KISIWA CHAMAUTI - 24
ILIPOISHIA
“Kwani Harish ameshaenda zake?” Mtu mmoja akamuuliza Yasmin.
“Ameshaondoka” nikamjibu mimi. “Angekuwepo Yasmin asingeweza kuja huku”
Tulikula pilau ikiwa ndani ya kapu. Tukashiba na kupata nguvu.
“Nimesahau kuwachukulia maji ya kunywa” Yasmin akatuambia.
“Na maji tuliyokuwa nayo yamekwisha” nikasema.
“Lakini kwa leo Harishi hatarudi, mnaweza kuja nyumbani” Yasmin akatuambia.
SASA ENDELEA...
“Mh! Nyumbani kwako kunaogopesha,” nikamwambia Yasmin.
“Tunaweza kwenda kunywa maji, halafu mtarudi huku huku.”
Tukajadiliana na Yasmin, mwisho tukaamua turudi katika lile jumba. Tukarudi.
Tulipofika, alitupatia maji ya kunywa. Tukamshukuru kwa wema wake.
“Bado mna wasiwasi?” Yasmin akatuuliza.
“Kuwa na wasiwasi ni lazima,” nikamjibu na kuongeza. “Tunajiona kama tuko kwenye vita.”
“Kwa leo msiwe na wasiwasi. Yule jini hatarudi tena. Kama ni kurudi, ni kesho. Tunaweza kukaa tukaongea hadi usiku, mkaenda zenu.”
Tukashauriana na kukubaliana tukae hadi usiku, kwa vile mwenyeji wetu ameshatuhakikishia kuwa tutakuwa salama. Pia tulikuwa tunamuhurumia Yasmin aliyekuwa mpweke katika jumba lile. Tukaona tukae tumchangamshe.
Tukakaa kwenye ule ukumbi pamoja na Yasmin na kuanza kuzungumza.
Yasmin alitupa hadithi ya jinsi alivyofikishwa katika jumba lile na jinsi alivyokuwa akilia katika siku za mwanzo mwanzo.
“Lile jini hata ukilia, halijali. Linakwambia utazoea tu. Na ni kweli, kadiri siku zilivyokwenda, nilijikuta nikizoea,” Yasmin aliendelea kutuhadithia.
“Sasa mnaishije, wakati wewe ni mtu na yule ni jini?” Mwenzetu mmoja akamuuliza.
“Tunaishi kama mke na mume, ingawa mwenzangu ni jini, lakini ndio nimeshamzoea. Ameshaniambia kwamba nitaishi naye hadi kufa kwangu.”
“Je, kama akifa yeye?” nikamuuliza.
“Amesema yeye hatakufa haraka. Umri wa majini ni mrefu sana. Pale alipo ana miaka mia tatu na anaweza kuishi hadi miaka mia tano.”
“Loh! Wewe utakufa, yeye ataendelea kuishi kwa miaka mingi sana,” mtu mmoja akamwambia Yasmin.
“Lakini mimi ningependa kujua hisia zako. Unajisikiaje unapohisi kuwa utaishi ndani ya jumba hili hadi ufe, wakati bado ni msichana mdogo?” Mimi nilimuuliza Yasmin swali hilo.
Yasmin akabetua mabega.
“Nasikia vibaya, lakini nitafanyaje sasa? Nimelia, nimechoka, sasa silii tena.”
“Kwa hiyo ndio unaishi ukisubiri kifo chako kitokee humu humu ndani?” Mtu mwingine alimuuliza. Lilikuwa si swali zuri. Sikulipenda. Lakini Yasmin alimjibu.
“Wakati mwingine najidanganya kwamba iko siku yaweza kutokea miujiza nikaokolewa kwa namna nisiyoijua.”
“Na tangu uishi humu, hakujatokea watu kama sisi wakaingia katika jumba hili?” nikamuuliza.
“Nyinyi ndio watu wa kwanza kuwaona tangu nianze kuishi katika jumba hili.”
Tukaendelea kuzungumza na Yasmin hadi alipotuambia kuwa anakwenda kupika chakula cha usiku.
