Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KISIWA CHA MAUTI - 23

KISIWA 23 Pict

ILIPOISHIA

“Nyinyi mna bahati sana. Angeweza kushikwa mmojawenu…” nikawa nayakumbuka maneno ya Yasmin huku mwili ukinisisimka kwa hofu.

Mara kwa mara nilikuwa nikitupa macho kila upande wa chumba hicho kwa hisia kwamba Harishi angeweza kutokea mle chumbani.

Asubuhi kulipokucha Yasmin alikuja kutugongea mlango.

“Amkeni. Kumeshakucha” Alikuwa akituambia wakati akigonga. Tukatambua kuwa alikuwa ni yeye.

SASA ENDELEA...


Tukafungua mlango.

“Mmeamkaje?” akatuuliza.

“Tunashukuru tumeamka salama,” nilimjibu kwa niaba ya wenzangu.

Wenzetu waliolala chumba kingine hawakuwa na habari ya tukio lililotokea usiku. Nikawaeleza mbele ya Yasmin. Wakasikitika sana na kupata hofu.

“Sasa nendeni mkaoge, halafu niwaandalie chai,” Yasmin akatuambia.

Tukaenda kuoga. Kwanza waliingia watu wanne, kwa vile vyoo vilikuwa vinne. Walipotoka, nikaingia mimi na mwenzangu.

Yasmin akatuandalia chai pale sebuleni. Ilikuwa chai iliyotengenezwa kwa maziwa ya unga na iliyoungwa kwa iliki, tangawizi na mdalasini. Pia alitupa mikate iliyotengenezwa kwa mayai.

Yeye mwenyewe alikunywa chai pamoja na sisi. Nikamuona amefurahi na kuchangamka, licha ya kwamba usiku wa jana yake tu tulishuhudia machungu ya kuuawa kwa mwenzetu.

“Ningekuwa nakula na wageni kila siku namna hii ningechangamka, lakini mh!” Yasmin alisema kama aliyekuwa akisema peke yake.

“Ni kweli, Yasmin, lakini tutafanyaje? Tunapenda kukusaidia, lakini hatuna uwezo. Kama hivyo umeona mwenzetu ameshauawa na sisi hatujui maisha yetu yatakuwaje!” nikamwambia Yasmin kwa huzuni.

“Kusema ukweli, napenda niendelee kuwa na nyinyi hapa ili nipate wenzangu wa kuzungumza nao. Lakini haitawezekana nyinyi muwepo hapa mkiwa hai.”

“Na pia hatuna mahali pengine pa kwenda,” nikamwambia Yasmin.

“Huu ni mtihani. Sijui mtatumia mbinu gani muwe salama.”

“Labda tuendelee kujificha humu ndani,” mwenzetu mmoja akaingilia yale mazungumzo.

“Humu ndani atawagundua tu,” Yasmin akamjibu.

“Sasa tutakwenda wapi, jamani!”

“Mimi sijui niwaambie nini, ndugu zangu!” Yasmin akatuambia.

Tulipomaliza kunywa chai, Yasmin aliondoa vyombo. Alituacha tumekaa tukiendelea kujadiliana. Baadaye kidogo alirudi akiwa na karata.

“Hizi karata ziko siku zote. Huyu mwendawazimu ananiletea. Lakini sina mwenzangu wa kucheza naye.”

Tulipoona karata tukazunguka duara. Yasmin akakaa na kutugawia.

“Tunacheza mchezo gani?” nikamuuliza Yasmin.

“Tunacheza mchezo wa arbasitini.”

Mchezo huo ulikuwa maarufu kule Zanzibar na Comoro.

Tukaanza kucheza karata. Tukasahau kabisa habari ya Harishi. Mchezo ulinoga sana. Kelele zetu zikawa zinasikika hadi nje.

Ilipofika saa tano, Yasmin akavunja mchezo na kutuambia tukatembee tembee. Tukiona jua la saa saba ndio turudi kula chakula. Muda ule alitaka kwenda kupika chakula.

“Niwapikie nini?” akatuuliza.

“Tupikie chochote tu utakachopenda,” nikamwambia.

