Dili iliyokufa - 49
ILIPOISHIA
Baada ya kuongozwa na wakili wa serikali ikafika zamu ya kuhojiwa maswali na wakili wa utetezi. Mganga huyo aliwekewa wakili na serikali. Kitendo hicho kinafahamika kisheria kwamba mshitakiwa wa kesi ya mauaji ambaye hana uwezo wa kuweka wakili huwekewa na serikali.
Wakili huyo aliniyumbisha sana akautia matundu ushahidi wangu ili usikubalike na mahakama. Alinihoji maswali mpaka jasho likanitoka.
Baada ya mimi kumaliza kuhojiwa akafuatia mume wangu kutoa ushahidi. Naye alihojiwa maswali na wakili wa utetezi mpaka na yeye jasho likamtoka.
SASA ENDELEA...
Polisi wote waliokwenda kumkamata mganga huyo siku ile nao waliitwa kutoa ushahidi kwa nyakati tofauti. Wakili wa utetezi, japokuwa alijitahidi kutaka kuuharibu ushahidi wa polisi hao, alijisumbua bure. Polisi hao walieleza mambo yanayoeleweka na yaliyotokea kweli. Kila ushahidi ulikuwa unaungwa mkono na ushahidi mwingine.
Shauri hilo lilichukua miezi minane kuunguruma mahakamani. Baada ya upande wa mashitaka kumaliza kuleta mashahidi wake, jaji aliwauliza washitakiwa kama walikuwa na mashahidi.
Washitakiwa hao wakasema kwamba hawakuwa na mashahidi. Jaji akautaka upande wa mashitaka kutoa maelezo yake ya mwisho yenye majumuisho ya kesi nzima ilivyoanza mpaka ilipofikia. Mwendesha Mashitaka akaahidi kutoa maelezo hayo pindi kesi itakapoitishwa tena.
Kesi ikaahirishwa kwa mara nyingine. Siku ambayo upande wa mashitaka ulitakiwa kutoa maelezo ya mwisho, Mwendesha Mashitaka akaeleza kwamba upande wa Jamhuri umethibitisha kuwa washitakiwa wana hatia ya kushirikiana kuteka nyara na kuwaua kwa kukusudia watu watatu.
“Ushahidi niliouleta hapa umethibitisha kwamba mshitakiwa wa kwanza ndiye aliyekuwa akiongoza zoezi hilo akisaidiwa na wake zake wawili ambao ni mshitakiwa wa pili na wa tatu,” Mwendesha Mashitaka alieleza na kuongeza.
“Kwa bahati njema, mwanamke mmoja ambaye naye alitekwa na mganga huyo lakini akaponea kuuawa ametueleza hapa jinsi alivyochukuliwa na mganga huyo akaishi naye kama mke wake huku akijua kuwa mwanamke huyo alikuwa na mume wake.”
Mwendesha Mashitaka akaendelea kueleza.
“Mwanamke huyo anayeitwa Esma binti Abdulrahmaan ametueleza jinsi alivyonusurika kuuawa baada ya kuokolewa na polisi waliovamia makazi ya mauaji ya mganga huyo.”
Mwendesha Mashitaka alinyamaza kidogo, akatoa kitambaa na kufuta jasho lililokuwa limetanda usoni mwake kabla ya kuendelea.
“Polisi waliokwenda kumuokoa Sharifa, ambaye ni mmoja wa mashahidi wetu, wameeleza jinsi walivyomkuta mshitakiwa wa kwanza akiwa amemdhibiti Esma tayari kwa kumfyonza damu kutokana na imani yake ya kishirikina.”
Mwendesha Mashitaka aliendelea.
“Mshitakiwa huyo, akiwa pamoja na wake zake wote wawili, walionyesha mahali ambapo mshitakiwa wa kwanza alizika miili ya wanawake watatu aliowaua na kuwakata vichwa. Vichwa vitatu vilipatikana ndani ya sanduku na miili ya vichwa hivyo ilifukuliwa ardhini.”
