Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KISIWA CHA MAUTI -13

Muktasari:

  • Yule mrakibu alikuwa na magazeti kadhaa juu ya meza yake. Akachukua gazeti mojawapo na kunionesha.

ILIPOISHIA

Yule mrakibu alikuwa na magazeti kadhaa juu ya meza yake. Akachukua gazeti mojawapo na kunionesha.

“Habari yako hii hapa imeandikwa”

“Swali nililouliza mimi, nimemuua nani?”

Mrakibu akalitupia macho lile gazeti haraka haraka.

“Unatuhumiwa kumuua Edda mfanyakazi wa hoteli ambayo wewe ulikwenda juzi na kufanya mauaji hayo kisha ukatoroka” akaniambia kwa kujiamini kama vile ile habari ndiyo msema kweli.

“Mbona huyo Edda ninayetuhumiwa kumuua  nimekamatwa naye?” nikauliza kwa jazba.

“Yuko wapi?”

“Ni mimi” Edda  akajibu.

“We msichana unataka kuleta utani! Unajua sisi tuko kazini. Ninaweza kukuweka ndani sasa hivi!” Mrakibu wa polisi akamwambia.

“Mimi ndiye Edda Ibrahimu. Mimi ndiye niliyekuwa nikimhudumia Masha alipokuja pale hoteli. Mimi ndiye ninayedaiwa kuuawa” Edda akasisitiza bila uoga.

Nilimpenda!

“Wewe unafanya kazi pale hoteli?” Mrakibu wa polisi akamuuliza..

SASA ENDELEA...


“NDIYO”

“Ngoja nipige simu niulizie. Kama unaniletea utani nitakuweka ndani sasa hivi!”

“Piga!”

Edda alikuwa ngangari kweli!

Mrakibu huyo wa polisi akawa anahangaika kutafuta namba ya simu kwenye makabrashia. Namba hakuiona.

“Hivi unayo namba ya pale hoteli?” akamuuliza  Edda.

“Unamuhitaji nani?” Edda akamuuliza.

“Yule meneja ndiye ambaye tumekuwa tukiwasiliana naye”

“Ninayo namba yake, ngoja nikupe”

Edda akaangalia kwenye simu yake kisha akamtajia namba ya meneja wao.

Mrakibu huyo akaitumia ile namba kupiga simu. Alipiga simu ya mezani ambayo ilikuwa juu ya meza yake.

Baada ya sekunde chache, simu ikapokelewa.

“Mimi ni Mrakibu Masaidizi wa Polisi Paul Makamba. Niko kituo kikuu cha polisi. Ninataka kujua ninaongea na nani?”

Alipojibiwa na bila shaka aliyemjibu alikuwa ni meneja mwenyewe, alisema.

“Nataka kukujulisha kuwa tumemkamata yule  mtuhumiwa wa mauaji tuliyekuwa tunamtafuta, sasa tunakutaka ufike hapa kituo cha polisi kwa utambulisho”

Mrakibu huyo alisikiliza kidogo kisha akajibu.

“Ndiyo, ni Masha yule mwandishi wa habari. Tumemkamata sasa hivi nyumbani kwa msichana mmoja ambaye anadai kuwa yeye ndiye aliyeandikwa kuwa ameuawa”

Mrakibu huyo alisikiliza tena kisha akasema.

“Ndiyo. Anasema yeye ni Edda…”

Mrakibu wa polisi akamtazama Edda kisha akamuuliza.

“Unaitwa Edda  nani?”

“Naitwa Edda Ibrahim” Edda akamjibu.

Mrakibu wa polisi akauelekeza mdomo wake kwenye mdomo wa simu na  kuzungumza..

“Anasema anaitwa Edda Ibrahim”

“Unakubali kwamba ni mfanyakazi wenu…na ndiye yeye mliyeandika kwamba ameuawa?”

Mrakibu wa polisi alisikiliza kwa muda mrefu huku akiitikia kisha akasema.

