Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KISIWA CHA MAUTI - 19

KISIWA - 19 Pict

ILIPOISHIA

Gari la hospitali lilikuwa limeshafika. Yasmin alipakiwa na kukimbizwa hospitali. Gari hilo la hospitali lilifuatana na gari la maofisa usalama na gari la rais mwenyewe.

Lakini gari alilopakiwa Yasmin likapata ajali kabla ya kufika hospitali. Tairi lake la mbele la upande wa kulia lilipasuka na kusababisha gari hilo kuyumba na kuligonga gari jingine kabla ya kupindukia kwenye mtaro uliokuwa kando ya barabara.

Heka heka ikawa kubwa! Magari ya maofisa usalama yakasimama. Maafisa hao wakashuka na kukimbilia kutoa msaada.

Dereva wa gari la hospitali alipotolewa alikutwa akiwa ameshakufa. Yasmin mwenyewe hakuonekana. Wauguzi wawili waliokuwa naye walikutwa wamezirai. Tukio hilo lilizua taharuki kubwa..

SASA ENDELEA...


RAIS Abdulatif hakuamini macho yake, akawa anauliza kwa ukali “Binti yangu yuko wapi?”

Lakini hakukuwa na aliyejua. Yasmin alikuwa ametekwa ghafla. Kila aliyeshuhudia alishangaa.

Harusi ikavunjika. Badala ya furaha sasa ikawa huzuni. Bwana harusi na mke wa Rais Sharif Abdullatif Bi Kulthum  walikuwa wanalia kutokana na muujiza huo.

Usiku uleule Rais Abdullatif aliita masheikh ikulu na kuwauliza kama walikuwa wanajua kilichomtokea binti yake.

Kila sheikh alisema lake. Wako waliomwambia kuwa binti yake alikuwa amechukuliwa na wachawi. Wako waliomwambia kuwa haikuwa muafaka kwa binti yake kuolewa na Abubakar ndiyo sababu tukio hilo limetokea. Na wako waliomwambia kuwa Yasimin alikuwa amechukuliwa na jinni aliyekuwa amemchunuka.

Rais Abdullatif hakujua ashike kauli ya sheikh yupi. Kwa vile lilikuwa limeshamfika alikubaliana na mashekh wote na kuwataka mashikh hao kutumia elimu zao kumrudisha binti yake. Aliahidi mamilioni ya shilingi za ki Comoro kwa sheikh yeyote atakayefanikiwa kumrudisha Yasmin.

Licha ya Rais Abdullatif kusubiri kwa zaidi ya miezi mitatu. Hakukuwa na sheikh yeyote aliyefanikiwa kumrudisha Yasmin! Yasmin akabaki kuwa historia kwani hakupatikana tena. Ulikuwa msiba ambao kila mkazi wa Comoro alihisi kuwa hautasahaulika.

Hivi sasa mwaka mmoja umeshapita tangu tukio hilo la kuhuzunisha litokee. Tangu wakati ule sikuwahi tena kurudi Moroco. Nilikuwa Pemba nikiendelea na shughuli zangu za uvuvi.

Sasa siku moja ambayo sitaisahau maishani mwangu tulikuwa kwenye boti letu tukielekea maji makuu kuvua samaki. Ndani ya boti hilo tulikuwa wavuvi saba.

Ilipofika saa nne asubuhi tulikuwa mbali sana. Boti yetu ilipigwa na dharuba kali. Mashine ya boti ikazima ghafla. Tilijaribu kuiwasha lakini boti haikuwaka. Ikawa inakokotwa na maji.

Tulipumzika kidogo kisha tulijaribu kuiwasha tena na tena lakini hatukufanikiwa kuiwasha, Mashine ilitugomea kabisa. Hatukujua ilikuwa imepatwa na hitilafu gani.

Hapo ndipo tulipoanza kufadhaika. Hatukuwa na la kufanya, tukawa tunatazamana!.

Tulikuwa tumepelekwa mbali sana kiasi kwamba hatukuweza kuona vyombo vyovyote ambavyo vingeweza kutusaidia. Tukakata tamaa kabisa.

Injini ya boti inapozima boti inakuwa kwenye hatari ya kupigwa na dharuba na kupinduka. Kama hilo lingetokea ungekuwa ndio mwisho wetu!

