Kitwana Manara Simba, Yanga ya Nyamagana haijawahi kutokea

Kitwana Manara Simba, Yanga ya Nyamagana haijawahi kutokea

Muktasari:

Dereva wa treni iliyotubeba wachezaji, kwa furaha alipiga honi mfululizo kutoka Mikese hadi Dar es Salaam, alipofika Stesheni na yeye kibarua chake kikaota nyasi pale pale,” ndivyo anaanza kusimulia Kitwana Manara mshambuliaji nyota wa zamani wa Yanga akiizungumzia fainali dhidi ya Simba ya mwaka 1971.

Dereva wa treni iliyotubeba wachezaji, kwa furaha alipiga honi mfululizo kutoka Mikese hadi Dar es Salaam, alipofika Stesheni na yeye kibarua chake kikaota nyasi pale pale,” ndivyo anaanza kusimulia Kitwana Manara mshambuliaji nyota wa zamani wa Yanga akiizungumzia fainali dhidi ya Simba ya mwaka 1971.

Anasema haijawahi kutokea mechi ya Simba na Yanga kama ile katika historia yake ya soka tangu alipoanza kucheza mwaka 1958.

“Mpaka sasa hakuna mechi ya Simba na Yanga iliyowahi kuwa gumzo kama ile, haijatokea,” anasimulia.

Timu hizo za watani wa jadi zilitinga fainali ya mashindano ya .... ambayo iliamuliwa ikachezwe kwenye uwanja wa Nyamagana, Mwanza.

“Tuliifunga Simba mabao 2-1, magoli yetu yalifungwa na Sembuli na Sunday, lile la Simba lilifungwa na Mchachu, naikumbuka ile mechi ilikuwa na mambo mengi sana, kocha wetu Tambwe Reya alitupa mazoezi si ya kawaida.

Anasema baada ya mechi ile Simba ilikuwa na ratiba ya kwenda kambini nchini Poland na Yanga Romania.

“Ilikuwa mechi ngumu kwa kila upande, tuliposhinda wakati tunarudi kila mkoa ilikuwa ni sherehe, dereva wa treni iliyobeba wachezaji naye alikuwa shabiki mnazi wa Yanga.

“Ile furaha ya ushindi, alijikuta akipiga honi kutoka Mikese hadi tunaingia Dar es Salaam, wachezaji tukishangilia na mashabiki wetu kwenye kila eneo tulilopita, furaha ile ikampotezea ajira,” anasimulia.


Kisa Simba, Yanga waita waganga 10

Kitwana Manara ambaye ameitumikia Yanga na Taifa Stars kwa mafanikio anasimulia namna mechi ya watani iliyokuwa na matukio mengi ikiwamo ya ushirikina.

“Haya mambo yapo tukiwa wachezaji yamefanyika sana, ila ni imani tu, hakuna lolote,” anasimulia Kitwana akikumbushia moja ya mechi akiwa mchezaji ambapo Yanga iliwaita waganga 10 katika maandalizi ya mechi yao na Simba.

Anasema wakati huo Simba walikuwa wamerejea kutoka Poland, hivyo wakawa wanatamaba wao mambo ya ushirikina wameiachia Yanga, wao ni mpira na ufundi uwanjani.

“Tuliwafunga, lakini sio kwa msaada wa waganga, la hasha ni uwezo wa wachezaji, sema zamani wazee wetu walikuwa na imani hizo sana.

“Nakumbuka mmoja wa wale waganga aliomba kichwa cha fisi, tukashtuka kichwa cha fisi tena, lakini kuna watu wana mapenzi na hizi timu asikwambie mtu.

“Kilienda kikaletwa kichwa cha fisi kweli, halafu mganga yule akaambiwa ole wako tusishinde, akatoa sharti kwamba kichwa kile kikafukiwe uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) mchana wa jua kali.

Anasema mtihani mwingine ukawa ni nani atafanikiwa kwenda uwanja wa Taifa kufukia kichwa kile cha fisi mchana wa jua kali.

