KISIWA CHAMAUTI - 22
ILIPOISHIA
Wakati Yasmin anatuhadithia kile kisa, nilimuuliza, “Umetuambia huyo jini anafyonza damu za watu na kuwaua, je, wewe utaendelea kuwa salama kweli?”
“Mimi nimeshakuwa mke wake. Ameniambia damu yangu ni haramu kwake. Hawezi kuniua, ila hatanirudisha tena kwetu. Nitaendelea kuishi hapa hadi mauti yanikute,” Yasmin alituambia.
Kwa kweli, hayakuwa maneno ya kuogopesha tu, bali pia yalikuwa yanasikitisha sana.
Maisha ya Yasmin yalikuwa yanasikitisha. Alionesha wazi kukata tamaa, pia niliona kwa vyovyote itakavyokuwa, maisha yake yatakuwa mafupi.
“Kwa hiyo sisi hatutapona?” Mwenzetu mmoja akamuuliza Yasmin.
“Siwezi kuwaficha, nawaeleza ukweli ili mjue kuwa saa zenu zimekaribia sana.”
“Je, kama tutaondoka ndani ya jumba hili na kwenda kujificha mahali pengine?”
SASA ENDELEA...
MTAJIFICHA wapi ambapo hafiki. Kisiwa chote hiki amekimiliki yeye. Halafu yeye ni jini, lazima atawagundua tu”
“Sisi tuko watu saba. Kweli ataweza kutuua sisi sote kwa pamoja?”
“Nyinyi atawaua mmoaja mmoja. Leo akiua mmoja, kesho anarudi tena kuua mwingine hadi mtamalizika nyote. Akishaua mtu anamtupa nje aliwe na kunguru”
Msichana akatikisa kichwa peke yake kabla ya kuendelea.
“Halafu hataki kuona mtu humu ndani. Wivu wake ni mkali sana. Siku nyingine anakuja na hasira, anasema anasikia harufu ya mtu humu ndani, basi hunipiga hadi nazimia kisha huenda zake”
Kila mmoja wetu aliguna na kumtazama mwenzake.
“Unadhani atakuja lini tena?” nikamuuliza.
“Anakuja kila wiki mara moja na kwenda zake. Au kama nina dharura ninamuita. Kuna siku niliona nyoka nikamuita, akaja muda ule ule”
“Sasa unamuitaje?”
“Alinipa chupa. Mnaiona ile chupa iliyopo juu ya kabati? Chupa ile iko wazi. Kifiniko chake kipo pembeni. Ameniambia nisiifunge. Anapotaka kuja ile chupa inajaa moshi halafu inavuma. Ule moshi ukishajaa unatoka kwenye mdomo wa ile chupa na kuunda umbile la jini halafu anakuwa jini kabisa.
“Sasa nikitaka kumuita nachukua ile chupa naiweka karibu na mdomo wangu kisha nataja jina lake mara tatu, hazitapita dakika mbili chupa itajaa moshi. Moshi ule utatoka kwenye mdomo wa chupa na kugeuka Harishi”
“Sasa kama anakuja kila wiki tutapata muda wa kuishi na pengine tunaweza kupata msaada kwani tutakwenda kukaa fukweni kusubiri vyombo vinavyopita.” Nikamwambia Yasmin
“Jaribuni hahati yenu. Nawaombe Mungu awasalimishe” Yasmin alituambia kwa unyonge.
Nikawambia wenzangu. “Jamani maneno mmeyasikia. Hapa hapakaliki.”
“Sasa tuondoke?” Mtu mmoja akauliza.
“Inabidi tuondoke tusalimishe maisha yetu”
“Sasa tutakwenda wapi?” Mwingine akauliza.
“Twende ufukweni tuangalie vyombo vinavyopita, tunaweza kupata msaada”
“Sasa huyu msichana naye tumchukue?” Mtu mwingine naye akauliza.
“Itakuwa ni jambo zuri tukimchukua kama mwenyewe atakubali.” Nikawambia wenzangu kisha nikamtazama Yasmin.
