KISIWA CHA MAUTI – Sehemu ya 4
KWA KIFUPI
Kulikuwa na vivuli sita vya kadi za magari yake zilizokuwa na majina yake pamoja na vivuli vya leseni mbili za hoteli zake zilzoko Dar. Kwa bahati njema hati zote zilikuwa ni za nyumba zilizoku-wa hapo hapo Dar.
Baada ya kuridhika na hati hizo nilizikusanya nikazitia kwenye ule mfuko kisha nikamfuata mhariri wangu.
“Nimerudi” nilimwambia huku nikikaa kwenye kiti kilichokuwa mbele ya meza yake.
SASA ENDELEA...
Nikavitoa vile vivuli vya hati vilivyokuwa kwenye mfuko na kumuonesha.
“Hizo ni nyaraka gani?” akaniuliza kabla ya kuzipokea.
“Ni vivuli vya hati za nyumba za Makita pamoja na kadi za magari yake na leseni za hoteli zake.”
Mhariri akashangaa.
“Umezipata wapi mara moja hivi?”
Kwanza nilicheka kidogo kwa sababu alikuwa akinitazama huku akinitolea tabasamu la kunisifu.
Nikamueleza jinsi nilivyovipata vivuli vya hati hizo.
Wakati ninamueleza, mhariri huyo naye alikuwa akizitupia macho hati hizo.
“Huyo wakili wa marehemu aliyekuwa mke wa Makita ndiye alitaka kutumia hati hizi mahakamani akitaka mali za Makita zigaiwe?”
“Ndiyo. Lakini kesi haikuendelea baada ya mama huyo kufariki dunia huku kukiwa na madai kuwa alipigwa risasi.”
“Sasa sikiliza nikwambie...”
“Ndiyo.”
“Hapa unaweza kupata habari zaidi ya moja. Kuna habari ya utajiri wa Makita na habari ya kuuawa kwa mtalaka wake wakati amefungua kesi ya madai dhidi yake.”
Mhariri wangu aliponiambia hivyo alinyamaza na kunitazama kuona kama nilikuwa na hoja. Alipoona nilikuwa kimya nikimsikiliza, akaendelea.
“Sasa kwanza fanya uchunguzi ujue nyumba hizi ziko wapi. Kwa vile una kamera yako, unaweza kupiga picha za nyumba kadhaa, hasa zile za kifahari, ili tuzioneshe. Halafu mtafute Makita umpe madai yake usikie atakwambia nini.”
Mhariri akanyamaza tena na kunitazama. Ilikuwa ni kawaida yake, anapokueleza kitu, kusita na kukutazama. Pengine alitaka kujua kama kimeingia akilini mwangu au alitaka kujua kama nilikuwa na swali. Alipoona natingisha kichwa changu kuonesha nimemuelewa, akaongeza.
“Halafu uende ukamuone Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani umuulizie kuhusu ukweli wa kuuawa kwa mtalaka wa Makita. Na pia akueleze uchunguzi wa mauaji hayo umeishia wapi. Sijui kama umenielewa vizuri.”
“Nimekuelewa vizuri.”
“Utaifanya lini hiyo kazi?”
“Nitaanza kuifanya kesho.”
“Kuanzia kesho nitakuruhusu utumie pikipiki ya kampuni kwa ajili ya kuzifuatilia hizo nyumba.”
“Sawa.”
Mazungumzo yetu yakaishia hapo.
Usiku wa siku ile, nikiwa nyumbani kwangu, Sofia akanipigia simu na kuniuliza kama nilikuwa nafuatilia ile habari.
“Nafuatilia. Hivi kesho nataka nianze kuzifanyia utafiti zile nyumba zinazodaiwa kuwa ni za Makita.”
“Utazijuaje sasa?”
“Nitazijua kwa sababu nimeshapata baadhi ya hati za nyumba hizo. Si unajua hati inaonesha nyumba iko wapi?”
“Umezipata wapi hizo hati?”
“Nimezipata kutokana na uchunguzi wangu.”
