Sitaki tena Urais – Sehemu ya 03
UTANGULIZI
Shanga alishtuka.
“Ulijuaje?”
“Kujua mambo ni moja ya kazi zetu. Hilo lisikutie wasiwasi.”
“Ni kweli, kuna watu walikuja na kunieleza kuwa mimi ni Freemason, kwa hiyo si vizuri nionekane na wewe.”
“Hao watu utaonana nao leo usiku.”
“Wapi?”
“Katika huo msafara wetu.”
“Unajua, nilishapata mawazo tofauti?”
SASA ENDELEA
“HAPANA, usibadili mawazo kwa sababu ya watu hao. Tumeshamjulisha kiongozi wetu kuhusu ujio wako. Jitahidi utimize ahadi yako. Kumbuka kwamba wewe tayari ni rais wa nchi hii.”
“Sikiliza Lisha, mimi kama sitapata urais nitajitoa”
“Bila ya shaka yoyote. Sisi tuna uhakika na tunachokisema”
“Sawa, sasa ninataka tukutane sehemu nyingine mbali ya Pasific”
“Basi tukufuate nyumbani kwako. Tutakuchukua kwa gari letu. Hakuna mtu ambaye atajua nini kinaendelea”
“Sawa, basi nitawasubiri muda huo”
“Sawa”
Shanga akakata simu. Wakati anaiweka simu aliona benzi jeusi likimpita kwa kasi. Alipolitazama kwa nyuma alishangaa alipogundua lilikuwa ni lile benz la freemason, wanalitumia Lisha na Bosco.
Walikuwa wapi? Shanga akajiuliza.
Wakati nazungumza na Lisha kwenye simu walikuwa wananiandama nyuma? Akaendelea kujiuliza.
Benzi hilo lililokuwa linakwenda kwa kasi lilikata kona kulia na kutoweka. Yeye alikata kona kushoto na kushika barabara iliyokuwa inaelekea kwenye mtaa aliokuwa anaishi.
*************
Saa moja jioni Shanga alikuwa ameshamaliza kula chakula cha jioni. Alimwambia mke wake kuwa alikula mapema kwa vile ikifika saa mbili usiku alihitaji kwenda kukutana na wafadhili wa chama chake katika hoteli ya Pasific ili wajadili mwendo wa kampeni.ambayo ilitarajiwa kuanza wakati wowote.
“Kampeni ina gharama kubwa. Inabidi tujadiliane na wafadhili wetu tuone watatusaidiaje” Shanga alimdanganya mke wake.
Mara baada ya kula chakula Shanga aliketi sebuleni kuwasubiri wageni wake wa freemason.
Ilipofika saa mbili kamili simu yake ikaita, alipoipokea Lisha alimwambia.
“Tuko nje ya nyumba yako tunakusubiri”
“Sawa, ninakuja”
Shanga alirudisha simu yake mfukoni akanyanyuka na kumwambia mke wake kuwa anatoka.
“Wenzangu wameshafika wako nje”
“Utarudi saa ngapi?”
“Muda wa kurudi utategemea urefu wa mazungumzo yetu lakini sitarajii kuchelewa sana”
Alipotoka nje Shanga alikuta benz jeusi linamsubiri huku mlango mmoja wa nyuma ukiwa wazi. Alikwenda kwenye mlango huo akajipakia. Katika siti ya nyuma alikaa Lisha. Bosco ndiye aliyekuwa anaendesha. Wote wawili walikuwa wamevaa suti nyeusi za kifreemaso.
Alipojipakia Shanga alifunga mlango.
“Habari ya saa hizi?”
“Nzuri bwana Shanga, karibu sana” Lisha alimjibu.
Bosco akaondoa gari.
“Ndiyo tunaelekea huko?” Shanga aliuliza akionekana kuwa na wasiwasi.
“Ni kama tulivyokubaliana” Lisha alimjibu.
