Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KISIWA CHA MAUTI - 15

KISIWA 15 Pict

ILIPOISHIA

“Pengine aliwekewa wakati alipokwenda kujisaidia”

“Sasa huo ni uzembe wake mwenywe na sisi hatuwezi kuhusika na jambo hilo. Kwanza siamini kama kweli aliwekewa hayo madawa”

“Tulikwenda kumpima leo na imegundulika kuwa alitumia hayo madawa”

“Sasa kama alitumia labda yeye ni mtumiaji wa madawa ya kulevya. Asisingizie watu wengine”

SASA ENDELEA...


“Kilichotupa shaka ni kwamba hayo si madawa ya kulevya tunayoyafahamu. Ni aina ya dawa zinazotumika hospitalini kwa ajili ya watu wanaofanyiwa operesheni. Dawa hizo mtu hawezi kutumia mwenyewe; ni dawa za kumlaza mtu usingizi.”

“Sasa kama ni hivyo, mbona yeye hakulala usingizi? Alikodi chumba akataka aendelee kuhudumiwa chumbani huku akiwa na ajenda yake ambayo alikuwa ameshaipanga. Mtu mwenye usingizi anaweza kuua?”

Mrakibu wa polisi akanitazama.

“Unayasikia maneno hayo?” akaniuliza.

“Maneno anayosema si ya kweli, sikubaliani nayo. Bado ninasisitiza kwamba niliwekewa hiyo dawa pale pale hotelini ili kunilaza au kuharibu akili yangu, halafu waje waniambie kuwa nimeua,” nikasema.

“Wewe ni mwandishi bwana! Hebu rekebisha maneno yako. Wewe umeua, si kwamba umeambiwa kuwa umeua. Ulikodi chumba au hukumkodi?”

“Sikukodi.”

“Umeua au hukuua?”

“Sikuua.”

Majibu yangu yalimuudhi mrakibu wa polisi. Akanitazama kwa hasira, halafu akapunguza jazba mwenyewe.

“Sawa. Tunakwenda kisheria. Sisi hatukulazimishi ukubali kosa. Hapa si mahakamani. Hata mahakamani hawakulazimishi ukubali kosa. Ni hiari yako kukana kosa au kukubali kosa. Kinachoangaliwa ni ushahidi.”

Kwa vile nilimwona amekasirika, sikutaka kubishana naye, nikamwambia.

“Lakini nataka ukumbuke kwamba kabla ya mambo yote kutokea nilikueleza kuwa nilipewa rushwa ya shilingi milioni kumi nikazikataa...!”

Hapo hapo mrakibu wa polisi akaugeuza uso wake kwa meneja wa Hoteli ya Makita.

“Kuna madai ya rushwa ameyatoa. Amesema wewe ulitaka kumpa rushwa ya shilingi milioni kumi akazikataa!”

Meneja wa hoteli akaruka kimanga.

“Nani alitaka kumpa rushwa?”

“Hebu taja, nani alitaka kukupa rushwa?” Mrakibu akaniuliza.

“Ni huyo huyo meneja. Aliniletea shilingi milioni kumi juu ya meza.”

“Una kichaa nini! Nikupe shilingi milioni kumi za nini?”

“Hapa matusi hayaruhusiwi,” Mrakibu wa polisi akamuonya.

“Anataka kuniletea uzushi wake. Wewe unatakiwa ujibu tuhuma za mauaji zinazokukabili, si kusingizia watu mambo yasiyokuwepo. Nikupe wewe shilingi milioni kumi? Umeniuzia nini?”

“Ulinipa shilingi milioni kumi ili nisiandike habari zinazohusu mali anazomiliki bosi wako.”

“Sasa ziko wapi hizo shilingi milioni kumi?”

“Nilizikataa.”

“Ungezichukua halafu ukazifikisha polisi. Kwanini ulizikataa?”

“Hebu subirini. Madai ya rushwa yanahitaji ushahidi,” Mrakibu alituambia, kisha akanitazama mimi.

“Je, unao ushahidi kwamba alikupa rushwa ya shilingi milioni kumi?”

“Tulikuwa mimi na yeye. Huyo shahidi atatoka wapi!”

