KISIWA CHA MAUTI - 22
ILIPOISHIA
Kwanza tulinyata kwenye madirisha. Tukawa tunachungulia na kutega masikio kusikiliza. Hatukusikia sauti yoyote. Kulikuwa kimya. Ndipo tukaamua tuingie.
Tukaingia ndani ya jumba hilo lililokuwa linawaka taa ndani. Lakini tuliingia kwa kunyata ili hatua zetu zisisikike. Jumba hilo lilikuwa kimya kama vile tulivyoliacha mchana.
Kila tulipofikia kona tulichungulia kwanza kabla ya kuendelea kwenda. Tukaenda hadi katika kile chumba tulichomkuta Yasmin binti wa rais wa Comoro.
SASA ENDELEA...
Mlango wa chumba hicho ulikuwa umefungwa. Tukaenda jikoni tukapekua pekua na kukuta vyakula vilivyokuwa vimebaki. Tukakaa chini na kuanza kula kwani njaa ilikuwa inatuuma na hatukutarajia kupata chakula usiku huo.
Baada ya kula tulitoka humo jikoni tukaamua kutafuta mahali pa kulala ndani ya jumba hilo hilo. Karibu vyumba vyote tulivyofungua ukiacha kile cha Yasmin vilikuwa na vitanda. Kila kitanda kilikuwa na chumba kimoja kilichowezesha kulala watu wawili.
Tukaamua tulale kila chumba watu wawili. Tulikuwa tupo saba. Mmoja wetu akaamua kuchukua godoro kutoka chumba kingine na kuliingiza katika chumba tulichokuwemo mimi na mwenzangu. Akalilaza chini. Kwa vile yeye hakuwa na mwenzake wa kulala naye na asingeweza kulala peke yake, ndipo aliamua kuja kulala na sisi.
Mvua likuwa inaendelea kunyesha na radi ilikuwa inapiga. Kama tungekuwa tuko kwenye boti yetu tungejuta.
Mimi nilisoma aya zangu kisha nikajifunika shuka. Naamini na wenzangu kila mmoja alisoma dua yake kabla ya kulala.
Tulikuwa tumepanga tuamke alfajiri tutoke kwenye hilo jumba bila hata kumshitua Yasmin.
Hata hivyo usingizi hatukuupata kirahisi kwa sababu ya hofu. Tuliendelea kukaa macho hadi usiku mwingi. Wenzangu walipata usingizi lakini mimi sikulala.
Kulikuwa na wakati usingizi ulikuwa umeanza kunijia nikaamshwa na mwenzetu aliyekuwa amelala chini.
“Unasemaje?” Nikamuuliza.
“Mkojo umenibana nisindikize chooni” akaniambia.
Vyoo vilikuwa nje.
Nikatenga shuka na kunyanyuka. Mwenzangu niliyelala naye alikuwa anakoroma.
“Twende!” nikamwambia yule aliyeniamsha.
Tukatoka pamoja. Vyoo vilikuwa ukumbini karibu na mlango wa kutokea.
Tulikwenda hadi karibu na milango ya vyoo. Kulikuwa na vyoo vinne. Mwenzangu alishaingia choo kimojawapo. Mimi nikasikia hatua za mtu nyuma yangu nikageuka. Alikuwa ni yule mwenzetu tuliyemuacha amelala, naye aliamka na kutufuata.
Alikuwa anakuja harakaharaka kutukimbizia. Nilijua ni sababu ya uoga. Wakati huo huo nikaona mlango wa chumba cha Yasmin unafunguliwa. Nikaingia chooni haraka ili niweze kumchungulia aliyekuwa anatoka bila yeye kuniona.
Ghafla nikaliona jitu likitoka katika kile chumba. Lilikuwa jitu la kutisha lililojifunga kilemba kikubwa. Lilikuwa na msitu wa nywele zilizotokeza nje ya kilemba chake. Lilivaa kanzu nyeupe iliyochafuka kwa madoa ya damu na iliyokatwa mikono.
Mikono yake minene iliyoota manyoya marefu ilikuwa imeshupaa. Mkono mmoja alishika upanga mrefu.