“Makomandoo wa timu achana nao, kama nilivyosema kuna watu walikuwa na mapenzi na Simba na Yanga, hilo nalo halikuwa tatizo, ulisukwa mpango makomandoo wakaenda.

“Kufika mmoja akaingia na kumdhibiti mlinzi, akamwambia kaa hivyo hivyo kama unataka kuwa salama, wakamtoa eneo la uwanja akapiga mluzi kuwaita wengine waliokuwa nje wakafanya kazi yao na kuondoka, lakini zilikuwa imani tu, mpira ni mazoezi,” anasimulia.


Kama si Mao Tse-tung, wachina waliamini nyota Stars ni nyani

Mwaka 1966, Kitwana akiwa miongoni mwa makipa wa timu ya soka ya Tanzania (sasa Taifa Stars) walialikwa na rais wa China, Mao Zedong au Mao Tse-tung kama alivyojulikana.

“Tulikaa China kwa siku 14, siku ya kwanza tulipowasili nchini humo, tulikuwa na mechi ya kirafiki na timu ya kule, Wachina walitushangaa wakawa wanatuita monkey ‘nyani’.

Anasema kama sio Mao Tse-tung kuondoa sintofahamu ile, mashabiki wa nchi hiyo waliokuwa uwanjani sanjari na wachezaji waliamini wanacheza na nyani.

“Wakati tunasalimiana wachezaji, Wachina wakawa wanatusugua ngozi wakifikiri inabanduka, hawakuamini kabisa kama kuna watu wana ngozi nyeusi, Mao Tse-tung alitangaza kupitia spika za uwanjani kwamba hao mnaowaona uwanjani sio nyani kama mnavyofikiri, ni wachezaji kutoka Tanzania, taifa lenye msaada mkubwa katika uhuru wetu,” anasimulia.

Anasema tangazo la kiongozi huyo aliyependa kujiita Mwenyekiti Mao, kidogo likatuliza sintofahamu ya mashabiki na wachezaji pale uwanjani japo Stars ilichapwa mabao 6-0 siku hiyo.

“Hata baada ya mechi, tulipokuwa tukienda kufanya ‘shopping’ mtaani bado baadhi yao walitushangilia wakijua ni nyani wanatembea mtaani, wakati ule hawakuamini kabisa kama kuna binadamu mweusi, walituona watu wa ajabu. hatukujali, na sisi tuliwachukulia kama walivyoamini na kuwafurahisha,” anasimulia Kitwana huku akicheka kwa kukumbuka tukio hilo.

Anasema walikaa China kwa siku 14 wakicheza mechi kwenye majimbo tofauti ya nchi ile na kila jimbo hali ilikuwa ni hivyo hivyo, wapo Wachina waliokwenda kwenye mechi kama kufanya utalii wa kushuhudia nyani.


Atoa siri ya Stars kucheza vifua wazi

Katika moja ya matukio yanayobaki kwenye kumbukumbu ya Taifa Stas ni mechi ya kirafiki kati ya Tanzania na Sudan ya mwaka 1972 ya maadhimisho ya Sabasaba, kwenye uwanja wa Uhuru (zamani Taifa).

“Tulikuwa na jezi pea moja, hivyo timu yetu ya pili ilikwenda nazo Zanzibar ambako walikuwa na mechi na timu ya Madagascar,” anasimulia Kitwana.

Anasema walitarajia baada ya mechi ile, jezi zinfgewahi kurejeshwa Dar es Salaam na wao wakazitumia.

“Mwalimu Nyerere alikuwa amemteua Sarakikya (Mirisho amewahi kuwa waziri wa michezo na mkuu wa majeshi) kuwa meneja wa timu, Sarakikya akamteua Khalifa Abdallah kuwa msaidizi wake.

Anasema siku ya mechi wakiwa kambini jeshi la wokovu, wakasikia king’ora cha Mwalimu Nyerere akielekea uwanjani.

