Dili iliyokufa - 48
ILIPOISHIA
Baada ya kutupa maelezo marefu akatuambia tuwe tayari kwa matokeo yoyote yatakayopatikana na tutapata ushauri nasaha hivyo hata kama mmoja wetu au sisi sote tutagunduliwa kuwa na virusi tutafundishwa jinsi ya kuishi na virusi hivyonamaishayakaendelea kama kawaida.
Aliyenza kutolewa damu alikuwa mume wangu kisha nikatolewa mimi.
Tukaambiwa tusubiri majibu wakati wateja wengine wakipewa ushauri nasaha.
Tulisubiri kwa karibu saa moja kasorobo. Majibu yetu yaliwekwa katika bahasha. Kila mmoja bahasha yake.
SASA ENDELEA...
Moyo wangu ukaanza kunienda mbio hasa nilipokumbuka kwamba yule mganga alikuwa malaya aliyewalaghai wanawake wengi na kuwafanya wake zake. Isitoshe, alikuwa akifyonza damu za watu akiwa hajui kama walikuwa wameathirika au la.
Nikahisi kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kukutwa nimeathirika.
Uso wa mhudumu aliyekuwa akituhudumia ulikuwa umefadhaika na alikuwa akitutazama kwa kutuibia macho kama vile alikuwa akisoma mawazo yetu kisirisiri. Nikajua pana tatizo. Nikamtazama mume wangu, nikaona uso wake pia ulikuwa umefadhaika na hakutaka kunitazama.
“Sasa tumefika patamu,” mhudumu huyo akatuambia na kututazama kwa zamu huku akijaribu kutabasamu, lakini tabasamu lenyewe lilikuwa kama la kujilazimisha tu. Halikuwa la furaha.
“Kila mtu nimpe bahasha yake akasome mwenyewe au...?”
“Sisi ni wanandoa, hatuwezi kufichana kitu. Kama kuna tatizo ni wajibu wetu tujuane, na kama tuko salama vilevile ni wajibu wetu tujuane,” mume wangu alimwambia mhudumu huyo, lakini sauti yake ilikuwa imebadilika. Nikajua alikuwa amepatwa na hofu.
“Kama ni wanandoa, nitakachofanya mimi ni kumpa mume bahasha ya mke na mke bahasha ya mume ili muweze kujuana vizuri, au sivyo jamani?”
Nikamtazama mume wangu kuona atasema nini. Na yeye akanitazama mimi. Hakukuwa na aliyesema kitu kwa mwenzake. Tulitazamana tu.
“Basi kila mmoja nitampa bahasha yake. Mnaweza kuzifungua na kuzisoma hapa hapa ili mjitambue na mpate ushauri wetu.”
Hapo moyo wangu ukalipuka. Nikajua nimeambukizwa virusi na pengine nimeshamuambukiza mume wangu.
Tulipewa zile bahasha. Niseme ukweli, mkono wangu ulikuwa ukitetemeka waziwazi wakati napokea ile bahasha.
Nikaifungua haraka na kuisoma.
Sikuamini macho yangu nilipoona maandishi yaliyoashiria kuwa damu yangu ilikuwa salama. Nikarudia tena kusoma. Nikaona ni vilevile. Uso wangu ukakunjuka, nikamtazama mume wangu. Kumbe naye alikuwa ameshasoma yake na alikuwa akinitazama mimi.
Alipoona uso wangu ulikuwa umekunjuka akatabasamu na kuniuliza,
“Vipi?”
Jinsi alivyotabasamu na kuniuliza swali hilo, nikajua yeye pia damu yake ilikuwa salama.
“Chukua usome, hebu nipe ya kwako,” nikamwambia.
Mume wangu akanipa cheti chake na mimi nikampa changu. Nilipokisoma cheti hicho nikaona mambo yalikuwa safi.
Nikasikia kicheko kutoka kwa mhudumu. Nikageuza uso wangu haraka na kumtazama. Nikamuona anacheka.
