Mtoto wa Zuchu apewa jina la Sanura
Muktasari:
- Kuzaliwa kwa mtoto huyo kunafungua ukurasa mpya katika maisha ya wawili hao ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakifuatiliwa kwa karibu na mashabiki kutokana na safari yao ya kimapenzi na maisha ya familia.
Msanii wa Bongo Fleva, Zuchu, amejifungua mtoto wa kike aliyepewa jina la Sanura, ambalo ni la Sanura Kassim maarufu Mama Dangote ambaye ni mama mzazi wa mume wake, Diamond Platnumz.
Akizungumza na Mwanaspoti, Esma Platnumz, ambaye ni dada wa Diamond, amethibitisha taarifa hizo na kusema Zuchu na mtoto wake wanaendelea vizuri baada ya kujifungua.
"Ni kweli amejifungua mtoto wa kike na amepewa jina la Sanura," amesema Esma.
Esma amesema mtoto huyo amepewa jina la Sanura kwa heshima ya bibi yake, jambo lililopokewa kwa furaha na familia.
Habari za kujifungua kwa Zuchu zilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii tangu jana, huku mashabiki wengi wakituma salamu za pongezi kwa familia ya Diamond na Zuchu.
Kuzaliwa kwa mtoto huyo kunafungua ukurasa mpya katika maisha ya wawili hao ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakifuatiliwa kwa karibu na mashabiki kutokana na safari yao ya kimapenzi na maisha ya familia.