“Sasa tunakutaka ufike hapa kituo cha polisi sasa hivi”

Akasikiliza tena simu ya upande wa pili kisha akaendelea.

“Uko wapi…Kibaha…utarudi lini?”

Baada ya kusikiliza tena aksema.

“Basi kesho saa tatu asubuhi ufike hapa kituoni uniulizie mimi. Sawa?”

Baada ya hapo akaweka mkono wa simu chini.

“Amekubali kwamba wewe ni mfanyakazi wao lakini amesema kwamba jina lako lilingizwa kwa makosa, atakuja kesho asubuhi kutoa ufafanuzi”

“Kwa hiyo nitabaki hapa hadi saa ngapi?”

“Mimi ninakuruhusu uende zako isipokuwa kesho saa tatu uje uonane na mimi. Bosi wako atakuwepo hapa. Sisi tutabaki na mtuhumiwa wetu maana kesi ya mauaji haina dhamana”

“Ni sawa. Sasa kama mtu niliyedaiwa kumuua yuko hai, mimi ninatuhumiwa  kumuua nani” nikamuuliza mrakibu huyo wa polisi.

“Kama hao waliouliwa mfanyakazi wao wamekosea kutupa jina, mimi nitakutajia nani?”

“Kwa hiyo…?”

“Lakini tuna utaratibu wetu wa kumuonesha mtuhumiwa mwili wa marehemu anayetuhumiwa kumuua. Tutakwenda na wewe hospitali ya Muhimbili uliokohifadhiwa mwili huo ili uuone lakini jina la marehemu utalipata kesho”

Nikashusha pumzi ndefu. Nilijua ninakwenda kuoneshwa mwili wa maiti ya yule msichana niliyekuwa naye katika kile chumba cha hoteli. Mwanzo nilimdhani alikuwa Edda lakini sasa inabainika kwamba hakuwa Edda.

Edda akaachiwa. Mimi nikawekwa ndani kwa muda. Baadaye nilitolewa na kupakiwa kwenye gari nikapelekwa hospitali ya Muhimbili.

Nilikuwa nimefuatana na yule mrakibu wa polisi pamoja na polisi wengine wawili.

Tulipofika Muhimbili nilipelekwa Mochwari ambako nilioneshwa mwili wa msichana niliyedaiwa  kumuua. Wakati ule niliweza kumtazama vizuri sura yake.

Kutokana na uso wake kuvimba na  kuwa mweusi huku ukiwa na mikwaruzo ya kukatwakatwa na kitu kama chupa au kisu, sikuweza  kumtambua kama nilikuwa namfahamu. Mwili huo ilikuwa bado uko kwenye sare za hoteli ya Makita.

“Umeweza kumtambua” Marakibu wa polisi akaniuliza.

Nikatikisa kichwa.

“Simtambui na sijapata kumuona popote” nikamjibu.

“Sasa mimi nakueleza msichana uliyemuua ndiye huyu hapa. Uchunguzi wa madaktari umeonesha kuwa ulimkaba na ulimkatakata kwa kitu chenye makali kama kisu au vipande vya chupa”

Nikaendelea kutikisa  kichwa.

“Sijawahi kufanya upuuzi huo”

Ilikuwa nusura mrakibu wa  polisi anipige kibao.

“Unasema nini?” akaniuliza kwa ukali akiwa amenikazia macho.

Nikanyamaza kimya.

“Wewe usituletee bangi zako, nitakunyoosha! Jaribu kutumia lugha nzuri” akaniambia.

Sikutaka kushindana naye nikamuacha atulize hasira zake zisizo na sababu za msingi.

Baada ya hapo nilirudishwa tena kituo cha polisi na kupelekwa katika ofisi ya mrakibu huyo wa polisi ambaye aliniambia nikae kwenye kiti.

Akaniuliza jina langu, umri wangu na mahali nilipokuwa ninaishi.

Baada  ya kumjibu akaniambia.