Kumbe vile alivyojifanya amekunja uso wakati anakuja na zile bahasha alikuwa anatutega. Alishajua kuwa hatukuwa na tatizo. Nilipogundua hivyo na mimi nikacheka. Mume wangu alipoona tunacheka na yeye akacheka. Ilikuwa furaha tupu.
Nikaona tumekuwa kama wapumbavu, nikainuka kwenye kiti na kumshika mkono mume wangu.
“Twenzetu mume wangu,” nikamwambia.
“Subirini kwanza,” mhudumu huyo akatuambia.
Nikarudi kwenye kiti.
“Mnatakiwa mje mpime tena baada ya miezi mitatu. Kwa kawaida virusi vya UKIMWI vinaonekana kwenye damu baada ya miezi mitatu.”
“Umesikia mke wangu?” mume wangu akaniuliza.
“Hakuna tatizo, tutakuja kupima.”
“Kuna kingine?” akamuuliza mhudumu.
“Ni hicho tu.”
“Sawa. Tunakwenda.”
“Karibuni sana.”
Tukaondoka. Ingawa tuliambiwa hivyo, lakini sikuwa na wasiwasi. Nikajua hata baada ya miezi mitatu, huenda tutakapokwenda kupima tutakuwa tuko salama.
Tukarudi nyumbani tukiwa na furaha sote wawili. Baada ya kupita wiki mbili, kachero mmoja wa polisi alikuja nyumbani kwetu saa nne asubuhi. Ilikuwa siku ya Jumapili. Mume wangu hakuwa amekwenda kazini.
Yule kachero, baada ya kubisha mlango, aliuliza kama ile ilikuwa nyumba ya Mashaka ambaye alikuwa ni mume wangu.
Tukamwambia, “Ndiyo.”
Akatufahamisha kwamba yeye alikuwa askari wa upelelezi na alikuwa na maongezi na sisi. Tukamkaribisha ndani.
Tukiwa tumekaa sebuleni akatuambia kwamba yeye ndiye aliyekuwa mpelelezi wa kesi ya yule mganga muuaji na kwamba uchunguzi wa ile kesi ulikuwa umekamilika, na kwamba walikuwa wakisubiri jalada la uchunguzi huo lirudishwe kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashitaka kwa ajili ya kumpeleka mganga huyo pamoja na wake zake wawili mahakamani.
Kachero huyo aliendelea kutueleza jinsi walivyosumbuka kuwapata jamaa wa wale wanawake waliouawa, ambao walikiri kwamba ndugu zao walitoroshwa na yule mganga.
Alituambia kwamba mganga huyo, baada ya kuminywa kidogo, aliwataja ndugu wa wanawake aliowaua, na walipofuatiliwa walionyesha picha za ndugu zao hao walipokuwa hai.
Kachero huyo alimsifu mganga huyo kwamba alikuwa hodari wa kuchagua wanawake, kwani wanawake hao walikuwa wazuri na wawili miongoni mwao walikuwa wake za watu ambao aliwatorosha kwa waume zao.
Akatuambia kwamba aliwaua wanawake hao kwa miaka tofauti baada ya kuishi na kila mmoja wao kama mke wake.
“Tumetayarisha ushahidi wote pamoja na vielelezo. Hivi sasa jalada la uchunguzi liko kwa Mkurugenzi wa Mashitaka kwa uhakiki. Tunatarajia wiki ijayo litarudishwa, na nitakuja tena kuwafahamisha. Muwe tayari kutoa ushahidi wenu,” kachero huyo akatuambia.
Baada ya maelezo yake marefu akaondoka. Baada ya wiki mbili akaja tena nyumbani kutuambia kwamba jalada la kesi limeshawasili na kesho yake mganga huyo atafikishwa mahakamani.