Tukabaki sisi peke yetu na kuendelea kuzungumza na kujadiliana kuhusu maisha ya Yasmin na maisha yetu wenyewe.
Jua lilipokuwa limechwa, nilimfuata Yasmin jikoni nikamwambia kwamba tunaondoka.
“Kwanini… subirini mle chakula. Nimepika chakula kingi kwa ajili yenu,” Yasmin akaniambia.
“Giza linaingia. Tuna hofu yule jini anaweza kutokea. Acha tuondoke tu.”
“Jamani, mkiwepo mnanichangamsha na mimi. Sasa mnataka kwenda wapi?”
“Tunarudi kule kule ulikotukuta.”
“Kwanini, jamani? Nimewambia Harishi hawezi kurudi leo, labda kwa kesho. Mnaweza hata kulala hapa na mkawa salama. Muhimu ni kuamka kabla hakujapambazuka, mwende zenu.”
“Unajua tuna hofu na wasiwasi, wenzetu wawili wameshauawa humu humu ndani.”
“Sasa kule mtakaaje usiku huu na baridi? Je, mvua ikinyesha usiku huu mtafanyaje? Si bora mlale hapa hapa?”
“Ngoja nikawashauri wenzangu,” nikamwambia Yasmin na kurudi kule ukumbini. Yasmin naye akanifuata.
“Yasmin amesema tusubiri chakula na pia tunaweza kulala hapa hapa,” nikawambia wenzangu.
“Tulale hapa hapa?” Mtu mmoja akaniuliza kwa mshituko.
“Hakuna neno. Mnaweza kulala tu ilimradi muamke alfajiri kabla ya kupambazuka, mwende zenu,” Yasmin akawambia.
“Una hakika kwamba Harishi hatakuja usiku huu?”
“Hatakuja tena kwa leo, ila kesho anaweza kuja. Sasa kwa vile sijui atakuja saa ngapi, ndio maana ninawambia muondoke alfajiri.”
Yasmin alipoona wenzangu wameduwaa wakitazamana kutafakari yale maneno yake, akatuambia.
“Jamani, kuweni na mimi. Hivi nashukuru kupata wenzangu wa kunichangamsha. Harishi hatakuja tena leo.”
“Mimi naona tumsikilize mwenyeji wetu, acha tukae,” nikawambia wenzangu kwa kumuonea huruma Yasmin.
Pia huko tulikotaka kwenda hakukuwa salama. Tungeweza kushambuliwa na wanyama usiku ule au kunyeshewa na mvua.
Tukakubaliana kuwa tubaki na Yasmin.
“Hakuna lolote litakalotokea, kaeni kwa roho moja. Mimi ndiye ninayejua kawaida na nyendo za Harishi. Mnachotakiwa ni kujihimu wakati wa alfajiri, muondoke humu ndani ili kama kesho atatokea asiwakute,” Yasmin akatusisitizia kabla ya kurudi jikoni.
Baada ya muda kidogo alituletea chakula, tukala pamoja na yeye.
Tulipomaliza kula, Yasmin aliondoa vyombo. Aliporudi tena alikuwa ameshika karata. Akaketi na kutuambia, “Sasa tucheze karata, tukichoka tunakwenda kulala.”
Akagawa karata, tukacheza hadi usiku mwingi. Wenzangu wengine walikuwa wameshaanza kusinzia. Tukavunja mchezo na kwenda kulala.
Tuliingia katika vyumba viwili. Chumba kimoja waliingia watu wawili na chumba kingine waliingia watu watatu. Mmoja aliweka godoro chini. Mimi nilikuwemo katika kile chumba walichingia watu watatu. Nililala kitandani. Na mwenzetu mmoja ndio alilala chini.
Licha ya Yasmin kututoa wasiwasi kuwa Harishi hatatokea usiku ule, hatukulala kwa raha. Mara kwa mara nilikabiliwa na hofu. Nilipolala kidogo, nilijikuta ninagutuka na kutupa macho huku na huku.
Wakati inakaribia kuwa alfajiri ndipo nilipopata usingizi wa uhakika. Nikalala moja kwa moja.
