Ligi Kuu 2025/26: Kumeanza kuchangamka
Muktasari:
- Lakini wakati ligi ikiwa imesimama, tayari zimechezwa raundi tatu zilizojumuisha mechi 21, kukiwa na viporo vya mechi za vigogo tu, Yanga dhidi ya Mtibwa Sugar, Azam itakayovaana na Singida BS na Simba dhidi ya TRA United, ili kukamilisha mechi 24 zinazotakiwa kwa raundi hizo.
LIGI Kuu Bara imesimama ikiwa zimeshachezwa jumla ya mechi 21 tangu ilipoanza rasmi Septemba 17, ili kupisha Kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA). Ligi hiyo inatarajiwa kurejea tena Oktoba 17 mara baada ya mechi za kimataifa kwa timu za taifa, huku Simba, Yanga, Singida BS na Azam zenyewe kwanza zikianzia kwenye majukumu ya mechi za raundi ya pili za Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.
Lakini wakati ligi ikiwa imesimama, tayari zimechezwa raundi tatu zilizojumuisha mechi 21, kukiwa na viporo vya mechi za vigogo tu, Yanga dhidi ya Mtibwa Sugar, Azam itakayovaana na Singida BS na Simba dhidi ya TRA United, ili kukamilisha mechi 24 zinazotakiwa kwa raundi hizo.
Mwanaspoti linakuchambulia takwimu za raundi hizo tatu zilizochezwa hadi sasa kuonyesha namna gani Ligi ya msimu huu imeanza kuchangamka mapema, kutokana na rekodi zilizowekwa na timu sambamba na wachezaji binafsi. Tiririka nayo...!
BAO LA KWANZA
Mshambuliaji wa KMC, Daruweshi Saliboko ndiye mchezaji aliyefunga bao la kwanza la msimu huu wa 2025-26. Alifanya hivyo, Septemba 17 wakati KMC ikipata ushindi wa bao 1-0 nyumbani dhidi ya Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam.
Saliboko alifunga bao hilo katika dakika ya 56, akishindwa kulipiku bao la kwanza la msimu uliopita lililofungwa katika dakika ya 33 baada ya kipa Daniel Mgore kujifunga katika mechi ya pili kati ya Dodoma Jiji na wenyeji Mashujaa iliyoshinda, kwani mechi ya kwanza ya msimu iliisha kwa suluhu na ilikuwa ni kati ya wageni wa Ligi hiyo Pamba Jiji na maafande wa Tanzania Prisons.
MABEKI WAMO
Licha ya kwamba mabeki kazi yao kubwa ni kuzuia, lakini wamekuwa na mchango katika kucheka na nyavu ambapo waliofanikiwa kufunga ni wanne na wote wa kigeni. Hakuna beki mzawa aliyefunga hadi sasa. Katika mabeki hao wanne, wamefunga jumla ya mabao matano. Waliofunga ni Rushine De Reuck wa Simba aliyefunga mawili, Fode Konate (TRA United), Anthony Tra Bi Tra (Singida BS) na Chamou Karaboue (Simba).
Washambuliaji waliopachika mabao ni Paul Peter (JKT Tanzania) amefunga mawili. Wengine waliofunga mojamoja ni Daruweshi Saliboko (KMC), Habib Kyombo (Mbeya City), Mundhir Vuai (Mashujaa), Abdulaziz Shahame ‘Haaland’ (Namungo), Athumani Masumbuko ‘Makambo’ (Coastal Union), Nassor Saadun (Azam), Oscar Mwajanga (Tanzania Prisons), Yassin Mgaza (Dodoma Jiji), Andrew Simchimba (Mtibwa Sugar), Seleman Mwalimu ‘Gomez’ (Simba), Fabrice Ngoy (Namungo), Jonathan Sowah (Simba), Elvis Rupia (Singida BS), Mohamed Bakari (JKT Tanzania).
Viungo waliofunga ni Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam ana mawili. Wenye mojamoja ni Jean Charles Ahoua (Simba), Mudathir Yahya (Yanga), Cleophace Mkandala (Coastal Union), Idrisa Stambuli (Mashujaa), Shaphan Siwa (Pamba Jiji) na Lassine Kouma (Yanga).
Mawinga wana bao mojamoja ambao ni Benno Ngassa (Dodoma Jiji), Iddi Kipagwile (Dodoma Jiji), Salehe Masoud Karabaka (JKT Tanzania), Joseph Akandwanaho (TRA United) na Maxi Mpia Nzengeli (Yanga).
MPISHI WA MABAO
Kuna orodha ya wachezaji wengi waliotengeneza mabao, kwa maana ya kutoa asisti, lakini beki wa Dodoma Jiji, Abdi Banda ndiye kinara hadi sasa akiwa nazo tatu.
KIKOTI, HAROUB WANA MAJANGA
Kiungo wa Namungo, Lucas Kikoti na beki wa kati Haroub Abdallah anayecheza Coastal Union, wameanza na majanga kila mmoja akiwa na lake.
Kikoti ndiye mchezaji wa kwanza kuonyeshwa kadi nyekundu, tukio hilo lililotokea Septemba 21, 2025 katika mechi ambayo Namungo iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi. Hadi sasa ni kadi moja pekee nyekundu imeonyeshwa. Msimu uliopita kulikuwa na kadi nyekundu 17.
