Zuchu, Beyonce mbinu yao ni moja!
Muktasari:
- Hata hivyo, wasanii wamekuwa wakijitahidi kuhakikisha muziki wao unafika mbali zaidi - nje ya Afrika Mashariki kwa kujumuisha maneno kutoka lugha za kigeni ili kuwavutia wasikilizaji wasiofahamu Kiswahili.
BADO muziki wa Bongofleva unaendelea kufanya vizuri Afrika Mashariki na Kati kutokana na ukweli kwamba mataifa mengi ya ukanda huu yanazungumza lugha ya Kiswahili ambayo inatumika zaidi katika muziki huo.
Hata hivyo, wasanii wamekuwa wakijitahidi kuhakikisha muziki wao unafika mbali zaidi - nje ya Afrika Mashariki kwa kujumuisha maneno kutoka lugha za kigeni ili kuwavutia wasikilizaji wasiofahamu Kiswahili.
Mbinu hiyo sio ya wasanii wa Bongofleva pekee, bali imekuwa ikitumika hata na wanamuziki wa kimataifa kutoka maeneo mbalimbali duniani, na imekuwa na matokeo mazuri kwa baadhi yao.
Kwa sasa sio ajabu kusikia wasanii wa Nigeria kama Yemi Alade, Rema na Ayra Starr awakizipa nyimbo zao majina ya Kiswahili au kutumia naneno ya Kiswahili katika nyimbo hizo lengo likiwa ni kupata wasikilizajii wa hapa.
Mfano mwingine mzuri katika hilo ni Zuchu, staa kutoka WCB Wasafi ambaye anaendelea kuonyesha ubunifu mkubwa tangu alipotoka miaka mitano iliyopita, hatua iliyomfanya kuitwa ‘Beyonce wa Afrika’.
Ikumbukwe Zuchu alipata umaarufu kimuziki kwa mara ya kwanza baada ya kuachia Extended Playlist (EP) yake I Am Zuchu (2020) ambayo ilikaa kwenye chati za Boomplay Music kwa wiki zaidi ya 75.
Pindi alipotoa wimbo wake Cheche (2020) akiwa amemshirikisha Diamond Platnumz, ndipo ubunifu wake ulionekana kwa sababu wimbo huo umechanganya lugha ya Kiswahili na Kihispania, jambo lililoupa mvuto wa kipekee hadi kuvuka mipaka ya Afrika.
Maneno kama ‘Te amor, Te amor, Le te quiero, quiero’ yanayosikika mwanzoni mwa wimbo huo yalivutia wasikilizaji wengi duniani huku video yake hadi sasa ikiwa imetazamwa zaidi ya mara milioni 41 YouTube.
Kituo kikubwa cha televisheni cha LaSexta nchini Hispania kupitia kipindi cha Zapeando kilijadili video ya wimbo huo na kutoa pongezi nyingi kwa Zuchu, mshindi wa AFRIMMA mara mbili.
Watangazaji wa kipindi hicho walionyesha kufurahishwa na uchezaji wa Zuchu na hata kufikia hatua ya kumuita Beyonce wa Afrika, sifa ambayo anazidi kuthibitisha anaistahili kwa jinsi ukuaji wake wa kimuziki umekua.
Mfano kwa sasa Zuchu ndiye msanii namba mbili wa kike Afrika kuwa na wafuatiliaji (subscribers) wengi zaidi YouTube akiwa nao milioni 4.3, akiwa ametanguliwa na mshindi wa Grammy kutoka Afrik Kusini, Tyla mwenye milioni 5.1.
Hivyo wimbo wa Cheche haukuwa tu wa kujifurahisha, bali ni mfano wa ubunifu wa kimataifa unaoonyesha jinsi muziki wa Bongofleva unavyoweza kusimama bega kwa bega na kupenya maeneo ya mbali duniani.
Mbinu aliyotumia Zuchu hadi muziki ukafika Hispania ndio aliyotumia mwanamuziki wa Marekani, Beyonce Knowles katika wimbo wake ‘Spirit’ ambao ni sehemu ya filamu na albamu, The Lion King: The Gift (2019).
Wimbo huo ulianza kwa maneno ya Kiswahili - ‘Uishi kwa muda mrefu mfalme’ jambo lililoonyesha dhamira yake ya kuunganisha muziki wa Marekani na tamaduni za Kiafrika, lakini kubwa zaidi kulishika zaidi soko la Afrika.
Beyonce alitumia lugha mbalimbali za Kiafrika ikiwemo Kiswahili, Pidgin English, Zulu, Xhosa na Yoruba, huku akiwashirikisha wasanii kadhaa barani Afrika kama Wizkid, Burna Boy, Yemi Alade, Tiwa Savage, Tekno na Shatta Wale.
Licha ya kukosolewa kwa kutoshirikisha wasanii wa Afrika Mashariki na kuonekana kuwapendelea wale wa Nigeria, hatua hiyo kwa Beyonce ililenga zaidi upande wa kibiashara, ikizingatiwa kwamba Nigeria ina soko kubwa la watu zaidi ya milioni 230.
Beyonce, mwanachama wa zamani wa kundi la Destiny’s Child, hakufanya hivyo kwa sababu ni msanii mdogo, yeye tayari ni mkubwa tangu mwishoni mwa miaka ya 1990, lengo lake lilikuwa kutanua wigo wa biashara yake ya sanaa. Na kweli, mradi huo ulikuja kuwa na matokeo mazuri, mathalani filamu yake ndani ya wiki tatu tu ilipata mauzo ya zaidi ya Dola1 bilioni, na kuwa filamu ya nne chini ya Disney kufikia kiwango hicho kwa mwaka huo.
Ikumbukwe baada ya Beyonce kufanya vizuri na Destiny’s Child, aliachia albamu yake kwanza kama solo, Dangerously in Love (2003), iliyompa mafanikio makubwa kimuziki na hadi sasa ametoa albamu nane.
Staa huyo wa Houston, tayari ameshinda tuzo 35 za Grammy na kumfanya kuwa kinara duniani baada ya hapo Februari 2023 kuivunja rekodi ya George Solti mwenye tuzo 31, huku nafasi ya tatu ikienda kwa Quincy Jones aliyeshinda tuzo 28.