Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KISIWA CHAMAUTI - 37

KISIWA 37 Pict

ILIPOISHIA

Hewa ile ilikuwa inaniliwaza kuliko manukato ambayo hujitia mwilini mwake.

“Nitasubiri. Sina la kufanya” nikamwambia kwa sauti nzito ya huzuni.

“Tutakutana mahabuba wangu. Sitakuacha” Yasmin akaniambia kwa sauti ya chini. Hakutaka isikiwe na wengine.

Sasa msafara ulikuwa unakwenda kiwanja cha ndege. Na mimi nililazimika kuwasindikiza nikiwa pamoja na maofisa usalama.

SASA ENDELEA...


GGiza lilikuwa limeshaanza kuingia na taa za mji wa Unguja zilikuwa zimewashwa. Tulikuwa katika basi dogo ambalo liliweza kutupakia sote. Gari la maofisa usalama lilikuwa limetutangulia.

Tulipofika kiwanja cha ndege, niliagana na kaka wa Yasmin, kisha nikaagana na Yasmin mwenyewe. Kwa mara ya kwanza, Yasmin hakuona aibu kunikumbatia mbele ya macho ya kaka yake.

Kwa mujibu wa tamaduni za Wangazija wa Comoro, kitendo hicho kwa watu wa jinsia tofauti ambao si ndugu kilikuwa ni cha faragha sana. Lakini Yasmin alikifanya kuonyesha mapenzi yake kwangu.

Wakati ananiachia, aliupeleka haraka mkono wake kwenye macho yake kufuta machozi yaliyoanza kumtiririka.

“Kwaheri, tutaonana,” akaniambia na kunisisitizia, “Nitakusubiri Comoro. Usichelewe kuja. Usiwe na majonzi, tutaonana.”

Yasmin alijaribu kutabasamu licha ya uso wake kujaa huzuni. Tabasamu lake lilinifariji sana.

Maofisa usalama walikuwa wakimtazama Yasmin alivyokuwa ananiaga kabla ya kugeuka na kuungana na wenzake.

Sikuondoka hapo kiwanjani hadi ndege waliyosafiri kina Yasmin iliporuka na kuanza safari.

Nilijisikia mwenye majonzi sana lakini nilijikaza.

“Wewe hujui kama yule ni binti wa rais?” Afisa usalama mmoja aliniuliza wakati tunaondoka kiwanjani hapo.

“Ninajua,” nikamjibu.

“Sasa mbona unataka kututia aibu? Unataka kwenda naye wapi?”

Swali hilo lilinikera sana. Nikamtazama yule afisa usalama aliyetaka kunishushua.

“Yeye ndiye aliyeomba aondoke na mimi,” nikamwambia.

“Wewe pia si ulikuwa unataka kwenda?”

Nilijua kuwa yule afisa alikuwa ameona donge. Nilitaka kumuuliza, “Sasa kinakuuma nini?” lakini nilimstahi. Nikamwambia, “Ni baada ya yeye kutaka aondoke na mimi.”

“Sasa yule ni binti wa rais, wewe huwezi kufuatana naye. Ukifika huko utasema nini?”

Niliona nisijibizane naye. Nikaamua kubaki kimya.

Maofisa hao walinipakia kwenye gari na kunirudisha kule hotelini. Wakaniambia nitalala pale na asubuhi nirudi Pemba.

“Tutakufuata asubuhi tukupeleke bandarini,” afisa mmoja akaniambia.

Nikamjibu, “Sawa.”

Nililala pale hotelini. Usiku kucha nilikuwa namuwaza Yasmin. Asubuhi, simu iliyokuwa mle chumbani ikaita. Nilipoipokea, niliambiwa nipokee simu yangu kutoka Comoro.

Hapo hapo nilisikia sauti niliyoitambua kuwa ni Yasmin ikinisalimia.

“Subalheri muadhamu (asubuhi njema mpendwa).”

“Subalnuur azizi (asubuhi yenye nuru mrembo).” Kwa kutaka kuhakikisha kuwa alikuwa Yasmin, nikamuuliza, “Wewe ni Yasmin?”

“Naam, ndiye mimi. Nilitaka kukujulia hali.”

