KISIWA CHA MAUTI - 20
ILIPOISHIA
“Wewe nani?” akaniuliza kwa mshangao akitumia lugha ya kingazija ambayo nilikuwa siijui vizuri. Lakini nilimjibu kwa Kiswahili.
“Mimi ni mgeni katika kisiwa hiki na katika jumba hili, je wewe ni nani?”
Alikuwa anajua Kiswahili. Akanijibu kwa Kiswahili cha kipemba.
“Miye ni Yasmin, binti wa Rais Shariff Abdilatif wa Comoro!”
Nilishituka sana aliponiambia yeye ni binti wa Sharif Abdulatif wa Comoro.
Papo hapo nikakumbuka ile harusi iliyovunjika kati ya binti wa rais wa Comoro na mwana wa mkuu wa majeshi ya ulinzi nchini humo.
SASA ENDELEA...
Mimi nilikuwa mmoja wa waalikwa kutoka Zanzibar na nikashuhudia maajabu. Yasmin alitoweka katika mazingira ya kutatanisha baada ya gari iliyokuwa inampeleka hospitali kupasuka tairi na kuingia kwenye mtaro. Yasmin alikuwa anakimbizwa hospitali baada ya kuanguka ghafla wakati baba yake, Rais Sharif Abdulatif, akitaka kutoa idhini ya kumuozesha binti yake.
Baada ya kutoweka ghafla kwenye gari, Yasmin hakupatikana tena na sasa mwaka ulikuwa umeshapita.
Ingawa sikuwahi kuonana naye uso kwa uso, niliona picha zake katika magazeti na televisheni wakati habari zake zilipokuwa zinaandikwa na kutangazwa.
Alikuwa ndiye Yasmin kweli, binti wa Rais Sharif Abdulatif wa Comoro.
Kwa kweli, tukio la kumkuta ndani ya jumba hilo na katika kisiwa kile kisicho na watu, mbali na kunishitua, liliniongezea hofu mara dufu.
“Wewe ni binti wa Rais wa Comoro?” nikamuuliza kwa mshangao.
Huku akinyanyuka kwenye kitanda na kuketi, msichana huyo alinijibu.
“Ndiye mimi. Rais Sharif Abdulatif ni baba yangu.”
Nikiwa kwenye mshangao, niliendelea kumtazama msichana huyo bila kumaliza kumtazama. Alikuwa amevaa shumizi inayonyesha. Alipoketi, alijifunga ile shuka kwenye mwili wake kama mtu aliyekuwa anaona baridi. Lakini nilijua alikuwa anajisitiri kwa sababu shumizi aliyovaa ilikuwa inaonyesha.
Kwa tamaduni za Kiislamu na za kule Comoro, mwanamke hatakiwi kuonekana mwili wake pamoja na nywele zake. Lakini Yasmin, kwa sababu ya kutaharuki, alisahau kujifunika kichwa. Nywele zake za mawimbi zilizokuwa ndefu zilikuwa zimeshuka na kumfikia mabegani.
“Yasmin, umefikaje huku?” nikamuuliza.
Yasmin akanitazama. Macho yake makubwa yenye mboni za rangi ya kahawia yalinifanya nikiri kimoyomoyo kuwa Yasmin alikuwa mzuri.
Badala ya Yasmin kunijibu, na yeye akaniuliza.
“Kwani wewe umefikaje hapa?”
“Mimi siko peke yangu, nina wenzangu na tumefika hapa kwa bahati mbaya. Sisi ni wavuvi kutoka Zanzibar. Chombo chetu kilipigwa na dharuba kikapata hitilafu. Kwa siku nne kilikuwa kinaelea kwenye maji, hatujui tunakokwenda. Leo siku ya tano ndiyo tumetokea kwenye kisiwa hiki.”
“Huko ulikopita hadi umetokea hapa, umeona nini?”
“Tumekuta nyumba hazina watu. Pia tumekuta mafuvu na mifupa ya watu kila mahali.”
“Basi na nyinyi ndiyo mtakuwa hivyo hivyo, hamtapona.”
Yale maneno yalinitisha na kunifadhaisha.
