Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KISIWA CHAMAUTI - 29

KISIWA 29 Pict

ILIPOISHIA

“Yasmin unaweza kusema maneno hayo hapa kwa vile hatuna matumaini ya kupona. Lakini kama tutafanikiwa kuondoka hapa unaweza kubadilika na kuniona mimi kama takataka”

“Nakuhakikishia kaka yangu mpenzi sitabadilika. Mimi si kinyonga”

“Tuombe tuokoke katika balaa hili lililotukabili”

“Ishaalah tutaokoka. Tena wewe ndio utaniokoa mimi”

“Sio wewe uniokoe mimi?”

“Mimi nataka wewe uniokoe mimi”

SASA ENDELEA...


“Basi ishaala itakuwa hivyo unavyotaka.”

“Nikuimbie nyimbo?”

“Niimbie.”

Yasmin aliacha kutembea na kusimama mbele yangu akiwa amenigeukia. Kitendo hicho kilisababisha na mimi nisimame. Akapeleka mikono yake kwenye mabega yangu.

“Mimi ni nani wako?” akaniuliza huku akinitazama machoni.

“Wewe ni mpenzi wangu.” Nilijua kuwa alikuwa anataka jibu hilo.

Nilipomjibu hivyo, alitabasamu na kuishusha mikono yake mabegani mwangu, kisha akageuka.

“Sasa ngoja nikuimbie,” akaniambia huku tunaendelea kwenda.

Akaimba wimbo mzuri kwa lugha ya Kikomoro. Wakati akiimba, alikuwa akitingisha-tingisha kichwa chake kufuatia mawimbi ya sauti yake. Wakati akiimba, alikuwa akitia muziki kwa mdomo. Alionekana kuwa hodari sana wa kuimba na kutia muziki. Wimbo huo ulikuwa unavutia, ingawa sikujua tafsiri yake.

Alipomaliza kuimba, alinitafsiria kwa Kiswahili. Akaniambia, “Ndege wawili, dume na jike, wamepotea juu ya bahari. Hawajui watokako wala waendako. Wanalia swi! swi! swi!”

“Wamesafiri mchana kutwa bila kupata mahali pa kutua. Sasa jua limekuchwa na giza linaingia. Hawataweza kusafiri usiku. Wanalia swi! swi! swi!”

Japo niliufurahia wimbo huo, tafsiri yake ilinisisitisha. Nikahisi kama ndege wawili hao walikuwa ni mimi na yeye.

“Kumbe Yasmin, unajua sana kuimba!” nikamwambia.

“Hapana, najaribu tu.”

“Si kujaribu, unajua.”

“Kweli eh?”

“Umeniburudisha sana.”

“Ukinioa nitakuwa nakuimbia kila siku.”

Tulikuwa tumeshafika kwenye lile jumba analokaa.

Nikasimama kwenye mlango.

“Mimi sitaingia ndani,” nikamwambia.

“Kwanini?” Yasmin akaniuliza.

“Si nimekusindikiza tu.”

“Ukinisindikiza ndio huingii ndani? Mbona siku nyingine unaingia?”

“Yasije yakanikuta yaliyomkuta Masudi.”

“Mimi naamini wewe huko kama Masudi, lakini kama umeamua uwahi kurudi, unaweza kurudi na nakutakia usiku mwema. Tutaonana kesho.”

“Asante. Usiku mwema na kwako.”

Nikamuacha Yasmin amesimama akinitazama. Mimi nikarudi kule nyumbani tulikotoka. Nilirudi kwa mwendo wa haraka-haraka ili kiza kisinikute njiani, kwani jua lilikuwa limekuchwa sana.

Nilijikuta nikiwa na furaha na mwenye matumaini kutokana na maneno ya Yasmin. Upendo aliouonyesha kwangu ulitosha kunipa hamasa, ingawa tulikuwa katika hali ngumu.

Nilipofika katika ile nyumba, niliwakuta wenzangu tayari wameshaanza kupata wasiwasi.

“Ilibaki kidogo tu tukufuate, kwa maana tuliona unachelewa,” Haji akaniambia.

“Mlijua na mimi nimeshakwenda na maji?” nikawatania.