Kwa upande wa Haroub, amekuwa mchezaji wa kwanza kujifunga wakati Coastal Union ikilala kwa mabao 2-1 dhidi ya Dodoma Jiji, Septemba 27, 2025 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma. Mbali na Haroub, pia beki wa Fountain Gate, Lamela Maneno amejifunga wakati timu hiyo ikifungwa 2-0 na Mtibwa Sugar, Septemba 28, 2025. Tulishuhudia mabao 16 yakipatikana kwa kujifunga msimu uliopita.
FOUNTAIN GATE KIMEO
Katika raundi tatu zilizochezwa, Fountain Gate imetia aibu, si kwa kuwa na idadi ndogo ya wachezaji kutokana na changamoto ya usajili iliyokumbana nayo, bali ni matokeo ya uwanjani.
Timu hiyo iliyoponea kushuka daraja msimu uliopita baada ya kushinda mechi za raundi ya pili ya mtoano dhidi ya Stand United, hadi sasa ndiyo timu pekee ambayo haijaambulia pointi hata moja.
Mbali na kushindwa kukusanya pointi, pia timu hiyo katika mechi tatu ilizocheza haijafunga bao huku yenyewe ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara sita, ikiwa ndiyo iliyoruhusu mabao mengi zaidi. Ina wastani wa kuruhusu mabao mawili kila mechi.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa Fountain Gate, vinara wa msimamo wa ligi, Simba SC wamekuwa na ushindi wa asilimia mia kufuatia kushinda mechi mbili walizocheza sawa na Singida Black Stars. Tofauti yao ni mabao ya kufunga, zote zikiwa hazijaruhusu nyavu kutikiswa. Simba imefunga mabao sita ikiwa na wastani wa kufunga mabao matatu kila mechi, Singida Black Stars inayo mawili, wastani ni bao moja kwa mechi.
Ni timu tatu pekee hazijaonja ladha ya ushindi hadi sasa, ukiiweka kando Fountain Gate ambayo haina pia pointi yoyote, nyingine ni TRA United na Pamba Jiji lakini kila moja ina pointi mbili kufuatia sare ilizopata.
Hii ikiwa ni raundi ya tatu imemalizika huku timu sita pekee zikiwa zimeshuka dimbani mara mbili, jumla ya mechi 21 zimechezwa na kufungwa mabao 36, ikiwa ni wastani wa bao 1.7 kwa mechi.
Wastani huo wa ufungaji ni mdogo kulinganisha na msimu uliopita wa 2024-2025 ambao katika raundi tatu za kwanza, licha ya kuchezwa mechi nyingi 24, pia yalifungwa mabao mengi 42 kwa wastani wa bao 1.8 kwa mechi.
WAZAWA 21, WAGENI 13
Katika mabao 36 yaliyofungwa kwenye mechi 22, wazawa wamefunga mengi ambayo ni 21, huku wageni wakipachika 13. Mawili yametokana na kujifunga wakifanya hivyo wazawa.
Lakini ile listi ya ufungaji, vinara ni watatu ambao kila mmoja ana mabao mawili. Kuna wazawa Paul Peter wa JKT Tanzania na Feisal Salum ‘Fei Toto’ anayecheza Azam. Wa kimataifa mmoja ambaye ni beki wa kati wa Simba, Rushine De Reuck.
VITA YA MAKIPA
Kuna makipa watatu wenye clean sheet mbili kila mmoja, huku katika orodha hiyo yumo Djigui Diarra wa Yanga, ambaye katika maisha yake ya kucheza Ligi Kuu Bara, tayari ana tuzo mbili za kipa bora alizobeba msimu wa 2021-2022 na 2022-2023. Wengine ni Amas Obasogie (Singida BS) na Beno Kakolanya (Mbeya City).
Kinara wa msimu uliopita kipa wa Simba Moussa Camara ndiye aliyekuwa kinara wa clean sheet akiwa na 19 akifuatiwa na Diarra aliyekuwa na 17, huku Patrick Munthari akifuatiwa na 14.
PENALTI ZOTE IMO
Jambo zuri ni kwamba, penalti mbili zilizopatikana, wafungaji hawajafanya makosa, wametikisa nyavu ambao ni Habib Kyombo dhidi ya Fountain Gate (Septemba 18, 2025) na Iddi Kipagwile dhidi ya TRA United (Septemba 20, 2025).
Msimu uliopita hadi unakamilika zilipigwa jumla ya penalti 94 ikiwa ni rekodi ambayo haijawahi kutokea kwa miaka ya hivi karibuni, huku 17 zikikoswa, vinara wakiwa ni Elvis Rupia wa Singida BS na Stephane Aziz Ki aliyekuwa Yanga ambao kila mmoja alikosa mbili. Wakali wa penalti kwa msimu uliopita walikuwa ni Leonel Ateba na Jean Charles Ahoua wote wakiwa ni wachezaji wa Simba.
HILI BADO
Msimu uliopita, hat-trick ya kwanza ilipatikana Desemba 19, 2024 kupitia Prince Dube wa Yanga, kisha Stephane Aziz KI aliyekuwa Yanga akapiga ya pili Februari 14, 2025. Akahitimisha Steven Mukwala wa Simba, Machi 1, 2025.
Msimu huu, bado hatujashuhudia hat-trick, lakini pia si hilo tu, hata mchezaji mmoja kufunga mabao mawili kwenye mechi moja haijatokea.
Haijulikani kama ni ubora wa mabeki na makipa au?