“Ndugu wa marehemu hao wameeleza hapa jinsi mshitakiwa alivyowachukua wanawake hao kwa ujanja akijifanya amewaoa, kumbe alitaka kwenda kuwatoa roho zao,” akasema.
Wakati wote Mwendesha Mashitaka akitoa maelezo hayo, mganga huyo alikuwa ameinamisha uso wake. Wake zake ndio waliokuwa wakimtazama Mwendesha Mashitaka.
Mwendesha Mashitaka akaendelea kueleza.
“Ushahidi mzuri ni wa wake wa mshitakiwa wa kwanza ambao, licha ya wao kuwa washitakiwa, wameeleza mahakamani hapa kwamba mume wao aliwaua wanawake hao kwa kuwafyonza damu na kwamba kitendo hicho ndicho agizo la majini wake.”
Mwendesha Mashitaka akaendelea.
“Ingawa wake wa mganga huyu wamemtupia mpira mume wao kwamba ndiye aliyekuwa akifanya hivyo, lakini mazingira ya matukio yaliyotokea yanaonyesha kwamba wanawake hao walikuwa washirika wa mganga huyo. Kama wasingekuwa washirika wake, wangekwenda kumripoti mume wao polisi kama alivyofanya Sharifa.”
Mwendesha Mashitaka huyo alieleza kwamba hakubaliani na utetezi wa washitakiwa hao kwamba waliogopa kumripoti mshitakiwa wa kwanza kwa sababu angewaua.
“Angewaua vipi wakati huo akiwa ameshatiwa mikononi mwa serikali? Mbona hakumuua Esma?” Mwendesha Mashitaka alihoji.
“Kutokana na ushahidi huo, ninaiomba mahakama hii iwaone washitakiwa wote watatu wana hatia ya kuteka nyara na hatia ya mauaji ya kukusudia ya wanawake watatu ambao miili yao ilipatikana kwa mshitakiwa wa kwanza.”
Mwendesha Mashitaka akashindilia msumari wa mwisho aliposema:
“Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, adhabu ya kosa la kuua kwa kukusudia ni kunyongwa hadi kufa. Ni imani ya upande wa Jamhuri kwamba washitakiwa hao watakabiliwa na adhabu hiyo ili kukomesha vitendo vya aina hii na pia kutoa fundisho kwa wengine ambao wanaendelea na mchezo wa aina hii.”
Wakati mganga huyo alikuwa amenyamaza kimya akimsikiliza Mwendesha Mashitaka, wake zake walikuwa wameanza kuangua vilio baada ya kusikia kuwa adhabu ya makosa yao ilikuwa ni kifo.
Kama kulikuwa na watu waliokuwa wakiwahurumia wanawake hao kwa shauri yao, mimi sikuwahurumia hata chembe kwa sababu wote walijua kuwa siku ile ningeuawa na hakukuwa na yeyote kati yao aliyeona huzuni au kumsihi mume wao asiniue.
Mimi ningewahurumiaje watu katili kama wao? Na wanyongwe tu, iwe fundisho kwa wengine kama alivyosema Mwendesha Mashitaka. Nikajiambia kimoyomoyo.
Baada ya jaji kusikiliza maelezo ya upande wa mashitaka aliwataka washitakiwa hao wajitetee.
Mshitakiwa wa kwanza ndiye aliyetangulia kujitetea. Kwa vile walikuwa wamewekewa viti vya kukaa, ilimbidi mshitakiwa huyo kusimama. Baada ya kusimama alisema:
“Mheshimiwa Jaji, nakuomba usinihukumu ninyongwe kwa sababu katika maisha yangu sikuwahi kuua mtu.”
Akaendelea kueleza.
“Hii kesi yote imepangwa kwa sababu watu wananichukia. Hao wanawake ambao ninadaiwa nimewaua walikufa wenyewe. Labda kosa langu lilikuwa kuwakata vichwa tu, ambavyo polisi waliviona kwenye sanduku. Na kumzika mtu aliyekufa ni kitu cha kawaida.”
