Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbeki ahamia KVZ, aweka hadi ya kutetea ubingwa

Muktasari:

  • Kati ya misimu mitano aliyoichezea Mlandege, bila shaka 2025-2026 ulikuwa bora zaidi kwake kwani jina lake limetajwa sana kiasi cha kuzivutia timu mbalimbali na hatimaye KVZ ikafanikiwa kuinasa saini yake.

BAADA ya kuitumikia Mlandege kwa misimu mitano mfulululizo, beki wa kushoto, Said Mussa Said maarufu kwa jina la Mbeki, anakwenda kukiwasha KVZ ambayo ni bingwa wa Ligi Kuu Zanzibar msimu wa 2025-2026.

Kati ya misimu mitano aliyoichezea Mlandege, bila shaka 2025-2026 ulikuwa bora zaidi kwake kwani jina lake limetajwa sana kiasi cha kuzivutia timu mbalimbali na hatimaye KVZ ikafanikiwa kuinasa saini yake.

Miongoni mwa mambo yaliyompa umaarufu zaidi msimu huo ni kutokana na uwezo wake wa kupiga krosi na faulo.

Mbali na hilo, Mbeki amekuwa na wakati mzuri ndani ya uwanja kutokana na uwezo wake wa kupanda na kushuka na kufanya uamuzi wa haraka kwenye maeneo hatari.

Uwezo wake unatajwa kwamba haujaibuka ghafla, bali tangu akiwa anacheza katika Ligi za vijana ikiwemo Juvenile, Junior na Central Wilaya Mjini kisiwani Unguja.

Wataalamu wanasema historia ya mtu huandikwa kwa mikono yake na Mbeki ameandika historia ya kucheza timu ya vijana ya taifa ya Zanzibar inayojulikana kama Karume Boys.

Mbeki aliyeanza kucheza Ligi Kuu Zanzibar akiitumikia Mlandege katika msimu wa 2021-2022, 2022-2023, 2023-2024, 2024-2025 na 2025-2026, hatimaye anabadilisha makazi na sasa 2026-2027 anakwenda kuitumikia KVZ.

Mwanaspoti limepiga stori na beki huyo ambaye ana malengo makubwa ndani ya KVZ, lakini pia nje ya kikosi hicho kinachokwenda kushiriki 2026-2027 kikiwa bingwa mtetezi wa Ligi Kuu Zanzibar, lakini pia ikiiwakilisha Zanzibar kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.


MLANDEGE YAMPA NJIA

Beki huyo anasema katika utumishi wake wa misimu mitano ndani ya Mlandege aliitumikia kwa mafanikio makubwa ikiwemo kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar (2024-2025) na Kombe la Mapinduzi 2023 na 2024, ambapo alikuwa panga pangua ndani ya kikosi cha kwanza, hali iliyomfungulia njia ya kufahamika zaidi.

Anasema, licha ya msimu uliopita 2025-2026 kuwa bora kwake, lakini anajilaumu sana kwa kitendo cha kikosi chao cha Mlandege kushindwa kutetea ubingwa wa ligi, hivyo anatamani 2026-2027 isijirudie ndani ya KVZ anapokwenda kuanza maisha mapya.

Mbeki anaeleza kwamba, amefurahia dili lake la kutua KVZ kutimia kwani itakuwa ndio mwanzo wa safari yake ya kutimiza malengo ya kucheza soka la kulipwa nje ya Zanzibar.


UGUMU WA KUONDOKA MLANDEGE

Mbeki anasema haikuwa rahisi kwa upande wake kufanya uamuzi wa kuondoka Mlandege baada ya kucheza kwa misimu mitano, huku akifichua kwamba hapo palikuwa kama nyumbani kwake.

Anafafanua kuwa, Mlandege ndio sehemu ambayo alikaa muda mrefu jambo ambalo lilikuwa kikwazo kwake kuondoka hususani kwa namna alivyozoena na wenzake.

Anaeleza kuwa, hata KVZ ilipoonesha nia ya kuhitaji huduma yake, hakuwa na uhakika wa dili hilo kuja kutiki kutokana na kuzoea kukaa Mlandege.

“Kulikuwa na ugumu kuondoka, Mlandege ni sehemu niliyoichezea muda mrefu na mazoea ndio ambayo yalinitesa zaidi, hivyo sikuwa na uhakika kama dili hili la kwenda KVZ litakamilika,” anasema.


MAZINGIRA MAPYA

Beki huyo anasema, licha ya kuwa na ugeni kwenye timu hiyo, laki ana furaha kuwepo kwenye kikosi hicho na kilichobaki ni kuisaidia timu iweze kufanya vizuri. Anaeleza kuwa, timu hiyo itakuwa ni sehemu salama kwake na kumpa anachokitarajia kukipata ndio maana ameridhika kuitumika KVZ.

Anasema, kitu kinachompa furaha zaidi ni ushirikiano anaoupata kutoka kwa wachezaji waenzake, benchi la ufundi na viongozi wa timu, hivyo anaamini mafanikio yapo karibu naye.


MAPOKEZI YAKE

“Kwa kweli nimepokelewa vizuri tangu siku ya kwanza hadi leo, viongozi, wachezaji wenzangu pamoja na mashabiki wa timu ya KVZ wote wameniunga mkono kuwa sehemu yao ya kikosi kwa msimu huu,” anasema.


MIPANGO YA 2026-2027

Beki huyo anasema amejipanga vizuri kuhakikisha anacheza kwa jasho na damu ili kuendelea walipoishia na kuisaidia timu kufanya vizuri.


KUHUSU UCHEZAJI WAKE

Mbeki ameliambia Mwanaspoti kuwa, hakuna mtu yeyote ambaye alimshawishi kucheza nafasi ya beki wa kushoto bali amejikuta akiitumikia nafasi hiyo.

Amesema, tangu alivyokuwa mdogo alicheza nafasi hiyo, lakini pia ana uwezo wa kucheza winga zote mbili, kushoto na kulia.


CHANGAMOTO

Anasema miongoni mwa changamoto mojawapo aliyokutana katika safari yake ya soka ni kutukanwa na kudharauliwa bila ya kujua sababu ya hilo.

Lakini, anasema hakuwahi kukata tamaa badala yake alivumilia hayo hadi kufikia alipo sasa jambo ambalo anajivunia upande wake.


NENO LAKE KWA ZFF

Amesema, kwa mtazamo wake mpira wa Zanzibar unazidi kuimarika kwa misimu ya hivi karibuni, hivyo amelisihi Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) kukubali kukusolewa kwani hiyo ndio njia pekee ya kuendelea kufanya vizuri.

Mbali na hilo, ametoa pongezi kwa ZFF kusimamia mpira na kuibua vipaji vya vijana waliopata nafasi ya kuajiriwa kupitia mpira wa miguu.


ANAOWAKUBALI

“Mimi wachezaji ninaowakubali wa ndani ni Ali Machupa, Mussa Hassan, Fahad Mahrez na Harouna Zaha, lakini wa nje ni Theo Hernandez, Nuno Mendez na Aubrey Modiba.


AHADI KWA KVZ

“Kwa ujumla mashabiki wa KVZ watarajie mambo mazuri kutoka kwangu kwani nitapambana kadiri ya uwezo wangu kuhakikisha tunatetea ubingwa wa ligi,” anasema Mbeki.