“Sasa hilo dai lako lifute kwani huwezi kulithibitisha. Tuendelee na hizi tuhuma zinazokukabili wewe. Usipende kuzungumzia kitu kisicho na ushahidi.”

Yalikuwa ni maneno ya kweli ingawa yaliniumiza moyo wangu. Kwa vile nisingeweza kuyathibitisha madai yangu ya kupewa rushwa ya shilingi milioni kumi na yule meneja, niliona ninyamaze. Nilifanya upumbavu kutozichukua zile pesa na kuzifikisha kwenye ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

“Sikiliza afande nikueleze,” meneja wa Makita akamwambia mrakibu, kisha akaongeza.

“Huyu bwana alifika pale hotelini kwetu akaniambia kwamba alikuwa anamuhitaji bosi wetu. Sijui ana habari yake ambayo alitaka kumhoji. Kwa vile hakuwa na ahadi naye, ilikuwa si rahisi kumpata mtu ambaye ana shughuli nyingi. Amekuja karibu mara tatu. Sasa juzi alikuja tena kumsubiri.”

Meneja huyo aliyependa kugeuza maneno aliendelea kumwambia mrakibu.

“Bosi alikuwa na wageni akaniagiza nimwambie amsubiri. Sasa tukamuuliza tumpatie kinywaji gani wakati anamsubiri bosi. Akasema apatiwe bia. Tulichokigundua baadaye, huyu bwana licha ya kujidai alikuwa anamhitaji bosi wetu, alikuwa na ajenda zake zilizokuwa zinamfikisha pale hotelini. Unanielewa?”

“Ninakuelewa.”

“Kulikuwa na msichana alikuwa anamtaka, kwani baada ya kunywa bia tatu ambazo tulimpa bure, alikunywa bia zaidi kwa pesa zake mwenyewe, kisha akakodi chumba pale pale na kutaka ahudumiwe chumbani. Yule mhudumu wetu alimuona ni mteja tu, akawa anampelekea bia chumbani. Matokeo yake ndiyo alimtaka kimapenzi. Nafikiri mwenzake akakataa, akaamua kumuua.”

“Unajua mfa maji hakosi kutapatapa. Hii tuhuma hawezi kuikwepa. Huyu ni muuaji tu. Tutamfikisha mahakamani. Kama ana madai yake, atayafikisha huko,” mrakibu alisema. Kila alipoutazama uso wa mrembo aliyekuwa mbele ya meza yake alijikuta akinikandia tu.

“Sasa afande mimi ninahitajika ofisini. Karibu hotelini kwetu uje angalau upate soda.”

“Si kwa sababu ya soda, lazima nifike kwa sababu za kiuchunguzi,” mrakibu wa polisi akavunga.

“Utafika leo?”

“Naweza kufika jioni.”

“Basi utanikuta.”

“Sawa.”

“Nadhani kwa muda huu tumemaliza mazungumzo.”

“Tutakuwa tumemaliza kwani tulikuhitaji utoe ufafanuzi wa jina la mtu aliyeuawa na pia umtambue mtuhumiwa tuliyemkamata. Kwa vile tumeshapata ufafanuzi na umemtambua mtuhumiwa, unaweza kwenda zako.”

“Sawa.”

Meneja wa Hoteli ya Makita akainuka kwenye kiti.

“Tutaonana muda huo.”

“Hakuna tatizo.”

Wakati meneja anatoka, mrakibu alikuwa akimtazama kwa nyuma jinsi alivyokuwa anatembea. Hakuyaondoa macho yake mpaka meneja huyo alipofungua mlango na kutoka.

Baada ya hapo nilichukuliwa alama za vidole, nikapigwa picha, kisha nikarudishwa mahabusu.

Sikuona ndugu, rafiki wala jamaa yoyote aliyekuja kuulizia habari zangu. Kama mhariri wangu alifika, basi hakuruhusiwa kuonana na mimi. Huenda alifika kwa kamanda wa polisi na kupata maelezo huko huko.

Nilishinda mahabusu mchana kutwa. Kazi yangu ilikuwa ni kubadili mikao.

Usiku nikaota ndoto ya kutisha. Niliota nimefikishwa mahakamani nikikabiliwa na shtaka la mauaji.

