KISIWA CHA MAUTI - 12
ILIPOISHIA
Edda, msichana mpole na mcheshi, akanitazama. Mara nyingi anaponitazama ninaona kama anatabasamu, lakini hatabasamu. Hivyo ndivyo anavyoonekana. Usipomgundua, na wewe unaweza kutabasamu ukidhani mnatabasamu nyote.
Nilipomwona anatabasamu nilijua ilikuwa ni kawaida ya uso wake. Akainuka na kutoka.
Baadaye kidogo nikasikia pikipiki ya bodaboda ikisimama barazani. Nikatoka mle chumbani na kwenda barazani. Nikamkuta Edda yuko mlangoni huku pikipiki ikiwa pembeni mwa baraza la nyumba.
“Nimeshakuja naye, mwelekeze niende naye mara moja,” Edda akaniambia..
SASA ENDELEA...
NIKAMUELEKEZA kijana wa bodaboda mtaa niliokuwa ninaishi pale Kinondoni pamoja na namba ya nyumba yetu.
Ramani aliyoizingatia ni tawi la chama kimoja cha siasa ambalo lilikuwa jirani na nyumba yetu.
Nilimlipa pesa kijana huyo kisha nikampa funguo Edda.
“Sasa nenda naye mara moja” nikamwambia.
Kijana huyo akawasha pikipiki. Edda akajipakia nyuma yake wakaondoaka. Moyoni niliumia sana nilivyoona amemkumbatia kijana huyo wa bodaboda.
Lakini nikajiambia wivu wangu haukuwa na maana yoyyote kwa vile sikuwa na uhakika ningekuwa uraiani kwa siku ngapi.
Nikaingia ndani. Niseme ukweli kwamba yule msichana nilimshukuru sana. Tulikuwa na siku mbili tu za kujuana lakini niliona kama tulikuwa na uhusiano wa miaka na miaka. Kitendo cha kunisitiri mvunguni mwa kitanda chake wakati meneja wake anakuja kilitosha kunionesha kuwa alikuwa na imani na mimi.
Kadhalika maswali aliyomuuliza meneja wake pia yalionesha alikuwa akijaribu kunipigania ili kupata ukweli wa mauaji yaliyofanyika huko Hotelini anakofanya kazi.
Wakati namsubiri Eddda achumbani kwake nilifikiria mengi. Kwanza nilifikiria niwashe simu niwasiliane na mhariri wangu nimueleze kwamba msichana aliyedaiwa kuuawa nimekutana naye na yuko hai na anahamishiwa katika hoteli nyingine iliyoko Kibaha.
Lakini kutokana na hofu niliyokuwa nayo niliogopa kuwasha simu. Nikajiambia Edda atakaporudi nitamuazima simu yake nimpigie mhariri badala ya kuwasha simu yangu.
Nilijua kuwa mhariri asingenisaidia kitu lakini angalau angepata picha ya kile kitu kilichopo.
Nilitarajia kwamba ningemuona Edda baada ya nusu saa lakini ilipita karibu saa nzima kabla ya Edda kutokea.
Nikatoka nje kumtazamia. Wakati natoka tu nikamuona yule kijana wa bodaboda anarudi peke yake. Aliponiona aliniuliza.
“Wewe ndiye yule kaka uliyemuagiza yule msichana niliyeondoka naye hapa?” akaniiuliza.
“Ndiyo, ni mimi”
“Yule msichana amekamatwa”
Nikashituka.
“Amekamatwa na nani?”
“Amekamatwa na polisi. Tulipofika pale nyumbani aliingia ndani. Mimi nilibaki nje. Lakini baadaye kidogo niliona anatoka na jamaa wawili ambao ni wakazi wa mle ndani”
Kijana huyo akaendelea kunieleza kuwa jamaa hao wawili walimwambia kwamba polisi wameagiza mwenye chumba alichokuwa anakifungua akionekana wawapigie simu polisi.
Wakaendelea kumwambia kwamba polisi hao waliwambia jamaa hao kama mwenye chumba hicho hatatokea, mtu yeyote atakayetokea na kufungua mlango wamzuie na wawaarifu polisi.