“Sasa kama ni kweli umepata hizo hati, nifuate ili nikuoneshe baadhi ya hizo nyumba kwa sababu ninazijua.”
“Nikufuate saa ngapi?”
“Niambie wewe.”
“Nitakuja kwako saa tatu asubuhi.”
“Utakuja kwangu au utakuja pale kwenye kituo cha daladala?”
“Nitakuja pale kwenye kituo cha daladala.”
“Sawa. Kama nitakuwa sijafika utanipigia simu.”
“Sawa.”
“Haya, usiku mwema.”
“Na kwako.”
Sofia akakata simu.
Asubuhi kulipokucha nikaenda zangu kazini. Baada ya kikao chetu cha kila asubuhi kinachowahusisha wahariri na waandishi, mhariri wangu akaniidhinishia nipewe pikipiki kwa ajili ya kazi maalumu.
Nilipopewa pikipiki, nilichukua pochi yangu ndogo iliyokuwa na kamera yangu, nikaenda Manzese. Nilisimama karibu na kituo cha daladala, nikatoa simu yangu na kumpigia Sofia.
“Mimi nimeshafika kwenye hiki kituo,” nikamwambia.
“Sawa. Nisubiri, nakuja.”
Nilisubiri kwa dakika ishirini hivi, Sofia akatokea. Hakuwa ameniona kwa vile nilikuwa juu ya pikipiki na pia hakujua kama ningekwenda kwa pikipiki. Alipita karibu yangu kabisa bila kunitambua, macho yake yakiangaza huku na huko. Nikamuita.
“Sofia!”
Akashituka na kushangaa kuniona nikiwa kwenye pikipiki.
“Sikukutambua. Nilikuwa nakupita. Kumbe umekuja na pikipiki!”
“Njoo upande twende,” nikamwambia.
Sofia akajipakia nyuma yangu. Mara moja nikaona hewa imebadilika. Manukato aliyokuwa amejipulizia yakabadilisha hewa iliyokuwepo.
Kwa upande mmoja manukato yake yalinikera, lakini kwa upande mwingine yalinifariji. Yalinikera kwa sababu yalinipa ushawishi wa kumtamani wakati nilikuwa kazini. Na yalinifariji kwa sababu kila kinachonukia vizuri ni utukufu.
“Sasa twende wapi?” nikamuuliza kabla ya kuondoka.
“Si ninakupeleka ukatazame zile nyumba zake?” akaniuliza.
“Ndiyo. Sasa tuanzie wapi kwa sababu ziko sehemu tofauti tofauti?”
“Tuanzie Masaki.”
Tukaondoka.
Tulipofika Masaki, Sofia alinionesha ile hoteli ya Makita ambayo nilikuwa naifahamu vizuri, ingawa sikuwa nikijua kuwa ilikuwa ni ya Makita.
Baada ya kunionesha hoteli hiyo, alinipitisha katika mitaa mbalimbali akanionesha baadhi ya nyumba ambazo vivuli vya hati zake nilikuwa navyo.
Tulipotoka Masaki tukaenda Msasani. Sofia alinionesha baadhi ya nyumba za Makita. Nazo nilizipiga picha. Tukaenda Oysterbay, kisha tukaenda Kigamboni. Huko kote nilipiga picha baadhi ya nyumba ambazo Sofia alizitambua.
Tulikuwa tumefanya mzunguko mkubwa, ikabidi niongeze mafuta kwenye pikipiki nikitarajia nitakwenda kurudishiwa pesa zangu.
Baada ya kuweka mafuta, nilimrudisha Sofia. Baada ya kumuacha Manzese, nikaona nirudi Masaki kwenye ile hoteli ya Makita.
Nilipofika, niliacha pikipiki nje, nikaingia ndani. Nilikwenda mapokezi na kumsalimia msichana niliyemkuta hapo.
“Karibu,” akanikaribisha akidhani ni mteja.