“Nashukuru, mimi sijambo. Je, mlifika salama?”

“Alhamdulilahi. Tulifika salama. Nimekutana na wazazi wangu na ndugu zangu na pia wananchi wenzangu. Wamefurahi kuniona na mimi nimefurahi kuwaona. Kumbe bado uko hapo hotelini?”

“Ninaondoka hii asubuhi kwenda Pemba na mimi nikaonane na wazazi wangu pamoja na ndugu zangu. Najua wameshanikatia tamaa.”

“Ni kweli. Basi ukifika unaweza kunipigia kwa kutumia zile namba ulizopewa na kaka.”

“Sawa, nitakupigia.”

“Ongea na mama yangu.”

Mara nikasikia sauti nyingine ikiniuliza, “Hujambo mwanangu?”

“Sijambo mama. Habari za huko?”

“Huku ni salama. Unajisikiaje, hali yako?”

“Hali yangu ni nzuri. Nashukuru.”

“Pole sana kwa masahibu yaliyowafika.”

“Tumeshapoa, mama.”

“Tunakusubiri kwa hamu huku. Utakuja lini?”

“Siku ya kuja nitawambia. Kwanza nataka nifike Pemba nikawaone wazazi na ndugu.”

“Basi utatujulisha siku utakayokuja tukupokee.”

“Asante mama. Nitawajulisha.”

“Nampa simu Yasmin.”

“Haya, mpe.”

“Hallo Zahran!” Sauti ya Yasmin ikasikika.

“Ndiyo, Yasmin.”

“Usijali kuwa mbali nami, inshallah tutakuwa pamoja. Nimeshamweleza mama yangu kilicho ndani ya moyo wangu kuhusu wewe.”

Aliponiambia hivyo, mwili wangu ulisisimka.

“Hakuna tatizo, Yasmin. Wewe pia usijali.”

“I miss you,” Yasmin akaniambia kwa Kiingereza.

“I miss you too.”

“Bye bye (baibai),” akaniaga.

“Bye…”

Simu ikakatwa.

Mara tu baada ya kupata kifungua kinywa, maafisa usalama wawili walifika hapo hotelini kunichukua.

Walinipakia kwenye gari wakanipeleka bandarini. Walikuwa wameshanikatia tikiti ya meli inayokwenda Pemba ambayo ingeondoka saa nne asubuhi ile.

Mara tu baada ya tangazo la kujipakia kwenye meli kutolewa, nilijipakia na kuketi kwenye siti. Muda wa safari ulipowadia, tukaondoka.

Safari ilikuwa njema na tulifika Pemba jioni ya siku ile. Huko Pemba nilikuwa nikiishi kijijini. Licha ya habari zangu kuandikwa kwenye magazeti ya siku ile pamoja na kutangazwa kwenye redio, watu wa kwetu hawakuwa na taarifa yoyote juu ya kupatikana kwangu.

Laiti ningekuwa na simu, ningewapigia na kuwajulisha kuhusu safari yangu, lakini sikuwa nayo. Tulishuka bandarini, nikaingia mjini nikiwa na begi langu lililokuwa na nguo zangu nilizozawadiwa. Nikaenda kwenye kituo cha mabasi na kutafuta basi linalokwenda kwetu.

Nilipolipata, nilijipakia na kuwafikiria wazazi wangu na ndugu zangu watakavyoshituka watakaponiona.

Muda ulipowadia, safari ya kuelekea kwetu ikaanza. Ulikuwa mwendo wa saa moja. Basi lilipofika kijijini kwetu, nilishuka. Nikaanza tena mwendo wa miguu kuelekea nyumbani kwa wazazi.

Ndugu zangu, jamaa na marafiki walikuwa wamekusanyika nyumbani kwa wazazi wangu wakijadiliana juu ya taarifa walizozisikia za kupatikana kwangu.

Kuna waliodai kuwa walizisikia taarifa hizo kupitia vyombo vya habari. Kuna waliosema taarifa hizo wamezisikia lakini Zahrani aliyetajwa siye mimi. Na kuna waliobisha kabisa kuwa hakukuwa na habari kama hizo.

