Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KISIWA CHA UMAUTI - 39

KISIWA 39 Pict

ILIPOISHIA

Haukupita muda polisi wakafika. Nikaambiwa niende kituo cha polisi kuandikisha maelezo yangu kwa vile tulipotea na chombo baharini na wenzangu walifikwa na umauti.

Polisi hao wakanichukua kituo cha polisi ambako walinihoji maswali wakitaka kujua jinsi chombo chetu kilivyozima moto siku ile hadi tukatokea katika kile kisiwa.

Nikawaeleza kila kitu walichoniuliza hadi wenzangu walivyouawa mmoja mmoja.

SASA ENDELEA...


Baada ya kuandikisha maelezo yangu, niliruhusiwa kuondoka.

Kusema kweli, licha ya furaha iliyokuwa nyumbani kwetu, kwa baadhi ya majirani zetu ilikuwa ni huzuni kutokana na vifo vilivyowakuta wenzangu.

Wengi wa marehemu hao waliacha wake na watoto na mimi ndiye niliyethibitisha vifo vyao. Iliwapa huzuni watu wengi kwa vile wenzangu waliokufa waliuawa kikatili.

Baada ya kupita wiki moja ndipo nilipoanza maandalizi ya kwenda Comoro. Nilikwenda Unguja kuulizia ndege itaondoka lini. Nilipojua siku ya kuondoka kwa ndege, nilirudi Pemba kuendelea na maandalizi yangu ya safari. Siku mbili kabla ya safari, nilipiga simu kwa namba aliyonipa Yasmin. Aliyepokea simu alikuwa kaka wa Yasmin.

Nikajitambulisha kwake kuwa ni Zahran wa Zanzibar, akanikumbuka.

“Oh, Zahran unaendeleaje?”

“Naendelea vizuri, sijui nyinyi huko?”

“Sisi hatujambo. Ngoja nikuunganishe na Yasmin kwenye simu yangu.”

Nilisubiri kidogo kisha nikasikia sauti ya Yasmin ikisema, “Hello!”

Nikataka kujibu lakini nikaisikia sauti ya kaka wa Yasmin ikisema.

“Zungumza na Zahran kutoka Zanzibar.”

“Hello Zahran!” Sauti ya kusisimua ya Yasmin ikasikika tena.

“Ndiyo Yasmin, hujambo?”

“Sijambo, nakuhofia wewe.”

“Mimi sijambo. Nataka kukufahamisha kuwa kesho kutwa ninakuja Comoro.”

“Njoo tu, usiwe na wasiwasi. Utaondoka saa ngapi?”

“Sijajua muda, lakini nitakufahamisha nitakapokata tikiti kesho.”

“Utanipigia simu kesho?”

“Ndiyo, nitakupigia kukufahamisha muda wa kuondoka kwa ndege.”

“Sawa. Nitasubiri simu yako.”

Siku ile ile niliondoka kwenda Unguja. Nilifuatana na kaka yangu Shaali. Unguja tulilala kwenye nyumba ya wageni. Siku ya pili yake nilikwenda kukata tikiti ya ndege ya kwenda Comoro.

Ndege ilikuwa inaondoka kesho yake saa mbili asubuhi. Baada ya kupata tikiti na kujua muda wa safari, nilimpigia tena simu kaka wa Yasmin ambaye aliniunganisha na Yasmin.

“Asalaam alaykum,” Yasmin akanisalimia.

“Wa alaykum salaam. Habari ya tangu jana?”

“Nzuri, sijui nyinyi?”

“Sisi hatujambo, tunashukuru. Nimeshakata tikiti ya ndege ya kesho.”

“Ndege itaondoka saa ngapi?”

“Itaondoka saa mbili asubuhi.”

“Basi tutakusubiri kiwanja cha ndege.”

“Nitashukuru sana.”

Nilipomaliza kuzungumza na Yasmin, kaka yangu aliniambia.

“Inaonekana utapata mapokezi makubwa. Natamani tungekuwa sote.”

Aliponiambia hivyo nikacheka.

Siku iliyofuata saa kumi na mbili asubuhi, mimi na kaka yangu tukawa kiwanja cha ndege cha Unguja. Kaka yangu alikuwa amefuatana na mimi kwa ajili ya kunisindikiza.