Sikuzinduka mpaka kumekucha. Kilichonizindua ni hisia zangu. Niliona kama mlango wa mle chumbani unafunguliwa na mtu aliyekuwa nje.
Nilipofumbua macho, niliona kweli mlango unafunguliwa na kulikuwa kumeshakucha, ingawa Yasmin alituambia tuamke alfajiri na kuondoka.
Nikajiuliza ni nani anayefungua mlango. Nikaona kanzu yenye madoa ya damu ikiingia ndani.
Alikuwa Harishi!
Nilishituka sana nilipogundua kuwa aliyefungua ule mlango alikuwa ni jini Harishi. Tulipaswa kujilaumu kwa uzembe wetu wa kulala hadi muda ule, wakati Yasmin alituambia tuondoke kabla hakujapambazuka.
Na kwa kweli haukuwa uzembe, bali tulipitiwa na usingizi, tena wakati mimi nazinduka wenzangu wote walikuwa bado wamelala.
Harishi aliingia ndani ya kile chumba. Sasa niliweza kuuona vizuri uso wake. Alikuwa na macho makubwa yenye makengeza.
Nikajifanya kama nimelala, lakini nilikuwa nikimuangalia kwa pembeni huku mwili wangu ukitetemeka kwa hofu.
Pengine ni kutokana na yale makengeza yake, Harishi alipoingia mle chumbani macho yake yalikwenda kwa yule mtu aliyelala chini.
Mara moja aliinama na kumshika shingo yake, kisha akamuinua na kutoka naye ukumbini.
Nikaisikia sauti ya Harishi akiuliza.
“Hii nyumba ni yako?”
Sikusikia jibu, bali nilimsikia mwenzetu akipiga ukelele mmoja tu.
“Jamani, nakufa!”
Halafu sikusikia kitu tena.
Hapo nilijua mwenzetu huyo alikuwa ameshatobolewa utosi na alikuwa akifyonzwa damu.
Ule ukelele aliopiga ulimwamsha mwenzangu niliyelala naye. Akainuka na kuketi kitandani.
“Kitu gani?” akaniuliza.
Nikaweka kidole changu cha shahada kwenye midomo yangu kumkataza asitoe sauti.
“Nini kwani?” Sasa sauti yake ilikuwa ya chini. Uso wake ulikuwa umeanza kushituka.
Nilishuka kitandani nikamnong’oneza, “Harishi!”
Akagutuka. Uso wake ukabadilika na kuvamiwa na hofu.
“Yuko wapi?” akauliza kipumbavu.
Sikumjibu. Nikamwambia, “Tuingie mvunguni mwa kitanda.”
Akakurupuka na kujiingiza kwenye mvungu huku akiburuza shuka aliyokuwa amejifunika. Tulipoingia kwenye mvungu huo, tukanyamaza kimya.
Tuliamua kujificha humo, japokuwa hatukuwa na uhakika kuwa tutapona. Baada ya muda kidogo tuliona mlango unafunguliwa tena.
Nilimuona mwenzangu anatikisa kichwa kwa hofu. Tuliona miguu ya Harishi ikiingia. Ilikuwa miguu mikubwa iliyochafuka na yenye vidole vyenye kucha ndefu. Ilikuwa pekupeku.
“Kumbe alikuwa ni yule peke yake!” Tukamsikia akisema. “Peke yake.”
Ile shuka ya mwenzangu aliyokuwa akiiburuza ilitokeza nje ya mvungu wa kitanda. Harishi akaiona!
Tukaona mkono wake ukishika ncha ya shuka na kuivuta. Jamaa akaiachia. Shuka yote ikavutwa na kuchukuliwa na Harishi.
“Hizi ni shuka zangu ninazoziiba kwa Wahindi. Imewekwa na nani huku mvunguni?” akajiuliza mwenyewe, kisha akaitupa chini.
Tukaona miguu inageuka na kutoka. Alipotoka, tulishukuru. Mimi nilitambaa hadi kwenye mlango, nikaufungua na kumchungulia.