“Kwa hiyo wamemzuia na wamepiga simu polisi. Polisi wamefika na kumhoji maswali. Mimi nikaondoka. Kwa hiyo nimekuja kukufahamisha”
Yule kijana aliponiambia hivyo akaondoka na pikipiki yake. Sasa hapo nikawa nimechanganyikiwa. Sikujua ningefanya nini. Msichana wa watu ameshakamatwa kwa ajili yangu. Na nilijua ni lazima atataja mahali nilipo ili aachiwe.
Nikaona ili nisikamatwe niondoke pale nyumbani kwani nilihisi Edda anaweza kuwaleta polisi hao pale nyumbani. Nilitaka niiache ile pikipiki ya kazini kwangu ili niwahi kuondoka kabla ya polisi hao kutokea lakini nilijiuliza ningetumia usafiri gani wakati bado nilikuwa nikiendelea kuhangaika pale jijini.
Nikaingia ndani na kufunga mlango wa chumba cha Edda kwa kuusindika. Nikatoka uani haraka haraka. Nikafungua geti na kuitoa ile pikipiki kisha nikafunga geti. Geti hilo hufungika kwa ndani. Hivyo ilibidi nirudi tena ndani nifunge geti kisha nizunguke tena na kutokea mlango wa mbele.
Nilifungua mlango nikaifuata pikipiki. Wakati naipanda mikaona gari la polisi linakuja kwa kasi. Nikajua bila shaka polisi hao wananifuata mimi. Nikaiwasha pikipiki haraka na kuiondoa kwa kasi. Nilisikia honi ikipigwa nyuma yangu lakini sikugeuka wala sikusimama. Niliongeza mwendo.
Kwa kutumia kioo cha kutazamia nyuma, niliona lile gari la polisi halikusimama nyumbani kwa Edda. Lilipitiliza moja kwa moja kunifukuzia mimi. Kutahamaki nililiona gari hilo likinipita na kwenda mbele kidogo kabla ya kuniziba njia.
Ulikuwepo upenyo wa kuweza kupita lakini kwa vile polisi walitoa mikono yao kwenye dirisha kuniashiria nisimame, sikutaka kushindana nao nikasimama.
Polisi wawili wakashuka haraka.
“Kwanini unatukimbia?” Polisi mmoja akaniuliza kwa hamaki.
“Sijawakimbia. Mimi nina safari zangu” nikawajibu nikiwa nimetulizana.
“Si tulikupigia honi kukusimamisha, kwanini hukusimama?”
“Sijajua kama mlikuwa mnanipigia honi mimi”
“Ulikuwa unakimbia kwa kujua kuwa tunakuja kukukamata, siyo?”
“Nikamatwe kwa kosa gani?”
“Hulijui kosa lako? Sasa twende kituoni utalijua. Waandishi wa habari sasa mmekuwa wauaji!”
“Nimemuua nani?”
Edda alikuwa ndani ya gari. Yule polisi aliyekuwa akinisemesha akamtazama Edda.
“Jamaa mwenyewe si ndiye huyu?” akamuuliza.
“Ndiye yeye” Edda akamjibu.
“Sasa nauliza nimemuua nani?” nikauliza tena swali langu.
“Mimi ndiye niliyeandikwa kwenye gazeti kuwa nimeuawa, mimi ndiye Edda” Edda akasema.
“Sasa kama ni wewe mbona uko hai?” Yule polisi akamuuliza.
“Nyinyi polisi ndio mjiulize” nikawambia.
“Nyie mnatuletea utani kwenye kazi! Kwanza wewe sijui ni Edda au nani, unakabiliwa na kosa la kumficha mhalifu unayetafutwa kwa mauaji. Wewe pia tutakuweka ndani”
“Mimi sijui kama ameua mtu” Edda akajitetea.
“Sasa utakwenda jua huko mbele ya safari. Shuka kwenye pikipiki yako mwandishi ochwara wewe!”
Nikashuka kwenye pikipiki.