Baada ya kukamilisha taratibu zote za safari, nikawa kwenye chumba cha abiria wanaosubiri kujipakia kwenye ndege. Nilikuwa nimeshaagana na kaka yangu na alikuwa akisubiri kuona tukijipakia kwenye ndege.

Muda ulipowadia, tangazo lilitolewa kuwa abiria wanaokwenda Comoro wajipakie kwenye ndege. Tangazo likaeleza kuwa ndege itaondoka saa mbili kamili.

Abiria wote tuliokuwa tunakwenda Comoro tukanyanyuka na kwenda kujipakia kwenye ndege. Tulisubiri kwa dakika kadhaa kabla ya tangazo la kuruka kwa ndege kutolewa.

Tulitajiwa majina ya marubani wetu na masafa ambayo ndege ingeruka.

Tangazo hilo lilitaka tujifunge mikanda ili tusipate usumbufu wakati ndege inaruka. Ndege ilianza kuvuta kasi. Wakati namaliza tu kujifunga mkanda, ndege ilianza kuruka.

Ilikuwa ni mara yangu ya tatu kupanda ndege. Mara ya kwanza ilikuwa ni wakati ninakwenda Comoro kwa ajili ya harusi ya Yasmin na mara ya pili niliporudi Zanzibar kutoka Comoro.

Ulikuwa mwendo wa saa nne. Ndege ilitua katika kiwanja cha Moroni, moja ya visiwa viwili vinavyounganisha Jamhuri ya Comoro.

Mlango wa ndege ulipofunguliwa, abiria tulianza kushuka kwenye ndege. Tulishuka ngazi ya ndege tukaingia kwenye mlango wa jengo la kiwanja cha ndege.

Mara tu nilipokamilisha taratibu za uhamiaji na kukaguliwa, niliingia katika ukumbi ambako nilikutana na Yasmin.

Yasmin alikuwa amesimama na kikundi cha watu wakinisubiri. Watu hao walinilaki kwa bashasha, nikajiona kama mfalme.

Yasmin alinitambulisha kwa mama yake na wadogo zake wawili wa kike. Pia alikuwepo kaka yake na maafisa usalama kadhaa.

Baada ya kuulizana hali, Yasmin alishika begi langu tukatoka nje ya kiwanja.

Kulikuwa na magari matatu ya familia ya rais na gari moja la serikali.

Mimi na Yasmin tulipanda gari la peke yetu. Nilijisikia furaha sana kupanda gari moja na Yasmin. Mama yake Yasmin alipanda gari la peke yake.

Kaka yake Yasmin na wadogo zake wawili walijipakia katika gari moja. Katika gari la serikali walipanda maafisa usalama peke yao.

Msafara wa magari wa kuelekea mjini ukaanza. Kilichokuwa kinaonekana hapo ni kuwa nilikuwa mgeni wa heshima kubwa.

Baada ya mwendo wa takriban nusu saa, msafara huo ulisimama mbele ya hoteli moja mashuhuri nchini Comoro.

Ilikuwa hoteli iliyokuwa ikimilikiwa na kaka wa Yasmin.

Tukashuka kwenye magari na kuingia katika hoteli hiyo iliyokuwa karibu na ufukwe wa bahari.

Nilikuwa nimekodishiwa sehemu ya familia ambayo ilikuwa na vyumba vitatu, sebule na chumba cha kulia chakula. Vyumba vya aina hiyo vilikuwa vinakodiwa na wageni mashuhuri kutoka nchi za nje. Mswahili kama mimi, ilikuwa ndoto kukaa mahali hapo kwa sababu gharama yake ilikuwa kubwa.

Nilihisi kuwa familia ya kina Yasmin ilikuwa imenipa heshima kubwa sana. Mara tu tulipofika hapo hotelini, walifika waheshimiwa wawili wa serikali ya Comoro. Mmoja alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na mwingine alikuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje.

Walizungumza na mimi kwa karibu nusu saa. Walitaka kupata maelezo yangu kuhusu kukutana kwangu na Yasmin katika kile kisiwa tulichokuwa. Baada ya mazungumzo yetu waliondoka.

Wakaja makachero wa serikali ya Comoro ambao pia walitaka kupata maelezo yangu. Wao walinihoji maswali mengi sana ambayo niliweza kuyajibu.

