelea kupambana kuwa na sehemu nzuri ya kuchezea.
UKARIBU NA MASHABIKI
"Kuna mikakati mingi lakini njia nzuri ya kuwa karibu na mashabiki ni kupata matokeo mazuri ndio maana tumejaribu kuboresha kikosi ili kwanza wachezaji walete matokeo mazuri.
"Hiyo ni njia mojawapo ya kuwa karibu na mashabiki na huwa tunafanya nao mikutano mara kwa mara, kutembelea katika matawi, kutengeneza hamasa mbalimbali kwenye michezo yetu. Hiyo programu tunaendelea nayo.
NENO KWA MASHABIKI
"Kwanza tunawashukuru sana mashabiki wa Dodoma waliopo ndani na nje kwani wamekuwa wakitusapoti kwa ari na mali wakati wote iwe kipindi cha furaha au majonzi.
"Kwa msimu huu, tunawaahidi mambo mazuri zaidi kwani tumeiangalia timu na kufanya tathmini ya kina tumeona udhaifu wa kila sehemu ndani ya kikosi ikiwemo kutengeneza nafasi na kufunga mabao, hivyo tumeboresha eneo la ushambuliaji na kiungo ili kutibu tatizo hilo.
"Lakini pia eneo lingine lililokuwa na changamoto ni ulinzi kwa maana ya beki ndiyo maana tumemleta Andy Bikoko kati ya wachezaji wa kigeni. Kwenye kipa ameondoka Alain Ngeleka, tukamleta Castor Mhagama ambaye atasaidiana na Mohamed Hussein na Daniel Mgore, pia kuna kijana wa timu yetu ya vijana tumempandisha.
"Maboresho yote hayo ni katika kuhakikisha mashabiki wetu wanakuwa na furaha na niwaombe tukicheza Uwanja wa Jamhuri Dodoma ama sehemu yoyote mkoani wajitokeze kwa wingi kwani sapoti yao inatupa nguvu ya kuendelea kupambana.
MSIKIE KOCHA VINCENT MASHAMI
Katika malengo ambayo viongozi wa Dodoma Jiji wamempa Kocha Mashami, ni kuiwezesha timu hiyo kumaliza nafasi tano za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara 2025-2026. Jambo hilo, amelikubali na kusema yupo tayari kulifanikisha.
Mashami ameliambia Mwanaspoti kuwa: "Nina malengo hapa Dodoma Jiji yakiwemo ya timu na yangu binafsi. Kwa upande wa timu ni kufanya vizuri kwa kuipandisha nafasi kutoka ilipokuwa, lakini pia kucheza vizuri ikiwemo kupandisha viwango vya wachezaji."
Kocha huyo pia amepigia hesabu mechi tano za kwanza za Ligi Kuu Bara ambapo anasema anataka kuhakikisha hapotezi pointi kwani anafahamu mechi hizo zinatoa dira ya uelekeo wa kufikia malengo.
"Kwa kawaida mechi tano za kwanza huwa ni ngumu kwa sababu wachezaji wanakuwa wanaanza upya wakiwa na nguvu mpya huku kila timu ikiwa imejiimarisha kwa kusajili wachezaji na zingine mabenchi ya ufundi, hivyo zinakuwa na njaa ya kusaka matokeo mazuri. Malengo ni kuona tunakusanya pointi nyingi mapema kwani ukianza vizuri inakufanya kuwa na matumaini ya kufikia malengo yako.
"Katika mechi hizo tano, nafahamu tunaanzia ugenini mechi mbili mfululizo, kisha tunarudi nyumbani, halafu tunaenda tena ugenini. Ya tano nyumbani. Ukiangalia timu tunazokwenda kucheza nazo, tatu nimeziona katika mashindano ya Pre-Season, hivyo naandaa mbinu za kuhakikisha tunafanya vizuri dhidi yao," anasema kocha huyo.
TANO ZA KWANZA DODOMA JIJI
KMC vs Dodoma Jiji (Septemba 17, 2025)
Tabora United vs Dodoma Jiji (Septemba 20, 2025)
Dodoma Jiji vs Coastal Union (Septemba 27, 2025)
Fountain Gate vs Dodoma Jiji (Oktoba 17, 2025)
Dodoma Jiji vs Mtibwa Sugar (Oktoba 22, 2025)
TAKWIMU ZA MISIMU MITANO
MSIMU: 2020-2021
NAFASI: 8
POINTI: 44
MECHI: 34
MSIMU: 2021-2022
NAFASI: 11
POINTI: 35
MECHI: 30
MSIMU: 2022-2023
NAFASI: 9
POINTI: 37
MECHI: 30
MSIMU: 2023-2024
NAFASI: 12
POINTI: 33
MECHI: 30
MSIMU: 2024-2025
NAFASI: 12
POINTI: 34
MECHI: 30