Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KISIWA CHA MAUTI - 14

KISIWA 14 Pict

ILIPOISHIA

“Si kweli kwamba nilitoroka ila ni kweli kwamba nilijikuta nimelala pale hoteli lakini maiti sikuiona. Msichana aliyekuwa akinihudumia ambaye ninadaiwa kuwa  nimemuua ndiyo yule niliyekamatwa naye”

Mrakibu wa polisi alinyamaza kimya akanitazama kwa karibu sekunde kadhaa. Bila shaka maelezo yangu yalikuwa yamempa utata.

“Kwa hiyo yule msichana niliyekwenda kukuonesha kule mochwari ni nani?”

“Huyo meneja akija kesho atakueleza yeye. Mimi simjui”

SASA ENDELEA...


“IInawezekana kweli ulale mahali halafu usiwe na kumbukumbu?”

“Hilo jambo linanishangaza hadi muda huu.”

“Yule marehemu alikutwa mle chumbani ulimolala. Una maana kwamba ulipotoka asubuhi ulikuwa na nani mle chumbani?”

Nikakwepa kusema ukweli.

“Nilikuwa peke yangu.”

Ukweli ni kwamba nililala na maiti ya yule msichana, na nilipotoka asubuhi niliiacha mle chumbani.

“Kwa hiyo unataka utuambie kuwa hawa jamaa wamekuzushia?”

“Ninaamini kuwa wamenizushia.”

“Unaonekana umepanga maelezo yako vizuri. Lakini kitu kimoja umesahau, kwamba upo ushahidi kuwa ulikodi chumba na ulimuua yule msichana aliyekuwa akikuhudumia. Inaaminika kwamba ulitaka kumbaka.”

Nikatikisa kichwa kukataa.

“Sijaua msichana.”

“Kwanini umekimbia kazini kwako na nyumbani kwako?”

Hapo akanibana kidogo, lakini nilipata pa kutokea.

“Sijakimbia. Niliona hizi habari kwenye magazeti zikanishitua kidogo. Ikabidi nimtafute yule msichana niliyedaiwa kumuua, na mpaka ninakamatwa nilikuwa nyumbani kwake.”

“Sawa. Kwanini unadai kwamba uliwekewa kitu kwenye bia ulizokuwa unaletewa?”

“Ni kwa sababu niliona nilipoteza kumbukumbu zangu ghafla.”

“Kwani huwezi kupoteza kumbukumbu baada ya kulewa kupita kiasi?”

“Sijalewa kupita kiasi.”

“Umejuaje kuwa hujalewa kupita kiasi wakati unadai kuwa ulipoteza kumbukumbu?”

“Labda nililewa kupita kiasi wakati sijielewi.”

“Sasa unakubali nini na unakataa nini?” Hapo sikuwa na jibu, nikanyamaza kimya.

Kwa mara ya kwanza nikamuona mrakibu huyo akizisokota ncha za sharubu zake na kuweka vishungi viwili kulia na kushoto.

Alikuwa kama anavuta fikira. Hatimaye aliniambia.

“Tatizo lililopo hapa nimeshalijua. Tatizo si kwamba wewe unakana kuwa umeua. Tatizo ni kwamba huna kumbukumbu za kuua.”

“Sasa kama sina kumbukumbu, utaniambiaje kuwa nimeua?”

“Sawa. Kama utathibitishiwa kwamba umeua, utakuwa tayari kukiri kosa kwa sababu tayari unakubali kuwa ulifika pale hotelini na ulilala hadi asubuhi, na msichana uliyemuua alikutwa ndani ya chumba ulicholala?”

“Hapo naona ni sawa na kunibambikia kesi ambayo siijui.”

“Utaijua. Uchunguzi unaendelea kufanyika, na kwa vile umetoa madai ya kuwekewa madawa ya kulevya kwenye bia, tutakupeleka kwa mkemia ili ufanyiwe uchunguzi wa damu na mkojo.”

Huo ukawa mwisho wa mahojiano yangu na mrakibu huyo.