“Bibie unaonaje kama tutakuchukua ili tukunusuru?” Nikamuuliza yasmin.
“Kunichukua mimi hakutakuwa nusura kwangu wala kwenu kwa sababu mpaka sasa hamna uhakika wa usalama wenu hata kama mtakwenda ufukweni mwa bahari kusuiri vyombo vinavyopita” Yasmin akatuambia.
“Kwanini unatuambia hivyo?” Nikamuuliza.
“Kwa sababu Harishi anaweza kututokea hapa hapa na kutuua sote kwa hasira’
Sote tukaguna na kutazamana. Yasmin aliendelea kutuambia.
“Kwanza akija hapa nyumbani hata kama mtakuwa mmeshaondoka atasema anasikia harufu ya binaadamu na atataka kujua ni nani aliyeingia humu na itakuwa ni balaa kubwa”
“Sasa unatushauri nini?” Nikamuuliza Yasmin katika hali ya kukata tamaa.
“Nawashauri muondoke ndani ya jumba hili. Mwende popote mtakapoona mtaweza kujiokoa. Mimi niacheni hapa hapa”
“Sawa. Basi sisi tunondoka”
Yule msichana kwa kuonesha wema na ukarimu alituambia tumpishe mle chumbani avae nguo. Tukatoka ukumbini. Yasmin alipovaa alitoka akaenda jikoni. Akachukua vyakula na kututilia ndani ya mfuko.
“Sasa nendeni, msikae karibu kabisa” akatuambia.
Tukamuaga na kutoka. Tukaanza kutembea haraka haraka kwa kufuata ile njia tuliokwendea.
Kisiwa kilikuwa kimya na kilichokuwa kinatisha. Kelele zilizosikika zilikuwa ni za kunguru waliokuwa wakilialia na kurukaruka kwenye miti kama waliokuwa wakiambizana “Hao! Hao! Hao!”
Tulikuwa tukiangalia huku na huku kwa hofu ya kutokewa na Harishi. Kuwa na silaha katika mazingira yale ilikuwa muhimu. Mimi nilikuwa na sime niliyokuwa nimeichomeka kiunoni. Wenzangu wawili walikuwa na mapanga. Wenzetu wengine walikuwa mikono mitupu.
Kwa sababu ya hofu iliyosababishwa na kelele za wale kunguru nilitoa sime yangu na kuishika mkononi. Sasa nikawa tayari kukabiliana na chochote kitakachotokea.
Mpaka tunatokea kule ufukweni mwa bahari tulizungukazunguka sana kwani tulikuwa tunapotea njia mara kwa mara. Kulikuwa na mti mkubwa ulioota kando ya bahari. Tukakaa chini ya ule mti.
Tulitoa vyakula tulivyopewa na Yasmin na kuanza kula. Vilikuwa vyakula vizuri vikiwa mchanganyiko wa mikate ya mayai, keki, sambusa na biriani.
Wakati tunakula mawazo yangu yalikuwa kwa yule msichana. Kwa kweli nilimuhurumia sana kwa kuishi maisha ya peke yake katika kisiwa kile cha kutisha. Laiti ningekuwa na uwezo wa kumuokoa ningemuokoa lakini ndio hivyo hatukuwa na uwezo na bado sisi wenyewe pia hatukuwa na uhakika wa maisha yetu.
Hata hivyo nilimsifu kwa kuwa na moyo wa kijasiri na wa kiume kwani asingeweza kuishi na kuendelea kuwa hai hadi leo wakati yuko kwenye jinamizi la mauti. Kuishi na jini anayeua watu peke yake lilikuwa ni jinamizi la mauti mbali ya kule kuishi peke yake katika kisiwa kile kinachotisha!.
Nikajiambia kama chombo chetu kingekuwa kizima tungeondoka naye hata kama angekataa. Baada ya kula kile chakula tulipata akili tukaanza kujadiliana.
“Sasa tufanye nini jamani?” Mwenzetu mmoja akauliza.
“Tuijaribu tena ile boti, inaweza kukubali” nikatoa wazo ambalo lilikubaliwa na wenzangu.
