Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dili iliyokufa - 50

HADITHI - 50 Pict

ILIPOISHIA

“Ushahidi mzuri ni wa wake wa mshitakiwa wa kwanza ambao, licha ya wao kuwa washitakiwa, wameeleza mahakamani hapa kwamba mume wao aliwaua wanawake hao kwa kuwafyonza damu na kwamba kitendo hicho ndicho agizo la majini wake.”

Mwendesha Mashitaka akaendelea.

“Ingawa wake wa mganga huyu wamemtupia mpira mume wao kwamba ndiye aliyekuwa akifanya hivyo, lakini mazingira ya matukio yaliyotokea yanaonyesha kwamba wanawake hao walikuwa washirika wa mganga huyo. Kama wasingekuwa washirika wake, wangekwenda kumripoti mume wao polisi kama alivyofanya Sharifa.”

SASA ENDELEA...


Mwendesha Mashitaka huyo alieleza kwamba hakubaliani na utetezi wa washitakiwa hao kwamba waliogopa kumripoti mshitakiwa wa kwanza kwa sababu angewaua.

“Angewaua vipi wakati huo akiwa ameshatiwa mikononi mwa serikali? Mbona hakumuua Esma?” Mwendesha Mashitaka alihoji.

“Kutokana na ushahidi huo, ninaiomba mahakama hii iwaone washitakiwa wote watatu wana hatia ya kuteka nyara na hatia ya mauaji ya kukusudia ya wanawake watatu ambao miili yao ilipatikana kwa mshitakiwa wa kwanza.”

Mwendesha Mashitaka akashindilia msumari wa mwisho aliposema:

“Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, adhabu ya kosa la kuua kwa kukusudia ni kunyongwa hadi kufa. Ni imani ya upande wa Jamhuri kwamba washitakiwa hao watakabiliwa na adhabu hiyo ili kukomesha vitendo vya aina hii na pia kutoa fundisho kwa wengine ambao wanaendelea na mchezo wa aina hii.”

Wakati mganga huyo alikuwa amenyamaza kimya akimsikiliza Mwendesha Mashitaka, wake zake walikuwa wameanza kuangua vilio baada ya kusikia kuwa adhabu ya makosa yao ilikuwa ni kifo.

Kama kulikuwa na watu waliokuwa wakiwahurumia wanawake hao kwa shauri lao, mimi sikuwahurumia hata chembe kwa sababu wote walijua kuwa siku ile ningeuawa na hakukuwa na yeyote kati yao aliyeona huzuni au kumsihi mume wao asiniue.

Mimi ningewahurumiaje watu katili kama wao? Na wanyongwe tu, iwe fundisho kwa wengine kama alivyosema Mwendesha Mashitaka, nikajiambia kimoyomoyo.

Baada ya jaji kusikiliza maelezo ya upande wa mashitaka, aliwataka washitakiwa hao wajitetee.

Mshitakiwa wa kwanza ndiye aliyetangulia kujitetea. Kwa vile walikuwa wamewekewa viti vya kukaa, ilimbidi mshitakiwa huyo kusimama. Baada ya kusimama alisema:

“Mheshimiwa Jaji, nakuomba usinihukumu ninyongwe kwa sababu katika maisha yangu sikuwahi kuua mtu.”

Akaendelea kueleza:

“Hii kesi yote imepangwa kwa sababu watu wananichukia. Hao wanawake ambao ninadaiwa nimewaua walikufa wenyewe. Labda kosa langu lilikuwa kuwakata vichwa tu, ambavyo polisi waliviona kwenye sanduku. Na kumzika mtu aliyekufa ni kitu cha kawaida.”

Mganga huyo aliuponda ushahidi wangu kuwa ni wa uongo na kwamba nilikuwa nimefundishwa niende nikaseme uongo ili apatikane na hatia.

“Mwanamke huyo sikuwa nikiishi naye na nilikuwa simjui. Siku aliyokuja kwangu ndiyo siku ambayo polisi walifika na kunikamata, na walinikuta nikimuagua,” mganga huyo akaeleza.

Nikajisemea moyoni mwangu kwamba mganga huyo anasema mimi ni muongo, lakini yeye alikuwa muongo namba moja. Siku ile alipotaka kunifyonza damu eti alikuwa akiniagua! Kama ilikuwa ni kuniagua, mbona alinipeleka kule mzimuni? Kwa nini hakuniagulia nyumbani kwake?

Mganga huyo akaendelea kueleza kwamba wake zake waliomtolea ushahidi kuwa aliwaua wanawake hao walikuwa wametishwa na polisi na walikuwa wanaropoka jambo wasilolijua kwa sababu ya hofu.

Baada ya kueleza hayo, mganga huyo alikaa kwenye kiti, lakini ghafla akasimama tena na kuendelea kueleza:

“Nilikuwa naomba mahakama inione sina kosa na iniachie huru ili niendelee kuwapa huduma za uganga wananchi mbalimbali ambao wanakuja kwangu kufuata huduma hiyo.”

Aliposema hivyo akakaa. Wakati wote jaji alikuwa kimya akimsikiliza na kuandika aliyokuwa akisema.

Baada ya mganga huyo kukaa, jaji alimuuliza:

“Umemaliza?”

“Ndiyo, Mheshimiwa,” mganga huyo akajibu kwa heshima.

Jaji akamwambia mshitakiwa wa pili naye ajitetee. Mshitakiwa wa pili alikuwa mke mkubwa wa mganga huyo. Mwanamke huyo akasimama na kumuunga mkono mume wake.

Alikanusha kila kitu alichokieleza mwanzo. Akasema kwamba mume wake hakuwaua wanawake hao bali walikufa wenyewe, na yeye akaenda kuwazika.