Nikarudishwa mahabusu. Nililala humo hadi asubuhi. Kulikuwa na mlevi mmoja aliyekuwa amewekwa humo. Alikuwa akizungumza peke yake usiku kucha. Mara kadhaa alikuwa akiambiwa na wenzake aache kelele, lakini alikuwa hajielewi kabisa. Alikuwa akijiona kama yuko kitandani chumbani mwake.

Asubuhi kulipokucha nikapelekwa kwa Mkemia Mkuu, ambako nilichukuliwa mkojo na damu. Baada ya saa moja tu, majibu yalitoka kwamba mkojo wangu ulikutwa na aina ya kemikali zinazosababisha usingizi.

Mfanyakazi mmoja katika Ofisi ya Mkemia Mkuu alimwambia mrakibu wa polisi niliyekuwa naye kwamba hata wagonjwa wanaotakiwa kulala kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji hupigwa sindano yenye dawa hiyo.

“Sasa unaamini kwamba kuna mchezo niliochezewa?” nikamwambia mrakibu huyo wa polisi hapo hapo.

“Sio kwamba huyu jamaa anatumia madawa ya kulevya?” mrakibu wa polisi akamuuliza afisa huyo wa maabara.

“Haihusiani na madawa ya kulevya. Hiyo ni kemikali maalumu ambayo hutumika katika mahospitali.”

“Inaingia kwa njia gani katika mwili?”

“Kwa njia ya kupigwa sindano.”

“Kama ni kwa njia ya kunywa, inaweza kumuathiri mtu?”

“Ndiyo, inaweza.”

“Sawa.”

Mrakibu huyo wa polisi aliandika maelezo yake kwenye daftari. Sijui alikuwa akiandika maelezo gani. Baada ya hapo tukaondoka.

Wakati nikiwa kwenye gari nilijiambia, kile kilichokuwa kwenye akili yangu sasa kilikuwa kimefichuka. Nilikuwa nikihisi tangu mwanzo kuwa haukuwa ulevi wa bia uliopoteza kumbukumbu zangu. Kulikuwa na kitu ambacho niliwekewa kwenye kile kileo.

Sasa swali likawa linakuja katika akili yangu, niliwekewa dawa hizo za kupoteza fahamu kwa sababu gani wakati nilikwenda pale hotelini kikazi na pombe niliyokunywa nilikaribishwa tu?

Nikahisi kulikuwa na kitu kingine kilichojificha ambacho kiliandaliwa dhidi yangu ili niingie katika matatizo.

Hata hivyo nikajiambia hata kama kulikuwa na kitu kimeandaliwa kinitie katika matatizo, itanisaidiaje wakati huu ambapo ninadaiwa kuwa nimeua na ushahidi upo kuwa nimeua? Na mwili wa msichana ninayedaiwa kumuua upo, na niliushuhudia kwa macho yangu ndani ya chumba cha hoteli nilimokuwa nimelala.

Polisi wataangalia chanzo cha mauaji au wataangalia kuwa nimeua? Nikajiuliza. Jibu nililopata ni kuwa polisi wataangalia kama nimeua. Wakiridhika na ushahidi uliotolewa, watanifikisha mahakamani hata kama wamethibitisha kuwa niliwekewa madawa ya kulevya.

Niliamini kuwa meneja wa hoteli anaweza kukataa kuwa niliwekewa madawa hayo pale hotelini na akasisitiza kuwa kama damu yangu iligundulika kuwa na madawa hayo, nilitumia mimi mwenyewe.

Polisi wanahitaji ushahidi kwa kila kitu kinachodaiwa. Mimi sikuwa na ushahidi kuwa niliwekewa madawa ya kulevya hapo hotelini, hivyo madai hayo yanaweza yasipatiwe uzito na polisi na kuchukuliwa kwamba mimi ni mtumiaji wa madawa hayo tangu awali.

Tulipofika Kituo Kikuu cha Polisi nilipelekwa katika ofisi ya mrakibu wa polisi. Bila shaka yeye ndiye aliyekuwa ameachiwa kazi ya kusimamia uchunguzi wa kesi yangu.

“Imethibitika kwamba damu yako imegundulika kuwa ulikuwa na dawa hizo. Sasa hatuna uhakika kwamba uliwekewa, kama unavyodai, au wewe mwenyewe unazitumia,” mrakibu huyo aliniambia mara tu alipoketi kwenye kiti chake.