“Tumeambiwa pia umekimbia na pikkipiki ya kazini kwako. Hilo ni kosa jingine la wizi”
Yule polisi kwa kunonesha jeuri alinitia pingu mikononi.
“Linaweza kukimbia hiri!” akaniambia na kuniamrisha niingie kwenye gari.
Wakati napanda nyuma ya gari, niliona ninashikwa kwa nyuma na kusukumizwa ndani ya gari.
Pikipiki niliyokuwa nikiiendesha ikapandwa na polisi mmoja.
Safari ya kuelekea kituo cha polisi ikaanza. Sikupelekwa kituo cha Kinondoni. Nilipelekwa kituo kikuu cha polisi. Vile nilivyokuwa mwandishi nilikuwa nangojewa kituoni hapo kama mpira wa kona.
Wakati nashushwa, kauli za polisi wengine waliokuwa hapo kituoni zilisikika.
“Mmerikamatia wapi….?”
“ Jiandishi uaji limetiwa mikononi!”
“ Ore wake, razima turiswage kwanza”
“Hivi hiri harina mke?”
Maneno ya kejeli yalikuwa yakisikika lakini nilinyamaza kimya. Japokuwa nilikuwa nikitembea kwa miguu yangu bado nilikuwa nasukumwa kwa nyuma, sijui kwa maana gani?
Kwanza nilifikishwa katika chumba kimoja mimi na Edda. Tulimkuta polisi mmoja amekaa nyuma ya meza. Tepe zake zilionesha kuwa alikuwa mrakibu wa polisi. Alikuwa ameweka mstari mwembamba wa sharubu.
“Afande tumekuja naye” Polisi mmoja miongoni mwa wale polisi waliotupeleka katika chumba hicho alimwambia mrakibu huyo.
Mrakibu huyo wa polisi aliyeonesha kuwa na roho mbaya alinitazama kwa macho makali.
“Wewe ndiye mwandishi Masha?” akaniuliza.
Yeye mwenyewe alikuwa mwembamba lakini sauti yake ilikuwa nzito na kali. Bila shaka alikuwa mvutaji sigara na mlevi.
“Ndiye mimi” nikamjibu.
“Hebu mfungueni pingu”
Yule polisi aliyenifunga pingu akanifungua.
“Unajua wewe ni mwandishi maarufu sana” mrakibu huyo wa polisi akaniambia.
“Ndiyo, mimi ni mwandishi maarufu” nikamkubalia.
“Sasa kulikuwa na tatizo gani, kwanini umefanya mambo ya ajabu kabisa?”
“Mnajua mpaka sasa sijui ni kwanini nimekamatwa. Hayo mambo ya ajabu niliyofanya, ninataka nielezwe”
“Si umeua?”
“Nimemuua nani?”
Yule mrakibu alikuwa na magazeti kadhaa juu ya meza yake. Akachukua gazeti mojawapo na kunionesha.
“Habari yako hii hapa imeandikwa”
“Swali nililouliza mimi, nimemuua nani?”
Mrakibu akalitupia macho lile gazeti haraka haraka.
“Unatuhumiwa kumuua Edda mfanyakazi wa hoteli ambayo wewe ulikwenda juzi na kufanya mauaji hayo kisha ukatoroka” akaniambia kwa kujiamini kama vile ile habari ndiyo msema kweli.
“Mbona huyo Edda ninayetuhumiwa kumuua nimekamatwa naye?” nikauliza kwa jazba.
“Yuko wapi?”
“Ni mimi” Edda akajibu.
“We msichana unataka kuleta utani! Unajua sisi tuko kazini. Ninaweza kukuweka ndani sasa hivi!” Mrakibu wa polisi akamwambia.
“Mimi ndiye Edda Ibrahimu. Mimi ndiye niliyekuwa nikimhudumia Masha alipokuja pale hoteli. Mimi ndiye ninayedaiwa kuuawa” Edda akasisitiza bila uoga.
Nilimpenda!
“Wewe unafanya kazi pale hoteli?” Mrakibu wa polisi akamuuliza.