Hata hivyo bahari ilikuwa tulivu. Tatizo letu ni kuwa safari yetu haikuwa na mwisho wala muelekeo maalumu. Boti yetu ilikuwa inakokotwa kufuata upepo unakokwenda.

Mpaka jua linakuchwa hatukuwa tumetokea kwenye nchi yoyote wala kisiwa chochote. Ndani ya boti tulikuwa na vyakula vya akiba lakini hakukuwa na yeyote miongoni mwetu aliyesikia njaa.

Usiku ukapita kwa taabu huku tukiendelea kupelekwa. Asubuhi tuliendelea tena na jitihada ya kuiwasha injini lakini injini ilikataa katakata kuwaka. Tukaendelea kukokotwa hadi jioni. Hapo tukatoa vyakula vyetu na maji tukala kidogo tu.

Tulilala tena kwenye boti hadi siku ya tatu na ya nne. Vyakula vikatuishia licha ya kwamba tulikuwa hatuli sana. Tulibakisha maji kidogo tu.

Sasa tukahisi kwamba kama hatutakufa maji tutakufa kwa njaa kwani kwa siku hizo nne tulizokuwa baharini tulikuwa tumekonda.

Alfajiri ya kuamkia siku ya tano ndipo tulipotokea kwenye kisiwa. Sote tukashukuru ingawa hatukujua kilikuwa kisiwa gani na kilikuwa katika eneo gani.

Kilikuwa kisiwa kikubwa ingawa hakikuwa kikubwa sana. Kwa vile tulikitokea wakati wa usiku hatukukiona kwa sababu ya giza. Tulikiona kulipoanza kucha. Wakati tunakiona tulikuwa tumekikaribia sana. Sote tukapata furaha na matumaini ya kuokoka.

Mawimbi yaliendelea kutusukuma kidogodogo na kutufikisha kwenye maji madogo kabisa.

Suala kwamba kisiwa hicho kilikuwa kisiwa gani na kipo wapi halikuwa na umuhimu kwetu. Kilichokuwa muhimu ni kuwa tumefika mahali ambapo tungeweza kuyasalimisha maisha yetu na pengine kupata msaada wa kutuwezesha kurudi kwetu.

Tulishusha nanga na kushuka kwenye boti. Maji yalikuwa yakitufikia kwenye magoti. Tukaliacha boti na kutembea kwa miguu kwa kuyasukuma maji hadi tukafika ufukweni mwa bahari. Mahali tulipotokea hapakuwa na muinuko mkubwa. Tukapanda kwenye nchi kavu na kuanza kutembea kwemye vichaka huku tukiangaza macho huku na huku.

Kulikuwa na kunguru wengi waliokuwa wakiruka ruka kwenye miti. Jinsi walivyokuwa wakipiga kelele walikuwa kama wanaotukaribisha katika kisiwa hicho kilichokuwa kimya.

Tukaendelea kutembea tukiingia ndani zaidi ya kisiwa. Mtarajio yetu yalikuwa kupata mji au kijiji kilichokuwa kinakaa watu ili tuweze kusaidiwa.

Baada ya mwendo wa kama nusu saa tulianza kuona vibanda vilivyokuwa vimebomoka. Tukapata matumaini kuwa kulikuwa na watu waliokuwa wanaishi katika kisiwa hicho. Pia tulikuta visima viwili vya maji ambavyo vilikuwa vimekauka.

Wakati tunaendelea kwenda ghafla tuliona tumetokea kwenye barabara pana ya changarawe. Tukaifuata ile barabara mpaka tukatokea katikati ya mji.

Ulikuwa mji mzuri uliokuwa na barabara na majumba. Lakini nyumba zote zilikuwa zimechakaa na kubomoka. Baadhi yake zilionekana kama mahame.

Jambo ambalo lilitushangaza ni kuwa hatukuona mtu hata mmoja. Mji wote ulikuwa kimya kabisa. Tulikuwa ni sisi peke yetu tu. Tulikatiza mtaa hadi mtaa kutafuta wenyeji wa kisiwa hicho lakini hatukuona mtu.

