KISIWA CHA MAUTI – Sehemu ya 3
KWA KIFUPI
“Mwambie Masha”
Msichana akafunga geti kisha akarudi ndani. Kitendo hicho kiliniudhi kidogo ingawa kilikuwa cha kiusalama.
Nikasimama kwa karibu dakika tatu hivi kabla ya geti kufunguliwa tena. Aliyefungua geti alikuwa msichana yule yule.
“Anakwambia upite ndani” akaniambia huku akinipisha kwenye mlango wa geti.
SASA ENDELEA...
Nikaingia. Msichana aliniongoza hadi kwenye sebule ya nyumba hiyo. Nikamuona kijana mmoja aliyekuwa ameketi kwenye kochi akicheza na simu.
Aliponiona, aliondoa kidole chake kwenye simu akanitupia jicho la shauku.
Kama alikuwa ni Kabwe mwenyewe, alikuwa na haki ya kuniambia nipite ndani kabla ya kunifahamu mimi ni nani na ninahitaji nini.
Mguu wake mmoja ulikuwa umefungwa P.O.P., yaani plasta ngumu, ukionekana kuwa umevunjika. Magongo ya chuma yalikuwa karibu yake.
Isitoshe, mbali na kufungwa P.O.P., alikuwa mnene aliyepitiliza kiasi kwamba hata kutembea kwa hatua chache kwake ingekuwa kazi.
“Karibu,” akanikaribisha. Licha ya kuwa mnene, sauti yake ilikuwa nyembamba.
Nikakaa kwenye kochi karibu yake kabla sijamjua kama alikuwa ndiye Kabwe mwenyewe.
“Habari gani?” nikamsalimia baada ya kuketi.
“Nzuri. Ndiye wewe uliyekuwa unaniulizia?”
Hapo nikatambua kuwa kijana huyo alikuwa ni Kabwe.
“Ndiye mimi. Naitwa Masha, natokea katika gazeti la Kumekucha.”
“Wewe ni mwandishi wa habari?”
“Ndiyo.”
“Nimeshawahi kusoma au kuona habari zako. Nina magazeti mengi hapa.”
Akanionesha rundo la magazeti yaliyokuwa kando yake, yakiwemo magazeti ya kampuni yetu.
Nilipouona ucheshi wake, nilimtolea kitambulisho changu nikamuonesha.
“Unanihitaji mimi?” akaniuliza.
“Wewe si ndiye Kabwe ambaye mama yako mdogo alikuwa mke wa Bwana Makita?”
“Ndiye mimi. Kuna matatizo gani?”
“Hakuna matatizo yoyote. Nilipata habari kuwa marehemu mama yako aliwahi kumfungulia kesi Makita, lakini mama akafariki kabla ya kesi kusikilizwa. Ni kweli?”
“Ni kweli,” kijana akanijibu kwa haraka kisha akaniuliza.
“Ndiyo unataka kuandika hiyo habari?”
“Ndiyo.”
“Mbona umechelewa sana? Unajua sisi tunaamini kuwa mama yetu aliuawa ili kuzima ile kesi.”
“Unao ushahidi wa madai hayo?”
“Ushahidi ni wa kimazingira tu. Tuliambiwa alikufa kwa ajali, lakini ilikuja kugundulika alipigwa risasi ya kichwa.”
“Sasa kwa nini hamkupeleka malalamiko yenu polisi?”
“Mpaka leo polisi wanachunguza kesi hiyo, lakini hatujaambiwa chochote.”
“Sasa tuache huko. Nilikuwa nataka kukuuliza kwamba marehemu mama yako alikuwa amejiandaa kwa kesi ile?”
“Ndiyo, alikuwa amejiandaa.”
“Alikuwa anadai nini?”
“Agaiwe mali na mume wake baada ya kuachika. Kuna mali ambazo walichuma wakiwa pamoja.”
“Alikuwa ameorodhesha hizo mali ambazo alitaka agaiwe?”