“Khalifa Abdallah alituita akasema mnamsikia mwalimu anapita, jezi hazijafika tunafanyaje? tukasema twende uwanjani tutakutana nazo huko huko.

“Tuliondoka kambini tunakimbia hadi uwanjani, kufika Sarakikya akashuka jukwaani akatufuata vyumbani, akatuita wanaumee... tukaita ndioo, akasema ingieni hivyo hivyo mkacheze,” anasimulia Kitwana.

Anasema waliingia uwanjani wakiwa vifua wazi, jambo ambalo lilipokelewa kwa mitizamo tofauti na mashabiki huku wengine wakizomea.

“Mwalimu alibaki amejishika tu, ilikuwa aibu, wapinzani wetu wakati huo wamependeza wako smati, tukasema ili kuwanyamazisha hawa lazima tuwafunge, tukafanya hivyo,” anasimulia.


Waletewa jezi hazijakauka

Kwa vijana wa sasa wangesema kauka nikuvae, ndivyo ilikuwa kwa Stars katika mechi hiyo ambayo Kitwana anasema walipokwenda mapumziko ndipo waliletewa jezi.

“Zilikuwa bado mbichi, zimetoka kufuliwa lakini hazijakauka, tukapewa na kuvaa hivyo hivyo, tulipiga mpira mwingi, Sudan na kupendeza wakatoka uwanjani vichwa chini,” anasimulia.


Stars ilikuwa ni mwendo wa adhabu wakifungwa

Moja ya matukio ambayo Kitwana anasema hatoyasahau ni adhabu ya kukimbizwa mchaka mchaka kwa timu ya Taifa ikifungwa.

“Sarakikya alikuwa akitoa adhabu za kijeshi, nakumbuka kuna mechi tulicheza ilikuwa ni maandalizi ya kwenda Ethiopia kwenye mashindano ya Afrika.

“Tulienda kwenye kambi China, tukacheza mechi za kirafiki kule, tulikubaliana tusifungwe, ikatokea moja ya timu ikatufunga, tuliporudi tulipewa adhabu ya kukimbia mchaka mchaka kutoka .... hadi ....

“Sarakikya alikuwa mjeshi kweli kweli, ingawa wakati ule Mwalimu Nyerere pia aliziwekea timu za Taifa mazingira mazuri, kwenda nje ya nchi kuweka kambi ilikuwa kitu cha kawaida sana, si soka tu, hata riadha na ngumi,” anasema.


Ukweli kuhusu Mwalimu Nyerere na Yanga

Kitwana ambaye amecheza soka kabla ya Uhuru na hata baada ya Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, amefunguka mapenzi ya baba wa Taifa na klabu ya Yanga.

“Unajua Young African (Yanga) ilikuwa ikitafsiriwa kama ni timu ya asili ya Kiafrika tofauti na Simba ambayo awali ilikuwa ikijulikana kama Sunderland.

“Mwalimu Nyerere na Karume walikuwa na mapenzi na Yanga, Karume alijionyesha dhahiri, lakini Nyerere alikuwa akisema watu wote ni wake, kuna wakati hata Yanga ikiwa na kesi ya migogoro anatuambia tumuone mama Maria (mkewe) ambaye pia alikuwa mpenzi wa klabu ya Yanga.


Atoboa siri ya jengo la Simba, Yanga

Katika mambo ambayo mashabiki wengi wa soka hawaelewi ni chimbuko la jengo la Msimbazi yalipo makao makuu ya Simba na lile la Yanga maeneo ya Twiga na Jangwani.

“Eneo yalipo makao makuu ya Simba kulikuwa na ofisi ya kuweka vitu bondi ambayo iliendeshwa na mzungu, yule mzungu alitaka kurudi kwao, hivyo kwa kuwa alikuwa na mapenzi na klabu ya Simba, akaamua kuwaachia eneo hilo (Msimbazi Kariako).

Anasema Yanga wakati huo hawakuwa na eneo, yalipo makao makuu ya klabu kulikuwa na watu waliokuwa wakifanya kazi ya udobi.

