Zuchu ni jeshi la mtu mmoja kama Fid Q!
Muktasari:
- Ni wimbo unaopatikana pia katika albamu ya kwanza ya Fid Q, Vina Mwanzo Kati na Mwisho (2005) ambayo ilishirikisha msanii mmoja tu wa kike ambaye ni Lady Jaydee aliyesikika katika wimbo uitwao Kadi na Ua Rose.
MWANAMUZIKI wa Hip Hop Bongo, Fid Q kupitia ngoma yake, Mwanza (2005) iliyotayarishwa na P-Funk Majani chini ya Bongo Records, alijitambulisha kama jeshi la mtu mmoja, akionyesha kuamini katika uwezo wake binafsi.
Ni wimbo unaopatikana pia katika albamu ya kwanza ya Fid Q, Vina Mwanzo Kati na Mwisho (2005) ambayo ilishirikisha msanii mmoja tu wa kike ambaye ni Lady Jaydee aliyesikika katika wimbo uitwao Kadi na Ua Rose.
“Fid ni jeshi la mtu mmoja, sikopeshi kwa nguvu ya hoja...,” aliachana Fid Q katika wimbo huo ambao umekuja kurudiwa (refix) na wasanii mbalimbali wa Hip Hop akiwemo Stamina ambaye toleo lake alilipa jina la Moro Moro, akimaanisha Morogoro anapotokea.
Ikumbukwe wimbo ndio ulimuwezesha Fid Q kushinda tuzo yake ya kwanza kutoka Tuzo za Muziki Tanzania (TMA), ambapo alishinda kipengele cha Wimbo Bora wa Hip Hop.
Ndivyo ilivyo na kwa mwimbaji kutokea WCB Wasafi, Zuchu kwa namna ambavyo amekuwa akifanya muziki wake na matokeo ambayo amekuwa akiyapata, hivyo naye ni jeshi la mtu mmoja kama ilivyo kwa Fid Q, mwanzilishi wa Cheusi Dawa Entertainment.
Zuchu aliyepata umaarufu kwa mara ya kwanza kupitia wimbo wake, Wana (2020), tangu wakati huo ameendelea kujenga himaya yake katika soko la muziki wa Bongofleva akivutia kundi kubwa la mashabiki hasa vijana.
Uandishi wa nyimbo zake na namma anavyoziwasilisha kwa njia rahisi juu ya midundo inayovutia, ni moja ya vitu vinavyopelekea Zuchu kuzidi kukubalika ingawa lebo yake ya WCB Wasafi ina mchango mkubwa kwa kila kitu ambacho anakifanya.
Huyu ni mwanamuziki wa pili wa kike kusainiwa na lebo hiyo yake Diamond Platnumz, wa kwanza alikuwa ni Queen Darleen ambaye alianza kusikika kimuziki mwanzoni mwa miaka ya 2000 baada ya kushirikiana na Dully Sykes.
Hivi karibuni Zuchu ameandika rekodi nyingine katika muziki wake baada ya video ya wimbo wake, Kwikwi (2022) kutazamwa (views) zaidi ya mara milioni 100 katika mtandao wa YouTube ikiwa ni miaka mitatu tangu imetoka.
Wimbo huo wenye mahadhi ya Amapiano na Afrobeats, umetayarishwa na S2kizzy ambaye ana historia ya kutengeneza nyimbo za Zuchu na WCB Wasafi ambazo zimefanya vizuri kwa kiwango cha juu zaidi.
Kwikwi unakuwa wimbo wa pili wa Zuchu kufanya hivyo baada ya awali ngoma yake, Sukari (2021) kuifikia rekodi hiyo mnano Machi 2024, ikiwa ni mara ya kwanza katika Bongofleva kwa mwanamuziki solo kufanya hivyo, kisha ikafuata Jeje (2020) yake Diamond hapo Agosti 2024.
Ikumbukwe kabla ya hapo, video za nyimbo zote zilizotazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 100 ni zile ambazo walishirikiana wasanii kuanzisha wawili, nazo ni Yope Remix (2019), Inama (2019) na Waah! (2020) zake Diamond, na Kwangwaru (2018) yake Harmonize.
Kwa matokeo hayo, Zuchu anakuwa msanii wa kwanza Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla, kuwa na nyimbo mbili ambazo video zake zimetazamwa zaidi ya mara milioni 100 YouTube, nyimbo ambazo ameimba peke yake, yaani bila kumshirikisha mwanamuziki mwingine (solo).
Ni rekodi ambayo hata Bosi wake Diamond hana!, hata Rayvanny, Harmonize na Jux hawana!, na inavyoonekana itawachukua miaka kadhaa kuja kufanya kitu kama hicho cha Zuchu, mziwanda wa nguli wa muziki na Taarab nchini, Khadija Kopa.
Ikumbukwe kwa sasa Zuchu ndiye msanii wa kike aliyetazamwa zaidi (most viewed) YouTube kwa muda wote ambapo kazi zake kwa ujumla zimeshatazamwa zaidi ya mara bilioni 1.25.
Kwa ujumla Zuchu anashika nafasi ya nne Tanzania nyuma ya Harmonize, Rayvanny na Diamond ambaye ni namba mbili Afrika kwa kutazamwa zaidi YouTube nyuma ya Burna Boy, mshindi wa Grammy 2021 kutokea Nigeria.
Zuchu anafanya hayo yote ikiwa ni miaka sita tangu ametoka rasmi kimuziki kupitia EP yake, I Am Zuchu (2020) ambayo aliwashirikisha wasanii wawili pekee, Khadija Kopa na Mbosso ambaye wakati huo bado alikuwa chini ya WCB Wasafi.
Kufanya vizuri kwa EP hiyo, kulipelekea Zuchu kushinda tuzo ya African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) kutoka Marekani kama Msanii Bora Chipukizi 2020, na baadaye alishinda tuzo ya pili kama Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki 2022.