Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KISIWA CHA MAUTI – Sehemu ya 5

KISIWA 05 Pict

KWA KIFUPI

Nikamkubalia na kutoka ofisini mwake. Nikarudi nyumbani.

Siku iliyofuatia nikaenda kazini kwangu. Nilifanya kazi hadi saa nane nikitazamia Makita au meneja wa hoteli yake wangenipigia simu. Lakini sikupata simu yoyote kutoka kwao. Nikaamua kupanda pikipiki na kwenda tena Masaki.

Nilipofika pale hotelini nililiona gari la kifahari ambalo nilishuku kwamba ndilo alilokuwa akilitumia Makita. Nikaacha pikipiki na kuingia ndani ya hoteli hiyo. 

SASA ENDELEA...


NILIKWENDA pale mapokezi nikaamulizia meneja. Nilipoambiwa yupo ofisini, nikaingia.

“Oh Karibu!” akaniambia aliponiona.

“Asante.  Habari ya tangu jana?” nikamsalimia huku nikikaa kwenye kiti.

“Nzuri. Vipi hajakupigia?” akaniuliza.

“Hajanipigia, ndiyo maana  nimerudi tena”

“Alipokuja leo asubuhi nilimfahamisha kwamba unamtafuta nikampa  namba yako ya simu. Akaniambia  kama utakuja tena  umueleze shida yako kwa maandishi. Uyawache hapa ili akija tumpe”

“Lakini hivi sasa si yupo, maana nimeona gari hapo nje. Ninahisi ni la kwake”

Yule  msichana alihamaki kidogo.

“Wewe unataka gari au unamtaka yeye mwenyewe?” akaniuliza akiwa amenikazia macho.

“Ninamtaka yeye mwenyewe lakini lile gari ni kielelezo kwamba yupo”

“Hata kama yupo. Yeye ameshatoa agizo  kwamba ukija umueleze shida yako kwa maandishi. Sasa unataka nini tena?’

“Nimekuelewa dada yangu. Shida yangu ni maswali tu. Kuna mambo ambayo tunataka ayatolee ufafanuzi”

“Sasa mwandikie maswali yako halafu majibu yake utayapata kupitia kwangu”

“Sitaweza kukutana  na yeye uso kwa uso?”

“Labda baada ya kuona maswali yako anaweza kutafuta muda wa  kuonana  na wewe. Unajua huyu mtu ana shughuli nyingi sana. Kila kitu ni lazima akipangie muda”

“Sawa. Nimekuelewa” nikamwambia huku nikitoa notibuku yangu ya mfukoni na kuiweka juu ya meza. Wakati nataka kuchomoa kalamu, yule msichana akanipa kalamu yake.

“Kalamu hii  hapa” akaniambia.

Nikaichukua ile kalamu na kuandika  maswali yangu, kwanza yalihusu kufunguliwa Makita kesi ya madai na aliyekuwa mke wake ambaye baadaye alifariki katika  mazingira ya kutatanisha. Na pili madai ya kumiliki mali yakiwemo majumba  ya kifahari katika maeneo mbali mbali ya jjiji la Dar es Salam pamoja na madai kwamba aliamua kujiuzulu mwenyewe wadhifa wake kwa kuogopa kufichuliwa utajiri wake ambao aliupata akiwa mtumishi wa umma.

Nilijua  maswali yale yangemkera lakini nilichokuwa ninakitaka mimi ni ufafanuzi wake tu.

“Kuna bahasha?” nikamuuliza yule msichana.

“Bahasha zipo” akanijibu na kufungua dawati la meza yake. Alichomoa bahasha moja ya kaki na kunipa.

Niliichomoa ile karatasi niliyokuwa nimeiandika, nikaikunja na kuitia ndani ya ile bahasha ambayo niliibana. Nikaiandika juu kisha  nikampa yule msichana.

“Basi akija tutampa” akaniambia.

“Sawa” nikamwambia huku  nikimrudishia kalamu yake na kuinuka.

Nikakumbuka swali muhimu.