“Si ajabu. Haa, tunahesabiana siku na saa tu.”

“Tusikate tamaa kiasi hicho. Sisi ni wanaume. Mmeshakula?”

“Tulikuwa tunakusubiri wewe,” Shazume akaniambia.

“Mimi nimeshakuja. Toeni chakula tule.”

Chakula kikatolewa. Tukakaa chini na kuanza kula.

Tulipomaliza kula, tulikaa uani, tukawasha moto na kuuzunguka. Kiza kilikuwa kimeshaingia na kulikuwa na baridi.

Tuliota moto hadi majira ya saa mbili usiku. Tukaingia vyumbani kulala. Usiku ule haukuwa wa mawazo sana. Nilipitiwa na usingizi mara moja.

Nilipoamka asubuhi, nilishituka nilipoona mlango wa nje ulikuwa umeng’olewa mzima mzima. Palibaki uwazi mtupu. Mlango wa chumba alicholala Haji pia ulikuwa umeng’olewa. Mlango wa chumba cha Shazume ulikuwa umefungwa.

Nikaenda katika ule mlango wa chumba cha Haji na kuchungulia. Nilimkuta Haji akiwa amelala chini amekufa. Kichwa chake kilikuwa kimetobolewa kwenye utosi. Damu iliyoganda ilionekana kwenye nywele zake.

Hapo nilijua kuwa tulikuwa tumeingiliwa. Bila shaka Harishi alikuwa amekuja usiku, akang’oa milango na kumuua Haji.

Lilikuwa tukio ambalo sikulitegemea. Katika kundi letu, Haji ndiye aliyekuwa mdogo kuliko sote. Kifo chake kilinisikitisha na kunikatisha tamaa kabisa.

Nilijiambia kama Harishi ameweza kutufuata huku na kumuua Haji, na sisi hatutabaki. Tulichokuwa tunasubiri ni siku na saa zetu ziwadie.

Baada ya kushangaa kwenye mlango kwa sekunde kadhaa, nilikwenda kumgongea Shazume. Shazume akaamka na kufungua mlango.

“Una habari gani?” nikamuuliza nikiwa nimetaharuki.

“Sina habari yoyote,” Shazume akanijibu huku akionyesha kupata hofu.

“Haji ameuawa!” nikamwambia.

Shazume akagutuka.

“Haa! Haji naye ameuawa? Si tulilala naye humu ndani jana usiku?”

“Tazama ule mlango wa nje.”

Nilimuonyesha Haji ule mlango uliong’olewa, kisha nikamwambia, “Harishi ameung’oa usiku.”

Shazume aliutazama huku akitikisa kichwa.

“Ameng’oa na mlango wa chumba cha Haji,” nikaendelea kumwambia.

Shazume akasogea kwenye mlango wa kilichokuwa chumba cha Haji. Alipoiona maiti ya Haji, alishituka sana.

“Mimi naona hatutapona.”

“Kupona tusitegemee, ndugu yangu. Harishi ameshajua tupo hapa, usishangae kesho tukiamka mmoja wetu akawa hayupo!”

“Hapa nyumbani hapafai tena kukaa. Tutafute sehemu nyingine ya kujificha.”

“Tutajificha wapi, Shazume?”

“Popote tu, nyumba ziko nyingi.”

“Sawa. Tumngoje Yasmin aje, tumueleze kuwa mwenzetu ameuawa.”

“Pia tumueleze kuwa tunaondoka hapa. Harishi akija tena asitukute.”

“Sawa, tutamueleza.”

Tukaenda kunawa uso na kusukutua maji bila kupiga mswaki. Tulikuwa tumeshachanganyikiwa. Tulipomaliza, tulikaa kumsubiri Yasmin.

Yasmin alikuja majira ya saa tatu hivi. Hakuwa amechukua kitu.

Akatusalimia na kutuuliza kwanini tumeng’oa milango.

“Hebu chungulia kwenye hicho chumba,” nikamwambia.

Yasmin akachungulia na kugutuka.

“Haji amepatwa na nini?”

“Haji ameuawa usiku na Harishi,” nikamwambia.

