Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sitaki tena Urais - Sehemu ya 01

RAIS 01 Pict

UTANGULIZI

Katika ramani ya kubuni ya Afrika kuna nchi moja iliyoko katika pembe moja ya Afrika inaitwa Kamisa. Mji mkuu wake ni Maloto.

Ni nchi ya kidemokrasia ambayo miaka michache nyuma iliingia katika mfumo wa vyama vingi vya kisiasa chini ya rais wake Abdallah Heris.

Katika uchaguzi wake wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi, chama tawala cha Wananchi na Maendelea (WM) kilivishinda vyama viwili vya upinzani, Umoja na Maendeleo (UM) na Maendeleo Haki na Usawa (MHU) vilivyoshiriki katika uchaguzi huo wa kwanza. Hivi sasa uchaguzi mwingine umekaribia. Vyama vya siasa vimeanza kujichua ili kujitosa katika uchaguzi huo kila kimoja kikitarajia kushinda.

Tayari chama cha UM kimemteua mwenyekiti wa chama hicho, Max Shanga kugombea urais kupitia chama hicho.

Max Shanga ni kijana mwenye umri wa miaka arobaini na mitano. Ana sifa ya uchapaji kazi na ukereketwa wa maendeleo. Aliwahi kuwa waziri katika serikali iliyopita kabla ya kujiunga na chama cha upinzani. Lakini anakabiliwa na changamoto kubwa ya kupata urais kwani anachuana na wagombea wawili ambao pia wanakubalika kwa wananchi akiwemo mgombea wa chama tawala. Hilo ndilo jambo linalomtia wasiwasi…

SASA ENDELEA





ALIKUWA amemaliza kula chakula cha usiku pamoja na mke wake, mtumishi wao alipowafuata na kuwambia.

“Kuna mtu anabisha kwenye mlango”

“Ni nani?” Max Shanga akamuuliza.

“Sijui ni nani?”

“Umemuuliza anamtaka nani?”

“Amesema anakuhitaj wewe”

“Mkaribishe sebuleni, ninakuja…”

“Si ungekwenda kumuona kwanza…? Mke wake alimkatiza.

“Nimeshakuwa mtu wa watu, mgombea urais. Natakiwa niwe na sifa ya ukarimu na ucheshi kwa kila mtu, ninayemjua na nisiyemjua…”

Shanga aliondoka kwenye kiti na kwenda sebuleni. Alimuona mtumishi wake akikakaribisha wageni wawili. Wote wawili walikuwa wamevalia suti nyeusi na tai.

Mara tu baada ya kuwaangalia, Shanga aligundua kuwa sura zao hazikuwa ngeni machoni mwake inagawa hakuweza kutambua mara moja walikuwa kina nani.

Alihisi huenda walikuwa wanachama wa chama chake au watu aliokuwa akikutana nao katika harakati zake za kisiasa.

“Karibuni sana,” Shanga aliwambia akiwa amesimama katikati ya sebule akiwasubiri.

“Asante mheshimiwa,” mmoja wa watu hao alimjibu Shanga na kumpa mkono.

“Habari ya jioni?”

“Nzuri. Habari zenu na nyie?” Shanga aliwauliza wakati akipeana mkono na mtu wa pili.

“Sisi tuwazima, tunashukuru,” mtu aliyekuwa akimpa mkono alimjibu.

“Karibuni kae,” Hashim aliwambia kabla ya kuketi.

“Sisi ni wageni wako, tunatoka katika jumuia moja muhimu sana. Mimi ninaitwa Dominick Lisha, mwenzangu ni John Bosco,” mmoja wa watu hao alisema.

Shanga aliwatazama kwa zamu na kuwambia.

“Nimefurahi kuwafahamu

“Sisi si wanachama wa chama chochote cha siasa lakini tunafuatilia kwa makini harakati za chama cha UM unachokiongoza wewe,” Dominick Lisha aliendelea kueleza.

