Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KISIWA CHAMAUTI - 27

KISIWA 27 Pict

ILIPOISHIA

“Mke si nilishamuacha?. Au wewe ulikuwa hujui?”

“Mimi najua watania tu lakini mke bado unaye”

“Basi na yaishe. Mimi niliuliza tu kutaka kujua. Kama unaye mke au huna hakuna tatizo” Yasmin akaingilia kati.

“Huyu bwana mdogo anapenda sana kuniingilia!” Masudi akaunguruma.

Nikaamua kunyamaza.

“Nimesema yaishe jamani. Ngoja tulete karata tucheze”

Yasmin alitumia hekima kuyageuza yale mazungumzo akaenda kuleta karata, tukawa tunacheza.

SASA ENDELEA...


“Hivi hizi karata ulikuwa unacheza na nani?” nikamuuliza Yasmin wakati tunacheza.

“Ninacheza na huyo aliyezileta.”

“Harishi?”

“Ndiye huyo huyo. Anapoona nimepooza, ananiambia kalete karata.”

“Anajua kucheza karata?” akauliza Masudi.

“Anajua. Hawa majini ni kama watu tu. Tofauti yetu ni ndogo sana. Wanafanya mambo mengi wanayofanya binadamu.”

Mazungumzo ya Harishi yalitufanya tukose amani. Yalitukumbusha wenzetu waliouawa. Mwenzetu mmoja, ambaye si Masudi, akatuambia:

“Tuondoke, twende kule tulikohamia.”

“Chukueni hizo karata, mwende nazo. Mtakwenda kucheza huko huko,” Yasmin akatuambia.

Ilibidi tuondoke twende katika ile nyumba, lakini Yasmin tulimuacha.

Tulipofika, tuliendelea kucheza karata. Baadaye sote tulipitiwa na usingizi tukalala.

Tuliamshana jioni tukaamua tutoke twende tukatembee-tembee. Tulizunguka sana katika kile kisiwa. Tulienda pia kuliangalia jahazi letu. Tuliporudi, jua lilikuwa limeshakwisha kuchwa.

Tulimkuta Yasmin akitusubiri. Alikuwa ametuletea chakula cha jioni.

“Mnatoka wapi?” akatuuliza.

“Tulikwenda kutembea-tembea kidogo,” Masudi akamjibu na kuongeza, “Kukaa tu kunachosha.”

“Umetuletea chakula?” nikamuuliza Yasmin.

“Nimewaletea kabisa. Ikifika usiku, sitaweza kuja huku. Harishi anaweza kuja wakati wowote,” Yasmin alituambia na kutuwekea chakula hicho juu ya meza.

“Ngoja nikusindikize,” Masudi akawahi kumwambia Yasmin. Nilijua alitaka kunipiku mimi, kwani alijua mimi ndiye ningemsindikiza.

Yasmin akakubali kuondoka na Masudi. Kwa upande wangu, kitendo kile cha Masudi nilikiona kama ulimbukeni uliopitiliza na kutaka kujipendekeza kwa Yasmin.

Walipoondoka, sisi tulikaa barazani mwa ile nyumba hadi giza likaingia.

“Mbona Masudi harudi?” tukawa tunaulizana.

Kusema kweli, kitendo chake cha kuchelewa kurudi kilinikera. Nikaamua nimfuate peke yangu nijue alikuwa anafanya nini muda wote huo.

Nikaenda huku nikiwa na hasira. Nilipofika, sikuingia ndani. Niliamua kufanya upelelezi kwa kuchungulia kwenye madirisha.

Wakati nachungulia, nilianza kusikia sauti ya Yasmin ikiwa katika dhihaka, mwenyewe sikumuona. Nilibadilisha dirisha na ndipo nilipowaona wote wawili. Masudi alikuwa akikimbizana na Yasmin mle ndani kama waliokuwa wakicheza. Wakati mwingine Masudi alimkamata Yasmin na kuanguka naye chini akiwa amemshika kiuno.

“Kumbe wana mchezo huu, ndiyo maana amesahau kurudi,” nikajisemea kimoyomoyo.