“Mimi situmii madawa ya kulevya, na mtaalamu amesema hayo si madawa ya kulevya ya kawaida bali ni dawa maalumu ambayo hutumika mahospitalini kuwalaza watu wanaotakiwa kufanyiwa upasuaji. Mimi nitatumia dawa hiyo ya kazi gani?” nikamwambia, kisha nikaangeza.

“Hiyo dawa niliwekewa kwenye bia walizonipa pale hotelini. Nilipokunywa nikapoteza fahamu. Sasa ni kwanini walifanya hivyo halafu waje waseme kuwa nimeua?”

Mrakibu wa polisi alishusha pumzi ndefu, akaniambia.

“Tuko kwenye uchunguzi, bwana mdogo. Kila kitu kitafahamika, lakini kwa vile umeua, sidhani kwamba utaweza kujinusuru na kosa hilo hata kama ungewekewa bangi!”

Sikumjibu kitu, nikabaki kumkodolea macho.

“Tunakuweka ndani wakati tunaendelea na uchunguzi wetu.”

Nikarudishwa mahabusu. Sikukaa kwa muda mrefu nikatolewa tena na kupelekwa ofisini kwa mrakibu huyo. Nilimkuta meneja wa Hoteli ya Makita.

Alikuwa amekaribishwa kwenye kiti, mimi nikaambiwa nisimame huku polisi mmoja akiwa amenisimamia.

“Grace, unaweza kumtambua huyu mtu?” mrakibu wa polisi akamuuliza meneja huyo wa Hoteli ya Makita.

Hapo ndipo niligundua kuwa anaitwa Grace.

Meneja huyo mwenye uso wa kijeuri akageuza uso wake na kunitazama.

“Huyu si ndiye aliyekuja hotelini kwetu na kutuletea matatizo?” akasema.

“Matatizo gani niliyoyaleta?” nikamuuliza.

“Nani amekuruhusu uulize maswali?” mrakibu wa polisi akanionya.

Nikanyamaza.

“Matatizo uliyoleta ni tuhuma za mauaji ambazo zinakukabili hapa!” mrakibu huyo wa polisi akaniambia kwa msisitizo akiwa amekasirika.

Aliendelea kunitazama kwa macho makali kuona kama nitapinga kauli yake. Alipoona nimeamua kubaki kimya, akaendelea na yule meneja.

“Umesema kwamba mfanyakazi wenu aliyeuawa anaitwa Sofia na si Edda kama ilivyoandikwa?”

“Ndiyo. Ni Sofia. Waliotoa hizo taarifa walikosea jina.”

“Jana nilimpeleka mtuhumiwa hospitalini na kumuonesha mwili wa marehemu, akasema haumtambui.”

“Ni lazima aseme hivyo, lakini yule msichana ndiye aliyekuwa akimhudumia chumbani, na inaonekana alikuwa akimtaka kimapenzi. Alipokataliwa ndipo akaona amuue, halafu asubuhi akatukimbia. Hata pesa za chumba hakulipa.”

“Na amedai kwamba eti mlimpa pombe nyingi ili kuharibu akili yake.”

“Si kweli. Alikaribishwa bia mbili tu. Nyingine alinunua mwenyewe kwa pesa zake.”

“Pia amedai kuwa katika bia alizopewa aliwekewa dawa za kulevya.”

“Hakuna aliyemuwekea dawa za kulevya. Sisi hatuuzi dawa za kulevya. Chupa inafunguliwa mbele ya macho yake. Hizo dawa atawekewa wapi?”

“Pengine aliwekewa wakati alipokwenda kujisaidia.”

“Sasa huo ni uzembe wake mwenyewe, na sisi hatuwezi kuhusika na jambo hilo. Kwanza siamini kama kweli aliwekewa hayo madawa.”

“Tulikwenda kumpima leo na imegundulika kuwa alikuwa na dawa hizo mwilini.”

“Sasa kama alitumia, labda yeye ni mtumiaji wa madawa ya kulevya. Asisingizie watu wengine.”