“Sasa nije lini kufuata majibu yangu?”

“Njoo kesho muda kama  huu”

“Asante. Kwaheri” nikamuaga na kuelekea kwenye  mlango.

Wakati nafungua mlango niligeuza uso wangu nyuma, nikamuona akinitazama kwa makini.

Nikageuza uso wangu  na kutoka.

Wakati nikiwa nje ya  hoteli, Kabwe akanipigia simu.

“Habari yako kaka?” akanisalimia baada ya kupokea simu yake.

“Nzuri. Habari ya tangu juzi?”

“Ni nzuri pia. Vipi maendeleo?”

“Tunashukuru Mungu”

“Ile habari bado sijaiona  kwenye gazeti”

“Bado tunaifanyia kazi. Tutakapoichapisha nitakufahamisha”

“Sawa kaka. Asante sana”

Akakata simu.

Ndipo nilipoifuata pikipiki na kuiwasha. Pikipiki ilipowaka nikapanda na kuondoka. Wakati naendesha nilihisi kuwa Makita alikuwa amepatwa na hisi ya hatia baada ya kuambiwa kuwa anatafutwa na mwandisi wa habari. Hicho ndicho kilichomfanya asitake  kukutana  na mimi na badala yake akataka niandike maswali yangu.

Kwa vile shida yangu ilikuwa ni  kupata ufafanuzi  kutoka kwake hata kama ni wa maandishi, sikuona  vibaya kuacha maswali kwa msaidizi wake.

Nilirudi ofisini kwetu, nikaingia ofisini kwa mhariri wangu na kumueleza kilichotokea katika hoteli ya Makita.

“Kama ametaka uache maswali yako na umeyaacha ni sawa. Hakuna tatizo.Tunachotaka sisi ni maelezo yake yawe ya mdomo au maandishi” Mhariri wangu akaniambia.

“Bila shaka aliposikia anatafutwa na mwandishi wa habari ameingia uoga, hajui ataulizwa nini”

“Inaelekea ni mtu ambaye anaishi kwa wasiwasi. Anajua wakati  wowote vyombo vya habari vinaweza kumfichua. Lakini  wewe nenda tena hapo kesho ufuatie majibu yake”

“Sawa”

“Sasa kamanda wa polisi wa mkoa wa Pwani utakwenda kumhoji lini? Au umeshasahau?”

“Sijasahau. Nimeona kwanza nianze na Makita  halafu nitakwenda kumuona huyo kamanda”

“Sawa. Kuwa makini”

“Umakini ndiyo hulka yangu mkuu”

Nilipomwambia hivyo mhariri, niliinuka nikamuaga na kuondoka. Stori ile ya Makita ilikuwa kama imenipa likizo  nisifanye kazi zingine. Baada ya kuondoka ofisini kwa mhariri nilitafuta kompyuta iliyokuwa tupu nikakaa na kuingia kwenye mitandao.

Jua lilipokuchwa nikarudi nyumbani.

Siku iliyofuata nilisubiri hadi saa nane.Nilipoona sijapigiwa simu nikachukua pikipiki na kurudi tena Masaki.

Nilipofika  niliingia hotelini na kufanikiwa kuonanana tena na meneja.

Hakuonesha kunifurahia kama jana yake na juzi yake. Nikashuku huenda Makita alimhadharisha kuhusu waandishi wa habari.

“Nimefuatia majibu yangu” nikamwambia  baada ya kusalimiana naye.

“Nimempa bosi karatasi iliyokuwa na maswali yako, ameisoma lakini hakunipa jibu lolote. Alichoniambia ni kwamba utakapokuja nimpigie simu kumfahamisha ili muongee. Kwa hiyo ametaka umsubiri ukumbini” Meneja akaniambia huku akiinuka kwenye  kiti.

“Twende nikupeleke mahali ambapo utamsubiri.” Nikatoka mle ofisini na yule msichana. Akanipeleka katika  ukumbi  mdogo wa hoteli hiyo ambao haukuwa na mtu yeyote.

“Utakaa hapa mpaka atakapokuja” akaniambia.