Licha ya moyo wangu kuuma, nilijiambia chaguo la Yasmin ni mimi, Masudi alikuwa akijipendekeza tu.

Macho yangu yaliwashuhudia wakiwa wamelala chini. Masudi alikuwa kama akimbembeleza kitu Yasmin. Yasmin alikuwa ametulia akimsikiliza.

Sikuweza kufikiria chochote zaidi ya kuhisi kuwa Masudi alikuwa akimtongoza Yasmin na alikuwa akinifitini mimi.

Sikutaka tena kuuona upumbavu wake. Nikaamua kuondoka, kwani usiku ulikuwa unazidi kushamiri.

Yasmin hawezi kumkubali Masudi, Yasmin amenipenda mimi, nilijiambia kujifariji wakati naondoka.

Nilirudi kwa wenzangu huku nikiuzuia moyo wangu usitaharuki kutokana na kitendo kile cha Masudi kumkumbatia Yasmin.

“Umemkuta?” wenzangu wakaniuliza.

“Sikufika,” nikawadanganya. “Nimeamua kurudi njiani, naona usiku mwingi huu.”

“Au twendeni sote?” mmoja akaniuliza.

“Tumsubirini tu hapa hapa.”

Sikutaka kuwambia ukweli kuwa nilimkuta akifanya vitendo vya kipuuzi. Nilihisi wangeweza kuja kumwambia mwenyewe, halafu kwa akili za Masudi tunaweza kugombana bure.

Tukakaa kumsubiri hadi saa tatu. Tulipoona hatokei, tuliamua kula chakula na kumbakishia chake.

Nilikuwa nimebaki na wenzangu wawili, Shazume na Haji. Kwa upande wangu, nilishakijua kilichokuwa kinamchelewesha Masudi, lakini wenzangu walikuwa na wasiwasi kwamba huenda Masudi amepata matatizo.

Walikuwa wakisisitiza kuwa twende tukamuangalie.

“Kutoka usiku huu si vizuri,” nikawaambia. “Acheni tungoje kesho asubuhi, tutakwenda kumuangalia.”

“Kaka Masudi ana matatizo sana. Kwanza hatuelewi ni kitu gani kilichomfanya amsindikize yule msichana,” Shazume akasema.

“Tusiwe na wasiwasi naye sana. Huenda mwenyewe ameamua kubaki,” nikawambia wenzangu.

“Atabakije kule wakati anajua kuwa lazima Harishi atakuja?” Haji akauliza.

“Kila mtu ana akili yake, jamani. Tusimuhukumu,” nikawambia Shazume na Haji.

“Atajua mwenyewe, shauri yake,” ilikuwa sauti ya kukata tamaa ya Haji.

Baada ya kujadiliana kwa kirefu, tuliamua kwenda kulala. Kila mtu aliingia kwenye chumba chake.

Unapofika wakati wa kulala, mawazo hubadilika. Fikira zote huondoka na kichwa kujaa mawazo ya Harishi.

Nilikuwa na hakika kuwa sikuwa mimi peke yangu, bali wenzangu wote walikuwa na mawazo kama yangu. Lakini hatukuwa na lolote la kufanya zaidi ya kukubali matokeo yatakayotokea usiku huo kwa Masudi.

Usiku ule tulilala na kuamka salama, ingawa tulilala kwa mashaka.

Lakini Masudi hakuwa miongoni mwetu. Tukadhani kwamba atatokea wakati ule wa asubuhi baada ya kushindwa kurudi usiku. Lakini tulikaa hadi majira ya mchana bila kumuona yeye wala Yasmin.

“Wenzangu, mnaonaje twende tukamuangalie Masudi au tuendelee kumsubiri?” nikawauliza wenzangu.

“Kwenda kumuangalia ni jambo zuri, lakini tunaweza kukutana na Harishi,” Haji akasema.

“Nina wasiwasi kwa sababu Yasmin pia amekaa kimya. Kwa kawaida muda huu angekuwa ameshakuja,” nikawambia wenzangu.

“Hatuwezi kujua, lolote linaweza kuwa limetokea,” Shazume naye akasema.

