Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sitaki tena Urais – Sehemu ya 02

URAIS 02 Pict

UTANGULIZI

Alichokuwa anahitaji ni kupata hakikisho kuwa kujiunga kwake na freemaso hakutaingilia wala kuathiri shughuli zake za kisiasa.

Pia Shanga alitaka kumjua mfadhili wa chama chake aliyedokezwa na watu hao. Alijiambia kama watamleta na mwenyewe akathibitisha kuwa ni freemaso, Shanga angekuwa tayari kujiunga na kundi hilo.

Asubuhi kulipokucha kama kawaida yake Shanga alifika ofisini kwake saa mbili asubuhi na kuendelea na shughuli zake za kila siku.

SASA ENDELEA


Ilikuwa bado wiki moja tu kabla ya kuanza kwa kipindi cha kampeni, hivyo chama chake kilikuwa katika utaratibu wa kupanga ratiba za kampeni zake jijini humo.

Shanga alishughulika hadi saa nane mchana, alipoondoka ofisini na kurejea nyumbani.

Mnamo saa mbili usiku, alilisimamisha gari mbele ya Hoteli ya Pacific iliyokuwa katika mtaa mtulivu.

Wakati akishuka kwenye gari, aliona benzi jeusi nalo likiingia katika eneo la maegesho. Alifunga mlango wa gari kisha akageuka na kulitazama tena benzi hilo. Aliwaona watu watatu wakishuka. Kutokana na mwanga wa taa, aliweza kuwatambua watu walioshuka katika gari hilo. Wawili miongoni mwao walikuwa ni wale waliofika kwake usiku uliopita. Lakini mmoja alikuwa rafiki yake wa karibu sana.

Kama yeye alivyowaona, wao pia walikuwa wamemwona. Wakamfuata pale pale alipokuwa amesimama karibu na gari lake.

Wote walimsalimia na kupeana mikono.

“Tumefika kwa pamoja. Inaonekana nia yetu pia ni moja,” Lisha alimwambia Shanga, ambaye alikenua mdomo na kucheka kidogo.

“Ni kweli. Karibuni hotelini,” akawaambia.

Waliingia ndani ya hoteli, wakatafuta sehemu ya faragha na kuketi. Wakati wote, mawazo ya Shanga yalikuwa kwa yule mtu wa tatu ambaye alikuwa akimfahamu vyema. Alikuwa akijiuliza kwa nini mtu huyo alikuwa amefuatana na watu hao.

Mara tu walipoketi, Lisha alimuuliza Shanga kama alikuwa akimfahamu mwenzao waliyekuwa naye.

“Kwa kweli, si kwamba namfahamu tu, bali tunafahamiana vizuri. Ni rafiki yetu, ni mwenzetu na ni mtu muhimu katika chama changu,” Shanga aliwaambia.

“Naamini sikukosea nilipokuambia kuwa huyu bwana ni mfadhili mkubwa wa chama cha UM?”

“Ni kweli, na ndiyo sababu nikasema ni mtu muhimu katika chama changu.”

“Yeye ni Bwana Jacob Niwako. Ni mwenzetu, na ndiye tuliyekufahamisha jana kuwa tutafika naye.”

Shanga akaduwaa kidogo.

“Unajua, sikutegemea kuwa angekuwa ni yeye,” Shanga alisema huku akitabasamu. Kisha alimtazama Niwako mwenyewe na kutaka kumuuliza:

“Wewe ni…?”

Alitaka kumuuliza, “Wewe ni Freemason?” lakini hakumalizia sentensi yake.

“…Freemason!” Niwako akamalizia sentensi hiyo, akimkubalia.

“Wewe ni Freemason?” Shanga alimuuliza tena, kana kwamba hakuamini.

“Mimi ni Freemason, kama ulivyoambiwa.”

“Kweli?”

“Kweli kabisa. Tunakutaka ujiunge nasi. Tunakuhakikishia kuwa utakuwa rais wa jamhuri yetu.”