Alikuja na maelezo yangu na ya mume wangu ambayo tuliyaandika polisi siku ile mganga huyo alipokamatwa. Tukatakiwa tujikumbushe tulichoandika ili tuwe tayari kutoa ushahidi utakapohitajika. Mimi na mume wangu tukasoma maelezo hayo. Tukagundua kuwa hakukuwa na ambacho tulikuwa tumekisahau.
Siku iliyofuata tukaenda mahakamani.
Tulimshuhudia mganga wa Mwahako na wake zake wawili wakifikishwa mahakamani. Yeye na wake zake hao walisomewa mashitaka matatu. Shitaka la kwanza lilikuwa la kutorosha wake za watu. Shitaka la pili lilikuwa la kujaribu kuniua mimi, na shitaka la tatu lilikuwa la kuua kwa kukusudia wanawake watatu.
Hawakutakiwa kukiri wala kukana mashitaka kwa vile shauri hilo lilikuwa katika hatua ya kupelekwa Mahakama Kuu.
Baada ya kusomewa mashitaka walirudishwa mahabusu. Kesi hiyo ilichukua miezi mitatu hadi kupelekwa Mahakama Kuu, ambako washitakiwa hao walikana makosa yote matatu na usikilizaji wa kesi ukaanza.
Ilipofika hatua ya kutoa ushahidi, walitangulizwa jamaa na ndugu ambao ndugu zao waliuawa na mganga huyo baada ya kuwatorosha, kuwafanya wake zake na hatimaye kuwaua kwa kuwafyonza damu.
Kulikuwa na mashahidi zaidi ya kumi. Shahidi mmoja alieleza kuwa mdogo wake alitoroshwa na mganga huyo baada ya kumuona siku ambayo mganga huyo alifika nyumbani kwao kwa ajili ya kutoa uchawi.
Akaeleza kwamba mganga huyo, alipoona kwamba mwanamke huyo alikuwa na mume wake, alimpa sumu aje ampe mume wake ili amuue. Mwanamke huyo alifanya hivyo bila kujua kwamba dawa aliyopewa ampe mume wake ilikuwa ni sumu. Mume wa mwanamke huyo alifariki dunia siku tatu baada ya kutiwa sumu hiyo kwenye chai.
Wakati ushahidi huo unatolewa, mganga huyo alikuwa anaonekana kama anasikitika. Lengo lake lilikuwa kuidanganya mahakama ionekane kwamba alikuwa anasikitika kwa kuzushiwa uongo kwamba ameua, wakati haikuwa kweli.
Shahidi mwingine alieleza mahakamani kwamba baada ya binti yake kutoroshwa na mganga huyo, mganga huyo alikwenda kwake na kumwambia kwamba binti huyo amekimbia nyumbani kwake baada ya kumuibia na kwamba alikuwa ametoa ripoti polisi ili atafutwe na kukamatwa.
Akaeleza kwamba wakati mganga huyo akimweleza hayo, kumbe alikuwa amemuua binti yake na kwenda kumzika, na alitoa maelezo ya uongo ili ijulikane kwamba mwanamke huyo alikuwa amejificha sehemu.
Ilipofika zamu yetu kutoa ushahidi, mimi ndiye niliitwa kwanza. Nikatoa ushahidi wangu huku nikiongozwa na wakili wa serikali. Kwa vile yale maelezo niliyoyaandika polisi bado yalikuwa kichwani mwangu, sikubabaika.
Baada ya kuongozwa na wakili wa serikali, ikafika zamu ya kuhojiwa maswali na wakili wa utetezi. Mganga huyo aliwekewa wakili na serikali. Kitendo hicho kinafahamika kisheria kwamba mshitakiwa wa kesi ya mauaji ambaye hana uwezo wa kuweka wakili huwekewa wakili na serikali.
Wakili huyo aliniyumbisha sana akautoboa ushahidi wangu ili usikubalike na mahakama. Alinihoji maswali mpaka jasho likanitoka.
Baada ya mimi kumaliza kuhojiwa, akafuatia mume wangu kutoa ushahidi. Naye alihojiwa maswali na wakili wa utetezi mpaka jasho likamtoka.