Udadisi ukatufanya tuanze kuingia katika zile nyumba. Tuliingia katika  nyumba ya kwanza. Tukakuta vitu vya ndani vilivyochakaa na kukongoroka. Vilikuwa kama vitu vya zamani visivyotumika tena. Katika kutafiti tafiti tulishituka tulipokuta mafumvu na mifupa ya binaadamu. Kuna iliyokuwa imelala kwenye kitanda na mengine ilisambaa ovyo.

Tukatoka haraka katika nyumba ile na kuingia katika nyumba nyingine, nako tulikuta vitu mbalimbali vya ndani ya nyumba vilivyokuwa vimechakaa na mifupa ya binaadamu.

Tukawa tunatazamana kwa hofu. Kila mmoja wetu alikuwa akijiuliza moyoni mwake, kulikoni? Lakini hatukupata jibu.

Katika mitaa mengine tulikuta mafuvu na mifupa ya binaadamu ikiwa barazani mwa nyumba na kando kando ya barabara.

Tulivyozidi tena kwenda mbele tulikuta mifupa ya mikono na ya miguu ya binaadamu ikining’nia kwenye miti. Tukawa tunazidi kuitazama ile mifupa huku tunazidi kwenda.

Ghafla tukatokea kwenye jumba moja kubwa. Jumba hilo ndilo lililokuwa kubwa na zuri kuliko jumba lolote katika kisiwa hicho.

Mbele ya jumba hilo kulikuwa na bustani ya maua na miti ya vivuli. Kutokana na uzuri wa jumba hilo tukaona tuingie ndani ili tuangalie lilivyo.

Tulipoingia tu pua zetu zilikaribishwa na harufu nzuri ya manukato yaliyokuwa yananukia humo ndani. Tulitembea katika sakafu ya marumaru iliyonakishiwa maua ya kupendeza.

Tulikuwa tumeingia katika ukumbi mpana uliokuwa na madirisha  na mapazia ya hariri. Tulikuta meza, viti na makabati. Zilikuwa fanicha za kifahari sana.

Baada ya kuupita ukumbi huo tulitokea katika kumbi nyingine ndogondogo zilizokuwa na vyumba vipana.

Tukawa tunaingia kila chumba kuchunguza.

Katika chumba cha kwanza tulikuta kitanda kilichotandikwa vizurii. Pia tulikuta makabati ya vioo yaliyokuwa yanapendeza.

“Inaelekea kuna watu wanaoishi ndani ya jumba hili” Mwenzetu mmoja akasema.

“Lakini mbona hatuwaoni hao watu?” Mwingine akauliza.

“Ndiyo hatuelewi sasa” aliyesema mwanzo akamjibu.

Tulitoka katika kile chumba tukaingia katika chumba kingine. Pia tulikuta kitanda na makabati. Tukawa tunatazamana kwa mshangao. Kutoka hapo tulichangukana. Kila mmoja akawa anafungua chumba alichotaka na kuangalia ndani.

Mimi niliingia katika vyumba viwili. Nilipoingia chumba cha tatu nilishituka nilipomuona msichana mzuri amelala kitandani. Alikuwa amelala usingizi kabisa huku amejifinika shuka kuanzia miguuni hadi shingoni. Uso wake uliokuwa wazi ulikuwa umeelekea upande wangu.

Nilipomuona nilisita kwenye mlango na kujiuliza msichana huyo ni nani na kwanini alikuwa peke yake katika jumba hilo.

Baada ya kusita kidogo niliingia ndani. Nilikuwa nataka kuhakikisha kama alikuwa hai kweli au amekufa.

Nilipofika karibu yake, msichana huyo alifumbua macho ghafla. Akashituka aliponiona.

“Wewe nani?” akaniuliza kwa mshangao akitumia lugha ya kingazija ambayo nilikuwa siijui vizuri. Lakini nilimjibu kwa Kiswahili.

“Mimi ni mgeni katika kisiwa hiki na katika jumba hili, je wewe ni nani?” Alikuwa anajua Kiswahili. Akanijibu kwa Kiswahili cha Kipemba.

“Miye ni Yasmin, binti wa Rais Shariff Abdilatif wa Comoro!”

Nilishituka sana aliponiambia yeye ni binti wa Sharif Abdulatif wa Comoro.

Papo hapo nikakumbuka ile harusi iliyovunjika kati ya binti wa rais wa Comoro na mwana wa mkuu wa majeshi ya ulinzi nchini humo.