Uso wake ulikuwa na ndevu nyingi na sharafa kiasi kwamba sura yake haikuweza kutambulika. Kilichoonekana kwenye uso wake ni pua yake iliyofura kama iliyopachikwa na macho yake makubwa yenye makengeza.
Miguu yake ilikuwa pekupeku. Alikuwa na vidole virefu na vinene vya miguu, tena vilikuwa na kucha ndefu kama kucha za mnyama.
Hapo hapo nikahisi kwamba yule alikuwa ndiye Harushi. Alikuwa ametufuma vizuri ndani ya hilo jumba.
Uso wake ukiwa na hasira kali, macho yake ya makengeza yalielekea kwa yule mwenzetu aliyekuwa anatufuata. Alikuwa ameshafika karibu yake kiasi kwamba jitu hilo lilinyoosha mkono wake wa kushoto na kumshika shati.
“Mimi nasikia harufu ya binaadamu humu ndani. Kumbe ni wewe!” Akamwambia yule mwenzetu aliyemshika shati. Sauti yake ilikuwa ya kuunguruma kama gari bovu.
Wakati anasema meno yake yalitoka nje. Yalikuwa meno marefu kama ya nyani!
Alipomshika mwenzetu shati alimvuta karibu yake.
“Umeingiaje humu ndani na umefuata nini….kwanza umetoka wapi?” Akamuuliza kwa hasira.
Ghafla Yasmin akatoka.
“Ni nani?” Akauliza huku akimtazama yule mtu ambaye alikuwa akitetemeka.
Yasmin alipomuona alimgundua.
“Itakuwa ni wavuvi walioharibikiwa na chombo chao, wameona nyumba wameingia wakidhani watapata msaada” Yasmin akaliambia lile jitu.
“Anaingia humu anamfuata nani. Huyu simuachi ng’o!” jitu hilo lilisema na kumshika yule mwenzetu kwenye kiuno kisha likamuinua juu kwa mkono mmoja na kumgeuza kichwa chini. Kichwa cha mwenzetu kikawa chini ya kichwa cha jitu lile jitu.
Ndipo jitu hilo lilipokita utosi wa yule mtu kwa ncha ya upanga wake. Mwenzetu huyo alipiga ukulele mmoja tu “Nakufaaa!” Kisha akawa kimya. Damu ikaanza kuchuruzika kutoka kwenye utosi wakei jitu hilo likakinga mdomo wake na kuanza kuifyonza!.
Aliendelea kuinywa ile damu iliyokuwa ikitoka kama maji ya bomba. Mwisho alibandika mdomo wake pale kwenye utosi na kuanza kufyonza.
Nilikuwa nikitetemeka kwa hofu kama niliyepatwa na homa ya baridi ya ghafla. Nilijua akimalizwa yule mwenzetu itaanza zamu yetu sisi kwani sote tulikuwa ndani ya lile jumba.
Midomo ya Harishi ilitapakaa damu. Damu nyingine ilikuwa inavuja midomoni mwake na kuingia kwenye ndevu zake na kisha kutiririka hadi kwenye kanzu yake.
Yasmin alikuwa ameshika kichwa chake kwa huzuni na alikuwa amekiinamisha kichwa chake chini ili asiangalie lile tukio.
Pamoja na huzuni na uchungu vilivyompata Yasmin bila shaka alikuwa akijiambia “Wameyataka wenyewe. Nilishawambia waondoke, kumbe wamerudi tena”
Nikaona mafunda ya Harish yanafutuka huku akitafuna kwa haraka haraka na kumeza. Kumbe alikuwa anafyonza ubongo wa mwenzetu na kuula. Aliula kwa ulafi. Mwingine ulimvuja midomoni na kuingia kwenye ndevu zake.
Alipotosheka alitupa chini ile maiti akaanza kujirambaramba midomo na kujifuta kwa mkono. Alipomaliza aliinama akaushika mguu wa yule mtu aliyemuua.
“Sasa nimeshiba vizuri, ngoja niondoke” alijisemea peke yake akiuinua ule mguu na kuuburuza kuutoa ule mwili nje. Aliuburuza huku akiendelea kujirambaramba. Alipofika kwenye mlango aliufungua na kutoka na ile maiti nje.