“Kutokana na klabu ya Yanga kuwa mstari wa mbele wakati wa mchakato wa kutafuta Uhuru, Karume (Abeid rais wa kwanza wa Zanzibar) alitoa Sh 4 Milioni kwa klabu kama zawadi, akataka timu ijenge uwanja wake,” anasimulia.

Anasema Mwalimu Nyerere alimgomea Karume akasema kwanini awape Yanga wakati na Simba ipo, bora awape wote.

“Simba wakati ule ilikuwa ina waarabu, wahindi na wazungu, Karume akasema hawezi kuwapa pesa yake, Nyerere akamwambia haitapendeza kwani watu wote ni wake, hivyo igawe kila klabu uipe Milioni 2,” anasimulia.

Anasema wakati huo Simba ilijulikana kama Sunderland, Karume akasema hawezi kuipa timu hiyo pesa yake, bora wabadili jina kutoka Sunderland na kuitwa Simba, ndipo akawapa Milioni 2 na Yanga wakapewa Milioni mbili.

“Sisi hatukuwa na uwanja, tukafanya mpango ili kuwatoa kwenye eneo la Jangwani wale waliokuwa wanafanya udobi pale, ikawezekana wakaondolewa ndipo klabu ikajenga makao makuu yake pale Janganwani,” anasimulia.


Nyerere aliwawekea wanamichezo mazingira mazuri

Katika mambo ambayo Kitwana anasema hawezi kuyasahau ni mazingira mazuri ya kuajiriwa ambayo wanamichezo wa wakati wa mwalimu Nyerere waliwekewa.

Kitwana ambaye amejenga Tabata jijini Dar es Salaam na ana miriki gari mbili aina ya Landcruiser zenye namba D na flemu kadhaa za biashara anasema pamoja na kwamba hawakupata kipato kikubwa kwenye mpira wakati ule, lakini walipata ajira zilizowapa kipato.

“Nyerere alisema kama mchezaji una kipaji lazima ufanye kazi, mpira au riadha au ngumi iwe sehemu tu ya kazi yako, wengine tulipelekwa Bandari, wengine wakaenda jeshini, wengine kwenye Shirika la Posta na mashirika mengine ya Umma,”.

Licha ya baadhi ya wanamichezo wa zamani kuwa katika maisha magumu, Kitwana anasema wakati ule walilipwa mishahara kwenye mashirika waliyofanyia kazi.

“Hata kama ulikuwa hujasoma lakini una kipaji, Nyerere alisema kaa bandari huko kwenye cargo, huwezi kushindwa kuhesabu hata maboxi, hivyo unakuwa mchezaji lakini huko kazini.

“Nilichojifunza wakati ule kwanza kama baba wa familia ni kuwa kiongozi na kuwasomesha watoto wako kama Mwenyezi Mungu atakuwa amekujalia, ndivyo nilifanya mimi,” anasimulia Kitwana.


Agoma kwenda Ulaya

Kitwana ambaye ni mchezaji wa kulipwa wa kwanza nchini anasimulia namna alivyokataa ofa ya kwenda kucheza soka la kulipwa nchini Ulaya.

“Kocha wa timu ya Taifa Mburgaria aliniita akaniambia Kitwana unatakiwa kwenda kucheza soka Ulaya, wakati ule kwa mchezaji wa Tanzania kusikia Ulaya ilikuwa ni jambo kubwa, nikamwambia siwezi,” anasema.

Anasema alipata ofa ya kwenda kucheza kwenye klabu ya Mombasa aliyohitaja kwa jina la Feisal.

“Wakati ule Jumuiya ya Afrika Mashariki tulikuwa kama tumeungana, hivyo nikaona Mombasa haitokuwa shida kucheza, nikakubali na kusajiliwa kwa pesa ya Kenya Sh 100,000.