“Kwa msaada wa wakili wake, alikuwa ameziorodhesha. Mume wake alikuwa na majumba na mahoteli hapa Dar. Alimpa mama yangu nyumba moja tu kama kumfunga mdomo.”
“Nyumba yenyewe ni ipi?”
“Ndiyo hii.”
“Mama yako alikuwa na ushahidi gani kwamba Makita alikuwa na majumba na mahoteli?”
“Njoo nikuoneshe faili ambalo aliliandaa pamoja na wakili wake.”
Kijana huyo alinyanyuka kwenye kochi, akachukua magongo yake na kuchechemea kuelekea ndani. Baadaye kidogo alirudi akiwa ameshika faili.
Alikaa tena kwenye kochi kisha akalifungua lile faili lililokuwa limejaa nyaraka.
“Angalia vivuli vya hati za nyumba zake hizi hapa. Nyumba karibu sitini. Ana mashamba na malori aina ya Fuso yanasomba miwa huko Mtibwa.”
Yule kijana alinipa lile faili. Nikashuhudia mimi mwenyewe vivuli vya hati mbalimbali za mali za Makita, zikiwemo nyumba na magari.
“Mama yako alizipataje hizi hati alizozitoa vivuli?”
“Sijui alizipataje. Wakili wake alihangaika sana ili kuthibitisha ukweli wa mali za Makita kabla ya kufungua kesi. Mama yangu alipokufa, ile kesi ikafutwa na yule wakili wa mama hakushughulika tena. Sijui alipewa pesa au alitishwa, hatujui.”
“Kwa hiyo, hivi sasa mna mpango gani?”
“Hatuna mpango wowote. Unajua yule ni mama mdogo na hakuzaa. Angekuwa na mtoto, angeweza kwenda kudai haki za mama yake.”
“Unaweza kuniruhusu nikatoe vivuli vingine vya hizi hati?”
“Kama unataka kuandika kwenye gazeti, uje kesho nitakutolea vivuli vingine.”
“Kama kuna mashine ya kutolea vivuli iliyo karibu, tungeweza kutoa hata hii leo.”
“Kutoa vivuli vya karatasi zote hizo, itanigharimu pesa nyingi.”
“Nitalipia mimi?”
“Kama utalipia wewe, mpe pesa huyu msichana aende akakutolee.”
“Sawa.”
Nikatia mkono mfukoni na kutoa pochi yangu. Nikaifungua na kutoa noti moja ya shilingi elfu kumi.
“Nadhani hii itatosha,” nikamwambia.
Kabwe akamuita yule msichana aliyenifungulia geti. Msichana alipofika, alimwambia achukue ile pesa aende akatoe vivuli vya zile hati zote zilizokuwa kwenye lile faili.
Msichana akachukua ile noti ya shilingi elfu kumi pamoja na lile faili, akatoka.
Nikaendelea kuzungumza na yule kijana, ambaye alinieleza mengi kuhusu Makita. Stori iliendelea, akanieleza mpaka Makita alivyomuacha mama yake na kumuoa Sofia, ambaye pia alimuacha.
“Sofia ndiye aliyetaka tumfichue huyu mtu,” nikamwambia.
“Kumbe Sofia ndiye aliyewaletea habari hizi?”
“Ndiyo.”
“Anataka nini?”
“Ametueleza kuwa Makita anamiliki mali nyingi kuliko inavyostahili. Hizi mali atakuwa amezipata kwa njia ya rushwa na pengine hujuma. Sofia ametueleza kwamba huyu mtu amejiuzulu wadhifa wake kwa hofu ya kuja kuulizwa alikozipata mali zake akiwa mtumishi wa umma.”
“Yeye pia alisababisha mama yangu kuachwa na mzee Makita, lakini kwa hilo la kutaka kumuanika huyu mzee, tuko pamoja.”
Nilizungumza na yule kijana kwa karibu saa moja ndipo yule msichana aliporudi. Alikuwa amenunua mfuko ambao aliweka vile vivuli alivyovitoa.