Tukaenda kwenye chombo chetu tukajaribu kukiwasha lakini chombo hakikuwaka. Kila mmoja wetu alijaribu kukiwasha kwa mkono wake. Hakukuwa na yeyote aliyefanikiwa. Tukaamua kujitia ufundi kuanza kuichokoresha mashine ya boti.
Kila mmoja alitia ufundi wake lakini pia hatukufanikiwa. Mimi nilijitupa chini kwenye mchanga nikawaacha wenzangu wakiendelea kushindana nayo.
Yalipita karibu masaa mawili. Hatimaye niliona wenzangu mmoja mmoja akiondoka kwenye boti na kutafuta mahali pa kukaa. Wote walikuwa wamekata tamaa kama nilivyokata mimi.
Mawazo yangu yakarudi kwa Harishi. Kama alivyotwambia Yasmin Harishi anaweza kutokea na kutumaliza kama alivyowamaliza watu wa kisiwa hicho.
Kwa muda sote tulikuwa kimya. Kila mmoja alikuwa akiwaza lake. Tulipokitokea kisiwa kile tuliona tumeokoka tukafurahi. Kumbe tumeepuka kufa maji, tumekwenda kwa muuaji mwingine anayefyonza damu.
Tuliendelea kukaa pale tukiangalia baharini hadi jua likaanza kuchwa. Hatukuona chombo chochote kilichopita karibu. Tulichokiona ni mawingu yaliyoonekana kama yanazama upeoni mwa macho yetu.
Wakati giza linaingia hatukujua tungejisitiri mahali gani usiku huo kwani kwa vyovyote vile tusingeweza kuupitisha usiku mahali hapo kutokana na baridi. Pia usalama wetu ulikuwa mdogo. Lolote lingeweza kutokea wakati wa usiku. Kuna vitu kama majoka na wanyama wakali ambao hujificha wakati wa mchana na kujitokeza wakati wa usiku.
Baada ya kuufikiria usalama wetu tulishauriana turudi tena katika lile jumba la yule msichana. Kuna waliopinga wakataka tupande juu ya mti ule tuupitishe usiku.
Lakini upepo mkali ulioanza kuvuma pamoja na ngurumo za radi ndio uliofanya tukubaliane kwa pamoja kurudi katika lile jumba kwani tulijua muda si mrefu mvua kali ingenyesha na kututosa. Si tu tuliona tungeweza kujisitiri katika lile jumba pia tungeweza kufanya uchunguzi wetu na kujua kama huyo Harishi tuliyeambiwa ameshakuja au bado.
Tukaanza tena safari ya kurudi katika lile jumba. Mvua ilikuwa imeshaanza kunyesha kidogo dogo huku upepo mkali ukiendelea kuvuma pamoja na radi.
Tulitembea kwa mashaka mashaka tukikwepa kuwa karibu na miti kwa kuhofia kupigwa na radi. Kulikuwa giza na hatukuweza kupata mwanga ila pale radi ilipopiga ndipo tulipoona tulikokuwa tunaelekea. Kutokana na giza hilo tulihangaika katika pori kwa muda kabla ya kufanikiwa kutokea katikati ya ule mji uliohamwa.
Tulikuwa tunaendelea kutota na mvua na huku tukiendelea kwenda. Tukawa tunalitafuta lile jumba. Tulidhani tusingeliona kwa urahisi lakini lilikuwa linawaka taa. Tukaliona kwa mbali. Tukalifuata.
Kwanza tulinyata kwenye madirisha. Tukawa tunachungulia na kutega masikio kusikiliza. Hatukusikia sauti yoyote. Kulikuwa kimya. Ndipo tukaamua tuingie.
Tukaingia ndani ya jumba hilo lililokuwa linawaka taa ndani. Lakini tuliingia kwa kunyata ili hatua zetu zisisikike. Jumba hilo lilikuwa kimya kama vile tulivyoliacha mchana.
Kila tulipofikia kona tulichungulia kwanza kabla ya kuendelea kwenda. Tukaenda hadi katika kile chumba tulichomkuta Yasmin binti wa rais wa Comoro.