“Sasa, jamani, mtaniwezeshaje kupata urais?” Shanga aliuliza swali hilo huku akiwatazama kwa zamu Niwako, Lisha na Bosco.

Watu hao watatu walitabasamu na kutazamana, kana kwamba waliona Shanga alihitaji kuelimishwa.

“Mbona ni kitu rahisi tu?” Lisha akamjibu.

“Sisi tunao uwezo huo, na ni kwa asilimia mia moja. Pengine huwezi kuamini, lakini huo ndiyo ukweli,” Bosco akaongeza.

Shanga akamtazama Niwako ili kuona naye atasema nini.

“Ndugu yangu, ninakushauri ujiunge tu, halafu utaona mwenyewe,” Niwako alimwambia.

“Siwezi kuelezwa kabla?”

“Inakuwa ni siri yetu. Hatuwezi kuitoa nje.”

“Kabla ya kuwa na biashara zako, sasa, Bwana Niwako, ulikuwa unafanya biashara gani?”

Niwako alicheka kabla ya kumjibu.

“Huwezi kuamini kuwa nilikuwa nikiuza machungwa!”

“Unataka kuniambia kuwa Freemason ndiyo walikuwezesha?”

“Bila shaka.”

“Maisha yako yamekuwaje baada ya kujiunga na Freemason?”

“Maisha yangu yamekuwa mazuri sana.”

“Kuna sharti lolote la kujiunga ambalo unadhani litakuwa gumu kwangu?”

“Hakuna sharti lolote gumu. Unachotakiwa ni kuwa na maamuzi thabiti,” Niwako alimjibu.

“Sawa. Mimi nimekubali kujiunga kwa ajili ya kuwezeshwa kupata urais.”

“Tumefurahi kuwa umefikia uamuzi huo!” Niwako alimwambia huku akimpa mkono. “Ni uamuzi wa busara sana.”

Lisha na Bosco pia walimpa mkono.

“Tunakuhakikishia kuwa lengo lako litatimia,” Lisha alimwambia.

“Sasa nitajiunga wapi? Labda kuna fomu za kujaza?”

“Fomu zipo. Utazijaza ofisini kwetu na kuzikabidhi hapo hapo. Sisi tutakwenda kumuarifu kiongozi wetu usiku huu ili kesho usiku tukufikishe ofisini kwetu ukutane naye,” Lisha alimwambia Shanga.

“Ofisi zenu zipo sehemu gani?”

“Utazijua kesho.”

Kikao kikamalizika.

Wakati wanatoka hotelini, Shanga alimuuliza Lisha:

“Kwa hiyo, tutakutana wapi kesho?”

“Tutakujulisha kwa simu.”

Walipotoka nje ya hoteli, waliagana na kuachana. Shanga alielekea kwenye gari lake, na watu hao watatu wakaelekea kwenye gari lao. Walingoja Shanga aondoke. Alipoondoka, nao wakaondoka.

Siku iliyofuata, Shanga akiwa ofisini kwake, alipata wageni wawili waliojitambulisha kuwa wanachama wakereketwa wa chama hicho.

“Tulikuwa na ushauri wetu,” mmoja wa wanachama hao alimwambia Shanga.

“Ninakaribisha ushauri wenu.”

“Wewe sasa hivi ni mwari wa chama chetu, ambaye tunakutarajia uwe rais wetu. Kuna jambo moja tumeliona na, kusema kweli, halikutupa picha nzuri.”

“Ni jambo gani hilo?”

“Kuna hili kundi la Freemason ambalo limekuwa tishio kwa watu wengi. Watu wanatiliana shaka kwa kudhaniana kuwa ni Freemason!”

Shanga aliposikia neno Freemason, aligutuka kidogo.

“Wana nini hao Freemason?”

“Jana usiku tulikuona umekaa na watu fulani katika Hoteli ya Pacific. Mmoja wa watu wale anashukiwa kuwa Freemason!”

“Ni kweli, jana usiku nilikaa na watu watatu katika Hoteli ya Pacific. Lakini sijui kama mmojawapo anashukiwa kuwa Freemason. Ni yupi?”