Alinirudishia chenji. Nilitaka nimuachie, lakini sikutaka kujifanya nina pesa, nikaipokea.
Lile faili pamoja na ule mfuko alimpa Kabwe.
Kabwe alichomoa baadhi ya karatasi akazitupia macho kisha akazirudisha.
“Umetoa vivuli vya hati zote?”
“Nimetoa hati zote.”
“Sawa.”
Kabwe akanipa ule mfuko uliokuwa na vivuli vilivyotolewa. Nami nikachomoa baadhi ya karatasi nikazitazama kama zilitoka vizuri kisha nikazirudisha kwenye mfuko huo.
“Unapomuandika mtu kuwa ana mali hii na hii, anaweza kukwambia, lete ushahidi kuwa mali hii ni yangu. Sasa hapa ushahidi ninao wa kutosha. Nimeona pia barua ya afisa wa ardhi,” nikamwambia Kabwe.
“Hiyo kazi ilifanywa na mama yangu pamoja na wakili wake. Mama alipokufa, wakili wake alikuja kutaka hivi vivuli, lakini hatukumpa.”
“Kwa nini hamkumpa?”
“Yeye hakutaka tumtolee vivuli vingine kama wewe. Alitaka tumpe hili faili lote, tukakataa kwa sababu vivuli vingine anavyo ofisini kwake.”
“Sawa. Sasa nashukuru kwa kunipatia vivuli vya hizo hati. Nitakwenda kuzifanyia kazi.”
“Hiyo habari itatoka lini, kesho?”
“Hapana. Ninakwenda kuzisoma kwanza hizi hati zote. Pengine nitakwenda kumuona Kamanda wa Polisi ili anieleze uchunguzi wa kesi ya kuuawa mama yako mdogo uliishia wapi. Pia nitataka kwenda kumuona Makita mwenyewe. Hii itanichukua siku mbili, tatu.”
“Sasa mimi nitajuaje kama hii habari imetoka?”
“Nitachukua namba yako ya simu.”
Kijana akanitajia namba yake na mimi nikampa namba yangu. Kusema kweli, alifurahi sana. Si tu alifurahi kuwa ile habari ikiandikwa itamkomoa Makita, bali pia alifurahia kujuana na mwandishi maarufu.
Licha ya kijana huyo kushindwa kuja kwenye geti nilipokwenda kumuulizia, wakati natoka alichukua magongo yake akanisindikiza hadi kwenye geti hilo.
Tuliagana tukiwa nje ya geti.
“Asante. Kwaheri,” nikamwambia huku nikimuaga kwa kumpa mkono.
“Asante. Tafadhali jitahidi sana. Huenda jitihada zako zikafanikisha upuuzi huu wa huyu mtu kufichuka au haki ya mama yangu kupatikana,” akaniambia akionesha kupata matumaini.
“Niamini, nitajitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu.”
“Asante, ndugu mwandishi.”
Tulipoachiana mikono, niliondoka na yeye akageuka na kuingia ndani.
Nilikwenda kupanda daladala nikarudi ofisini kwetu Magomeni.
Niliingia katika chumba cha habari, nikaketi kwenye meza ya peke yangu na kuanza kuvikagua vivuli vya zile hati. Nilikikagua kivuli kimoja baada ya kingine. Vilikuwa ni vivuli vya baadhi ya nyumba zake na zilikuwa na majina yake.
Kulikuwa na vivuli sita vya kadi za magari yake zilizokuwa na majina yake, pamoja na vivuli vya leseni mbili za hoteli zake zilizoko Dar. Kwa bahati njema, hati zote zilikuwa ni za nyumba zilizokuwa hapo hapo Dar.
Baada ya kuridhika na hati hizo, nilizikusanya nikazitia kwenye ule mfuko kisha nikamfuata mhariri wangu.
“Nimerudi,” nilimwambia huku nikikaa kwenye kiti kilichokuwa mbele ya meza yake.