“Nilipoichenji ilikuwa Sh 200,000 za Tanzania, ile pesa unajua wachezaji wa zamani tulikuwa tunapendana sana, niliitumia na wachezaji wenzangu, nikamugawia kila mmoja kwenye timu kama ishara ya kuwaaga mimi nikabaki na kidogo,” anasimulia.

Anasema alianza maisha mapya nchini Kenya akicheza soka la kulipwa ambapo alipewa mshahara Sh 4000 ya Kenya kwa mwezi.

“Niliishi maisha ya kistaa kule, kila nilichokuwa nataka kwenye ile timu nilipewa, huko ndiko nilikutana na Baba yake Raila Odinga, wakati huo Odinga Jr akiwa kijana mdogo.

“Odinga Sir alinifuata hotelini mwaka 1963 nikiwa Kenya kwenye mashindano ya Chalenji, nilikuwa staa kweli kweli, hilo tukio Odinga Jr hajawahi kulisahau ndiyo sababu alipokuja Tanzania kwenye fainali ya Sportpesa timu ya Gor Mahia ilipocheza alinitafuta, hakuamini aliponiona, akatoa dola 40,000 kunipa,”.


Yanga walimtumia bibi yake kumrejesha nchini

Tofauti na usajili wa sasa, Kitwana anasema enzi zao familia ndiyo ilikuwa inaamua kijana wao ni timu ipi acheze kati ya Simba au Yanga na ndivyo ilikuwa kwake.

“Bibi yangu alikuwa kindakindaki wa Yanga, nikiwa Mombasa wazee wa klabu walimfuata wakamwambia wewe umemruhusu kijana wako kwenda Kenya, kwanini asirudi kucheza Yanga,” anasimulia.

Anasema aliporejea likizo, bibi yake alimfuata akamwambia mjukuu wangu kwanini usirudi nyumbani kuichezea Yanga?.

“Nilibaki namtizama tu bibi, kwani mwanzoni yeye ndiye alikuwa akiniambia nisicheze kwenye timu hizo nitarogwa, nikamwambia bibi kwa hiyo umeamua mjukuu wako nikarogwe?, akasema hakuna kitu kama hicho, wewe rudi nyumbani ujiunge na Yanga timu ya wananchi.

Anasema siku aliporejea Mombasa kumbe uongozi wa Feisal ulishapata taarifa kwamba yuko mbioni kurudi Tanzania kujiunga na Yanga.

“Ile nimefika klabuni, nikawakuta wazee wa ile klabu wako kwenye kisomo, wanaongea kwa kiarabu hakuna nilichoambulia, nikiwa nje miguu ilikuwa mizito, kuondoka eneo hilo nataka kuingia ndani nataka, basi nikabaki nimeganda,” anasimulia.

Anasema baada ya muda alipata ujasiri na kuingia ndani, ambako alikwenda kuaga na kwenda kuchukua mizigo yake kurudi Tanzania, kuanza maisha mapya kwenye klabu ya Yanga.

“Nilipofika Yanga nilikuta tayari wana golikipa, hivyo mimi nikawa nacheza namba tisa, pale Yanga sikuwahi kucheza kipa kama nilicheza si chini ya mara mbili, lakini muda wote nilikuwa mshambuliaji namba tisa,” anasimulia.


Yanga wamtorosha

Mwaka 1977, Yanga iliingia kwenye mgogoro ambapo Kitwana anasema kocha aligombana na Sunday Manara.

“Tulikuwa tunajiandaa na mechi, tuko kambini kocha akasema hataki wachezaji kutoka, ikaja taarifa kuwa Sunday katoka, ikabidi kocha awe mkali, katika kuzozana na Sunday wakapigana,” anasimulia.

Anasema baada ya ugomvi ule, kocha alitishia kuondoka, mashabiki na wanachama wakambembeleza akasema ili yeye abaki lazima Sunday aondoke.

“Nilimwambia Sunday mdogo wangu, wewe kubali kuondoka, akaondoka lakini kuna watu ambao walimfuata pia, ndipo ikaenda kuanzishwa Pan African.