Nikavuta kiti katika  meza moja na kukaa.

“Nikuagizie kinywaji gani?” akaniuliza.

“Kinywaji? Nadhani sitahitaji kinywaji chochote”

“Ni agizo la Makita kwamba utakapokuja, wakati unamsubiri upewe kinywaji chochote utakachohitaji”

Nikafikiri kidogo  kabla ya kumwambia.

“Nipatie bia ya Kilimanjaro, moja tu.”

Nilimwambia “moja tu” ili kumpa taarifa kuwa sitahitaji kunywa zaidi ya chupa moja.

Meneja akaondoka. Baada ya muda mfupi akaja msichana  mwingine mhudumu wa hoteli, akiwa na chano kilichokuwa  na bia  moja ya Kilimanjaro pamoja na bilauli.

Akanisalimia kisha akaiweka ile chupa juu ya meza pamoja na  bilauli kisha akaichukua ile chupa na kuitoa kizibo, akanimiminia bia kwenye bilauli.

“Karibu” akaniambia na kuondoka.

Nikaanza kunywa kidogo kidogo huku nikiwaza. Nilijiuliza Makita anataka kunieleza nini? Kwanza alitaka nimpe maswali yangu kwa maandishi nikitarajia angenijibu kwa maandishi. Lakini ghafla alitaka tukutane, jambo ambalo alilikwepa awali.

Nikaamini kwamba ile  stori ilikuwa imemgusa sana.

Wakati nakunywa bia, yule  msichana wa kwanza ambaye alikuwa meneja wa hoteli ile, alikuja  tena akiwa ameshika mkoba wake. Akakaa nami.

“Nina ujumbe wako” akaniambia.

“Ujumbe gani?” nikamuuliza.

“Unatoka kwa Makita” akaniambia huku akifungua ule  mkoba wake.

Alitoa burungutu la noti nyekundu na kuniwekea kwenye  meza.

“Ameniambia nikupatie hizi shilingi milioni kumi uende zako na hataki akuone tena hapa hoteli”

Nikashituka.

“Ananipa milioni kumi za nini?” nikamuuliza.

“Uende zako. Kwani wewe hutaki pesa?”

“Pesa nazitaka lakini nataka kujua  ni za nini?”

“Ni zawadi amekupa”

“Ananipa zawadi burebure tu? Na kuhusu yeye kuja hapa tuzungumze lile suala itakuwaje?”

“Yeye hatakuja, yuko ofisini kwake na ana wageni”

“Si amniambia nimsubiri?”

“Atachelewa sana”

“Mimi niko tayari kumsubiri hadi muda wowote wageni wake watakapoondoka”

Meneja akawa amegwaya.

“Una maana kwamba hutaki hizi pesa?”

“Sijajua ni za nini”

“Amekupa ili mmalizane.  Bosi wangu hataki kuandikwa kwenye magazeti”

“Ina maana yale madai niliyomueleza anakubaliana nayo kuwa ni ya kweli?”

“Hayo mengine sasa mimi sijui.  Ninajua  hili alilonituma na ametaka nikampe jibu”

“Jibu langu ni kuwa kama ananipa  pesa ili kuzima hizi habari sitazipokea. Bado nahitaji majibu yake”

“Au unaziona ndogo, akuongeze?”

|Siwezi kuona ni ndogo kwa sababu sijahitaji pesa. Mimi  nimekuja hapa kwa ahadi yetu ya jana kwamba angenipa ufafanuzi wa madai niliyomuandikia”

Hapo kidogo niliona sura ya  yule msichana ikichuja kama ambaye alihamaki au alipata fadhaa. Akalirudisha lile burungutu  ndani ya mkoba wake kisha akainuka. “Ngoja  nikamfahamishe mwenyewe” akaniambia na kuondoka.

Nikawa namtazama kwa nyuma. Kwa asilimia mia moja niliamini kuwa yale madai ya Sofia na Kabwe yalikuwa na ukweli ambao Makita hakutaka utoke kwenye vyombo vya habari.