“Yasmin, kwa nini unaniambia hivyo? Mimi ni ndugu yako wa Zanzibar. Hata katika harusi yako na mwana wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Comoro nilialikwa na nilikuja Comoro, lakini wewe ulitoweka katika mazingira ya ajabu. Na leo ndiyo nakuona hapa,” nikamwambia Yasmin kwa hofu.
“Nashukuru kwamba leo nimetembelewa na ndugu yangu wa Zanzibar na nashukuru kwamba umenijua, lakini naona uchungu kuwa nitayashuhudia mauti yako muda si mrefu.”
“Kwa nini unaniambia hivyo, Yasmin? Niambie.”
Yasmin, badala ya kunijibu, aliangua kilio.
Wenzangu mmoja mmoja wakaanza kuingia mle chumbani na kushangaa kumuona yule msichana akilia.
“Je, ni nani huyu?” Mmoja wa wale wenzangu akaniuliza wakati wenzetu wengine walikuwa wamepigwa na butwaa.
“Ni msichana nimemkuta amelala humu chumbani. Nilipoingia alizinduka na kuniambia anaitwa Yasmin. Ni binti wa Rais wa Comoro,” nikawaeleza.
“Ni binti wa Rais wa Comoro?” Baadhi ya wenzangu wakaniuliza kwa mshangao. Walidhani labda nilikosea kusema.
“Ndiyo, mwenyewe ameniambia hivyo na mimi pia namfahamu. Nilihudhuria harusi yake nchini Comoro mwaka uliopita.”
“Si ilisemekana kuwa yule binti alitoweka?” Mmoja wa wenzangu akauliza.
“Ni kweli. Mimi pia nimeshangaa kumkuta katika kisiwa hiki, tena akiwa peke yake. Na amenieleza kitu cha kutisha.”
“Kitu gani?”
“Mh! Ameniambia anaona uchungu kuwa atayashuhudia mauti yetu muda si mrefu!”
Wenzangu wote wakashituka, ndipo nilipojua kuwa hakuna mtu anayependa kufa.
“Kwa nini amekwambia hivyo?” Sauti za kuuliza zilisikika kutoka kwa wenzangu.
“Ndiyo nilikuwa namuuliza, naona analia.”
“Asilie, atueleze ili tujue…”
“Usilie dada yangu, nyamaza utueleze ili tujue jinsi ya kujihami,” nikamwambia msichana huyo.
“Pia atueleze jinsi alivyofika katika kisiwa hiki cha ajabu,” mtu mwingine akasema.
Yasmin akajifuta machozi yake kwa shuka aliyokuwa amejifunga kisha akainua uso wake na kututazama.
Sasa macho yake yalikuwa mekundu na uso wake ulikuwa umeiva.
“Wiki moja kabla ya harusi yangu huko Comoro, nilikiota hiki kisiwa. Nikamuota kichaa mmoja akiniambia siku zangu zimekaribia za kuja kukaa katika kisiwa hiki,” Yasmin akaanza kutueleza. Tukawa tunamsikiliza kwa makini.
Akaendelea. “Nikamwambia yule kichaa, siwezi kuja kukaa hapa, mimi natarajia kufunga ndoa hivi karibuni. Nitakwenda kukaa Ufaransa, si hapa.
“Yule kichaa akaniambia, ndoa yangu nitafunga na yeye, kwani yeye alinichunuka tangu nilipokuwa nasoma na hatakubali niolewe na mtu mwingine.
“Nilipoamka asubuhi, nilipuuza ile ndoto. Sikumuelezea mtu yeyote na kwa kweli nilifanya kosa kuipuuza, pengine nisingekuwa hapa leo hii. Yaani mpaka leo hii ninajuta.”
Msichana huyo akaendelea kutueleza. “Ile siku ya harusi yangu ilipofika saa mbili usiku, niliona kizunguzungu. Macho yangu yakafunga kiza. Nikaona kama moyo wangu unanisokota na ghafla nikapiga ukelele na kuanguka chini. Baada ya hapo sikujijua tena.
“Nilizinduka asubuhi na kujikuta nimo ndani ya jumba hili katika kisiwa hiki. Mbele yangu nikamuona yule kichaa niliyemuota akiniambia kuwa nitakuja kukaa hapa.”