Mganga huyo aliuponda ushahidi wangu kuwa ni wa uongo na kwamba nilikuwa nimefundishwa niende nikaseme uongo ili mganga huyo apatikane na hatia.
“Mwanamke huyo sikuwa nikiishi naye na nilikuwa simjui. Siku aliyokuja kwangu ndiyo siku ambayo polisi walifika na kunikamata, na walinikuta nikimuagua,” mganga huyo akaeleza.
Nikajisemea moyoni mwangu kwamba mganga huyo anasema mimi ni muongo, lakini yeye alikuwa muongo namba moja. Siku ile alipotaka kunifyonza damu eti alikuwa akiniagua! Kama ilikuwa ni kuniagua, mbona alinipeleka kule mzimuni? Kwa nini hakuniagulia nyumbani kwake?
Mganga huyo akaendelea kueleza kwamba wake zake waliomtolea ushahidi kuwa aliwaua wanawake hao walikuwa wametishwa na polisi na walikuwa wanaropoka jambo wasilolijua kwa sababu ya hofu.
Baada ya kueleza hayo mganga huyo alikaa kwenye kiti, lakini ghafla akasimama tena na kuendelea kueleza.
“Nilikuwa naomba mahakama inione sina kosa na iniachie huru ili niendelee kuwapa huduma za uganga wananchi mbalimbali ambao wanakuja kwangu kufuata huduma hiyo.”
Aliposema hivyo akakaa. Wakati wote jaji alikuwa kimya akimsikiliza na kuandika aliyokuwa akisema.
Baada ya mganga huyo kukaa, jaji alimuuliza.
“Umemaliza?”
“Ndiyo, Mheshimiwa,” mganga huyo akajibu kwa heshima.
Jaji akamwambia mshitakiwa wa pili naye ajitetee. Mshitakiwa wa pili alikuwa mke mkubwa wa mganga huyo. Mwanamke huyo akasimama na kumuunga mkono mume wake.
Alikanusha kila kitu alichokieleza mwanzo. Akasema kwamba mume wake hakuwaua wanawake hao bali walikufa wenyewe na yeye akaenda kuwazika.
Akamuomba jaji awaachie huru kwa sababu hawakuwa na kosa walilotenda, bali polisi waliwaonea.
Alipomaliza maelezo yake naye akakaa.
“Mshitakiwa wa tatu, na wewe jitetee,” jaji akamwambia mke wa pili wa mganga huyo.
Kila mtu alitarajia mwanamke huyo angeungana na wenzake kukana kosa, lakini aliendelea kushikilia msimamo kwamba hausiki na kosa lililofanywa na mume wake na kwamba hata siku alipokamatwa alikutwa nyumbani akiwa amelala.
“Kama mume wangu aliua, ni yeye mwenyewe. Mimi sikuhusika, na hata sikusikia ushahidi uliosema kuwa nilihusika. Nilishangaa kuona ninakamatwa na kuhusishwa na makosa ambayo hayanihusu,” akasema.
Maneno yake yalimfanya mganga na mke wake wa kwanza kumkodolea macho ya tuhuma.
Bila kujali kwamba washitakiwa wenzake walikuwa wakimtazama, mwanamke huyo aliendelea kueleza kuwa anajuta kuolewa na mume huyo na kwamba tangu aishi naye hakuwahi kupata faraja yoyote zaidi ya mateso.
“Naomba mahakama isiniingize katika makosa yasiyonihusu na iniachie huru kwa sababu sijatenda kosa lolote,” akamaliza na kukaa.
Baada ya mke mdogo wa mganga huyo kumaliza kutoa utetezi wake, jaji alitoa tarehe ya kusoma hukumu yake ambayo ilikuwa wiki nne kutoka siku ile.
Kesi ikaahirishwa tena. Washitakiwa wote watatu wakarudishwa mahabusu, na mimi na mume wangu tukarudi nyumbani.