Yule meneja wa Makita alifika mahakamani na kutoa ushahidi wa uongo mtupu. Mrakibu wa polisi naye alifika akatoa maelezo yake yasiyokuwa na ukweli dhidi yangu. Jambo ambalo lilikuwa la ajabu ni kwamba msichana niliyedaiwa kumuua, ambaye mwili wake ulikuwa mochwari, alikuwa pale pale mahakamani kwenye safu za mbele.

Ingawa watu walikuwa hawamuoni, mimi nilikuwa namuona ananitazama huku analia. Nyuma yake aliketi bosi wa Makita.

Nikaisikia sauti ya jaji aliyekuwa akisikiliza kesi yangu akisema.

“Mahakama hii imeridhika na ushahidi uliotolewa dhidi ya mshitakiwa. Ushahidi huo umeonesha kuwa ni kweli mshitakiwa aliyepo mbele yangu alifanya kosa hilo la mauaji alilodaiwa kulifanya ndani ya chumba cha hoteli.”

Jaji huyo wa kwenye ndoto aliendelea kueleza.

“Kutokana na upande wa mashitaka kuthibitisha bila kuacha shaka kwamba mshitakiwa ametenda kosa hilo la mauaji, mahakama hii inamtia mshitakiwa hatiani.”

Jaji alipofika hapo nikaona yule msichana niliyedaiwa kumuua akaanza kucheka, sasa mimi ndiye niliyeanza kulia.

“Hukumu!” jaji akasema na kunishitua. Nikamkazia macho.

“Kwa kuwa kosa la mauaji ya kukusudia halina adhabu nyingine zaidi ya adhabu ya kifo, ninakuhukumu ku...”

“Wewe!” nilisikia sauti nzito ikiniambia hivyo, kisha nikahisi kuna mtu ananitikisa.

Hapo hapo nikazinduka.

Nikagundua kuwa nilikuwa ninaota. Mtu aliyenitikisa alikuwa mahabusu mwenzangu ambaye nilikuwa nimelala naye karibu.

“Kitu gani?” nikamuuliza nikiwa nimemkodolea macho.

“Nimekusikia unalia, unalia nini?” akaniuliza.

Nikaduwaa kidogo, kisha nikamjibu.

“Labda nilikuwa naota.”

“Unaota nini?”

“Nimeota ninahukumiwa kifo!”

“Inaelekea umelala ukiwa na mawazo hayo.”

“Inawezekana.”

“Jipe matumaini kuwa utashinda kesi yako.”

“Kesi ya mauaji si kesi ya kujipa matumaini. Na hata kama nitakuja kuachiwa, nitakuwa nimesota mahabusu vya kutosha.”

“Pamoja na hayo, bado unatakiwa ujipe matumaini. Unaweza kuachiwa tu.”

Baada ya hapo tukanyamaza. Lakini sikupata usingizi tena. Nilikesha macho nikiwaza. Ile ndoto ndiyo iliyonitibua. Niliona kama vile yalikuwa maono ya kweli yaliyokuwa yakinijia kwamba nitanyongwa.

Kabla ya kuzinduka kutoka usingizini, jaji wa kwenye ndoto alikuwa akinihukumu. Aliishia kuniambia,

“Ninakuhukumu ku...” Yule mahabusu mwenzangu akaniamsha. Pale jaji alikuwa ananiambia, “Ninakuhukumu kunyongwa kwa kitanzi mpaka ufe!”

Mwili ulinisisimka nilipokiwaza kitanzi kikikaza kwenye shingo yangu.

Nikawaza mengi. Nikamkumbuka hadi mfungwa mmoja wa kisiasa wa nchi za nje aliyekatika kichwa wakati ananyongwa. Jambo hilo halikuwa la kuwaza wakati kama ule wa usiku. Lazima akili ipate maruweruwe.

Hata hivyo nikapuuza mambo ya ndoto na kushikilia msimamo alionieleza mahabusu mwenzangu kuwa nijipe matumaini kwamba nitashinda kesi, ingawa upande mwingine wa akili yangu ulikuwa ukiamini kile nilichokiota.