Dulla, Gigy Money wapamba uzinduzi wa Fursa Hub
Muktasari:
- Hafla hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, iliwakutanisha wasanii, watengenezaji wa maudhui pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya ubunifu, huku wageni wakishuhudia kutambulishwa rasmi kwa programu hiyo inayolenga kuwaunganisha wabunifu na fursa mbalimbali kupitia teknolojia.
Wasanii mbalimbali wa muziki wa Bongo Fleva akiwemo Dulla Makabila, Gigy Money na Dogo Pateni, wamepamba uzinduzi wa programu ya Fursa Hub katika usiku maalumu uliobeba kaulimbiu ya "Kitaa Kimehamia Mtandaoni."
Hafla hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, iliwakutanisha wasanii, watengenezaji wa maudhui pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya ubunifu, huku wageni wakishuhudia kutambulishwa rasmi kwa programu hiyo inayolenga kuwaunganisha wabunifu na fursa mbalimbali kupitia teknolojia.
Usiku huo ulipambwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali pamoja na MC Gara B, huku wageni wakipata nafasi ya kufahamu zaidi kuhusu namna programu hiyo inavyolenga kuwasaidia watumiaji kutumia vipaji na maudhui yao katika kupata fursa mbalimbali.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, mwanzilishi wa Fursa Hub, Meena Ally, alisema programu hiyo imeanzishwa kwa lengo la kuwapa nafasi wasanii, watengenezaji wa maudhui na watu wa rika zote kutumia teknolojia kama njia ya kujipatia kipato.
Alisema kupitia Fursa Hub, watumiaji wataweza kutengeneza na kupakia maudhui yao pamoja na kupata nafasi ya kufikia fursa mbalimbali zinazohusiana na ajira na shughuli za kiuchumi.
"Hii ni habari njema kwa watengenezaji wa maudhui, wasanii vijana na watu wa rika zote. Sasa kitaa kimehamia mtandaoni kupitia Fursa Hub. Ukitengeneza maudhui na kuyapakia kwenye app, unalipwa hapo hapo. Pia ni sehemu inayokuunganisha na fursa mbalimbali za ajira na maendeleo," amesema Meena.
Kwa upande wake, Dulla Makabila amesema ujio wa Fursa Hub umefika wakati muafaka, hasa kwa vijana wenye vipaji ambao wanahitaji sehemu ya kuonyesha uwezo wao na kufikia fursa mbalimbali.
Dulla amesema teknolojia imekuwa sehemu muhimu katika kukuza vipaji, hivyo mifumo kama hiyo inaweza kusaidia wasanii na wabunifu wengi kupata nafasi ya kujulikana zaidi.
"Fursa hizi zimekuja kwa muda muafaka. Kuna vijana wengi wenye vipaji na wanahitaji kujua vitu wanavyohitaji ili kufikia malengo yao. Kama watatumia nafasi hizi vizuri, zinaweza kuwasaidia sana," amesema Dulla.
Mbali na Dulla Makabila, uzinduzi huo ulihudhuriwa na mastaa mbalimbali akiwemo Lamata pamoja na Team Jua Kali ambao walionyesha kuunga mkono jitihada za kutumia teknolojia kufungua milango mipya kwa wasanii na wabunifu.
Uzinduzi wa Fursa Hub unaingia wakati ambapo wasanii na watengenezaji wa maudhui wamekuwa wakitafuta njia mpya za kutumia majukwaa ya kidijitali kukuza kazi zao na kupata kipato.