“Basi nitawapikia pilau.”

“Tutashukuru sana.”

“Sasa mtakapokuja, kwanza mchungulie na kusikiliza. Mkimuona Harishi msiingie ndani, rudini huko huko mtakakotoka. Anaweza kuja ghafla.”

“Tumekuelewa,” nilimjibu.

Baada ya hapo tulitoka, tukarudi kule kwenye boti letu.

Ni tabia ya maumbile ya binadamu kutokata tamaa na kujaribu kubahatisha kila mara, hasa kwa watu kama sisi ambao tulikuwa katika hatari. Kwa mara nyingine tulijaribu tena kuliwasha lile boti. Kila mmoja wetu alijaribu kuliwasha bila mafanikio.

Tukakaa chini ya mti na kuanza kujadiliana. Hata hivyo, mjadala wetu ulikuwa kama usio na maana yoyote, kwani haukutupa ufumbuzi wa jinsi ya kusalimisha maisha yetu.

Kikubwa tulichokizingatia ni kujaribu kumkwepa Harishi kadiri itakavyowezekana. Tuliona kama tutafanikiwa kumkwepa, tunaweza kuendelea kuishi.

Tuliendelea kukaa pale chini ya mti hadi saa saba, tulipoamua kurudi kwa Yasmin. Tulimtuma mmoja wetu aingie akachunguze kama Harishi yuko ndani, aje atuambie.

Mwenzetu huyo akaingia ndani. Sisi tukawa tunamchungulia kwenye dirisha. Alinyata hadi ndani. Tukawa hatumuoni tena. Tukahamia kwenye dirisha jingine. Tukamuona amesimama pembeni mwa ukumbi akiangalia huku na huku. Akaenda jikoni kuchungulia, kisha akatoka.

Alipotoka jikoni, alikwenda moja kwa moja kwenye mlango wa chumba cha Yasmin na kutega masikio yake kwenye mlango. Alisikiliza kwa muda kidogo, kisha akaanza kugonga mlango taratibu.

Mlango ukafunguliwa ghafla. Aliyetoka alikuwa Yasmin. Alitoka haraka haraka, akaufunga mlango, kisha akamuashiria yule jamaa aondoke. Nikajua kuwa hapakuwa salama.

“Moshi unajaa kwenye chupa, Harishi anakuja!” Yasmin alimwambia.

Yule mwenzetu aliposikia vile, aligeuka ili aondoke, lakini ghafla tena mlango ukafunguliwa. Harishi akaibuka mbele ya yule mtu. Alikuwa ameshika upanga wake. Akamshika yule jamaa kwa mkono mmoja.

“Unataka ukimbie wapi wewe?” akamuuliza akiwa amemtolea macho.

Mwenzetu aliishiwa na nguvu kabisa. Akawa amemkodolea macho Harishi.

“Mimi nasikia harufu zenu tangu jana.”

Mwenzetu kimya. Sasa mwili wake ulikuwa ukitetemeka waziwazi.

“Sheikh, nisamehe sana…” Sauti yake ikasikika kwa mbali ikiomba.

“Chombo chetu kiliharibika jana.”

Harishi alikuwa akimtazama kama vile alikuwa hamuelewi.

“Wasemaje?”

“Nisamehe sana… nakuomba,” jamaa alikuwa analia.

“Kwani wewe huna damu? Ngoja nione.”

Hapo hapo Harishi akamuinua juu mwenzetu huyo kwa mkono mmoja tu. Akamgeuza kichwa chini.

Kiasi cha kufumba na kufumbua tu, alishamtoboa utosi kwa ncha ya upanga wake.

Yasmin alipoona hivyo, alikimbilia nje. Akatuona tumeinamia dirisha.

“Jamani, balaa gani hili?” akajisemea peke yake.

Idadi yetu sasa tulikuwa watu watano, wenzetu wawili walikuwa wameshauawa. Na sisi pia hatukuwa na matumaini kuwa tungebaki.

Tulijua kuwa kama hatutakufa kwa njaa, tutauliwa na lile jini la Yasmin. Kila mmoja wetu alikuwa ameshikwa na hofu na fadhaa. Tulitamani angalau kipite chombo kituokoe kuliko vile tulivyokuwa tumatuma tukisubiri kufa.