Akamuomba jaji awaachie huru kwa sababu hawakuwa na kosa walilotenda bali polisi waliwaonea.

Alipomaliza maelezo yake naye akakaa.

“Mshitakiwa wa tatu, na wewe jitetee,” jaji akamwambia mke wa pili wa mganga huyo.

Kila mtu alitarajia mwanamke huyo angeungana na wenzake kukana kosa, lakini aliendelea kushikilia msimamo kwamba hausiki na kosa lililofanywa na mume wake na kwamba hata siku alipokamatwa alikutwa nyumbani akiwa amelala.

“Kama mume wangu aliua, ni yeye mwenyewe. Mimi sikuhusika, na hata sikusikia ushahidi uliosema kuwa nilihusika. Nilishangaa kuona ninakamatwa na kuhusishwa na makosa ambayo hayanihusu,” akasema.

Maneno yake yalimfanya mganga na mke wake wa kwanza kumkodolea macho ya tuhuma.

Kutokana na utetezi uliotolewa na mke mdogo wa yule mganga, mimi na mume wangu tuliamini kuwa mwanamke huyo angeweza kunusurika na adhabu kwa sababu alikuwa amejitoa katika makosa ya wenzake.

Nilimwambia mume wangu kuwa mwanamke huyo angeweza kuachiwa huru. Mume wangu akakubaliana nami. Kwa maoni yake, pia aliona kwamba yule mwanamke alijitetea vizuri, ingawa mimi ambaye niliishi nyumbani kwao kwa muda nilijua kuwa alikuwa anahusika na makosa yote ya wenzake isipokuwa alikuwa anajaribu kujinasua.

Siku zikapita na wiki nne zikakamilika. Kesi ikaitishwa tena kwa ajili ya hukumu. Siku ile niliwaona washitakiwa hao wakiwa wamechoka sana.

Mganga ambaye siku zote alipoletwa mahakamani alionekana kuwa na ujasiri, alikuwa amenywea na alionekana kama alikuwa anaumwa. Mwili wake ulikuwa umeisha. Uso wake ulikuwa mwembamba na macho yalikuwa yamemtoka.

Hukumu ilipoanza kusomwa, jaji alianza kuchambua ushahidi uliokuwa umetolewa huku akisisitiza kuwa kesi yoyote inakamilika kwa ushahidi.

Akaeleza kwamba ushahidi ndio unaochukuliwa na mahakama na kutumika katika hukumu.

“Ushahidi ndio unaoonesha kuwa washitakiwa wana hatia au la,” akasema.

Alianza kuuchambua ushahidi wa upande wa mashitaka, kisha wa upande wa utetezi. Hatimaye akaupambanisha ushahidi wote ili kutenganisha mchele na chuya.

Kazi ya kusoma ushahidi na hatimaye kuupambanisha ilichukua saa nzima. Baada ya kuupambanisha ushahidi huo, jaji alisema kwamba ilikuwa dhahiri kuwa washitakiwa wote watatu walitenda makosa ambayo wameshitakiwa.

Akaeleza kwamba kosa la mauaji ya watu watatu limethibitika kwa mshitakiwa wa kwanza ambaye ni mganga mwenyewe.

“Ushahidi umeonesha kwamba mshitakiwa wa pili alikuwa akifahamu kuwa mume wake aliwaua kwa kuwafyonza damu marehemu watatu ambao miili yao ilikuwa imefukiwa,” akasema na kuongeza:

“Lakini mbali na ushahidi kuonesha kwamba mshitakiwa huyo alikuwa akifahamu, hakuna ushahidi ulioonesha kwamba na yeye alishiriki kuwaua.”

“Mshitakiwa wa tatu amejaribu kujitoa katika makosa, lakini bado kosa la kujua kilichokuwa kinaendelea na kuficha siri kwa kuogopa vitisho vya mshitakiwa wa kwanza haliwezi kumuepuka.”

Jaji akaendelea kueleza kwamba kwa sababu amewaona washitakiwa wote watatu wana makosa, amewatia hatiani.

“Sasa ni adhabu. Naanza na mshitakiwa wa kwanza. Kwa sababu wewe umeua kwa kukusudia kwa sababu za kishirikina, inabidi na wewe uuawa. Hakuna adhabu mbadala. Ninakuhukumu kunyongwa kwa kitanzi hadi ufe.”

Mganga alikuwa ameuinua uso wake akimtazama jaji. Iliposomwa hukumu hiyo, aliuinamisha uso wake na kutazama chini. Bila shaka alikuwa anajuta kwa makosa yake.

“Mshitakiwa wa pili, wewe umeepuka adhabu ya kifo kwa sababu ya kukosekana kwa ushahidi kuwa ulishiriki katika tendo la kuua. Wewe ninakuhukumu kifungo cha miaka kumi na mitano jela kwa kosa la kujua kuwa mume wako alikuwa anaua watu na wewe ukakaa kimya, jambo ambalo linaonesha kuwa mlikuwa na njama moja.”

Jaji akaendelea kutoa adhabu ya mshitakiwa wa tatu ambapo alisema anamfunga kifungo cha miaka mitatu jela kwa kosa la kujua kilichokuwa kinatendeka nyumbani kwao lakini hakutoa ripoti polisi.

“Ninakuhukumu adhabu hii ndogo kwa sababu ushiriki wako katika makosa mliyoshitakiwa haupo, ila ulikuwa unajua na uliamua kukaa kimya.”

Mke wa pili wa mganga aliangua kilio kikali baada ya hukumu kusomwa. Polisi walimsomba na kumkokota haraka kumtoa nje ya mahakama.

Washitakiwa wote walipakiwa kwenye karandinga la polisi na kupelekwa gerezani kwenda kutumikia adhabu zao.