Kutokea kwangu ndiko kulikomaliza ubishi huo. Nilitokea ghafla. Watu wote walishituka waliponiona. Hawakuamini kuwa nilikuwa mimi.

Nikatoa, “Assalam alaykum,” kubwa.

Badala ya watu kuitikia salamu yangu, walipatwa na mshangao.

“Wewe ni Zahran?” Baba yangu akaniuliza.

Sikuwa na muda wa kumjibu, bali nilimkumbatia kwa furaha. Kwa muda wa dakika kumi hivi nilikuwa na kazi ya kukumbatia watu mbalimbali kwa furaha.

Mama yangu ndiye aliyenitia huzuni. Aliponiona tu, aliangua kilio.

Nikamnyamazisha na kumwambia asilie kwa sababu nimepona.

“Mama, ungelia kama ningekufa,” nikamwambia.

Mama akanielewa, akanyamaza.

“Pole sana mwanangu, sisi tulijua umeshakufa. Hizi habari za kuja kwako tulizisikia lakini hatukuziamini.”

“Nimepona, mama, lakini nimeponea tundu la sindano,” nikasema nikiwa nimewaelekea watu walionizunguka.

“Hebu tueleze mkasa uliowafika,” baba yangu akaniambia.

Nikaanza kueleza jinsi chombo chetu kilivyozimika moto ghafla na kuelea baharini kwa siku kadhaa hadi tukaishiwa chakula na maji.

“Nakumbuka ni siku ya tano tulipotokea kwenye kisiwa kisicho na watu lakini kina mji wenye majumba na visima vya maji,” nikawaeleza.

“Ni kisiwa gani hicho?” Mmoja wa ndugu zangu akaniuliza.

“Sikijui, ndiyo tulikiona siku hiyo. Tulipokiona kisiwa hicho tulidhani tumesalimika, kumbe ndiyo tulikuwa tumeingia kwenye hatari kubwa iliyosababisha wenzangu wote kuuliwa.”

Nilivyoanza kueleza jinsi tulivyomkuta binti wa Kikomoro aliyekuwa amekumbwa na jini siku ya harusi yake na kupelekwa katika kisiwa hicho, watu wote walipigwa na butwaa.

“Ni binti wa Rais wa Comoro aliyekuwa akiishi peke yake katika kisiwa hicho,” nikawaeleza na kuendelea.

“Yeye ndiye aliyetueleza kuwa kuna jini anayeitwa Harishi ambaye ameua watu wote katika kisiwa hicho na kwamba maisha yetu na sisi yalikuwa mashakani!”

Nikaeleza jinsi Harishi alivyofika katika jumba alilokuwa akiishi binti huyo na kumuua mwenzetu wa kwanza kwa kumtoboa utosi na kumfyonza damu na kumla ubongo.

Nikaendelea kueleza jinsi wenzangu wote walivyouawa kikatili na Harishi mmoja baada ya mwingine huku tukiendelea kuhangaika kutafuta pa kujificha.

Watu waliokuwa wananisikiliza walianza kububujikwa na machozi waliposikia habari za mauaji ya kikatili yaliyowatokea wenzangu na mateso tuliyopata.

Lakini walipatwa na mshangao zaidi niliposimulia jinsi tulivyosalimika mimi na Yasmin, mwenyeji wangu niliyemkuta katika kisiwa hicho.

Tukio lile la kumfungia Harishi kwenye chupa na kwenda kuizamisha kwenye bahari lilivuta hisia za watu wote, wakajikuta wananipa mkono wa kunipongeza.

Mwisho, niliwaeleza tulivyookolewa kutoka katika kisiwa hicho na kupelekwa Unguja kwa helikopta. Huko Unguja tukafanikiwa kukutana na Rais wa Zanzibar.

“Jana ndege ya Comoro ilikuja kumchukua Yasmin kumrudisha kwao. Alitaka aondoke na mimi lakini sikuwa na paspoti na pia sikuwa nimewaona ndugu zangu,” nikawaambia na kuongeza.

“Yasmin nimempenda na yeye amenipenda. Ameniahidi kuwa tutaoana. Leo asubuhi mama yake mzazi amenipigia simu kunijulia hali na kuniuliza nitakwenda lini Comoro.”