“Yule mtu niliyemuota hakuwa binadamu, bali alikuwa jini aliyekuwa amenichunuka. Siku ile nilipomuota nilimuona katika sura ya kibinadamu, kichaa, lakini nilipozinduka nikiwa katika jumba hili alikuwa katika sura na umbile la kijini,” Yasmin aliendelea kutueleza. Kisa chake kilikuwa kimetushangaza na kutuogopesha.
Akaendelea. “Huyo jini aliponiona nimeshituka, aliniambia, ‘Yasmin, usiogope, umeshafika nyumbani kwako, mimi ndiyo nitakuwa mume wako. Utaishi katika jumba hili na hutarudi tena kwenu.’
“Akaniambia kwamba yeye ni jini wa ukoo wa Kisubiani Makata. Jina lake ni Harishi wa Harishan. Chakula chake ni damu ya binadamu. Ameniambia wazi kuwa yeye ni jini mbaya aliyelaaniwa na ameshaua watu wengi.
“Akanihadithia kisa cha kisiwa hiki. Aliniambia kilikuwa kinaishi watu zamani na mfalme wao alikuwa akiishi katika jumba hili. Lakini yeye Harishi ndiye aliyewaua mmoja mmoja kwa kuwafyonza damu hadi kukimaliza kisiwa chote.
“Watu wachache waliobaki waliondoka na kukiacha kisiwa kikiwa kitupu. Ndiyo sababu mlikuta magofu matupu na mifupa ya watu waliouawa na Harishi. Siku za mwanzo mwanzo mji huu ulikuwa haukaliki kwa harufu zilizotokana na maiti za watu. Kunguru wa Zanzibar walihamia hapa kujipatia riziki zao. Sasa hivi iliyobaki ni mifupa mitupu.
“Kwa sasa kisiwa hiki kinajulikana kama Kisiwa cha Mauti. Wavuvi ambao hawajui habari za kisiwa hiki wakifika hapa kushona nyavu zao, Harishi aliwaua mmoja mmoja kwa kuwafyonza damu.”
Maelezo ya Yasmin yalitufanya tutazamane mara kwa mara huku nyuso zetu zikiwa zimepigwa na butwaa. Hatukuwahi kusikia kisa cha ajabu kama kile.
“Mimi nilikuwa nikilia peke yangu hadi sasa silii tena. Ni kama nimeshazoea kuishi na yule jini,” Yasmin aliendelea kutueleza.
“Kila wiki anakuja mara moja. Au kama nina dharura ninamuita, anakuja. Humu ndani mna kila kitu. Mna kila aina ya vyakula. Huwa najipikia mwenyewe chakula ninachotaka. Vyakula vikipungua, ananiletea vingine.
“Pia ananiletea nguo za kifalme pamoja na dhahabu. Huwa anaiba nguo hizo katika kasri za wafalme na marais. Kila kitu ninachotaka ananileta, lakini hainisaidii. Maisha ya upweke yananifanya nijione kama nimo ndani ya kaburi.”
Wakati Yasmin anatuhadithia kile kisa, nilimuuliza, “Umetuambia huyo jini anafyonza damu za watu na kuwaua, je, wewe utaendelea kuwa salama kweli?”
“Mimi nimeshakuwa mke wake. Ameniambia damu yangu ni haramu kwake. Hawezi kuniua, ila hatanirudisha tena kwetu. Nitaendelea kuishi hapa hadi mauti yanikute,” Yasmin alituambia.
Kwa kweli, hayakuwa maneno ya kuogopesha tu, bali pia yalikuwa yanasikitisha sana.
Maisha ya Yasmin yalikuwa yanasikitisha. Alionesha wazi kukata tamaa, pia niliona kwa vyovyote itakavyokuwa, maisha yake yatakuwa mafupi.
“Kwa hiyo sisi hatutapona?” Mwenzetu mmoja akamuuliza Yasmin.
“Siwezi kuwaficha, nawaeleza ukweli ili mjue kuwa saa zenu zimekaribia sana.”
“Je, kama tutaondoka ndani ya jumba hili na kwenda kujificha mahali pengine?”