“Ndiyo, nimefarijika sana kusikia hivyo.

“Tumefurahi kusikia kuwa chama chako kimekuteua kugombea urais. Sisi tumekuja kukueleza nia yetu ya kukuunga mkono na kukuhakikishia kuwa tutakuwa bega kwa bega na wewe hadi urais.

“Nitashukuru sana. Ningeomba mnifahamishe mnatoka katika jumuia gani kwani sura zenu si ngeni machoni mwangu.

“Sura zetu si ngeni kwako kwa sababu tunashiriki katika mikutano yako mingi na pia tunafika katika ofisi za chama chako. Bila shaka utakuwa unatuona bila kututambua,” Lisha akamueleza Shanga.

“Ni kweli, inawezekana.

“Kama utakubaliana na sisi uwezekano wa wewe kupata urais ni wa asilimia mia moja.

“Hamjanitambulisha, mnatoka katika jumuia ipi?

“Sisi tunatokea katika jumuia ya kiraia na ipo katika nchi mbalimbali hapa Afrika, Asia na pia nchi za Ulaya na Marekani,” Lisha alijibu.

“Jumuia yenu inaitwaje na inashughulika na nini?

“Kwa kifupi sisi ni Freemaso.”

Max Shanga alishituka. Ili kuficha uso wake usioneshe mshituko alitabasamu. Tabasamu hilo la uongo lilionekana kwenye uso wake tu lakini mshituko uliendelea kubaki ndani ya moyo wake!

“Nyinyi ni Freemaso? Shanga aliwauliza huku akiwatazama tena kwa zamu kama vile ilikuwa ndio kwanza anawaona.

“Ndiyo, sisi ni Freemaso au wajenzi huru,” John Bosco aliyekuwa kimya muda wote alimjibu.

“Nimekuwa nikisikia tu kuhusiana na Freemaso lakini sifahamu shughuli zao ni nini?

“Huwezi kuzijua shughuli zetu kwa undani mpaka uingie ndani ya kundi letu. Na wewe tunakushauri uingie ili uweze kupata mafanikio ya kisiasa,” Bosco alimjibu.

“Mnaweza kunidokeza kidogo?

“Tunachoweza kukudokeza ni kuwa Freemaso tupo kusaidia watu, kuendeleza watu pamoja na kuwapa watu fikira mpya za kimaendeleo. Tuna misingi yetu ambayo kama utaifuata ni lazima utafankiwa kupata urais.

“Ningependa mnipe ufafanuzi zaidi, mnawasaidiaje watu?”

Bosco alitoa kicheko.

Ni siri yetu. Haturuhusiwi kutoa siri zetu za ndani isipokuwa tunakushauri uingie ndipo utakapojua mengi.

“Na kwa vile unagombea urais, hii ni nafasi muhimu kwako ya kupata urais. Kama tulivyokwambia kama utafuata misingi yetu uwezekano wa wewe kupata urais ni wa asilimia mia moja,” Lisha akaongeza.

Uwezekano wa kupata urais ni wa asilimia mia moja! Shanga aliwaza kwa mhangao.

Huku moyo wake ukianza kupata chembe za matumaini aliuliza.

“Sasa mtanisaidiaje ili niweze kupata huo urais?

“Ni mpaka uingie ndipo utakapouona msaada wetu,” alimjibu Lisha.

“Kuna masharti gani ya kujiunga?

“Hakuna masharti yoyote. Mtu yoyote anaruhusiwa kujiunga.

“Na ofisi zenu ziko wapi?

“Hapo utakapohitaji tutakupeleka.”

Shanga alibaki kimya kwa muda akiwaza kisha aliuliza.

“Niliwahi kusikia kuwa Freemaso ni aina ya dini na mnaabudu mashetani, ni kweli?