Makachero hao walipoondoka, walifika waandishi wa habari wa Comoro. Walikuwa waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari kuanzia magazeti, redio na televisheni.

Walinihoji maswali mengi hadi walipoondolewa na maafisa usalama. Wakaondoka.

Baada ya hapo nikapata nafasi ya kuzungumza na ndugu na jamaa wa Yasmin ambao walifika pale hotelini kuniona na kunitakia maisha mema.

Mchana nilikaribishwa chakula nyumbani kwa mke wa rais. Kilikuwa chakula cha heshima kubwa ambacho kilihudhuriwa na watu wa familia ya rais, ingawa rais mwenyewe hakuwepo.

Saa tisa mchana nilipelekwa Ikulu ambako nilikutana na Rais wa Comoro. Katika dakika kadhaa za mazungumzo yetu niligundua kuwa rais huyo alikuwa mtu mcheshi na mkarimu sana.

Alinishukuru na kunipongeza sana, kisha alinikaribisha rasmi nchini Comoro.

Kwa muda wa wiki nzima nilikuwa katika pilikapilika za kupelekwa huku na huku kama mgeni wa shani. Wakati wote Yasmin alikuwa sambamba na mimi.

Pale hotelini nilipofikia nilikuwa nikihudumiwa na wafanyakazi wa hoteli na kupewa heshima wanayopewa watu wa familia ya rais.

Baada ya kupita wiki moja ndipo Yasmin alipoanzisha mazungumzo ya ahadi yetu ya kuoana. Kila tulipokuwa peke yetu alikuwa akinikumbusha tulivyokuwa katika kile kisiwa cha Harishi.

Aliniambia kwamba wapelelezi wa Kifaransa walikwenda kukichunguza kisiwa hicho ili kuthibitisha kama kweli tulikuwa katika kisiwa hicho.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, Yasmin aliniambia, kisiwa hicho kilikumbwa na gharika miaka mia moja iliyopita na kusababisha watu wote kufa na kubaki majumba pekee.

Yasmin akanieleza kuwa wapelelezi hao walidai kuwa kila baada ya miaka mia moja gharika hutokea katika kisiwa hicho.

“Lakini sisi tuliona si kweli kwa sababu tulimshuhudia wenyewe kiumbe aliyekuwa anaua watu katika kisiwa kile na si mwingine bali ni Harishi,” Yasmin akaniambia.

“Wazungu wanaamini zaidi sayansi. Madai ya mashetani au majini hawayaamini. Lakini wazazi wangu na wananchi wa Comoro wameyasadiki maelezo yetu,” Yasmin aliendelea kuniambia.

Akaniambia, “Baba yangu aliniitia masheikh wakanifanyia visomo na kuniombea dua.”

Kuhusu mazungumzo ya uchumba wetu, Yasmin akaniambia niandike barua ya uchumba kwa wazazi wake.

“Oh, ninaogopa sana!” nikamwambia.

“Unaogopa nini sasa? Huo ndio utaratibu. Wao wanajua kila kitu lakini ni lazima ufuate utaratibu. Si unajua mimi ni binti wa rais?”

Siku iliyofuata nikaandika barua ya uchumba. Barua hiyo ilipelekwa kwa wazazi wa Yasmin. Siku mbili baadaye nikapata jibu kuwa ombi langu limekubaliwa.

Baba wa Yasmin aliniambia, “Nitakuoza binti yangu bila kutaka mahari yoyote kutoka kwako na nitakupa makazi hapa Comoro.”

Ilikuwa furaha iliyoje kupata jibu hilo.

Mimi na Yasmin tukaandaliwa kwa ajili ya harusi. Wazazi wangu pamoja na kaka yangu mkubwa waliitwa kutoka Zanzibar.

Siku iliyopangwa harusi ikawadia. Nikaozeshwa Yasmin katika sherehe iliyofana sana.

Hadi ninasimulia kisa hiki, niko Comoro ambako ninaishi na mke wangu Yasmin. Tumeshapata mtoto mmoja wa kiume mwenye afya njema. Maisha yetu ni ya furaha.

Siku moja Yasmin aliniambia, “Kweli ndoa hupangwa mbinguni. Mume wangu ulikuwa ni wewe. Nitakupenda mpaka kufa!”