Yasmin alikuwa bado amesimama akimtazama.
“Lakini mimi niliwambia ila hawakunisikia” akajisemea peke yake huku akitikisa kichwa.
Kwa sababu ya kuzidiwa na hofu na kujua kuwa sote tutakufa nilijitokeza pale nilipokuwa nimejificha. Nikamfuata Yasmin.
Yasmin alishituka aliponiona.
“Na wewe umetokea wapi?” Akaniuliza kwa kutaharuki.
“Nilikuwa nimejificha chooni” nikamjibu kwa sauti ya kutetemeka.
“Unaiona damu hii ya mwenzenu?”
Yasmin akanionesha damu iliyokuwa imedondoka chini.
“Nimeiona na nimeona pia alivyouawa”
“Si niliwambia mwendezenu?”
“Tulirudi huu usiku tulipoona kuna mvua na hatukuwa na mahali pa kujisitiri”
“Sasa mmerudi na Harishi ametokea. Mwenzenu ameonekana”
“Kwani atarudi tena usiku huu?”
“Usiku huu hatarudi tena lakini kama ameshasikia harufu zenu anaweza kurudi hata kesho akijua atapata mlo mwingine. Yule hali kitu isipokuwa damu na ubongo. Watu wa kisiwa chote hiki amewamaliza yeye na ana nguvu zisizo za kawaida. Yule mtu amemuinua juu kwa mkono mmoja tu”
“Na amempeleka wapi?”
“Amekwenda kumtupa nje ili asubuhi aliwe na kunguru”
“Sasa sijui sisi tutakimbilia wapi kwani chombo chetu kimekataa kabisa kuwaka”
“Mimi sina la kuwambia kwani popote mtakapokwenda ndani ya kisiwa hiki atawagundua na atawamaliza mmoja mmoja”
Nilibaki kuduwaa na kutikisa kichwa. Kwa mara ya kwanza niliona kazi ya uvuvi ilikuwa mbaya. Laiti kama ningejua kuwa chombo chetu kingeharibika baharini nisingeshiriki katika safari ile.
“Wenzako wengine wako wapi?” Yasmin akaniuliza.
“Nikwambie ukweli Yasmin, sisi tulirudi mapema huu usiku tukaingia jikoni na kula chakula chako kwa sababu tulikuwa na njaa. Tukaingia vyumbani kulala. Sasa tulitoka watu wawili kuja kujisaidia. Huku nyuma mwenzetu mmoja naye alitoka peke yake, Ndiye yule aliyekamatwa na kuuawa”
“Wenzako wengine wako wapi?”
“Mmoja amejificha chooni na wenzetu wengine wako vyumbani”
“Sasa na nyinyi nendeni mkalale, asubuhi mtafanya maarifa. Yule jini hatarudi kwa leo, ameshashiba”
Yule mwenzangu aliyekuwa chooni aliposikia maneno yale alitoka haraka. Yasmin akamtazama.
“Nyinyi mna bahati sana. Angeweza kushikwa mmojawenu”
“Ni kweli kwa sababu sisi ndio tuliotoka kwanza” nikamwambia Yasmin.
“Basi nendeni mkalale”
Tukarudi kwenye vile vyumba. Yasmin alikuwa bado amesimama akituangalia hadi tulipofungua mlango na kuingia chumbani’
Wala hatukulala kamwe. Mimi nilikaa macho usiku kucha nikimuwaza yule mwenzetu aliyeuawa kikatili.
“Nyinyi mna bahati sana. Angeweza kushikwa mmojawenu…” nikawa nayakumbuka maneno ya Yasmin huku mwili ukinisisimka kwa hofu.
Mara kwa mara nilikuwa nikitupa macho kila upande wa chumba hicho kwa hisia kwamba Harishi angeweza kutokea mle chumbani.
Asubuhi kulipokucha Yasmin alikuja kutugongea mlango.
“Amkeni. Kumeshakucha” Alikuwa akituambia wakati akigonga. Tukatambua kuwa alikuwa ni yeye.