“Ni yule aliyekuwa mwembamba na mrefu.”

“Anaitwa nani?”

“Hatujui jina lake, lakini anashukiwa kuwa Freemason.”

Shanga alitambua kuwa alikuwa Lisha. Ilimbidi ajitetee.

“Wale ni watu ninaofahamiana nao, na tulikuwa na mazungumzo ya kikazi.”

“Kwa kweli, sisi tulishtuka sana tulipokuona umekaa na mtu yule. Tunaamini kuwa yule ni Freemason. Wanachama wako wanaweza kukufikiria vibaya, mheshimiwa. Hili linaweza kukuathiri katika uchaguzi!”

Shanga alitulia kumsikiliza yule mtu. Alipomaliza, alimwambia:

“Nashukuru kwa kunifahamisha. Nilikuwa sijui kama yule mtu anadhaniwa kuwa Freemason.”

“Ni Freemason. Ukionekana naye mara kwa mara, watu watakushuku vibaya.”

“Ni kweli. Nitajitahidi kumuepuka. Lakini nataka niwafahamishe kwamba si kweli kuwa kila anayedhaniwa kuwa Freemason ni Freemason kweli!”

“Lakini mashaka ya watu tu yanatosha kukuharibia jina.”

“Tuko pamoja, ndugu zangu. Asanteni sana.”

“Asante na wewe kwa kutusikiliza.”

Watu hao wakamuaga Shanga na kuondoka. Walimuacha Shanga na lindi la mawazo. Alijiambia kuwa tangu ateuliwe na chama chake kuwa mgombea urais, wananchi walikuwa wakichunguza nyendo zake ili kupima tabia yake. Hakujua kama alipokuwa amekaa katika Hoteli ya Pacific akiwa na Lisha na wenzake, kulikuwa na watu waliokuwa wakimwangalia.

Kuhusu suala la kujiunga na Freemason, Shanga alijiambia kuwa ingembidi afikirie tena, kwani endapo ingefahamika kuwa alikuwa Freemason, angeweza kukosa kura zote isipokuwa kura yake na ya mke wake.

Akaendelea kujiambia kuwa, ingawa alitaka kujiunga na Freemason ili apate urais, kujiunga huko kungeweza kumharibia. Aligundua kuwa wananchi wengi waliwaona Freemason kama watu hatari.

Sasa afanye nini? Akajiuliza. Ni nani ambaye angemweleza ili ampe ushauri, wakati jambo hilo lilikuwa siri yake?

Saa nane mchana, akiwa ndani ya gari akirejea nyumbani kwake, alipokea simu kutoka kwa namba asiyoitambua.

“Halo!” akasema kwenye simu.

“Ndiyo, ni Lisha hapa. Habari za mchana, mheshimiwa?” Sauti ya Lisha ikasikika kwenye simu.

“Nzuri, Bwana Lisha. Unaniambiaje?”

“Tutakufuata saa mbili usiku, mahali pale pale pa jana usiku.”

“Pale hapafai. Tutafute mahali pengine.”

“Kwanini?”

“Watu wanatuona.”

“Wakituona itakuwa nini?”

“Wataanza kunitilia mashaka wakiniona na nyinyi. Jambo hili ninataka liwe siri.”

“Wanatujuaje?”

“Lisha, unafahamika.”

“Mimi ninajua kuwa kuna watu wawili waliofika ofisini kwako leo, wakakuambia maneno yaliyokutia hofu. Lakini uliwajibu vizuri.”

Shanga alishtuka.

“Ulijuaje?”

“Kujua mambo ni moja ya kazi zetu. Hilo lisikutie wasiwasi.”

“Ni kweli, kuna watu walikuja na kunieleza kuwa mimi ni Freemason, kwa hiyo si vizuri nionekane na wewe.”

“Hao watu utaonana nao leo usiku.”

“Wapi?”

“Katika huo msafara wetu.”

“Unajua, nilishapata mawazo tofauti?”