“Nilikuwa namuhitaji Bwana Makita,” nilimwambia nikiwa sina uhakika wa asilimia mia moja kama Makita anahusika na ile hoteli, ila nilijiambia kama kweli ndiye mwenyewe, mhudumu huyo wa mapokezi ataniambia kama yupo au hayupo.
Msichana akanitazama vizuri, kisha akaniuliza.
“Unamhitaji nani?”
“Bwana Makita.”
“Kamuulize meneja, mimi sijui kama yupo au hayupo.”
Msichana akanionesha ofisi ya meneja. Nikaenda. Meneja wake pia alikuwa msichana. Alinikaribisha kwenye kiti, kisha akaniuliza.
“Nikusaidie nini?”
“Nilikuwa namhitaji Bwana Makita.”
“Wewe ni nani na unatoka wapi?”
Nikatoa kitambulisho changu na kumuonesha.
“Mimi ni mwandishi wa habari, natokea Gazeti la Kumekucha.”
Meneja huyo nilipomwambia mimi ni mwandishi wa habari, aligutuka kidogo akanikazia macho.
“Una ahadi naye?” akaniuliza.
“Sina ahadi naye.”
“Unajua huyu bwana ana shughuli nyingi, si rahisi kumpata bila kuwa na ahadi naye.”
“Sasa unanishauri nini?”
“Kwani wewe ulikuwa na shida gani naye?”
“Ingekuwa vyema kama ningempata yeye mwenyewe.”
“Yeye mwenyewe kwa sasa hayuko.”
“Labda ni muda gani ninaweza kumpata kesho?”
“Kama nilivyokwambia, ili kumpata ni lazima uwe na ahadi naye. Hata kama atatokea sasa hivi, hamuwezi kuzungumza. Ni lazima kwanza ajue anakutana na nani na kwa ajili gani. Sasa kwa ufupi acha jina lako na namba yako ya simu. Akija tutamueleza kuwa unamtafuta. Anaweza kukupigia na kukuuliza shida yako.”
Nikamuachia yule msichana jina langu na namba yangu ya simu.
“Na mimi unaweza kunipatia namba yake?” nikamuuliza.
“Hii namba yako inatosha. Atakapokupigia utaiona namba yake.”
Sikushangaa kwa kukataa kunipa namba ya bosi wake kwani nilifahamu watumishi wengi huogopa kuwapa watu, hasa waandishi wa habari, namba za mabosi wao.
Nikainuka.
“Asante. Umfahamishe kwamba ni muhimu tuwasiliane.”
“Nitamfahamisha.”
Nikatoka mle ofisini. Sikupoteza tena muda nikatoka nje ya hoteli na kupanda pikipiki.
Nilipoondoka hapo hotelini, nikarudi Magomeni zilipokuwa ofisi zetu.
Jua lilikuwa limeshachwa, lakini mhariri wangu alikuwa bado yuko ofisini. Nikaingia ofisini kwake na kumueleza yaliyojiri kwa siku ile.
Alizitazama zile picha za nyumba za Makita nilizopiga pamoja na kumpa maelezo ya meneja wa hoteli ya Makita iliyokuwa Masaki.
“Utaendelea kumfuatilia. Ukingoja tu akupigie simu, anaweza kukukwepa,” mhariri akaniambia.
“Hiyo kazi nitaifanya kesho.”
“Sawa. Nenda kapumzike.”
“Tutaonana kesho.”
“Utaendelea kutumia pikipiki mpaka utakapokamilisha kazi yako.”
Nikamkubalia na kutoka ofisini mwake. Nikarudi nyumbani.
Siku iliyofuatia nikaenda kazini kwangu. Nilifanya kazi hadi saa nane nikitazamia Makita au meneja wa hoteli yake wangenipigia simu. Lakini sikupata simu yoyote kutoka kwao. Nikaamua kupanda pikipiki na kwenda tena Masaki.
Nilipofika pale hotelini nililiona gari la kifahari ambalo nilishuku kwamba ndilo alilokuwa akilitumia Makita. Nikaacha pikipiki na kuingia ndani ya hoteli hiyo.