“Sehemu gani?”
“Ofisi yetu moja iko katikati ya jiji lakini sisi tunakwenda kwenye makao yetu”
“Ni wapi?”
“Ni nje kidogo ya jiji”
“Ni mwendo utakaotuchukua muda gani?”
“Ni mwendo wa nusu saa tu.”
Benz ilikuwa inakwenda kasi kama vile walikuwa wanakimbilia kitu.
Baada ya mwendo wa dakika kumi waliingia katika eneo la Oseriver ambalo lilikuwa kando ya jiji hilo. Lilikuwa eneo walilokuwa wakiishi matajiri, wafanyabiashara wakubwa na maofisa wa juu wa serikali.
Baada ya kupita katika mitaa kadhaa, gari hilo lilisimama kwenye geti la nyumba moja. Ilikuwa nyumba kubwa ya ghorfa moja iliyozungushiwa ukuta mpana wa matofali.
Gari hilo liliposimama hapo geti hilo lilifunguliwa na askari ambaye pia alivaa suti ya kifreemaso. Gari hilo liliingia ndani na kwenda kusimama ndani ya banda la magari lililokuwa na magari zaidi ya kumi.
Walishuka kwenye gari na kuelekea kwenye jengo hilo la ghorofa ambalo lilikuwa likiwaka taa za rangi mbalimbali.
Karibu eneo lote lilikuwa na bustani ya kupendeza iliyotengenisha njia za kupita magari. Kulikuwa na njia ya kuingilia na njia ya kutokea. Mbali ya bustani kulikuwa na miti mingi ya vivuli.
“Nafikiri ndiyo hapa,” Shanga alimwambia Lisha.
“Hapa ndiyo kwenye makao yetu. Kiongozi wetu anaishi hapa”
Shanga alikuwa akilitupia macho jumba hilo wakati akitembea.
“Hili ni eneo la siri sana. Hakuna mtu yeyote anayefahamu ni shughuli gani zinazofanyika humu ndani. Pia eneo hili linalindwa kwa vifaa maalumu,” Lisha aliendelea kumwambia Shanga.
“Gari letu lilishaonekana tangu linakuja ndiyo maana tuliposimama tu kwenye geti askari alitufungulia bila kupiga honi. Hapa tulipo tunaonekana. Kuna kamera zinazotuchukua hadi tunakokwenda”
“Ni kweli kuna usalama wa kutosha” Shanga alisema akionekana kugwaya.
Walifika kwenye mlango. Lisha alibonyeza tarakimu kwenye kifaa kidogo kilichokuwa pembeni mwa mlango. Mlango huo ukafunguka.
“Karibu ndani,” Lisha alimwambia Shanga huku akitangulia kuingia.
Walipoingia mlango huo ulijifunga. Walitokea kwenye ukumbi ulioambatana na sebule iliyokuwa upande wa kushoto. Walitembea katika ukumbi huo. Mbele kulikuwa na ngazi iliyoelekea juu.
Walipanda ngazi na kufika ghorofani. Lisha akiwa amewatangulia wenzake alikwenda kwenye mlango na kubonyeza tarakimu kwenye kifaa kilichokuwa pembeni mwa mlango. Mlango huo ukafunguka.
Lisha aliingia na kumkaribisha Shanga aliyeonekana kunywea. Shanga aliingia na kuona kilikuwa chumba kipana kilichokuwa na makochi. Kulikuwa na watu sita waliokuwa wameketi wakiwa wamevaa suti za kifreemaso. Watu watano walikuwa wamekaa kwa pamoja wakati mtu mmoja alikaa peke yake. Alikuwa mtu mzima aliyekuwa ameshika kitabu.
Lisha na Bosco walisalimiana na watu hao kwa salamu za kifreemaso huku wakitabasamu. Shanga ambaye alikuwa kimya hakujua ni kwanini watu hao walitabasamu.