“Ilikuwa na mimi nijiunge na Pan African, mwenyekiti wake alinifuata Arusha, akiwa ananisubiri kuna wapenzi wa Yanga wakasikia, wakaja hotelini nilipokuwa wakati watu wa Pan wananisubiri getini, wale wapenzi wa Yanga wakatoboa seng’enge ya ile hoteli nikapenya chini, tukaondoka.

“Ilikuwa kama muvi, nikarudi klabuni kuendelea kuitumikia Yanga, ila asikwambie mtu, mgogoro ule ulituvuruga sana,” anasimulia.


Atoboa siri ya Yanga kumkataa Matola

Kipaji cha Suleiman Matola kilimuwezesha kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Simba, kuwa nahodha wa timu hiyo na sasa ni kocha msaidizi, ingawa Kitwana anasema mchezaji huyo aliletwa Dar es Salaam na Yanga.

“Baba yake Matola alikuwa rafiki yangu, tulikuwa na kucheza wote soka mkoani Kigoma tulikozaliwa,” anasimulia.

Anasema baada ya yeye Kitwana kustaafu kucheza, alikuwa mmoja wa viongozi kwenye klabu ya Yanga na alihusika na usajili wa klabu hiyo.

“Nilikwenda Kigoma kutafuta wachezaji, nikampata Makumbi Juma na Mziba, lakini pia nilimtaka kijana wa Matola (Selemani), baba yake akaniambia yuko Bukoba.

“Nikamwambia nitakwenda Bukoba kumuona ili asajiliwe Yanga sababu uwezo wake baba yake alikuwa ameniambia,” anasimulia.

Anasema mzee Matola alimpa barua ili akifika Bukoba ampe mwanae kuonyesha kuwa imetoka kwa baba yake, akasafiri hadi Bukoba na kufanikiwa kuonana na Suleiman.

“Alifurahi mno, nikamuachia nauli nikamwambia ajiandae ili aje kujiunga na Yanga, wakati huo tayari nilikuwa nimewachukua Makumbi Juma na Abeid Mziba kutoka Kigoma,” anasimulia.

Anasema Matola kweli alisafiri na kuja Dar es Salaam, lakini mmoja wa viongozi wa juu wa Yanga akamkataa bila hata kumuona uwanjani.

“Aliniuma sana, nikamwambia sasa utafanyaje, akaniambia mzee kwa kuwa mimi nimeshafika Dar es Salaam, basi niache nitajua nini nitafanya, ndipo baadae Simba wakamuona na kumchukulia hapa hapa Dar es Salaam wakati Yanga tulimsafirisha kutoka Bukoba,” anasimulia.


Hana mzuka wa kuifuatilia stars

Kama ni mpenzi wa soka na ulimtarajia Kitwana Manara kuwa shabiki kindaki ndaki wa timu ya Taifa, basi pole yako, nyota huyo wa zamani anasema hana mzuka wa kufuatilia mechi za timu hiyo.

“Niliwahi kwenda uwanjani nikasukumwa na kuzongwa na makomandoo kama mwizi, nikasema hivi kwanini nafanyiwa hivi, sababu ni mpira au? kuanzia hapo nikaacha kwenda uwanjani wala kuifuatilia timu ya taifa,” anasema.

Anasema kuzongwa huko kulisababishwa na yeye kutokuwa na tiketi, lakini aliamini kutokana na nafasi yake na mchango wake kwenye timu ya taifa angepewa heshima.

“Siyo peke yangu, wachezaji wengi wa zamani tunanyanyaswa na makomandoo tukienda uwanjani kuangalia mechi, kuna wakati unaweza kusukumwa hadi ukadondoka, halafu anatokea tu mtu hajulikani makomandoo hao hao kwa kuwa ni rafiki yao wanampitisha, hii iliniuma mno.

“Lakini siwalahumu makomandoo, nailaumu TFF kwani wao ndiyo wamewaweka pale getini, wangeweka utaratibu wa wachezaji wa zamani kupewa japo vitambulisho vya kuingilia uwanjani kama alivyokuwa akifanya Tenga (Leodger mwenyekiti staafu wa TFF).