“Basi tusiende, tuendelee kusubiri hapa hapa hadi atakapokuja Masudi au Yasmin,” nikawambia.

Wakati tunaendelea kujadiliana, tulimuona Yasmin akiingia. Sote tukageuka na kumtazama. Kitu kilichotushitua si tu alikuwa peke yake, bali macho yake yalikuwa mekundu yaliyoonesha alikuwa analia.

Akatusalimia na kutuambia kuwa amepatwa na fadhaa.

“Kwanini?” akatuuliza.

“Kaka yenu Masudi hakutumia busara hata kidogo,” Yasmin alituambia huku akitikisa kichwa kwa kusikitika.

“Kwanini hakutumia busara?” nikamuuliza huku nikifikiria mengine. Nilifikiria ama Masudi alitaka kumbaka Yasmin au alimbaka, kwani ile hali niliyowakuta nayo usiku uliopita haikuwa ya kawaida.

“Kama yeye amenipenda mimi kama alivyoniambia mwenyewe ni sawa, lakini kitendo alichokifanya si kizuri kwa sababu anajua mimi nimemilikiwa na Harishi.”

Hapo nilijua moja kwa moja kuwa Masudi amembaka Yasmin na ndiyo sababu alikuwa analia.

“Kwani amefanya nini?” nikamuuliza.

“Ungetueleza alichofanya,” Haji naye akamwambia.

“Jana usiku nilimwambia arudi huku, ulikuwa ni usiku. Lakini alikataa kurudi, akataka kulala na mimi. Nilimsihi sana arudi, lakini aligoma kabisa, tena alitaka alale na mimi chumba kimoja. Aliniambia ananipenda,” Yasmin akatueleza.

“Masudi ni kaka yetu, lakini ana matatizo sana,” Shazume akadakia.

“Sasa ikawaje?” na mimi nikauliza kwa pupa.

“Nilimuachia alale. Yule ni mwanaume, nisingeweza kumzuia.”

“Ulilala naye chumba kimoja?” nikamuuliza.

“Nilimuomba sana akalale chumba kingine kwa usalama wake. Nilimwambia Harishi akija na kukukuta atakuua. Akakubali kwenda kulala chumba kingine.”

“Sasa nini kimetokea?” Shazume akauliza.

“Harishi alikuja muda ule ule, akamkuta ukumbini anazungukazunguka, akashikwa.”

Alipofikia hapo, Yasmin alianza kulia.

“Sasa ameuliwa?” nikamuuliza.

“Harishi aliacha mtu siku gani?” Yasmin akaniuliza.

Mimi na Haji na Shazume tulitazamana tukiwa tumeacha midomo wazi.

“Aliyataka mwenyewe!” Yasmin akasema.

“Ni kweli aliyataka mwenyewe, kifo kilikuwa kinamuita,” nikamuunga mkono.

“Angekuja kulala na wenzake, pengine angenusurika,” Yasmin aliendelea kutuambia.

“Mbona hukuja mapema kutuambia?” nikamuuliza.

“Harishi ameondoka sasa hivi. Jana usiku alipokuja alikuwa amelewa na alipomuua Masudi hakuondoka tena hadi hii asubuhi.”

“Kumbe majini pia wanalewa?”

“Wanalewa kama watu. Harishi analewa sana.”

“Hiyo pombe anaipata wapi?”

“Sijui mwenyewe.”

“Na anapokuta mtu mle ndani, anakuuliza ni nani?”

“Anaua kwanza, halafu ndiyo anauliza. Mimi humwambia kwamba ni wavuvi wameingia kwa bahati mbaya. Lakini kama angenikuta nimelala naye, angejua ni mwanaume wangu.”

“Angekuua?”

“Sijui ingekuwaje?”

Pakapita kimya cha sekunde kadhaa. Sote tulikuwa tukimkumbuka kaka yetu Masudi.

“Mtanisamehe, sikuwaletea chai. Nilikuwa nimetaharuki sana,” Yasmin akatuambia baadaye.

“Misiba kama hii, kila siku anakufa mtu. Hamu ya kula pia inapotea,” nikamwambia.