Kwenye ukuta wa upande mmoja kulikuwa na TV zilizochomekwa kwenye kuta. TV hizo ambazo zilikuwa zimeunganishwa na kamera za usalama zilionesha picha ya kila kona ya jumba hilo pamoja na nje ya geti.Shanga aliwaza kwamba Lisha alipomwambia wanaonekana wakati wanafika, walikuwa wakionekana katika TV hizo.
Miongoni mwa watu waliokuwa wameketi, Shanga aligundua kuwa watu wawili walikuwa ni wale waliomfuata ofisini kwake mchana na kumwambia kuwa aepukane na Lisha kwa sababu Lisha ni freemas!
Shanga aliwatumbulia macho ya mshangao huku akijiuliza kimoyomoyo
“Watu hawa si ndio waliokuja ofisini kwangu na kunihadharisha juu ya kushirikiana na freemaso?”
Lakini hapo hapo aliyakumbuka maneno ya Lisha aliyomwambia kwenye simu akiwa kwenye gari. “Hao watu utaonana nao leo usiku”
Wakati Lisha akimwambia hivyo Shanga hakuwa amemuelewa, hivyo hakuyatilia maanani maneno yake.
Akashusha pumzi za kindanindani na kumfuata Lisha aliyeelekea kwa yule mzee. Watu hao watatu Lisha, Bosco na Shanga wakakaa kwenye sofa moja lililokuwa karibu na sofa alilokaa yule mzee.
“Tumekuja na mgeni wetu, anaitwa bwana Shanga” Lisha alimwambia mzee huyo. Wale watu watano nao walikuwa wakisikiliza.
Mzee aligeuza uso na kumtazama Shanga.
“Hujambo bwana Shanga?” Sauti yake ilikuwa kavu ya kukwaruza.
“Sijambo mzee. Habari za hapa?”
“Hapa ni kwema. Asante sana”
“Asante”
“Mimi ninaitwa Osaka, ni afisa mwandamizi wa freemaso. Mkuu wangu ameniambia tutapokea mgeni usiku huu”
Wakati Osaka akizungumza wale watu wawili ambao Shanga alikuwa amewatambua walinyanyuka na kutoka ghafla.
“Tumefurahi kuwa umefika. Kwa hiyo ngoja nikufikishe kwa kiongozi wetu ili uweze kuzungumza naye,” Osaka aliendelea kumwambia Shanga.
Kabla ya kuzungumza na kiongozi wenu kuna maswali ambayo ningependa kukuuliza”
“Uliza”
“Ndugu niliofika nao hapa walinifuata na kujitambulisha kwangu kuwa wao ni freemaso na wakanitaka na mimi nijiunge na kundi lao ili niweze kufanikiwa kupata urais. Swali langu ni je kama nitajiunga na kundi lenu, mnanihakikishia kuwa nitaweza kupata urais kwa asilimia mia moja?”
Osaka alikubali kwa kichwa na kwa mdomo.
“Hilo halina shaka. Tunahitaji kuwa na rais ambaye atatutambua na ambaye tumemuweka sisi kwenye madaraka. Wewe ni chaguo letu”
“Kama mnanihakikishia kuwa nitapata urais, mimi niko tayari kujiunga isipokuwa ninataka mniambie kanuni zenu na kama kuna masharti yoyote.”
“Kwa mujibu wa kanuni zetu mwanachama anaelezwa kila kitu baada ya kujiunga kwa sababu kila kitu cha freemaso ni siri ya freemaso, unapijua tayari wewe ni freemason.”
“Sawa, niko tayari kujiunga”
Osaka akanyanyuka.
“Tafadhali nifuate”
Kulikuwa na mlango mwingine wa kuingilia ndani. Osaka aliufuata mlango huo akaufungua. Shanga alikuwa ameshanyanyuka na kumfuata. Lisha na Bosco walibaki pale pale kwenye sofa.