Alisema Tenga aliweka utaratibu wa kuwapa vitambulisho wachezaji wa zamani na kuna wakati mechi inaendelea anamugawia kila mchezaji karatasi na kuomba amchagulie wachezaji ambao anafikiri wanastahili kuitwa kwenye timu ya taifa.

“Tulikuwa tunafanya hivi na baada ya mechi zile karatasi zinachukuliwa kuoanishwa na uteuzi wa kocha mkuu, kuna wakati mnajikuta uteuzi umefanana, ndivyo tulikuwa tunafanya.

“Alipoondoka Tenga, wachezaji wa zamani ni kama tumeachwa, hata ule utaratibu wa kupewa vitambulisho vya uwanjani ulifutwa, tunasukumwa, lakini wanasahau hata mchango wetu wa mawazo kwenye timu ya taifa unaweza kufaa, hatuhitaji kulipwa, tulijitoa kwa Tenga kutokana na mapenzi na uwezo wetu kwenye soka,” alisema.


Kabla ya soka alikuwa mwanamuziki

Kitwana ambaye amechangia baba na Sunday Manara alianza soka akiwa shule ya msingi Mchikichini.

“Mzee alitoka Kigoma kuhamia Dar es Salaam, nilijiunga na shule ya Mchikichini, lakini sikuwa na ndoto ya mpira,” anasema.

Anasema akiwa na miaka 16 alianzisha bendi ya Ndanda Jaz, yeye alikuwa mpiga drum maarufu na mzee Rajabu Diwani ndiye alimusaidia hadi kuanzisha bendi hiyo.

“Wakati wa kudai Uhuru, Bendi zilikuwa na ushindani, ikafikia hatua mashabiki wa bendi wakapigana, kuanzia pale mvuto wa bendi ukaanza kupotea ndipo nikaingia kwenye soka,” anasimulia.


Anasema alicheza timu za mtaani kabla ya kuchukuliwa na TPC ya Moshi.

“Wakati huo nilikuwa nacheza nafasi ya golikipa, nikiwa mazoezini timu yangu ilifungwa, nikajiuliza hivi siwezi kuingia nikacheza mbele?, nikaomba kubadili namba, ile nimeingia kucheza ndani nikafunga goli, hapo ndipo nikaanza kucheza ndani kama namba tisa na wakati mwingine narudi kucheza kipa.

Anasema kutokana na urefu wake, alikuwa mzuri kwa kufunga mabao ya vichwa.

“Nilipokuwa mazoezini nilifanya sana mazoezi ya kufunga kwa kichwa, hivyo nikajikuta namudu kucheza namba tisa lakini pia nikikaa golini unifungi,” anasimulia.

Anasema yeye ndiye kipa wa kwanza Afrika Mashariki kuibuka na staili ya kudaka kwa kudaivu.

“Staili hii nilifundishwa na Wahindi nilipokuwa nakwenda kwenye mazoezi ya beach kule Feri,” anasimulia.

Anasema wakati ule Wahindi walifurahi kumrushia mipira akiwa kwenye maji na yeye kudaka huku akidaivu.

“Walikuwa wakifurahi kuniona nafanya mazoezi hayo, kumbe na mimi nilikuwa najifunza, hivyo nikiwa kwenye mechi watu wanashangaa udakaji wangu.

“Makipa wa wakati ule wengi walikuwa warefu hivyo walikuwa wakijua kupangua mipira ya juu kutokana na urefu wao, lakini pia kuzuia mipira kwa kuiziba na miguu, kuadivu ilikuwa ni kitu kipya kwao,” anasimulia.

Kingine ambacho mpaka leo kinabaki kwenye kumbukumbu ya maisha ya soka ya Kitwana ni jinsi zamani ambavyo hawakuwa wakivaa njumu zaidi ya kucheza wakiwa wamevaa soksi tu.