“Tunataka maelezo yako kuhusiana na tukio  hili. Ilikuwaje ukamuua yule mwanamke? Kwa taarifa tuzizonazo ulianza kufika pale hoteli siku mbili kambla ya hilo tukio na ulikuwa ukimuulizia mwenye hoteli ile. Je ni kweli?”

“Ni kweli”

“Sasa tueleze ulikuwa unamuulizia kwa ajili gani?”

Nikamueleza kilichokuwa kikinipeleka pale hoteli.

“Kwa hiyo unakubali kuwa ulifika hotelini hapo?”

“Ndiyo nakubali”

“Tuliarifiwa kwamba siku ya tukio ulikwenda pale jioni na kuanza kunywa  pombe ovyo. Ilipofika saa tatu usiku ukakodi chumba. Je hilo ni kweli?”

“Si kweli”

“Ukweli ni upi?”

“Ukweli ni kwamba nilipofika pale niliambiwa na meneja wa hoteli ile nisubiri.  Yeye ndiye aliyeniletea pombe akaniambia bosi wake aliyekuwa na wageni ofisini ndiye aliyeagiza nipewe pombe wakati namsubiri”

“Enhe… baada ya kunywa pombe  nini kilitokea?”

“Kilichotokea ni kwamba mimi sikutaka kunywa bia nyingi lakini ilikuwa kama nililazimishwa niendelee kukaa na kunywa. Huyu msichana niliyekuwa naye ndiye aliyekuwa akinihudumia na nilijuana naye siku ile ile. Aliniambia meneja wake amemwambia niendelee kunywa tu nimsubiri bosi, umenielewa?” nikaeleza mrakibu huyo kwa utulivu

“Kama nimekuelewa au sikukuelewa nitajua mwisho wa maelezo yako, endelea”

“Nina wasiwasi kwamba huyu meneja aliniwekea kitu katika zile bia nilizokuwa ninaletewa…?”

Mrakibu huyo akashituka.

“Kitu, kama kitu gani?”

“Inawezekana ni madawa ya kulevya au kitu kingine cha kuharibu akili”

“Wewe unataka kuzusha madai mengine ambayo  hayapo. Kama ni madawa ya kulevya, unatumia mwenyewe, usisingizie watu!”

“Hapana. Mimi situmii madawa ya kulevya. Nina uhakika na  hiki kitu ninachokueleza’

“Kwanza sijakuelewa. Unasema alikuwekea hicho kitu au unahisi kuwa alikuwekea?”

“Ninahisi kuwa aliniwekea”

“Kwanini unahisi hivyo?”

“Ninahisi hivyo kwa sababu kumbukumbu zangu zinaonesha kuwa nilikunywa bia  tatu au nne lakini zilinipoteza fahamu. Sikukumbuka kitu tena mpaka asubuhi kumekucha”

“Una maana kwamba haya madai kwamba ulipangisha chumba pale na ukataka uhudumiwe chumbani mwako unayakana?”

“Ninayakana kwa sababu sina kumbukumbbu kichwani mwangu kuwa nilikodi chumba”

“Zile chupa za bia zilizokutwa na polisi katika chumba ulicholala zilikuwa za nani?”

“Hilo swali litajibiwa na wahudumu, mimi kama nilivyokwambia sina kumbukumbu ya kukodi chumba wala ya kuagiza bia nikiwa chumbani”

“Si kweli kwamba ulitoroka asubuhi katika chumba ulichokuwa umelala, ukaiacha maiti ya marehemu ikiwa chini?”

“Si kweli kwamba nilitoroka ila ni kweli kwamba nilijikuta nimelala pale hoteli lakini maiti sikuiona. Msichana aliyekuwa akinihudumia ambaye ninadaiwa kuwa  nimemuua ndiyo yule niliyekamatwa naye”

Mrakibu wa polisi alinyamaza kimya akanitazama kwa karibu sekunde kadhaa. Bila shaka maelezo yangu yalikuwa yamempa utata.

“Kwa hiyo yule msichana niliyekwenda kukuonesha kule mochwari ni nani?”

“Huyo meneja akija kesho atakueleza yeye. Mimi simjui.”