“Usisikilize maneno ya nje. Freemaso inasemwa kwa mengi yasiyo na ukweli. Ukweli halisi ni ule utakaoelezwa utakapoingia. Unajua Freemaso imeweka mkono katika chama chako bila wewe kujua?

“Mimi sijui kama Freemaso imeweka mkono katika chama changu, nyinyi ndio mnanieleza

“Mfadhili mkubwa wa chama chenu ni Freemaso!”

Shanga alishituka kidogo akawakazia macho Lisha na Bosco.

“Hebu niambie ni nani? Sisi tuna wafadhili wengi

“Yeye ni mfadhili mkubwa kuliko wote katika chama chako,” Lisha alimwambia.

“Mngenitajia jina lake niweze kumfahamu.

“Kama utakubaliana na sisi na utakuwa tayari kujiunga na jumuia yetu, tunaweza kuja naye kesho hapa kwako muda kama huu.

“Ni mfanyabiashara?

“Ndiyo ni mfanyabiashara. Huwezi kuamini kuwa kabla ya kujiunga na Freemaso alikuwa akiuza machungwa sokoni,” Lisha aliendelea kumueleza Shanga.

“Ningependa nimuone. Na kama mlivyosema mtakuja naye ni sawa isipokuwa nisingependa tukutane hapa nyumbani. Tutafute sehemu nyingine.

“Kama wapi?

“Kwenye hoteli yoyote.

“Ungependa tukutane hoteli gani?

“Pasific panafaa zaidi.

“Saa ngapi?

‘Tukutane saa mbili usiku”

“Sawa. Tutakuja hapo saa mbili usiku.

“Nitahamasika zaidi kama mtafika na huyo mfadhili wetu amabaye ni Freemaso.

“Tutafika naye.

“Nitafurahi kumuona na kumfahamu.

“Ni kina nani wale?” Joyce mke wa Shanga alimuuliza mume wake baada ya kuwatoa wageni hao walioondoka kwa benz jeusi.

“Ah! Ni wanachama wangu, wamemekuja kunipongeza kwa kuteuliwa kwangu kugombea urais,” Shanga alimdanganya mke wake. Hakutaka ajue kuwa watu hao walikuwa Freemaso.

Shanga hakujali kuona uso wa mke wake ukionesha mashaka, aliketi na kuwasha TV.

“Wakati niko jikoni nilisikia wakitaja neno Freemaso,” Joyce aliendelea kumwambia.

“Tulikuwa tunawazungumzia hao watu,” Shanga alisema huku macho yake yakiwa yameshughulika na TV. Ili kuzuia mke wake asiendelee kumdadisi alimwambia.

“Nataka kutazama taarifa ya habari.”

Joyce akaondoka kuelekea jikoni.

Ilimchukua Shanga muda mrefu kupata usingizi usiku wa siku ile. Akili yake ilikuwa ikiyatafakari yale maneno ya wale watu kwamba kama atajiunga na Freemaso uwezekano wa kupata urais ni wa asilimia mia moja.

Tatizo lake halikuwa kujiunga na Freemaso, tatizo lake lilikuwa ni kupata urais. Ndoto zake zilikuwa ni siku moja kuwa rais wa Jamhuri ya Kamisa.

Kama kujiunga na freemaso kutamuwezesha kupata urais, Shanga aliwaza, angekuwa tayari kujiunga na kundi hilo. Alichokuwa anahitaji ni kupata hakikisho kuwa kujiunga kwake na Freemaso hakutaingilia wala kuathiri shughuli zake za kisiasa. Pia Shanga alitaka kumjua mfadhili wa chama chake aliyedokezwa na watu hao. Alijiambia kama watamleta na mwenyewe akathibitisha kuwa ni freemaso, Shanga angekuwa tayari kujiunga na kundi hilo.

Asubuhi kulipokucha kama kawaida yake Shanga alifika ofisini kwake saa mbili asubuhi na kuendelea na shughuli zake za kila siku.