Tulitamani tusifike tena katika lile jumba la Yasmin, lakini tungekula nini, wakati kwa Yasmin ndiko tunakotarajia kupata riziki yetu. Kusema kweli tulichanganyikiwa na hatukujua la kufanya.

Tulikaa pale chini ya mti kwa karibu saa mbili. Ghafla tuliona mwanamke akitembea na ufukwe wa bahari akija upande wetu. Mkono mmoja alikuwa ameshika kapu.

“Jamani, ni nani yule?” Mwenzetu mmoja akauliza.

“Naona ni kama Yasmin,” nikajibu.

Mjadala ukaanza.

“Ni Yasmin kweli!”

“Amefuata nini huku?”

“Labda anatutafuta sisi.”

“Mmoja wetu atokeze ili atuone au aende akampokee lile kapu. Labda anatuletea chakula.”

“Hatujui Harishi yuko wapi. Unaweza kujitokeza ukajikuta unakamatwa!”

“Bila shaka Harishi ameshaondoka, Yasmin asingeweza kuja huku. Ngoja nimfuate.” Mimi ndiye niliyesema hivyo. Nikanyanyuka na kuanza mwendo kuelekea upande ule aliotokea Yasmin.

Yasmin akaniona.

“Nawatafuta nyinyi, mko wapi?” akaniuliza tangu akiwa mbali.

“Tuko huku chini ya mti. Tumekuona tangu ukiwa mbali.”

“Nimewaletea chakula.”

Nilikuwa nimeshamfikia. Nikampokea lile kapu.

Tukawa tunatembea pamoja kuelekea kule waliko wenzetu.

“Lile shetani limeshaondoka, ndio maana nimeweza kutoka,” Yasmin akaniambia.

“Halitarudi tena kwa leo?”

“Halitarudi labda kwa kesho.”

“Yule mwenzetu ndiye ameuawa?”

“Ndiyo, aliuawa. Si mliona wenyewe akikamatwa?”

Nikatikisa kichwa changu kusikitika.

“Wakati anabisha mlango niliona ile chupa ya Harishi ikijaa moshi. Nikajua kuwa Harishi anakuja. Nikawahi kutoka ili niwambie muondoke. Wakati nasemeshana na yule mwenzenu, Harishi akasikia, akawahi kutoka na kumkamata,” Yasmin aliendelea kunieleza.

“Sasa yule jini atatumaliza sote. Tulikuwa watu saba, sasa tumebaki watano tu.”

“Basi msije kule.”

“Sasa tusipokuja, utatuletea chakula?”

“Nitawaletea. Na leo ameshakula mtu mmoja, harudi tena hadi kesho.” Tukawa tumefika walipokuwa wenzetu.

“Leo tumepata msiba mwingine,” mtu mmoja akamwambia Yasmin.

“Nilishawambia tangu mapema kuwa usalama hapa ni mdogo sana kwa sababu ya Harishi. Sasa mnaona wenyewe, na sijui mtafanya nini, ndugu zangu.”

“Jamani, kwanza tuleni chakula. Yasmin ametuletea chakula. Tukanawe mikono kwa maji ya chumvi. Mazungumzo baadaye,” nikawaambia wenzangu.

Tukaenda kunawa maji ya bahari, kisha tukarudi pale chini ya mti, tukaketi. Yasmin naye akaketi na sisi. Tukaanza kula.

“Kwani Harishi ameshaenda zake?” mtu mmoja akamuuliza Yasmin.

“Ameshaondoka,” nikamjibu mimi. “Angekuwepo, Yasmin asingeweza kuja huku.”

Tulikula pilau ikiwa ndani ya kapu. Tukashiba na kupata nguvu.

“Nimesahau kuwachukulia maji ya kunywa,” Yasmin akatuambia.

“Na maji tuliyokuwa nayo yamekwisha,” nikasema.

“Lakini kwa leo Harishi hatarudi, mnaweza kuja nyumbani,” Yasmin akatuambia.