“Mama yangu!” Yasmin alimaka huku akijishika kichwa. “Kumbe Harishi alipotoka usiku alikuja huku?”

“Sisi tumeona asubuhi Harishi ameuawa na milango imeng’olewa.”

“Sasa tumepanga tuondoke hapa,” Shazume akamwambia Yasmin.

“Muondoke muende wapi?”

“Twende mahali pengine. Tukiendelea kukaa hapa, Harishi atakuja tena usiku.”

“Sasa mmepanga muende wapi?”

“Mimi naona kama tunajisumbua. Kama ni kufa tutakufa tu,” nikasema.

“Hata kama tutakufa, lakini hapa tuondoke,” Shazume akasisitiza.

“Ni sawa. Sasa tufikirie hapo pa kwenda. Tutakwenda wapi?”

“Nyumba ziko nyingi.”

“Yasmin, unatushauri nini?”

Machozi yalikuwa yanamtoka Yasmin. Bila shaka yalimtoka kutokana na ukweli kwamba sote tutakufa. Hakunijibu.

“Yasmin, usilie. Tunaomba ushauri wako,” nikamwambia.

Yasmin alijifuta machozi, kisha akatuambia, “Niwapeleke katika nyumba nyingine.”

“Huko utakakotupeleka Harishi hatafika?” nikamuuliza.

Yasmin akaguna, kisha akajibu, “Hatafika.”

Nilijua alitujibu hivyo kututia moyo tu, lakini mawazo ya Shazume yalikuwa tofauti.

“Ni mahali gani?” Shazume akamuuliza haraka.

“Kwanza twendeni mkanywe uji.”

“Turudi kule tena?” Shazume akamaka.

“Mnakunywa uji tu, halafu tunaondoka.”

Shazume akanitazama.

“Mimi sitakwenda.”

“Si tunakwenda kunywa uji tu?” nikamwambia.

“Kwanza, Harishi hatakuja muda huu,” Yasmin akasema.

“Mimi sitaki uji.”

“Utashinda hivyo hivyo na njaa?” Yasmin akamuuliza.

“Sioni njaa na ile hamu ya kula pia sina.”

“Kama tumeandikiwa kuuawa, tutauawa tu, Shazume. Hata kama hutakula, ni bora ule tu,” nikamwambia Shazume.

Shazume akatikisa kichwa bila kusema lolote.

“Kakangu, najua umepatwa na fadhaa, lakini tumbo lako likipata riziki ndio akili itakuja,” Yasmin akamwambia Shazume.

“Tulikuwa watu saba, sasa tumebaki wawili tu, bado nile? Sitakula!”

“Wewe ni mwanaume, Shazume, usiogope kula. Unatakiwa upambane mpaka dakika ya mwisho. Mnaweza kuokoka, ndugu zangu. Msikate tamaa kiasi hicho. Twende ukanywe uji japo kidogo!” Yasmin alimwambia.

Shazume akakubali kwenda. Tukaondoka sote kwenda kwa Yasmin. Ile maiti ya Haji tuliiacha pale pale. Tangu wenzetu walivyoanza kuuawa, hatukuzika maiti yoyote. Zote tuliziacha ziliwe na kunguru.

Kwa hisia zetu, tulikuwa kama watu tuliokuwa vitani. Akifa mtu, hakuna kuzika. Kuzika kuna utaratibu wake ambao, kutokana na hali tuliyokuwa nayo, tusingeuweza.

Tulipofika kwa Yasmin, alituandalia uji tukanywa. Mimi nilikunywa vikombe viwili, Shazume alikunywa kikombe kimoja.

Wakati tumepumzika, Shazume akawa anahimiza tuondoke.

“Tumeshakunywa uji, sasa tunaweza kwenda.”

“Tusubiri kidogo, nifikirie pa kuwapeleka,” Yasmin akamwambia. Baada ya kusubiri kwa muda kidogo, Yasmin akatuambia, “Haya, twendeni tukatafute nyumba nyingine.”

Tukatoka na Yasmin. Niliona wazi kuwa Yasmin alikuwa na wasiwasi. Alikuwa akitupeleka katika nyumba nyingine, lakini hakuwa mtu aliyeonyesha matumaini.